Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday, 4 December 2019

Kikombe Cha Asubuhi; Yeremia 3....


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu



Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..!

Huyo mwanamke akamwambia, “Mimi sina mume.” Yesu akamwambia, “Umesema kweli, kwamba huna mume. Maana umekuwa na waume watano, na huyo unayeishi naye sasa si mume wako. Hapo umesema kweli.”
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Huyo Mwanamke akamwambia, “Bwana, naona ya kuwa wewe u nabii. Babu zetu waliabudu juu ya mlima huu, lakini nyinyi mwasema kwamba mahali pa kumwabudia Mungu ni kule Yerusalemu.”
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Yesu akamwambia, “Niamini; wakati unakuja ambapo hamtamwabudu Baba juu ya mlima huu, wala kule Yerusalemu. Nyinyi Wasamaria mnamwabudu yule msiyemjua, lakini sisi tunamjua huyo tunayemwabudu, kwa maana wokovu unatoka kwa Wayahudi. Lakini wakati waja, tena umekwisha wasili, ambapo wenye kuabudu wa kweli watamwabudu Baba katika roho na ukweli. Maana Baba anawataka watu wanaomwabudu namna hiyo. Mungu ni roho, na watu wanaomwabudu lazima wamwabudu kwa Roho na ukweli.”
Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.

Mwisraeli asiye mwaminifu
1“Mume akimpa talaka mkewe,
naye akaondoka kwake,
na kuwa mke wa mwanamume mwingine,
je mume yule aweza kumrudia mwanamke huyo?
Je, kufanya hivyo hakutaitia nchi unajisi mkubwa?
Wewe Israeli, umefanya ukahaba na wapenzi wengi,
je, sasa unataka kunirudia mimi?
2Inua macho uvitazame vilele vya vilima!
Pako wapi mahali ambapo hawajalala nawe?
Uliwangoja wapenzi wako kando ya njia,
kama bedui aviziavyo watu jangwani.
Umeifanya nchi kuwa najisi,
kwa ukahaba wako mbaya kupindukia.
3Ndiyo maana manyunyu yamezuiliwa,
na wala mvua za vuli hazijanyesha.
Hata hivyo uko macho makavu kama kahaba,
huna haya hata kidogo.
4“Hivi punde tu si ulinililia ukisema:
‘Wewe u baba yangu,
ulinipenda tangu utoto wangu?
5Je, utanikasirikia daima?
Utachukizwa nami milele?’
Israeli, hivyo ndivyo unavyosema;
na kumbe umetenda uovu wote ulioweza.”
Israeli na Yuda sharti watubu
6Wakati wa utawala wa mfalme Yosia, Mwenyezi-Mungu aliniambia hivi: “Je, umeona jinsi Israeli asiye mwaminifu alivyofanya? Aliniacha, akapanda juu ya kila kilima kirefu na kwenda chini ya kila mti wenye majani mabichi, akafanya ukahaba wake humo! 7Mimi nilidhani kuwa baada ya kufanya yote hayo, atanirudia. Lakini wapi; hakunirudia. Yuda, dada yake mdanganyifu, alishuhudia yote hayo. 8Zaidi ya hayo, Yuda alishuhudia kuwa nilimpa Israeli talaka kwa sababu ya ukahaba wake na kwa kukosa uaminifu kwangu. Lakini hata hivyo, Yuda, dada yake mdanganyifu, hakuogopa; naye pia alikwenda na kufanya ukahaba! 9Na, kwa kuwa yeye aliona kuwa ukahaba ni jambo dogo sana kwake, aliitia nchi unajisi, na kufanya ukahaba kwa kuabudu mawe na miti. 10Pamoja na hayo yote, Yuda, dada mdanganyifu wa Israeli, hakunirudia kwa moyo wote, bali kwa unafiki tu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
11Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Mwasi Israeli amedhihirisha kuwa yeye ni afadhali kuliko Yuda mdanganyifu. 12Basi, nenda ukamtangazie Israeli maneno yafuatayo:
Rudi, ewe Israeli, usiye mwaminifu.
Nami sitakutazama kwa hasira
kwa kuwa mimi ni mwenye huruma.
Naam, sitakukasirikia milele.
13Wewe, kiri tu kosa lako:
Kwamba umeniasi mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako;
kwamba chini ya kila mti wenye majani,
umewapa miungu wengine mapenzi yako
wala hukuitii sauti yangu.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
14“Rudini, enyi watoto msio na uaminifu,
maana, mimi ndimi Bwana wenu.
Nitawachukua mmoja kutoka kila mji,
na wawili kutoka katika kila ukoo,
niwapeleke hadi mlimani Siyoni.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
15“Nitawapeni wachungaji wanipendao moyoni, watakaowalisha kwa maarifa na busara. 16Siku hizo, wakati mtakapokuwa mmeongezeka na kuwa wengi nchini, watu hawatalitajataja tena sanduku langu la agano. Hawatalifikiria kabisa, wala hawatalikumbuka tena; hawatalihitaji, wala hawataunda jingine. 17Wakati huo, mji wa Yerusalemu utaitwa ‘Kiti cha Enzi cha Mwenyezi-Mungu’, na mataifa yote yatakusanyika humo mbele yangu. Hawatafuata tena ukaidi wa matendo yao. 18Siku hizo, watu wa Yuda wataungana na watu wa Israeli, na wote kwa pamoja watatoka katika nchi ya kaskazini na kurudi katika nchi niliyowapa wazee wenu iwe mali yao.”
Watu wa Mungu waabudu sanamu
19Mwenyezi-Mungu asema,
“Israeli, mimi niliwaza,
laiti ningekuweka miongoni mwa wanangu,
na kukupa nchi nzuri ajabu,
urithi usio na kifani kati ya mataifa yote.
Nilidhani ungeniita, ‘Baba Yangu’,
na kamwe usingeacha kunifuata.
20Lakini kama mke asiye mwaminifu amwachavyo mumewe,
ndivyo ulivyokosa uaminifu kwangu.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
21“Kelele zasikika juu ya vilima:
Waisraeli wanalia na kuomboleza,
kwa kuwa wamepotoka katika njia zao,
wamenisahau mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wao.
22Rudini, enyi watoto msio na uaminifu,
mimi nitaponya utovu wenu wa uaminifu.
“Nanyi mwasema: ‘Tazama, sisi tunarudi kwako,
maana, wewe ndiwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.
23Kweli tumedanganyika mno kuabudu huko vilimani,
hakika wokovu wa Israeli
watoka kwake Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.
24“ ‘Tangu ujana wetu, tendo hili la aibu limeangamiza kila kitu walichotolea jasho wazee wetu: Makundi yao ya kondoo na ng'ombe, wana wao na binti zao. 25Hatuna budi kujilaza chini kwa aibu, na kuiacha fedheha yetu itufunike. Tangu ujana wetu hadi leo hii, wazee wetu na sisi wenyewe tumetenda dhambi mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, wala hatukumtii Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.’”

Yeremia3;1-25

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: