|
Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Tumshukuru Mungu katika yote....
Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana Mungu wa walio hai,Mungu mwenye huruma,Mungu wa upendo Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...Asante kwa wema na fadhili zako kwetu Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!
Katika sehemu hizo, walikuwako wachungaji wakikesha usiku mbugani kulinda mifugo yao. Malaika wa Bwana akawatokea ghafla, na utukufu wa Bwana ukawaangazia pande zote. Wakaogopa sana.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza, tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....
Malaika akawaambia, “Msiogope! Nimewaleteeni habari njema ya furaha kubwa itakayowapata watu wote. Kwa maana, leo hii katika mji wa Daudi, amezaliwa Mwokozi kwa ajili yenu, ndiye Kristo Bwana. Na hiki kitakuwa kitambulisho kwenu: Mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelazwa horini.”
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...
Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu, Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii.. Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako siku zote za maisha yetu... Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....
Mara kundi kubwa la jeshi la mbinguni likajiunga na huyo malaika, wakamsifu Mungu wakisema: “Utukufu kwa Mungu juu mbinguni, na amani duniani kwa watu anaowafadhili!”
Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu kila mmoja na mahitaji yake Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru... Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele... Amina...!!
Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake... Nawapenda. |
Yeremia na Warekabu
1Neno la Mwenyezi-Mungu lililomjia Yeremia wakati wa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda: 2“Nenda nyumbani kwa Warekabu, ukaongee nao. Kisha, walete katika chumba kimojawapo cha nyumba yangu mimi Mwenyezi-Mungu, uwape divai wanywe.” 3Basi, nikamchukua Yaazania mwana wa Yeremia, mwana wa Habazinia, na ndugu zake pamoja na wanawe wote na ukoo wote wa Warekabu, 4nikawaleta kwenye nyumba ya Mwenyezi-Mungu, katika chumba cha wana wa Hanani mwana wa Igdalia, mtu wa Mungu. Chumba hicho kilikuwa karibu na ukumbi wa wakuu, juu ya ukumbi wa Maaseya mwana wa Shalumu, mlinzi wa ukumbi. 5Kisha nikaleta vikombe na mabakuli yaliyojaa divai mbele ya hao Warekabu, nikawaambia, “Kunyweni divai.”
6Lakini wao wakajibu, “Sisi hatunywi divai, maana Yonadabu mwana wa Rekabu, mzee wetu, alituamuru hivi: ‘Msinywe divai; msinywe nyinyi wenyewe binafsi wala wana wenu milele. 7Msijenge nyumba, msilime mashamba, wala msiwe na shamba la mizabibu. Lakini mtaishi katika mahema siku zote za maisha yenu, ili mpate kuishi siku nyingi katika nchi mnamoishi kama wageni.’ 8Sisi tumeitii daima amri hiyo ya mzee wetu Yonadabu mwana wa Rekabu, kuhusu jambo alilotuamuru. Sisi hatunywi kamwe divai; sisi wenyewe hatunywi, wala wake zetu, wala watoto wetu wa kiume au wa kike. 9Sisi hatujijengei nyumba za kuishi. Hatuna mashamba ya mizabibu wala mashamba ya kulima na kupanda mbegu. 10Sisi tumeishi katika mahema na kutii mambo yote ambayo Yonadabu, mzee wetu, alituamuru. 11Lakini Nebukadneza, mfalme wa Babuloni alipofika, kuishambulia nchi hii, tuliamua kuja Yerusalemu ili tuliepe jeshi la Wakaldayo na la Waashuru. Kwa hiyo sasa tunaishi mjini Yerusalemu.”
12Kisha neno la Mwenyezi-Mungu likamjia Yeremia: 13“Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Nenda ukawaambie watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu hivi: Je, nyinyi hamwezi kupokea mafundisho na kusikia maneno yangu? 14Ile amri ambayo Yonadabu mwana wa Rekabu, aliwapa wanawe, kwamba wasinywe divai, imefuatwa; nao hawanywi divai mpaka siku hii ya leo, maana wametii amri ya mzee wao. Lakini mimi niliongea nanyi tena na tena, nanyi hamkunisikiliza. 15Niliwapelekea tena na tena watumishi wangu wote yaani manabii wawaambieni kila mmoja wenu aachane na mwenendo wake mwovu, arekebishe matendo yake na kuacha kuifuata na kuitumikia miungu mingine. Na kwamba mkifanya hivyo mtakaa katika nchi niliyowapa nyinyi na wazee wenu. Lakini nyinyi hamkunitegea sikio wala hamkunisikiliza. 16Wana wa Yonadabu mwana wa Rekabu, wameshika amri waliyopewa na mzee wao; lakini nyinyi hamkunitii. 17Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Ninawaletea watu wa Yuda na wakazi wote wa Yerusalemu maovu yote niliyotamka dhidi yao, kwa sababu mimi niliongea nao, lakini hawakunisikiliza; niliwaita, lakini hawakuniitikia.”
18Lakini Yeremia aliwaambia Warekabu hivi: Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: “Nyinyi Warekabu mmetii amri ya mzee wenu, mkashika maagizo yake yote na kutenda kama alivyowaamuru. 19Kwa hiyo mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema kwamba Yonadabu mwana wa Rekabu hatakosa hata mara moja mzawa wa kunihudumia daima.”
Yeremia35;1-19
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.
No comments:
Post a Comment