Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday, 21 January 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Yeremia 37....


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu



Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..!


Siku nane baadaye, wakati wa kumtahiri mtoto ulipofika, walimpa jina Yesu, jina ambalo alikuwa amepewa na malaika kabla hajachukuliwa mimba.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....




Siku zilipotimia za Yosefu na Maria kutakaswa kama walivyotakiwa na sheria, wazazi hao walimchukua mtoto, wakaenda naye Yerusalemu ili wamweke mbele za Bwana. Katika sheria ya Bwana imeandikwa: “Kila mzaliwa wa kwanza wa kiume atawekwa wakfu kwa Bwana.” Pia walikwenda ili watoe sadaka: Hua wawili au makinda mawili ya njiwa, kama ilivyotakiwa katika sheria ya Bwana.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Wakati huo huko Yerusalemu kulikuwa na mtu mmoja, mwema na mcha Mungu, jina lake Simeoni. Yeye alikuwa akitazamia kwa hamu ukombozi wa Israeli. Roho Mtakatifu alikuwa pamoja naye.
Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.

Sedekia anakwenda kuomba shauri kwa Yeremia
1Mfalme Nebukadneza wa Babuloni alimtawaza Sedekia mwana wa Yosia, kuwa mfalme wa Yuda mahali pa Konia mwana wa Yehoyakimu. 2Lakini Sedekia na maofisa wake pamoja na wananchi wa Yuda hawakusikiliza maonyo ya Mwenyezi-Mungu aliyotoa kwa njia ya nabii Yeremia.
3Mfalme Sedekia aliwatuma Yehukali mwana wa Shelemia, pamoja na kuhani Sefania mwana wa Maaseya kwa nabii Yeremia, wamwombe awaombee kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wao.
4Wakati huo, Yeremia alikuwa bado ana uhuru kutembea miongoni mwa watu, maana alikuwa bado hajatiwa gerezani. 5Tena jeshi la Farao lilikuwa limeondoka Misri, na jeshi la Wakaldayo lililokuwa limeuzingira mji wa Yerusalemu liliposikia habari hizo liliondoka.
6Ndipo neno la Mwenyezi-Mungu likamjia nabii Yeremia: 7“Mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Utamwambia hivi mfalme wa Yuda ambaye amekutuma uniombe kwa niaba yake: Tazama! Jeshi la Farao lililokuja kukusaidia, liko karibu kurudi makwao Misri. 8Na Wakaldayo watarudi kuushambulia mji huu. Watauteka mji na kuuteketeza kwa moto. 9Mimi Mwenyezi-Mungu nasema kwamba msijidanganye wenyewe na kusema kwamba jeshi la Wakaldayo litaondoka; kweli halitaondoka. 10Hata kama mkilishinda jeshi lote la Wakaldayo wanaopigana nanyi, wakabaki majeruhi tu katika mahema yao, majeruhi hao watainuka na kuuteketeza mji huu kwa moto.”
Yeremia anatiwa nguvuni
11Jeshi la Wakaldayo lilipoondoka Yerusalemu kuliepa jeshi la Farao lililokuwa linakaribia, 12Yeremia aliondoka Yerusalemu kwenda nchi ya Benyamini ili kupokea sehemu ya urithi wake.37:12 kupokea sehemu ya urithi wake: Maana katika Kiebrania si dhahiri. 13Alipokuwa katika lango la Benyamini, mlinzi mmoja aitwaye Iriya mwana wa Shelemia, mwana wa Hanania, alimkamata Yeremia na kumwambia, “Wewe unatoroka uende kujiunga na Wakaldayo!”
14Yeremia akamwambia, “Huo ni uongo! Mimi sitoroki na kwenda kujiunga na Wakaldayo.” Lakini Iriya hakusadiki maneno ya Yeremia. Basi akamtia nguvuni na kumpeleka kwa maofisa. 15Maofisa hao walimkasirikia sana Yeremia wakampiga, kisha wakamfunga gerezani katika nyumba ya katibu Yonathani iliyokuwa imegeuzwa kuwa gereza. 16Yeremia alipokuwa amefungwa gerezani kwa muda wa siku nyingi, 17mfalme Sedekia alimwita na kumkaribisha kwake. Mfalme akamwuliza kwa faragha wakiwa nyumbani mwake; “Je, kuna neno lolote kutoka kwa Mwenyezi-Mungu?” Yeremia akamjibu, “Naam! Lipo!” Kisha akaendelea kusema, “Wewe utatiwa mikononi mwa mfalme wa Babuloni.” 18Halafu Yeremia akamwuliza mfalme Sedekia, “Nimekukosea nini, au nimewakosea nini watumishi wako au watu hawa, hata unitie gerezani? 19Wako wapi manabii waliokutabiria wakisema, ‘Mfalme wa Babuloni hatakushambulia wewe wala nchi hii?’ 20Sasa nakuomba unisikilize, ee bwana wangu mfalme. Nakusihi sana ulikubali ombi langu. Tafadhali usinirudishe tena gerezani katika nyumba ya katibu Yonathani, nisije nikafia humo.”
21Basi, mfalme Sedekia akatoa amri Yeremia awekwe katika ukumbi wa walinzi akawa anapewa mkate kila siku kutoka kwa waoka mkate mpaka mikate ilipotoweka kabisa huko mjini. Basi, Yeremia alibaki katika ukumbi wa walinzi.


Yeremia37;1-21

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: