Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday, 12 February 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Tunamshukuru Mungu kwa kumaliza Kitabu cha Yeremia,Leo Tunaanza Kitabu cha Maombolezo 1....


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tunamshukuru Mungu kwa kutupa kibali cha
 kupitia kitabu cha "YEREMIA
"
Ni matumaini yangu kuna mengi tumejifunza/kufaidika
na kutupa mwanga/kuelewa kwenye kitabu hiki...


Leo tunapokwenda anza kupitia Kitabu cha"MAOMBOLEZO"tunamuomba Mungu wetu akatupe kibali,macho ya rohoni
 na akili ya kuelewa katika kujifunza NENO lake...
Ee Mungu  tunaomba ukatuongoze...!!

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!

Yesu alitoka hapo akaenda kando ya ziwa Galilaya, akapanda mlimani, akaketi. Watu wengi sana wakamjia wakiwaleta vilema, vipofu, viwete, bubu na wengine wengi waliokuwa wagonjwa, wakawaweka mbele ya miguu yake, naye Yesu akawaponya.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote 
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Umati ule wa watu ulishangaa sana ulipoona bubu wakiongea, waliokuwa wamelemaa wamepona, viwete wakitembea na vipofu wakiona; watu wakamsifu Mungu wa Israeli.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....

Basi, Yesu aliwaita wanafunzi wake, akasema, “Nawaonea huruma watu hawa kwa sababu wamekuwa nami kwa siku tatu, wala hawana chakula. Sipendi kuwaacha waende zao bila kula, wasije wakazimia njiani.” Wanafunzi wakamwambia, “Hapa tuko nyikani; tutapata wapi chakula cha kuwatosha watu wengi hivi?”
Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.


1Ajabu mji uliokuwa umejaa watu,

sasa wenyewe umebaki tupu!
Ulikuwa maarufu kati ya mataifa;
sasa umekuwa kama mama mjane.
Miongoni mwa miji ulikuwa kama binti mfalme;
sasa umekuwa mtumwa wa wengine.
2Walia usiku kucha;
machozi yautiririka.
Hakuna hata mmoja wa wapenzi wake wa kuufariji.
Rafiki zake wote wameuhadaa;
wote wamekuwa adui zake.
3Watu wa Yuda wamekwenda uhamishoni
pamoja na mateso na utumwa mkali.
Sasa wanakaa miongoni mwa watu wa mataifa,
wala hawapati mahali pa kupumzika.
Waliowafuatia wamewakamata wakiwa taabuni.
4Barabara za kwenda Siyoni zinasikitisha;
hakuna wapitao kwenda kwenye sikukuu.
Malango ya mji wa Siyoni ni tupu;
makuhani wake wanapiga kite,
wasichana wake wana huzuni,
na mji wenyewe uko taabuni.
5Adui zake ndio wanaoutawala na wanafanikiwa,
kwani Mwenyezi-Mungu ameutesa
kwa sababu ya makosa mengi.
Watoto wake wametekwa na kupelekwa mbali.
6Fahari yote ya watu wa Siyoni imewatoweka;
wakuu wake wamekuwa kama kulungu wasio na malisho.
Bila nguvu waliwakimbia watesi wao.
7Ukiwa sasa magofu matupu,
Yerusalemu wakumbuka fahari yake.
Ulipoangukia mikononi mwa maadui zake,
hakuna aliyekuwako kuusaidia.
Washindi wake walichekelea kuanguka kwake.
8Yerusalemu ulitenda dhambi mbaya,
ukawa mchafu kwa dhambi zake.
Wote waliousifia wanaudharau,
maana wameuona uchi wake.
Wenyewe wapiga kite na kujificha kwa aibu.
9Uchafu wake ulionekana waziwazi,
lakini wenyewe haukujali mwisho wake.
Anguko lake lilikuwa kubwa mno;
hakuna awezaye kuufariji.
Wasema:
“Tazama ee Mwenyezi-Mungu mateso yangu,
maana adui yangu ameshinda.”
10Maadui wamenyosha mikono yao,
wanyakue vitu vyake vyote vya thamani.
Naam umeona watu wa mataifa wakiingia hekaluni,
watu ambao Mwenyezi-Mungu aliwakataza
kujumuika na jumuiya ya watu wake.
11Watu wa Yerusalemu wote wanahangaika kutafuta chakula;
hazina zao wanazitoa kupata chakula,
wajirudishie nguvu zao.
Nao mji unalia,
“Hebu niangalie, ee Mwenyezi-Mungu,
ona jinsi nilivyogeuka kuwa duni.
12“Enyi wapita njia, hivi hamjali kitu?
Tazameni! Hakuna aliyepatwa na uchungu kama mimi,
uchungu alioniletea Mwenyezi-Mungu,
siku ya hasira yake kali.
13“Aliteremsha moto kutoka juu,
ukanichoma hata mifupani mwangu.
Alinitegea wavu akaninasa,
kisha akanirudisha nyuma,
akaniacha nimeduwaa na kuzirai mchana kutwa.
14“Aliyahesabu makosa yangu yote
akayakusanya mahali pamoja;
aliyafunga shingoni mwangu kama nira,
nikafyonzwa nguvu zangu kwa uzito wake.
Mwenyezi-Mungu aliniweka mikononi mwao
watu ambao siwezi kuwapinga.
15“Mwenyezi-Mungu aliwakataa askari walionilinda,
alitangaza wakati maalumu wa kuniadhibu
kuwaponda vijana wangu wa kiume.
Aliwaponda kama katika shinikizo
watu wangu wa Yuda.
16“Kwa sababu ya hayo ninalia,
machozi yanitiririka,
sina mtu yeyote wa kunifariji;
hakuna yeyote wa kunitia moyo.
Watoto wangu wameachwa wakiwa,
maana adui yangu amenishinda.
17“Nainyosha mikono yangu
lakini hakuna wa kunifariji.
Mwenyezi-Mungu ametoa amri dhidi yangu mimi Yakobo,
jirani zangu wawe maadui zangu.
Naam, mimi Yerusalemu nimekuwa kinyaa kwao.
18“Lakini Mwenyezi-Mungu amefanya sawa
kwa maana nimeliasi neno lake.
Nisikilizeni enyi watu wote,
yatazameni mateso yangu.
Wasichana wangu na wavulana wangu,
wamechukuliwa mateka.
19“Niliwaita wapenzi wangu,
lakini wao wakanihadaa.
Makuhani na wazee wangu
wamefia mjini
wakijitafutia chakula,
ili wajirudishie nguvu zao.
20“Ona, ee Mwenyezi-Mungu nilivyo taabuni.
Roho yangu imechafuka,
moyo wangu unasononeka
kwani nimekuasi vibaya.
Huko nje kumejaa mauaji,
ndani nako ni kama kifo tu.
21“Sikiliza ninavyopiga kite;
hakuna wa kunifariji.
Maadui zangu wote wamesikia juu ya taabu yangu:
Wanafurahi kwamba umeniletea maafa.
Uifanye ile siku uliyoahidi ifike,
uwafanye nao wateseke kama mimi.
22“Uwapatilize kwa ajili ya uovu wao wote.
Uwatende kama ulivyonitenda mimi
kwa sababu ya makosa yangu yote.
Nasononeka sana kwa maumivu
na moyo wangu unazimia.”


Maombolezo1;1-22

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: