1Neno la Mwenyezi-Mungu lililomjia Yeremia kuhusu watu wa mataifa.
Tamko la Mwenyezi-Mungu juu ya Misri
2Kuhusu Misri na jeshi la Farao Neko mfalme wa Misri, lililokuwa huko Karkemishi karibu na mto Eufrate ambalo Nebukadneza mfalme wa Babuloni alilishambulia mnamo mwaka wa nne wa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda:
3Tayarisheni ngao ndogo na kubwa
msonge mbele kupigana vita.
4Tandikeni farasi na kuwapanda,
Shikeni nafasi zenu na kofia za chuma mvae.
Noeni mikuki yenu,
vaeni mavazi yenu ya chuma!
5Lakini mbona nawaona wametishwa?
Wamerudi nyuma.
Mashujaa wao wamepigwa,
wamekimbia mbio,
bila hata kugeuka nyuma.
Kitisho kila upande.
Mwenyezi-Mungu amesema.
6Walio wepesi kutoroka hawawezi,
mashujaa hawawezi kukwepa;
huko kaskazini kwenye mto Eufrate
wamejikwaa na kuanguka.
7Nani huyo aliye kama mto Nili uliofurika
kama mito inayoumuka mawimbi?
8Misri ni kama mto Nili uliofurika
kama mito inayoumuka mawimbi
Ilisema: “Nitajaa, nitaifunika nchi,
nitaiharibu miji na wakazi wake.
9Songeni mbele, enyi farasi,
shambulieni enyi magari ya farasi.
Mashujaa wasonge mbele:
Watu wa Kushi na Puti washikao ngao,
watu wa Ludi, stadi wa kutumia pinde.”
10Siku hiyo ni siku ya Mwenyezi-Mungu wa majeshi,
ni siku ya kulipiza kisasi;
naam, siku ya kuwaadhibu maadui zake.
Upanga utawamaliza hao na kutosheka,
utainywa damu yao na kushiba.
Maana Mwenyezi-Mungu wa majeshi anayo kafara
huko kaskazini karibu na mto Eufrate.
11Pandeni Gileadi, enyi watu wa Misri,
mkachukue dawa ya marhamu.
Mmetumia dawa nyingi bure;
hakuna kitakachowaponya nyinyi.
12Mataifa yamesikia aibu yenu,
kilio chenu kimeenea duniani kote;
mashujaa wamegongana wenyewe kwa wenyewe,
wote pamoja wameanguka.
Misri inavamiwa
13Neno ambalo Mwenyezi-Mungu alimwambia Yeremia wakati alipofika Nebukadneza mfalme wa Babuloni kuishambulia nchi ya Misri:
14“Tangaza nchini Misri,
piga mbiu huko Migdoli,
tangaza huko Memfisi na Tahpanesi.
Waambie: ‘Kaeni tayari kabisa
maana upanga utawaangamiza kila mahali.’
15Kwa nini shujaa wako amekimbia?
Mbona fahali wako hakuweza kustahimili?
Kwa sababu mimi Mwenyezi-Mungu nilimwangusha chini!
16Wengi walijikwaa, wakaanguka,
kisha wakaambiana wao kwa wao:
‘Simameni, tuwaendee watu wetu,
turudi katika nchi yetu,
tuukimbie upanga wa adui.’
17“Naye Farao, mfalme wa Misri, mpangeni jina hili:
‘Kishindo kitupu!’
18Mimi naapa kwa uhai wangu
nasema mimi mfalme niitwaye Mwenyezi-Mungu wa majeshi,
kweli adui anakuja kuwashambulieni:
Ni hakika kama Tabori ulivyo mlima
kama mlima Karmeli uonekanavyo kutoka baharini.
19Enyi wakazi wa Misri
jitayarisheni na mizigo kwenda uhamishoni!
Maana mji wa Memfisi utaharibiwa kabisa,
utakuwa magofu yasiyokaliwa na watu.
20Misri ni kama mtamba mzuri wa ng'ombe,
lakini kipanga kutoka kaskazini amemvamia.
21Hata askari wake wa kukodiwa ni kama ndama wanono;
nao pia wamegeuka, wakakimbia pamoja,
wala hawakuweza kustahimili,
kwa maana siku yao ya kuangamizwa imefika,
wakati wao wa kuadhibiwa umewadia.
22Misri anatoa sauti kama nyoka anayekimbia;
maana maadui zake wanamjia kwa nguvu,
wanamjia kwa mashoka kama wakata-miti.
23Wataukata kabisa msitu wake, ingawa haupenyeki,
nasema mimi Mwenyezi-Mungu,
maana wao ni wengi kuliko nzige wasiohesabika.
24Watu wa Misri wataaibishwa,
watatiwa mikononi mwa watu kutoka kaskazini.”
25Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, alisema: “Tazama, mimi nitamwadhibu Amoni mungu wa Thebesi, nitaiadhibu Misri na miungu yake na wafalme wake, nitamwadhibu Farao na wote wanaomtegemea. 26Nitawatia mikononi mwa wale wanaotaka kuyaangamiza maisha yao, yaani Nebukadneza mfalme wa Babuloni na maofisa wake. Baadaye, nchi ya Misri itakaliwa na watu kama ilivyokuwa hapo zamani. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
Mwenyezi-Mungu atawaokoa watu wake
27“Lakini wewe usiogope, ee Yakobo mtumishi wangu,
usifadhaike, ee Israeli;
maana, kutoka mbali nitakuokoa,
nitakuja kuwaokoa wazawa wako
kutoka nchi walimohamishwa.
Yakobo utarudi na kutulia na kustarehe,
wala hakuna yeyote atakayekutia hofu.
28Usiogope, ee Yakobo mtumishi wangu,
kwa maana mimi niko pamoja nawe.
Nitayaangamiza kabisa mataifa yote
ambayo nimekutawanya kati yao,
lakini wewe sitakuangamiza.
Nitakuchapa kadiri unavyostahili,
sitakuacha bila kukuadhibu.”
Yeremia46;1-28
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.
No comments:
Post a Comment