Upanga wa Mwenyezi-Mungu
1 21:1 makala ya Kiebrania sura ya 21:6.Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: 2“Wewe mtu, ugeukie mji wa Yerusalemu, uhubiri dhidi ya sehemu zake za ibada, na kutoa unabii juu ya nchi ya Israeli. 3Waambie Waisraeli kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Mimi mwenyewe naja kupambana nanyi. Nitauchomoa upanga wangu alani mwake na kuwaua watu wema na wabaya. 4Tangu kaskazini hadi kusini, nitawakatilia mbali watu wote, wema na wabaya, kwa upanga wangu. 5Watu wote watajua kuwa mimi Mwenyezi-Mungu ndiye niliyeuchomoa upanga alani mwake na wala hautarudishwa tena ndani.
6“Nawe mtu, jikunje kama mtu aliyekata tamaa, uomboleze mbele yao. 7Wakikuuliza, ‘Kwa nini unaomboleza?’ Utawaambia: ‘Naomboleza kwa sababu ya habari zinazokuja.’ Kila mtu atakufa moyo, mikono yao yote italegea; kila aishiye atazimia na magoti yao yatakuwa kama maji. Habari hizo zaja kweli, nazo zinatekelezwa. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.”
8Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: 9“Wewe mtu, toa unabii useme: Mwenyezi-Mungu asema hivi:
Upanga! Naam, upanga umenolewa,
nao umengarishwa pia.
10Umenolewa ili ufanye mauaji,
umengarishwa umetamete kama umeme!21:10 katika makala ya Kiebrania maneno yaliyobaki hayaeleweki.
11Umenolewa na kungarishwa
uwekwe mkononi mwa mwuaji.
12Wewe mtu, lia na kuomboleza
upanga huo umenyoshwa dhidi ya watu wangu,
dhidi ya wakuu wote wa Israeli.
Wataangamizwa kwa upanga pamoja na watu wangu.
Jipige kifua kwa huzuni.
13Hilo litakuwa jaribio gumu sana.21:13 Baada ya neno jaribio gumu tafsiri hii imeacha maneno kadhaa yasiyoeleweka, ambayo neno kwa neno ni: Itakuwaje kama hakuna fimbo ya kudharauliwa? Taz mwisho wa aya 15 ambayo nayo maana yake si dhahiri.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
14Wewe mtu, tabiri!
Piga makofi,
upanga na ufanye kazi yake,
mara mbili, mara tatu.
Huo ni upanga wa mauaji
nao unawazunguka.
15Kwa hiyo wamekufa moyo
na wengi wanaanguka.
Ncha ya upanga nimeiweka katika malango yao yote.
Umefanywa ungae kama umeme,
umengarishwa kwa ajili ya mauaji.
16Ewe upanga, shambulia kulia, shambulia kushoto;
elekeza ncha yako pande zote.
17Nami nitapiga makofi,
nitatosheleza ghadhabu yangu.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Uamuzi wa Yerusalemu
18Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: 19“Wewe mtu! Chora njia mbili ambapo utapitia upanga wa mfalme wa Babuloni. Njia zote mbili zianzie katika nchi moja. Mwanzoni mwa kila njia utaweka alama ya kuonesha upande mji uliko. 20Utachora njia upanga utakapopitia kwenda kuufikilia mji wa Raba wa Waamoni, na njia nyingine inayoelekea mji wenye ngome wa Yerusalemu nchini Yuda. 21Mfalme wa Babuloni anasimama mwanzoni mwa hizo njia mbili, kwenye njia panda, apate kupiga bao. Anatikisa mishale, anaviuliza shauri vinyago vya miungu yake na kuchunguza maini ya mnyama.21:21 maini ya mnyama: Hapa Ezekieli anatuhabarisha baadhi ya njia za kupiga bao: Mishale miwili iliyotiwa alama tofauti ilitikiswa podoni na wa kwanza kutolewa ulitoa jibu. Vile vile watu walichunguza kufuatana na kanuni thabiti maini ya mnyama wa tambiko. 22Mshale unaodokezea ‘Yerusalemu’ umeangukia mkono wake wa kulia. Anaweka zana za kubomolea, anaamuru mauaji na kelele za vita zifanywe, zana za kubomolea malango zimewekwa, maboma na minara ya kuuzingira mji vimewekwa. 23Lakini watu wa Yerusalemu wataudhania kuwa ni utabiri wa uongo kwa sababu wamekula kiapo rasmi. Hata hivyo unabii huu utawakumbusha uovu wao na kusababishwa kukamatwa kwao. 24Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Wote wataweza kuziona dhambi zenu. Kila mtu atajua jinsi mlivyo na hatia. Kila kitendo mnachotenda kinaonesha dhambi zenu. Nyinyi mmehukumiwa adhabu nami nitawatia mikononi mwa maadui zenu.
25“Nawe mtawala wa Israeli wewe ni mpotovu kabisa. Siku yako imefika, naam, siku ya adhabu yako ya mwisho. 26Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nakuambia hivi: Vua kilemba chako na taji yako kwani mambo hayatabaki kama yalivyokuwa. Walio chini watakwezwa, walio juu watashushwa! 27Uharibifu! Uharibifu! Hamna chochote katika mji huu nitakachosaza. Lakini kabla ya hayo atakuja yule ambaye nimempa mamlaka ya kuuadhibu, ambaye mimi nitampa mji huo.
Adhabu ya Waamoni
28“Ewe mtu, tabiri kuhusu Waamoni na maneno yao ya dhihaka kwa Waisraeli: Waambie kuwa nasema:
Upanga, upanga!
Upanga umenyoshwa kuua,
umenolewa uangamize,
umengarishwa ungae kama umeme.
29Wakati nyinyi mmetulia katika maono yenu madanganyifu na utabiri wenu wa uongo, upanga utakuwa tayari kukata shingo za waasi na waovu. Siku imewadia ambapo maovu yenu yataadhibiwa.
30“Sasa rudisha upanga alani mwake! Nitawahukumu mahali palepale mlipoumbwa, katika nchi mlipozaliwa. 31Nitawamwagia ghadhabu yangu. Moto wa ghadhabu yangu nitaupuliza juu yenu. Nitawatia mikononi mwa watu wakatili, watu hodari wa kuangamiza. 32Mtakuwa kuni motoni, damu yenu itamwagika katika nchi. Mtu hatawakumbuka tena. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Ezekieli21;1-32
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.
No comments:
Post a Comment