Maombolezo juu ya Tiro
1Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: 2“Sasa ewe mtu, imba utenzi huu wa maombolezo juu ya mji wa Tiro, 3mji ule kando ya bahari, unaofanya biashara na mataifa ya pwani. Uambie: Bwana Mwenyezi-Mungu asema hivi:
Ewe Tiro, wewe umejigamba
u mzuri kwelikweli!
4Mipaka yako imeenea kwelikweli!
Umejengwa kama meli nzuri.
5Wajenzi wako walitumia misonobari kutoka Seniri
kupasua mbao zako zote;
walichukua mierezi kutoka Lebanoni
kukutengenezea mlingoti.
6Walichukua mialoni toka Bashani
wakakuchongea makasia yako;
walikitengenezea silaha
kwa misonobari ya kisiwa cha Kupro,
na kuipamba kwa pembe.
7Kitani kilichotariziwa kutoka Misri
kilikuwa kwa kupamba tanga lako
na kwa ajili ya bendera yako.
Chandarua chako kilitengenezwa
kwa rangi ya samawati na urujuani
kutoka visiwa vya Elisha.
8Watu wa Sidoni na Arvadi
walikuwa wapiga makasia wako.
Wenye hekima wako walikuwa ndani
wakifanya kazi kama wanamaji.
9Wazee wa Gebali na mafundi wao
walikuwa kwako kuziba nyufa zako.
Mabaharia waliokuwa wakipitia kwako
walifanya biashara nawe.
10Watu kutoka Persia, Ludi na Puti
walijiunga katika jeshi lako;
walirundika kwenye kambi zao za jeshi
ngao zao na kofia zao.
Wanajeshi hao walikupatia fahari.
11Watu wa Arvadi na wa Hele na jeshi lao walilinda kuta zako pande zote, nao watu wa Gamadi walilinda minara yako. Walitundika ngao zao kwenye kuta zako pande zote, na hivyo wakaukamilisha uzuri wako. 12Watu wa Tarshishi walifanya biashara nawe kwa sababu ya utajiri wako mwingi na wa kila namna. Walitoa fedha, chuma, bati, na risasi kupata bidhaa zako. 13Watu wa Yavani, Tubali na Mesheki, walifanya biashara nawe, wakakupatia watumwa na vifaa vya shaba wapate bidhaa zako. 14Bidhaa zako uliziuza huko Beth-togarma ili kujipatia farasi wa mizigo na wa vita, ngamia na nyumbu. 15Watu wa Dedani27:15 Dedani: Tafsiri ya Kigiriki ni Rode. walifanya biashara nawe. Nchi nyingi za pwani zilikuwa masoko yako maalumu. Watu wake walikuletea pembe za ndovu na mipingo kulipia bidhaa zako. 16Watu wa Edomu27:16 Edomu: Hati nyingine: Aramu. walifanya biashara nawe kwa sababu ya wingi wa bidhaa zako. Kwa kupata bidhaa zako walikupa akiki, vitambaa vya urujuani, vitambaa vilivyonakshiwa, kitani safi, matumbawe na yakuti. 17Hata watu wa Yuda na Israeli walifanya biashara nawe; walikupa ngano,27:17 makala ya Kiebrania ina maneno mawili yasiyoeleweka. zeituni, tini za mwanzoni, asali, mafuta na marhamu kulipia bidhaa zako. 18Watu wa Damasko walifanya biashara nawe kwa sababu ya wingi wa bidhaa zako; walikupa divai kutoka Helboni na sufu nyeupe. 19Vedani na Yavani walisafirisha bidhaa zako toka Uzali; hata chuma kilichofuliwa, mdalasini na mchaichai ili kupata bidhaa zako. 20Watu wa Dedani walifanya biashara nawe kwa kukupatia matandiko ya farasi. 21Waarabu na wakuu wote wa nchi ya Kedari walikuwa wachuuzi wako wakuu katika biashara ya wanakondoo, kondoo madume na mbuzi. 22Wachuuzi wa Sheba na wa Rama walifanya biashara nawe; walikuletea viungo vya chakula, vito vya thamani na dhahabu kujipatia bidhaa zako safi. 23Wakazi wa miji ya Harani, Kane na Edeni na wachuuzi wa Ashuru na Kilmadi walifanya biashara nawe. 24Hao walifanya nawe biashara ya mavazi ya fahari, nguo za buluu zilizotariziwa, mazulia ya rangi angavu vifundo na kamba zilizosokotwa imara. 2527:25-36 Taz Ufu 18:11-19 Merikebu za Tarshishi ndizo zilikusafirishia bidhaa zako.
Basi kama meli katikati ya bahari
wewe ulikuwa umejaa shehena.
26Wapiga makasia wako walikupeleka mbali baharini.
Upepo wa mashariki umekuvunjavunja
ukiwa mbali katikati ya bahari.
27Utajiri wako wa bidhaa na mali,
wanamaji wako wote chomboni,
mafundi wako wa meli na wachuuzi wako,
askari wako wote walioko kwako,
pamoja na wasafiri walioko kwako,
wote wataangamia baharini,
siku ile ya kuangamizwa kwako.
28Mlio wa mabaharia wako utakaposikika,
nchi za pwani zitatetemeka.
29Hapo wapiga makasia wote
wataziacha meli zao.
Wanamaji na manahodha watakaa pwani.
30Wataomboleza kwa uchungu wa moyo juu yako,
na kulia kwa uchungu mkubwa;
watajitupia mavumbi vichwani mwao
na kugaagaa kwenye majivu.
31Wamejinyoa vichwa kwa ajili yako
na kuvaa mavazi ya gunia.
Watalia kwa uchungu wa moyo juu yako.
32Wataimba wimbo wa ombolezo juu yako;
‘Nani aliyepata kuangamizwa kama Tiro
katikati ya bahari?’
33Bidhaa zako zilipowasili nchi za ngambo,
ulitosheleza mahitaji ya watu wengi!
Kwa wingi wa utajiri wa bidhaa zako
uliwatajirisha wafalme wa dunia.
34Lakini sasa umevunjikia baharini;
umeangamia katika vilindi vya maji.
Shehena yako na jamii ya mabaharia
vimezama pamoja nawe.
35Wakazi wote wa visiwani
wamepigwa na bumbuazi juu yako;
wafalme wao wameogopa kupindukia,
nyuso zimekunjamana kwa huzuni.
36Wachuuzi wa mataifa watakufyonya!
Umeufikia mwisho wa kutisha,
na hutakuwapo tena milele!”
Ezekieli27;1-36
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.
No comments:
Post a Comment