Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday, 22 April 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Ezekieli 46...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!

Nawaandikieni mpate kujua kwamba mnao uhai wa milele nyinyi mnaoamini kwa jina la Mwana wa Mungu. Na sisi tuko thabiti mbele ya Mungu kwani tuna hakika kwamba tukimwomba chochote kadiri ya matakwa yake, yeye hutusikiliza.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Yeye hutusikiliza kila tunapomwomba; na kwa vile tunajua kwamba yeye hutusikiliza kila tunapomwomba, twajua pia kwamba hutupatia yote tunayomwomba.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....

Mtu akimwona ndugu yake ametenda dhambi isiyompeleka kwenye kifo, anapaswa kumwombea kwa Mungu, naye Mungu atampatia uhai. Nasema jambo hili kuhusu wale waliotenda dhambi ambazo si za kifo. Lakini ipo dhambi yenye kumpeleka mtu kwenye kifo, nami sisemi kwamba mnapaswa kumwomba Mungu kwa ajili ya hiyo.
Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...

Nawapenda.

1“Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Lango la ua wa ndani unaoelekea mashariki litafungwa siku zote sita za kazi. Siku za sabato na siku za mwezi mwandamo litafunguliwa. 2Toka nje, mtawala ataingia ukumbi wa ndani kwa kupitia lango la ukumbi huo. Naye atasimama karibu na nguzo ya lango, wakati makuhani wanateketeza sadaka zake za kuteketezwa na sadaka za amani. Kisha mtawala huyo atasujudia kwenye lango na baadaye atatoka nje. Lango litabaki wazi hadi jioni. 3Kila siku ya sabato na sikukuu ya mwezi mwandamo, watu wote wataniabudu mimi Mwenyezi-Mungu mbele ya lango. 4Siku ya sabato, mtawala atamletea Mwenyezi-Mungu wanakondoo sita na kondoo dume mmoja, wote wasio na dosari, kama sadaka ya kuteketezwa nzima. 5Pamoja na kila kondoo dume, ataleta sadaka ya unga lita kumi na saba na nusu, lakini pamoja na kila mwanakondoo ataleta sadaka yoyote anayoweza. Na kwa kila sadaka ya unga, ataleta lita tatu za mafuta. 6Wakati wa sikukuu ya mwezi mwandamo atatoa fahali mchanga, wanakondoo sita, na kondoo dume mmoja; wote wasio na dosari. 7Pamoja na kila fahali na kila kondoo dume anayetolewa sadaka, ni lazima pawepo lita kumi na saba na nusu za unga, na pamoja na kila mwanakondoo, ni lazima pawepo chochote ambacho mtawala anatoa. Tena kwa kila sadaka ya nafaka, ni lazima kutoa lita tatu za nafaka.
8“Mtawala anapotoka ni lazima auache ukumbi kwa njia ileile aliyoingia nayo. 9Watu wanapokuja kumwabudu Mwenyezi-Mungu wakati wa sikukuu yoyote, wale walioingia kwa njia ya lango la kaskazini, watatoka kwa njia ya lango la kusini; na wale walioingia kwa lango la kusini, watatoka kwa njia ya lango la kaskazini. Mtu asirudi kwa njia ya lango aliloingilia, bali atatoka kwa njia ya lango lililo mbele yake. 10Mtawala ataingia ndani watu wanapoingia, na atatoka wanapotoka. 11Wakati wa siku za sikukuu na siku zilizopangwa, sadaka za nafaka zitakuwa lita kumi na saba zikiandamana na kila fahali au kondoo dume, na chochote ambacho anayeabudu anaweza kutoa kwa kila mwanakondoo. Kwa kila sadaka ya nafaka atatoa lita tatu za mafuta. 12Mtawala anapotaka kumtolea Mwenyezi-Mungu sadaka kwa hiari, iwe sadaka ya kuteketezwa au sadaka ya amani, watamfungulia lango la ukumbi wa ndani unaoelekea mashariki. Atatoa sadaka kama anavyofanya siku ya sabato, na anapotoka, lango lifungwe nyuma yake.
Dhabihu za kila siku
13“Kila siku asubuhi mtamtolea Mwenyezi-Mungu mwanakondoo wa mwaka mmoja asiye na dosari, ambaye atateketezwa mzima. 14Pia kila siku, sadaka ya kilo mbili za unga itatolewa asubuhi pamoja na lita moja ya mafuta ya zeituni yakichanganywa na unga. Ni lazima kufuata sheria za sadaka hii kwa Mwenyezi-Mungu milele. 15Mwanakondoo, unga na mafuta ni lazima vitolewe kila siku asubuhi kwa Mwenyezi-Mungu milele.
Mtawala na ardhi
16“Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Ikiwa mtawala anampa mmojawapo wa wanawe zawadi ya ardhi, zawadi hiyo itakuwa mali ya huyo kijana milele kama sehemu ya jamaa yake. 1746:17 Taz Lawi 25:10 Lakini ikiwa atampa mmoja wa watumishi wake sehemu yoyote ya ardhi yake, zawadi hiyo itakuwa mali yake mpaka mwaka wa kuachwa huru. Ndipo itakapomrudia mtawala. Ni yeye tu na watoto wake wa kiume wanaoweza kuimiliki daima. 18Mtawala kamwe asipore mali ya watu. Ardhi yoyote anayowapa watoto wake wa kiume ni lazima itokane na eneo lake mwenyewe. Hivyo hatawadhulumu watu wangu kwa kuwanyanganya ardhi yao.”
Majiko ya hekalu
19Kisha, yule mtu akanipitisha kwenye nafasi ya kupitia kuingia kwenye vyumba vitakatifu vya makuhani vinavyoelekea kaskazini, karibu na lango la kusini la ukumbi wa ndani. Akanionesha mahali, upande wa magharibi wa vyumba, 20akaniambia: “Hapa makuhani huchemsha nyama ya sadaka ya kuondoa hatia, sadaka ya kuondoa dhambi, na kuoka sadaka za nafaka. Kwa hiyo hawatoki nje ya ukumbi na chochote, ili watu wasije wakawa najisi kwa kugusa kitu kitakatifu.”
21Kisha akanipeleka kwenye uwanja wa nje, akanipitisha karibu na pembe nne za ua; kwa kila pembe ya ua kulikuwapo kiwanja kidogo, 22yaani, kwa pembe nne za ua vilikuwapo viwanja vinne vidogo vya urefu wa mita 20 na upana mita 15. 23Ulikuwapo ukuta kukizunguka kila kiwanja, na mahali pa moto mkabala na ukuta. 24Yule mtu akaniambia: “Haya ni majiko ambako watumishi wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu watachemsha sadaka wanazoleta watu.”


Ezekieli46;1-24

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)


"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: