1Waefraimu waliponena, watu walitetemeka;
Waefraimu walikuwa na uwezo mkubwa huko Israeli,
lakini walianza kumwabudu Baali, wakajiletea kifo.
2Waefraimu wameendelea kutenda dhambi,
wakajitengenezea sanamu za kusubu,
sanamu zilizotengenezwa kwa ustadi wao,
zote zikiwa kazi ya mafundi.
Wanasema, “Haya zitambikieni!”
Wanaume wanabusu ndama!
3Basi, watatoweka kama ukungu wa asubuhi,
kama umande utowekao upesi;
kama makapi yanayopeperushwa mahali pa kupuria,
kama moshi unaotoka katika bomba.
4Mwenyezi-Mungu asema:
“Lakini mimi, Mwenyezi-Mungu, ni Mungu wenu,
ambaye niliwatoa nchini Misri;
hamna mungu mwingine ila mimi,
wala hakuna awezaye kuwaokoeni.
5Ni mimi niliyewatunza mlipokuwa jangwani,
katika nchi iliyokuwa ya ukame.
6Lakini mlipokwisha kula na kushiba,
mlianza kuwa na kiburi, mpaka mkanisahau.
7Basi, nitakuwa kama simba kwenu nyote;
nitawavizieni kama chui njiani.
8Nitawarukieni kama dubu
aliyenyang'anywa watoto wake.
Nitawararua vifua vyenu
na kuwala papo hapo kama simba;
nitawararua vipandevipande kama mnyama wa porini.
9“Nitawaangamiza, enyi Waisraeli.
Nani ataweza kuwasaidia?
10Yuko wapi sasa mfalme wenu awaokoe?
Wako wapi wale wakuu wenu wawalinde?
Nyinyi ndio mlioomba:
‘Tupatie mfalme na wakuu watutawale.’
11Kwa hasira yangu mimi nikawapa mfalme,
kisha nikamwondoa kwa ghadhabu yangu.
12“Uovu wa Efraimu uko umeandikwa,
dhambi yake imehifadhiwa ghalani.
13Maumivu kama ya kujifungua mtoto yanamfikia.
Lakini yeye ni mtoto mpumbavu;
wakati ufikapo wa kuzaliwa
yeye hukataa kutoka tumboni kwa mama!
14Yanibidi kuwakomboa hawa watu kutoka kuzimu;
sharti niwaokoe kutoka kifoni!
Ewe Kifo, yako wapi maafa yako?
Ewe Kuzimu, yako wapi maangamizi yako?
Mimi sitawaonea tena huruma!
15“Hata kama Efraimu atastawi kama nyasi,
mimi Mwenyezi-Mungu nitavumisha upepo wa mashariki,
upepo utakaozuka huko jangwani,
navyo visima vyake vitakwisha maji,
chemchemi zake zitakauka.
Hazina zake zote za thamani zitanyakuliwa.”
16Watu wa Samaria wataadhibiwa kwa kosa lao.
Kwa sababu wamemwasi Mungu wao.
Watauawa kwa upanga,
vitoto vyao vitapondwapondwa,
na kina mama wajawazito watatumbuliwa.
Hosea13;1-16
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe