Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday, 25 May 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Hosea 9..

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah ni siku/wiki/nyingine tena Mungu wetu ametuchagua

na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Si kwamba sisi tumetenda mema sana wala si kwa nguvu zetu
si kwa utashi wetu wala si kwa akili zetu si kwamba sisi
ni wazuri mno si kwa uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii
Ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu....

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Basi, tukiwa wafanyakazi pamoja na Mungu, tunawasihi msikubali ile neema mliyopokea kutoka kwa Mungu ipotee bure. Mungu asema hivi: “Wakati wa kufaa nimekusikiliza, wakati wa wokovu nikakusaidia.” Basi, sasa ndio wakati wa kufaa; sasa ndiyo siku ya wokovu!
Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudshia Mungu wetu....!!

Tazama jana imepita ee Mungu wetu leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
 Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Jehovah usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona

Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona....

Kusudi tusiwe na lawama yoyote katika utumishi wetu, hatupendi kumwekea mtu yeyote kizuizi chochote. Badala yake, tunajionesha kuwa kweli watumishi wa Mungu kwa kila kitu: Kwa uvumilivu mwingi wakati wa mateso, shida na taabu.
Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu

Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Tumepigwa, tumetiwa gerezani na kuzomewa hadharani; tumefanya kazi tukachoka; tumekesha na kukaa bila kula. Tunajionesha kuwa watumishi wa Mungu kwa usafi wa moyo, elimu, uvumilivu na wema; kwa Roho Mtakatifu, kwa upendo usio na unafiki,
Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimamie Neno lako nalo likawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
kama inavyompendeza yeye....
Nawapenda.

Hosea anatangaza adhabu ya Israeli
1Msifurahi enyi Waisraeli!
Msifanye sherehe kama mataifa mengine;
maana, mmekuwa wazinzi kwa kumwacha Mungu wenu.
Mmefurahia malipo ya uzinzi,
kila mahali pa kupuria nafaka.
2Lakini ngano na mapipa ya divai haitawalisha,
hamtapata divai mpya.
3Hawatakaa katika nchi ya Mwenyezi-Mungu;
naam, watu wa Efraimu watarudi utumwani Misri;
watakula vyakula najisi huko Ashuru.
4Hawatamtolea Mwenyezi-Mungu sadaka ya divai,
wala hawatamfurahisha kwa tambiko zao.
Chakula chao kitakuwa kama cha matanga,
wote watakaokila watatiwa unajisi.
Kitakuwa chakula cha kuwashibisha tu,
hakitafaa kuletwa nyumbani kwa Mwenyezi-Mungu.
5Mtafanya nini katika sikukuu ile iliyopangwa,
au katika karamu ya Mwenyezi-Mungu?9:5 Labda ni sikukuu iitwayo ya vibanda, Taz fahirisi.
6Mtakapoyakimbia maangamizi ya nchi yenu,
Misri itawakaribisheni kwake,
lakini makaburi yenu yawangoja huko Memfisi.
Magugu yatamiliki hazina zenu za fedha,
miiba itajaa katika mahema yenu.
7Siku za adhabu zimewadia,
naam, siku za kulipiza kisasi zimefika;
Waisraeli lazima wautambue wakati huo!
Nyinyi mnasema, “Nabii ni mpumbavu;
anayeongozwa na roho ni mwendawazimu.”
Mnasema hivyo kwa sababu ya uovu wenu mkubwa,
kwa sababu ya chuki yenu kali dhidi yake.
8Nabii ni mlinzi wa Waefraimu kwa niaba ya Mungu;
lakini, kokote aendako anategewa mtego kama ndege.
Hata nyumbani mwa Mungu wake anachukiwa.
9 Taz Amu 19:21 Nyinyi mmezama katika uovu,
kama ilivyokuwa kule Gibea.
Mungu atayakumbuka makosa yao,
na kuwaadhibu kwa dhambi zao.
Dhambi ya Israeli na matokeo yake
10Mwenyezi-Mungu asema:
“Nilipowakuta Waisraeli
walikuwa kama zabibu jangwani.
Nilipowaona wazee wenu
walikuwa bora kama tini za kwanza.
Lakini mara walipofika huko Baal-peori,
walijiweka wakfu kuabudu chukizo Baali,
wakawa chukizo kama hicho walichokipenda.
11Fahari ya Efraimu itatoweka kama ndege;
watoto hawatazaliwa tena,
hakutakuwa na watoto wa kuzaliwa,
wala hakutakuwa na kuchukuliwa mimba!
12Hata kama wakilea watoto,
sitamwacha hai hata mmoja wao.
Ole wao, nitakapowaacha peke yao!”
13Kama nilivyokwisha ona hapo kwanza,
Efraimu alikuwa kama mtende mchanga penye konde zuri;
lakini sasa Efraimu itamlazimu kuwapeleka watoto wake wauawe.
14Uwaadhibu watu hawa ee Mwenyezi-Mungu!
Lakini utawaadhibu namna gani?
Uwafanye wanawake wao kuwa tasa;
uwafanye wakose maziwa ya kunyonyesha watoto wao!
Hukumu ya Mwenyezi-Mungu kwa Israeli
15Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Uovu wao wote ulianzia Gilgali;
huko ndiko nilipoanza kuwachukia.
Kwa sababu ya uovu wa matendo yao,
nitawafukuza nyumbani kwangu.
Sitawapenda tena.
Viongozi wao wote ni waasi.
16Watu wa Efraimu wamepigwa,
wamekuwa kama mti wenye mzizi mkavu,
hawatazaa watoto wowote.
Hata kama wakizaa watoto,
nitawaua watoto wao wawapendao.”
17Kwa vile wamekataa kumsikiliza,
Mungu wangu atawatupa;
wao watatangatanga kati ya mataifa.


Hosea9;1-17

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: