|
Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Tunamshukuru Mungu kwa kutupa kibali cha kupitia kitabu cha "HOSEA" Ni matumaini yangu kuna mengi tumejifunza/kufaidika na kutupa mwanga/kuelewa kwenye kitabu hiki... Leo tunapokwenda anza kupitia Kitabu cha"YOELI"tunamuomba Mungu wetu akatupe kibali,macho ya rohoni na akili ya kuelewa katika kujifunza NENO lake... Ee Mungu tunaomba ukatuongoze...!!Tumshukuru Mungu wetu katika yote...
Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana Mungu wa walio hai,Mungu mwenye huruma,Mungu wa upendo Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!
Neno la Mwenyezi-Mungu likanijia: “Nenda ukawatangazie waziwazi wakazi wote wa Yerusalemu kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Naukumbuka uaminifu wako ulipokuwa kijana, jinsi ulivyonipenda kama mchumba wako, ulivyonifuata jangwani kwenye nchi ambayo haikupandwa kitu.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza, tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....
Israeli, wewe ulikuwa mtakatifu kwangu, ulikuwa matunda ya kwanza ya mavuno yangu. Wote waliokudhuru walikuwa na hatia, wakapatwa na maafa. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...
Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu, Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii.. Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako siku zote za maisha yetu... Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....
Sikilizeni neno la Mwenyezi-Mungu, enyi wazawa wa Yakobo. Sikilizeni enyi jamaa zote za wazawa wa Israeli. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Wazee wenu waliona kosa gani kwangu hata wakanigeuka na kuniacha, wakakimbilia miungu duni, hata nao wakawa watu duni?
Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu kila mmoja na mahitaji yake Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru... Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele... Amina...!!
Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake... Nawapenda. |
1Neno la Mwenyezi-Mungu lililomjia Yoeli, mwana wa Pethueli:
Watu waombolezea mimea
2Sikilizeni kitu hiki enyi wazee;
tegeni sikio wakazi wote wa Yuda!
Je, jambo kama hili limewahi kutokea maishani mwenu,
au nyakati za wazee wenu?
3Wasimulieni watoto wenu jambo hili,
nao wawasimulie watoto wao,
na watoto wao wakisimulie kizazi kifuatacho.
4Nzige, makundi kwa makundi, wameivamia mimea;
kilichoachwa na nzige kimeliwa na tunutu,
kilichoachwa na tunutu kimeliwa na parare,
kilichoachwa na parare kimeliwa na matumatu.
5Enyi walevi, levukeni na kulia;
pigeni yowe, enyi walevi wa divai;
zabibu zote za kutengeneza divai mpya zimeharibiwa.
6 Taz Ufu 9:8 Jeshi la nzige limeivamia nchi yetu;
lina nguvu na ni kubwa ajabu;
meno yake ni kama ya simba,
na magego yake ni kama ya simba jike.
7Limeiharibu mizabibu yetu,
na kuitafuna mitini yetu.
Limeyabambua magamba yake na kuyatupa chini,
na matawi yake yameachwa meupe.
8Lieni kama msichana aliyevaa vazi la gunia
akiombolezea kifo cha mchumba wake.
9Sadaka za nafaka na kinywaji zimetoweka nyumbani kwa Mwenyezi-Mungu.
Makuhani, wahudumu wa Mwenyezi-Mungu, wanaomboleza.
10Mashamba yamebaki matupu;
nchi inaomboleza,
maana nafaka imeharibiwa,
divai imetoweka,
mafuta yamekosekana.
11Ombolezeni enyi wakulima;
pigeni yowe enyi watunza mizabibu.
Ngano na shayiri zimeharibika,
mavuno yote shambani yameangamia.
12Mizabibu imenyauka;
mitini imedhoofika;
mikomamanga, mitende na mitofaa imekauka,
naam miti yote shambani imekauka.
Furaha imetoweka miongoni mwa watu.
13Enyi makuhani, jivikeni magunia kuomboleza,
lieni enyi wahudumu wa madhabahu.
Ingieni hekaluni mkaomboleze usiku kucha!
Sadaka za nafaka na kinywaji zimetoweka nyumbani kwa Mungu.
14Toeni amri watu wafunge;
itisheni mkutano wa kidini.
Kusanyeni wazee na wakazi wote wa nchi,
nyumbani kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu,
na humo mkamlilie Mwenyezi-Mungu.
15Ole wetu kwa ile siku ya Mwenyezi-Mungu,
siku hiyo ya Mwenyezi-Mungu inakaribia;
inakuja pamoja na maangamizi,
kutoka kwa Mungu Mkuu.
16Mazao yetu yameharibiwa huku tunatazama.
Furaha na kicheko vimetoweka nyumbani kwa Mungu wetu.
17Mbegu zinaoza udongoni;
ghala za nafaka ni ukiwa mtupu,
ghala zimeharibika,
kwa kukosa nafaka ya kuhifadhi.
18Tazama wanyama wanavyolia kwa huzuni!
Makundi ya ng'ombe yanahangaika,
kwa sababu yamekosa malisho;
hata makundi ya kondoo yanateseka.
19Ninakulilia wewe, ee Mwenyezi-Mungu,
moto umemaliza malisho nyikani,
miali ya moto imeteketeza miti mashambani.
20Hata wanyama wa porini wanakulilia wewe,
maana, vijito vya maji vimekauka,
moto umemaliza malisho nyikani.
Yoeli1;1-20
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe
No comments:
Post a Comment