Sala ya Habakuki
1Sala ya nabii Habakuki:
2Ee Mwenyezi-Mungu, nimesikia juu ya fahari yako,
juu ya matendo yako, nami naogopa.
Uyafanye tena mambo hayo wakati wetu;
uyafanye yajulikane wakati huu wetu.
Ukasirikapo tafadhali ukumbuke huruma yako!
3Mungu amekuja kutoka Temani,
Mungu mtakatifu kutoka mlima Parani.
Utukufu wake umetanda pote mbinguni,
nayo dunia imejaa sifa zake.
4Mng'ao wake ni kama wa jua;
miali imetoka mkononi mwake
ambamo nguvu yake yadhihirishwa.
5Maradhi yanatangulia mbele yake,
nyuma yake yanafuata maafa.
6Akisimama dunia hutikisika;
akiyatupia jicho mataifa, hayo hutetemeka.
Milima ya milele inavunjwavunjwa,
vilima vya kudumu vinadidimia;
humo zimo njia zake za kale na kale.
7Niliwaona watu wa Kushani wakiteseka,
na watu wa Midiani wakitetemeka.
8Ee Mwenyezi-Mungu, je, umeikasirikia mito?
Je, umeyakasirikia maji ya bahari,
hata ukaendesha farasi wako,
na magari ya vita kupata ushindi?
9Uliuweka tayari uta wako,
ukaweka mishale yako kwenye kamba.
Uliipasua ardhi kwa mito.
10Milima ilikuona, ikanyauka;
mafuriko ya maji yakapita humo.
Vilindi vya bahari vilinguruma,
na kurusha juu mawimbi yake.
11Jua na mwezi vilikaa kimya katika makazi yao,
vilipoona miali ya mishale yako ikienda kasi,
naam, vilipouona mkuki wako ukimetameta.
12Kwa ghadhabu ulipita juu ya nchi,
uliyakanyaga mataifa kwa hasira yako.
13Ulitoka kwenda kuwaokoa watu wako,
kumwokoa yule uliyemweka wakfu kwa mafuta.
Ulimponda kiongozi wa jamii ya waovu,
ukawaangamiza kabisa wafuasi wake.
14Amiri jeshi ulimchoma mishale yako,
jeshi lilipokuja kama kimbunga kututawanya,
wakijigamba kuwaangamiza maskini mafichoni mwao.
15Kwa farasi wako ulitembea juu ya bahari,
bahari inayosukwasukwa na mawimbi.
16Nasikia hayo nami ninashtuka mwilini,
midomo yangu inatetemeka kwa hofu;
mifupa yangu inateguka,
miguu yangu inatetemeka.
Ninangojea kwa utulivu siku ile ya maafa,
ambayo inawajia wale wanaotushambulia.
17Hata kama mitini isipochanua maua,
wala mizabibu kuzaa zabibu;
hata kama mizeituni isipozaa zeituni,
na mashamba yasipotoa chakula;
hata kama kondoo wakitoweka zizini,
na mifugo kukosekana mazizini,
18mimi nitaendelea kumfurahia Mwenyezi-Mungu
nitamshangilia Mungu anayeniokoa.
19Bwana, Mwenyezi-Mungu ndiye nguvu yangu,
huiimarisha miguu yangu kama ya paa,
huniwezesha kupita juu milimani.
Habakuki3;1-19
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe
No comments:
Post a Comment