|
Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Tunamshukuru Mungu kwa kutupa kibali cha kupitia kitabu cha "Habakuki" Ni matumaini yangu kuna mengi tumejifunza/kufaidika na kutupa mwanga/kuelewa kwenye kitabu hiki... Leo tunapokwenda anza kupitia Kitabu cha"Sefania"tunamuomba Mungu wetu akatupe kibali,macho ya rohoni na akili ya kuelewa katika kujifunza NENO lake... Ee Mungu tunaomba ukatuongoze...!!Tumshukuru Mungu wetu katika yote...Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana Mungu wa walio hai,Mungu mwenye huruma,Mungu wa upendo Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!
Naipenda sana sheria yako! Naitafakari mchana kutwa! Amri yako iko nami daima, yanipa hekima kuliko maadui zangu.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza, tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....
Ninaelewa kuliko waalimu wangu wote, kwa kuwa nayatafakari maamuzi yako. Nawapita wazee kwa busara yangu, kwa sababu nazishika kanuni zako. Najizuia nisifuate njia mbaya, nipate kulizingatia neno lako.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...
Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu, Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii.. Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako siku zote za maisha yetu... Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....
Sikukiuka maagizo yako, maana wewe mwenyewe ulinifundisha. Maneno yako ni matamu sana kwangu; naam, ni matamu kuliko asali! Kwa kanuni zako napata hekima, kwa hiyo nachukia kila mwenendo mbaya.
Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu kila mmoja na mahitaji yake Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru... Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele... Amina...!!
Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake... Nawapenda. |
1Neno la Mwenyezi-Mungu lililomjia Sefania mwana wa Kushi, mwana wa Gedalia, mwana wa Amenia, mwana wa Hezekia, wakati wa utawala wa mfalme Yosia mwana wa Amoni, mfalme wa Yuda:
2Mwenyezi-Mungu asema:
“Nitavifagilia mbali viumbe vyote duniani:
3Wanadamu, wanyama, ndege wa angani
na samaki wa baharini;
vyote nitaviangamiza.
Waovu1:3 waovu: Kiebrania: Wanaokwaza. nitawaangamiza kabisa;
wanadamu nitawafagilia mbali duniani.
4Nitaunyosha mkono wangu dhidi ya nchi ya Yuda,
kadhalika na wakazi wote wa mji wa Yerusalemu.
Nitaangamiza mabaki yote ya Baali kutoka nchi hii,
na hakuna atakayetambua jina lao.
5Nitawaangamiza wote wanaosujudu juu ya paa,
wakiabudu jeshi la mbinguni.
Nitawaangamiza wale wanaoniabudu
na kuapa kwa jina langu,
hali wanaapa pia kwa jina la mungu Milkomu.
6Nitawaangamiza wote walioniacha mimi Mwenyezi-Mungu
wote walioacha kunitafuta na kuniuliza shauri.”
7Nyamazeni mbele ya Bwana Mwenyezi-Mungu,
kwani siku ya Mwenyezi-Mungu iko karibu.
Mwenyezi-Mungu ameandaa tambiko,
nao aliowaalika amewateua.
8Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Katika siku ile ya karamu yangu,
nitawaadhibu viongozi wa watu hao,
kadhalika na wana wa mfalme
pamoja na wote wanaoiga desturi za kigeni.
9Siku hiyo nitawaadhibu wote:
Wanaoruka kizingiti cha nyumba kama wapagani,
wanaojaza nyumba ya bwana wao1:9 nyumba ya bwana wao: Au hekalu la mungu wao. vitu vya dhuluma na wizi.
10“Siku hiyo, nasema mimi Mwenyezi-Mungu,
Kutasikika kilio kutoka Lango la Samaki,
maombolezo kutoka Mtaa wa Pili,
na mlio mkubwa kutoka milimani.
11Lieni enyi wakazi wa Makteshi!
Wafanyabiashara wote wameangamia,
wote wapimao fedha wamefutiliwa mbali.
12Wakati huo nitaupekua mji wa Yerusalemu kwa taa,
nitawaadhibu wanaoishi wametulia kama machicha ya divai,
wote ambao husema mioyoni mwao:
‘Mwenyezi-Mungu hatafanya kitu: Chema au kibaya.’
13Utajiri wao utanyakuliwa,
na nyumba zao zitaachwa tupu!
Watajijengea nyumba, lakini hawataishi humo.
Watapanda mizabibu, lakini hawatakunywa divai yake.”
14Ile siku kubwa ya Mwenyezi-Mungu imekaribia,
iko karibu na inakuja mbio.
Mlio wa siku ya Mwenyezi-Mungu ni wa uchungu;
hapo, shujaa atalia kwa sauti.
15Siku hiyo itakuwa siku ya ghadhabu,
ni siku ya dhiki na uchungu,
siku ya giza na huzuni;
siku ya uharibifu na maangamizi,
siku ya mawingu na giza nene.
16Siku hiyo ni ya mlio wa tarumbeta ya vita,
dhidi ya miji yenye ngome na kuta ndefu.
17Kwa kuwa watu wamemkosea Mwenyezi-Mungu,
yeye atawaletea dhiki kubwa,
hivyo kwamba watatembea kama vipofu.
Damu yao itamwagwa kama vumbi,
na miili yao kama mavi.
18Fedha yao wala dhahabu yao havitaweza kuwaokoa
katika siku hiyo ya ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu.
Kwa moto wa wivu wake
dunia yote itateketezwa.
Kwa ukamilifu na kwa namna ya kutisha
atawafanya wakazi wote duniani watoweke.
Sefania1;1-18
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe
No comments:
Post a Comment