|
Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Tunamshukuru Mungu kwa kutupa kibali cha kupitia kitabu cha "Hagai" Ni matumaini yangu kuna mengi tumejifunza/kufaidika na kutupa mwanga/kuelewa kwenye kitabu hiki... Leo tunapokwenda anza kupitia Kitabu cha"Zekaria"tunamuomba Mungu wetu akatupe kibali,macho ya rohoni na akili ya kuelewa katika kujifunza NENO lake... Ee Mungu tunaomba ukatuongoze...!!Tumshukuru Mungu wetu katika yote...Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana Mungu wa walio hai,Mungu mwenye huruma,Mungu wa upendo Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!
Ee Mwenyezi-Mungu, wewe ni mwadilifu; na hukumu zako ni za haki. Umetoa maamuzi yako, kwa haki na uthabiti. Upendo wangu kwako wanifanya niwake hasira, maana maadui zangu hawajali maneno yako.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza, tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....
Ahadi yako ni hakika kabisa, nami mtumishi wako naipenda. Mimi ni mdogo na ninadharauliwa; hata hivyo sisahau kanuni zako. Uadilifu wako ni wa haki milele; sheria yako ni ya kweli.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...
Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu, Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii.. Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako siku zote za maisha yetu... Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....
Taabu na huzuni vimenipata, lakini amri zako ndizo furaha yangu. Maamuzi yako ni ya haki daima; unijalie maarifa nipate kuishi.
Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu kila mmoja na mahitaji yake Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru... Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele... Amina...!!
Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake... Nawapenda. |
Mungu anawaita watu wake wamrudie
1Mnamo mwezi wa nane wa mwaka wa pili wa utawala wa mfalme Dario wa Persia, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia nabii Zekaria mwana wa Berekia, mjukuu wa Ido: 2“Mimi Mwenyezi-Mungu nilichukizwa sana na wazee wenu. 3Basi, waambie watu kuwa mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema hivi: Nirudieni, nami nitawarudieni nyinyi. 4Msiwe kama wazee wenu ambao manabii waliwaambia waachane na mienendo yao miovu na matendo yao mabaya, lakini wao hawakunisikiliza wala hawakunitii mimi Mwenyezi-Mungu. 5Wazee wenu, wako wapi? Na manabii, je, wanaishi milele? 6Je, wazee wenu hawakupata adhabu kwa sababu ya kukataa maagizo yangu na amri nilizowapa kwa njia ya watumishi wangu manabii? Wakati huo, wao walitubu na kusema kuwa mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, nilikusudia kuwatenda kulingana na mienendo yao na matendo yao, na kweli ndivyo nilivyowatenda.”
Maono ya kwanza: Farasi
7Mnamo siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kumi na moja, yaani mwezi wa Shebati, mwaka wa pili wa utawala wa Dario, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia mimi nabii Zekaria mwana wa Berekia, mjukuu wa Ido, kama ifuatavyo: 8Wakati wa usiku, nilimwona malaika amepanda farasi mwekundu. Malaika huyo alikuwa amesimama bondeni, katikati ya miti ya mihadasi. Nyuma yake kulikuwa na farasi wengine wekundu, wa kijivujivu na weupe. 9Basi, nikamwuliza, “Bwana, Farasi hawa wanamaanisha nini?” Malaika huyo aliyeongea nami akaniambia, “Nitakuonesha hao farasi wanamaanisha nini. 10Hawa ndio waliotumwa na Mwenyezi-Mungu kuikagua dunia.” 11Hao farasi wakamwambia huyo malaika wa Mwenyezi-Mungu aliyekuwa amesimama katikati ya miti ya mihadasi, “Tumeikagua dunia yote, nayo kweli imetulia.”
12Ndipo huyo malaika wa Mwenyezi-Mungu akasema, “Ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi, kwa muda gani utaendelea kutokuwa na huruma juu ya mji wa Yerusalemu na miji ya nchi ya Yuda ambayo umeikasirikia kwa muda wa miaka sabini?” 13Mwenyezi-Mungu akampa huyo malaika jibu jema na lenye matumaini. 14Basi, huyo malaika akaniambia, “Unapaswa kutangaza kwa sauti kwamba Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: ‘Moyo wangu umejaa upendo kwa mji wa Yerusalemu, naam, kwa mlima Siyoni. 15Walakini nimechukizwa sana na mataifa ambayo yanastarehe. Kweli niliwakasirikia Waisraeli kidogo, lakini mataifa hayo yaliwaongezea maafa. 16Kwa hiyo, nasema mimi Mwenyezi-Mungu, naurudia mji wa Yerusalemu kwa huruma; humo itajengwa nyumba yangu, na ujenzi mpya wa mji utaanza.’” 17Kisha malaika huyo akaniambia nitangaze ujumbe huu mwingine: “Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: ‘Miji yangu itafurika tena fanaka. Mimi Mwenyezi-Mungu nitaufariji tena mji wa Siyoni; nitauteua mji wa Yerusalemu kuwa wangu.’”
Maono ya pili: Pembe
18Katika maono mengine, niliona pembe nne. 19Nami nikamwuliza yule malaika aliyezungumza nami, “Pembe hizi zinamaanisha nini?” Yeye akanijibu, “Pembe hizi zinamaanisha yale mataifa ambayo yaliwatawanya watu wa Yuda, Israeli na Yerusalemu.”
20Kisha, Mwenyezi-Mungu akanionesha wafuachuma wanne. 21Nami nikauliza, “Watu hawa wanakuja kufanya nini?” Yeye akanijibu, “Watu hawa wamekuja kuyatisha na kuyaangamiza yale mataifa yenye nguvu ambayo yaliishambulia nchi ya Yuda na kuwatawanya watu wake.”
Zekaria1;1-21
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe
No comments:
Post a Comment