|
Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Haleluyah ni siku/wiki/Mwezi mwingine tena Mungu wetu ametuchagua na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii Si kwamba sisi tumetenda mema sana wala si kwa nguvu zetu si kwa utashi wetu wala si kwa akili zetu si kwamba sisi ni wazuri mno si kwa uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii Ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu....
Tumshukuru Mungu wetu katika yote... |
Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu Sifa na Utukufu tunakurudshia Mungu wetu....!!
Kwa macho yako mwenyewe utaangalia, na kuona jinsi watu waovu wanavyoadhibiwa. Wewe umemfanya Mwenyezi-Mungu kuwa kimbilio lako; naam, Mungu aliye juu kuwa kinga yako. Zaburi 91:8-9 Tazama jana imepita ee Mungu wetu leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea Jehovah usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona
Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona....
Kwa hiyo, hutapatwa na maafa yoyote; nyumba yako haitakaribiwa na baa lolote. Maana Mungu atawaamuru malaika zake, wakulinde popote uendapo. Watakuchukua mikononi mwao, usije ukajikwaa kwenye jiwe. Zaburi 91:10-12 Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe
Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu, watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia sauti yako na kuitii Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...
Utakanyaga simba na nyoka, utawaponda wana simba na majoka. Mungu asema: “Nitamwokoa yule anipendaye; nitamlinda anayenitambua! Akiniita, mimi nitamwitikia; akiwa taabuni nitakuwa naye; nitamwokoa na kumpa heshima. Nitamridhisha kwa maisha marefu, nitamjalia wokovu wangu.” Zaburi 91:13-16 Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu kila mmoja na mahitaji yake Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako wakasimamie Neno lako nalo likawaweke huru Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele Amina...!!
Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea kama inavyompendeza yeye.... Nawapenda.
|
Wageni kutoka mashariki 1Yesu alizaliwa mjini Bethlehemu, mkoani Yudea, wakati Herode alipokuwa mfalme. Punde tu baada ya kuzaliwa kwake, wataalamu wa nyota kutoka mashariki walifika Yerusalemu, 2wakauliza, “Yuko wapi mtoto, Mfalme wa Wayahudi, aliyezaliwa? Tumeiona nyota yake ilipotokea mashariki, tukaja kumwabudu.”
3Mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, yeye pamoja na wakazi wote wa Yerusalemu. 4Basi, akawaita pamoja makuhani wakuu wote na waalimu wa sheria, akawauliza, “Kristo atazaliwa wapi?” 5Nao wakamjibu, “Mjini Bethlehemu, mkoani Yudea. Ndivyo nabii alivyoandika:
6‘Ee Bethlehemu nchini Yudea,
wewe si mdogo kamwe kati ya miji maarufu ya Yudea;
maana kwako atatokea kiongozi
atakayewaongoza watu wangu, Israeli.’”
7Hapo, Herode aliwaita faraghani hao wataalamu wa nyota, akawauliza wakati hasa ile nyota ilipowatokea. 8Kisha akawatuma Bethlehemu akisema, “Nendeni mkachunguze kwa makini habari za mtoto huyo. Mkisha mpata nileteeni habari ili nami niende kumwabudu.”
9Baada ya kumsikiliza mfalme, hao wataalamu wa nyota wakaenda. Kumbe ile nyota waliyokuwa wameiona upande wa mashariki iliwatangulia hata ikaenda kusimama juu ya mahali pale alipokuwa mtoto. 10Walipoiona hiyo nyota, walifurahi mno. 11Basi, wakaingia nyumbani, wakamwona yule mtoto pamoja na Maria mama yake; wakapiga magoti, wakamsujudia. Kisha wakafungua hazina zao, wakampa zawadi: Dhahabu, ubani na manemane.
12Mungu aliwaonya katika ndoto wasimrudie Herode; hivyo wakarudi makwao kwa njia nyingine.
Kukimbilia Misri
13Baada ya wale wageni kuondoka, malaika wa Bwana alimtokea Yosefu katika ndoto, akamwambia, “Amka! Mchukue mtoto pamoja na mama yake, mkimbilie Misri. Kaeni huko mpaka nitakapokuambia, maana Herode anakusudia kumuua huyu mtoto.”
14Hivyo, Yosefu aliamka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake, akaondoka usiku, akaenda Misri. 15Akakaa huko mpaka Herode alipokufa. Jambo hilo lilifanyika ili neno alilosema Bwana kwa njia ya nabii litimie:
“Nilimwita Mwanangu kutoka Misri.”
Watoto wachanga wanauawa
16Herode alipogundua kwamba wale wataalamu wa nyota walikuwa wamemhadaa, alikasirika sana. Akaamuru watoto wote wa kiume mjini Bethlehemu na kandokando yake wenye umri wa miaka miwili na chini yake wauawe. Alifanya hivyo kufuatana na muda aliopata kujua kutoka kwa wale wataalamu wa nyota. 17Ndivyo yalivyotimia maneno yaliyosemwa kwa njia ya nabii Yeremia:
18“Sauti imesikika huko Rama,
kilio na maombolezo mengi.
Raheli anawalilia watoto wake,
wala hataki kutulizwa,
maana wote wamefariki.”
Kutoka Misri
19Baada ya kifo cha Herode, malaika wa Bwana alimtokea Yosefu katika ndoto kule Misri, 20akamwambia, “Amka! Mchukue mtoto pamoja na mama yake, urudi tena katika nchi ya Israeli, maana wale waliotaka kumuua mtoto huyo wamekwisha kufa.” 21Basi, Yosefu aliamka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake, akarejea nchini Israeli.
22Lakini Yosefu aliposikia kwamba Arkelao, mwanawe Herode, alikuwa mfalme wa Yudea mahali pa baba yake, aliogopa kwenda huko. Naye, baada ya kuonywa katika ndoto, alikwenda pande za Galilaya, 23akahamia katika mji uitwao Nazareti. Ndivyo yalivyotimia maneno yaliyonenwa kwa njia ya manabii:
“Ataitwa Mnazare.”
Mathayo2;1-23
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe
No comments:
Post a Comment