|
Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Tunamshukuru Mungu kwa kutupa kibali cha kupitia kitabu cha "Zekaria" Ni matumaini yangu kuna mengi tumejifunza/kufaidika na kutupa mwanga/kuelewa kwenye kitabu hiki... Leo tunapokwenda anza kupitia Kitabu cha"Malaki"tunamuomba Mungu wetu akatupe kibali,macho ya rohoni na akili ya kuelewa katika kujifunza NENO lake... Ee Mungu tunaomba ukatuongoze...!!Tumshukuru Mungu wetu katika yote...Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana Mungu wa walio hai,Mungu mwenye huruma,Mungu wa upendo Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!
|
Katika sehemu ya ndani kabisa ya jengo hilo, Solomoni alitayarisha chumba cha pekee ambamo sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu liliwekwa.
1 Wafalme 6:19 Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza, tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....
Chumba hicho kilikuwa na urefu wa mita 9, upana wa mita 9, na kimo cha mita 9; nacho kilipambwa kwa dhahabu safi. Pia, alitengeneza madhabahu kwa mbao za mierezi. 1 Wafalme 6:20 Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...
Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu, Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii.. Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako siku zote za maisha yetu... Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....
Solomoni aliipamba kwa dhahabu safi sehemu ya ndani ya nyumba, na mbele ya hicho chumba cha ndani akaweka minyororo ya dhahabu kutoka upande mmoja mpaka upande wa pili, aliipamba kwa dhahabu. Nyumba yote aliipamba kwa dhahabu, na madhabahu iliyokuwa katika chumba cha ndani kabisa. 1 Wafalme 6:21-22 Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu kila mmoja na mahitaji yake Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru... Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele... Amina...!!
Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake... Nawapenda.
|
1Kauli ya Mwenyezi-Mungu iliyomjia Malaki awaambie Waisraeli. Mwenyezi-Mungu anawapenda Waisraeli
2Mwenyezi-Mungu asema: “Daima nimewapenda nyinyi”. Lakini watu wa Israeli wanauliza, “Umetupendaje?” Naye Mwenyezi-Mungu asema: “Je, Esau hakuwa ndugu yake Yakobo? Hata hivyo nilimpenda Yakobo 3nikamchukia Esau. Nimeiharibu nchi ya milima ya Esau ambayo ni urithi wake, nikawaachia mbwamwitu wa jangwani. Nao wazawa 4wa Esau, yaani Waedomu, wanasema kwamba ingawa miji yao imeharibiwa, watajenga upya magofu yake. Lakini, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema kwamba wanaweza kuijenga upya, lakini mimi nitaibomolea mbali. Watu watawaita, ‘Taifa ovu ambalo Mwenyezi-Mungu amelikasirikia milele.’ 5Nanyi mtakapoyaona hayo kwa macho yenu, mtatambua na kusema: ‘Ukuu wa Mwenyezi-Mungu wafika hata nje ya mipaka ya nchi ya Israeli.’”
Mwenyezi-Mungu awakaripia makuhani
6Mwenyezi-Mungu wa majeshi anawaambia hivi nyinyi makuhani mnaolidharau jina lake: “Mtoto humheshimu mzazi wake, na mtumishi humheshimu bwana wake. Ikiwa mimi ndiye Baba yenu, mbona mwanivunjia heshima? Ikiwa mimi ni bwana wenu, mbona hamniheshimu? Nanyi mnauliza, ‘Sisi tumekudharauje?’ 7Mwanidharau kwa kunitolea madhabahuni pangu tambiko ya chakula najisi. Lakini nyinyi mnauliza, ‘Tumekitiaje najisi?’ Mnakitia najisi kwa kuidharau madhabahu yangu. 8Taz Kumb 15:21 Mnaponitolea tambiko ya mnyama kipofu, au kilema, au mgonjwa, je, huo si uovu? Je, mtawala atapendezwa au kukufanyia hisani ukimpa zawadi ya mnyama kama huyo?”
9Kwa hiyo sasa enyi makuhani, mwombeni Mungu ili atuhurumie. Ikiwa mnamtolea matoleo ya aina hiyo, je, kweli atakuwa radhi nanyi? 10Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema, “Laiti angepatikana mtu mmoja miongoni mwenu ambaye angefunga milango ya hekalu ili msiwashe moto usiokubalika kwenye madhabahu yangu! Sipendezwi nanyi na sitaikubali tambiko yoyote mnayonitolea. 11Watu wa mataifa kote duniani, toka mawio ya jua hadi machweo yake, wanalitukuza jina langu. Kila mahali wananifukizia ubani na kunitolea tambiko zinazokubalika; maana jina langu linatukuzwa miongoni mwao. 12Lakini nyinyi mnalibeza jina langu pale mnapoichafua madhabahu yangu, na chakula mnachotoa juu yake mnakidharau. 13Mnasema, ‘Mambo haya yametuchosha mno,’ na mnanidharau. Mnaniletea tambiko za wanyama mliowapata kwa unyang'anyi, au walio vilema au wagonjwa. Je, nipokee tambiko hizo mikononi mwenu? Mimi Mwenyezi-Mungu nauliza. 14Na alaaniwe mtu yeyote anidanganyaye, ambaye huahidi kwa kiapo kunitolea tambiko mnyama safi kutoka katika kundi lake, lakini hunitolea tambiko mnyama mwenye kilema. Tazama, mimi ni mfalme mkuu, na watu wa mataifa yote hunicha.”
Malaki1;1-14
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe
No comments:
Post a Comment