|
Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Tunamshukuru Mungu kwa kutupa kibali cha kupitia kitabu cha "Malaki" Ni matumaini yangu kuna mengi tumejifunza/kufaidika na kutupa mwanga/kuelewa kwenye kitabu hiki... Leo tunapokwenda anza kupitia Kitabu cha"Mathayo"tunamuomba Mungu wetu akatupe kibali,macho ya rohoni na akili ya kuelewa katika kujifunza NENO lake... Ee Mungu tunaomba ukatuongoze...!!Tumshukuru Mungu wetu katika yote...Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana Mungu wa walio hai,Mungu mwenye huruma,Mungu wa upendo Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!
|
Anayekaa chini ya ulinzi wa Mungu Mkuu, anayeishi chini ya kivuli cha Mungu Mwenye Nguvu, ataweza kumwambia Mwenyezi-Mungu: “Wewe ni kimbilio langu na ngome yangu; Mungu wangu, ninayekutumainia!”
Zaburi 91:1-2 Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza, tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....
Hakika Mungu atakuokoa katika mtego; atakukinga na maradhi mabaya. Atakufunika kwa mabawa yake, utapata usalama kwake; mkono wake utakulinda na kukukinga. Zaburi 91:3-4 Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...
Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu, Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii.. Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako siku zote za maisha yetu... Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....
Huna haja ya kuogopa vitisho vya usiku, wala shambulio la ghafla mchana; huna haja ya kuogopa baa lizukalo usiku, wala maafa yanayotokea mchana. Hata watu elfu wakianguka karibu nawe, naam, elfu kumi kuliani mwako, lakini wewe baa halitakukaribia. Zaburi 91:5-7 Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu kila mmoja na mahitaji yake Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru... Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele... Amina...!!
Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake... Nawapenda.
|
Ukoo wa Yesu Kristo (Luka 3:23-38)
1Yesu Kristo alikuwa wa ukoo wa Daudi, wa ukoo wa Abrahamu. Hii ndiyo orodha ya ukoo wake:
2Abrahamu alimzaa Isaka,
Isaka alimzaa Yakobo,
Yakobo alimzaa Yuda na ndugu zake,
3Yuda alimzaa Peresi na Zera (mama yao alikuwa Tamari),
Peresi alimzaa Hesroni,
Hesroni alimzaa Rami,
4Rami alimzaa Aminadabu,
Aminadabu alimzaa Nashoni,
Nashoni alimzaa Salmoni,
5Salmoni alimzaa Boazi (mama yake Boazi alikuwa Rahabu)
Boazi na Ruthu walikuwa wazazi wa Obedi,
Obedi alimzaa Yese,
6naye Yese alimzaa Mfalme Daudi.
Daudi alimzaa Solomoni (mama yake Solomoni alikuwa Bath-Sheba mke wa Uria).
7Solomoni alimzaa Rehoboamu,
Rehoboamu alimzaa Abiya,
Abiya alimzaa Asa,
8Asa alimzaa Yehoshafati,
Yehoshafati alimzaa Yoramu,
Yoramu alimzaa Uzia,
9Uzia alimzaa Yothamu,
Yothamu alimzaa Ahazi,
Ahazi alimzaa Hezekia,
10Hezekia alimzaa Manase,
Manase alimzaa Amoni,
Amoni alimzaa Yosia,
11Yosia alimzaa Yekonia na ndugu zake.
Huo ulikuwa wakati Wayahudi walipopelekwa uhamishoni Babuloni.
12Baada ya Wayahudi kupelekwa uhamishoni Babuloni,
Yekonia alimzaa Shealtieli,
Shealtieli alimzaa Zerubabeli,
13Zerubabeli alimzaa Abiudi,
Abiudi alimzaa Eliakimu,
Eliakimu alimzaa Azori,
14Azori alimzaa Zadoki,
Zadoki alimzaa Akimu,
Akimu alimzaa Eliudi,
15Eliudi alimzaa Eleazari,
Eleazari alimzaa Mathani,
Mathani alimzaa Yakobo,
16Yakobo alimzaa Yosefu, mumewe Maria mama yake Yesu aitwaye Kristo.
17Basi, kulikuwa na vizazi kumi na vinne tangu Abrahamu mpaka Daudi, vizazi kumi na vinne tangu Daudi mpaka Wayahudi walipochukuliwa mateka Babuloni, na vizazi kumi na vinne tangu kuchukuliwa mateka mpaka wakati wa Kristo.
Kuzaliwa kwa Yesu
(Luka 2:1-7)
18Basi, hivi ndivyo Yesu Kristo alivyozaliwa: Maria, mama yake, alikuwa ameposwa na Yosefu. Lakini kabla hawajakaa pamoja kama mume na mke, alionekana kuwa mjamzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. 19Yosefu, mumewe, kwa vile alikuwa mwadilifu, hakutaka kumwaibisha hadharani; hivyo alikusudia kumwacha kwa siri. 20Alipokuwa bado anawaza jambo hilo, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akamwambia, “Yosefu, mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Maria awe mke wako, maana amekuwa mjamzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. 21Atajifungua mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yesu, kwa kuwa yeye ndiye atakayewaokoa watu wake katika dhambi zao.”
22Basi, haya yote yalitukia ili litimie lile neno Bwana alilosema kwa njia ya nabii:
23“Bikira atachukua mimba,
atamzaa mtoto wa kiume,
nao watampa jina Emanueli”
(maana yake, “Mungu yuko nasi”).
24Hivyo, Yosefu alipoamka usingizini alifanya kama malaika huyo alivyomwambia, akamchukua mke wake nyumbani. 25Lakini hakulala naye hata Maria alipojifungua mtoto wa kiume. Naye Yosefu akampa jina Yesu.
Mathayo1;1-25
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe
No comments:
Post a Comment