Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday, 9 September 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Mathayo 19....


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..!



Wasiwasi moyoni humkosesha mtu raha, lakini neno jema humchangamsha.

Methali 12:25

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Mtu mwadilifu huuepa uovu, lakini njia ya waovu huwapotosha wenyewe.

Methali 12:26

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu 
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 

katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Mwindaji mvivu hatapata anachowinda, lakini mwenye bidii atafanikiwa. Uadilifu ni njia ya uhai, lakini uovu huongoza katika mauti.

Methali 12:27-28

Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.



 Kuhusu talaka

(Marko 10:1-12)
1Yesu alipomaliza kusema maneno hayo, alitoka Galilaya, akaenda Yudea, ngambo ya mto Yordani. 2Watu wengi walimfuata huko, naye akawaponya.
3Mafarisayo kadhaa walimjia, wakamwuliza kwa kumtega, “Je, ni halali mume kumpa talaka mkewe kwa kisa chochote?” 4Yesu akawajibu, “Je, hamkusoma katika Maandiko Matakatifu kwamba Mungu aliyemuumba mtu tangu mwanzo alimfanya mwanamume na mwanamke, 5na akasema: ‘Kwa sababu hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake, ataungana na mke wake, nao wawili watakuwa mwili mmoja?’ 6Kwa hiyo, wao si wawili tena bali mwili mmoja. Basi, alichounganisha Mungu, binadamu asikitenganishe.”
7Lakini wao wakamwuliza, “Kwa nini basi, Mose alituagiza mwanamke apewe hati ya talaka na kuachwa?” 8Yesu akawajibu, “Mose aliwaruhusu kuwaacha wake zenu kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu. 9Lakini haikuwa hivyo tangu mwanzo. Basi nawaambieni, yeyote atakayemwacha mke wake isipokuwa kwa sababu ya uzinzi, akaoa mke mwingine, anazini.”
10Wanafunzi wake wakamwambia, “Ikiwa mambo ya mume na mkewe ni hivyo, ni afadhali kutooa kabisa.” 11Yesu akawaambia, “Si wote wanaoweza kulipokea fundisho hili, isipokuwa tu wale waliojaliwa na Mungu. 12Maana kuna sababu kadhaa za kutoweza kuoa: Wengine ni kwa sababu wamezaliwa hivyo, wengine kwa sababu wamefanywa hivyo na watu, na wengine wameamua kutooa kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Awezaye kulipokea fundisho hili na alipokee.”
Yesu anawabariki watoto wadogo
(Marko 10:13-16; Luka 18:15-17)
13Kisha watu wakamletea Yesu watoto wadogo ili awawekee mikono na kuwaombea. Lakini wanafunzi wakawakemea. 14Yesu akasema, “Waacheni hao watoto waje kwangu, wala msiwazuie; maana ufalme wa mbinguni ni wa watu walio kama watoto hawa.” 15Basi, akawawekea mikono, kisha akaondoka mahali hapo.
Kijana tajiri
(Marko 10:17-31; Luka 18:18-30)
16Mtu mmoja alimjia Yesu, akamwuliza, “Mwalimu, nifanye kitu gani chema ili niupate uhai wa milele?” 17Yesu akamwambia, “Mbona unaniuliza kuhusu jambo jema? Kuna mmoja tu aliye mwema. Ukitaka kuingia katika uhai, shika amri.”
18Yule mtu akamwuliza, “Amri zipi?” Yesu akasema, “Usiue, Usizini, Usiibe, Usitoe ushahidi wa uongo, 19Waheshimu baba yako na mama yako; na, Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.”
20Huyo kijana akamwambia, “Hayo yote nimeyazingatia; nifanye nini zaidi?” 21Yesu akamwambia, “Kama unapenda kuwa mkamilifu, nenda ukauze mali yako, uwape maskini fedha hiyo, nawe utakuwa na hazina mbinguni, kisha njoo unifuate.” 22Huyo kijana aliposikia hayo, akaenda zake akiwa mwenye huzuni, maana alikuwa na mali nyingi.
23Hapo Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kweli nawaambieni itakuwa vigumu sana kwa tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni. 24Tena nawaambieni, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano, kuliko kwa tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.” 25Wale wanafunzi waliposikia hivyo walishangaa sana, wakamwuliza, “Ni nani basi, awezaye kuokoka?” 26Yesu akawatazama, akasema, “Kwa binadamu jambo hili haliwezekani, lakini kwa Mungu mambo yote huwezekana.”
27Kisha Petro akasema, “Na sisi je? Tumeacha yote tukakufuata; tutapata nini basi?” 28Yesu akawaambia, “Nawaambieni kweli, Mwana wa Mtu atakapoketi katika kiti chake cha enzi kitukufu katika ulimwengu mpya, nyinyi mlionifuata mtaketi katika viti kumi na viwili mkiyahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli. 29Na kila aliyeacha nyumba, au ndugu, au dada, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, atapokea mara mia zaidi, na kupata uhai wa milele. 30Lakini walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza.

Mathayo19;1-30

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: