Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday, 15 September 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Mathayo 23....

 



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!



Naye Roho mwenyewe anathibitisha na roho zetu kwamba sisi ni watoto wa Mungu. Basi, kwa vile sisi ni watoto wa Mungu, tutapokea baraka zote Mungu alizowawekea watu wake, na tutashiriki urithi huo pamoja na Kristo; maana, tukiyashiriki mateso yake Kristo, tutaushiriki pia utukufu wake.

Waroma 8:16-17

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....



Naona kuwa mateso ya wakati huu wa sasa si kitu kamwe kama tukiyalinganisha na ule utukufu utakaodhihirishwa kwetu. Viumbe vyote vinangojea kwa hamu Mungu awadhihirishe watoto wake.

Waroma 8:18-19

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....




Kwa maana, viumbe viliwekwa katika hali ya kutojiweza kabisa, si kwa hiari yao, ila vilifanywa hivyo kwa mapenzi ya Mungu. Hata hivyo yapo matumaini, maana hivyo viumbe navyo vitaokolewa kutoka katika utumwa wa uharibifu, vishiriki uhuru mtukufu wa watoto wa Mungu.

Waroma 8:20-21

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...

Nawapenda.


Yesu anawalaumu waalimu wa sheria na Mafarisayo 
(Marko 12:38-39; Luka 11:43,46; 20:45-46)
 1Kisha Yesu akauambia umati wa watu pamoja na wanafunzi wake, 2“Waalimu wa sheria na Mafarisayo wana mamlaka ya kufafanua sheria ya Mose. 3Kwa hiyo shikeni na kutekeleza chochote watakachowaambieni. Lakini msiyaige matendo yao, maana hawatekelezi yale wanayoyahubiri. 4Hufunga mizigo mizito na kuwatwika watu mabegani, lakini wao wenyewe hawataki kunyosha hata kidole wapate kuibeba. 5Wao hufanya matendo yao yote ili watu wawaone. Huvaa tepe zenye maandishi ya sheria juu ya panda la uso na mikononi na hupanua pindo za makoti yao. 6Hupenda nafasi za heshima katika karamu na viti vya heshima katika masunagogi. 7Hupenda kusalimiwa kwa heshima sokoni na kupendelea kuitwa na watu: ‘Mwalimu.’ 8Lakini nyinyi msiitwe kamwe ‘Mwalimu,’ maana mwalimu wenu ni mmoja tu, nanyi nyote ni ndugu. 9Wala msimwite mtu yeyote ‘Baba’ hapa duniani, maana Baba yenu ni mmoja tu, aliye mbinguni. 10Wala msiitwe ‘Viongozi,’ maana kiongozi wenu ni mmoja tu, ndiye Kristo. 11Aliye mkubwa miongoni mwenu ni lazima awe mtumishi wenu. 12Anayejikweza atashushwa, na anayejishusha atakwezwa. 

Yesu analaumu unafiki 
(Marko 12:40; Luka 11:39-42,44,52; 20:47) 
13“Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnaufunga mlango wa ufalme wa mbinguni mbele ya macho ya watu. Nyinyi wenyewe hamwingii ndani, wala hamwaruhusu wanaotaka kuingia waingie. [14Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnawanyonya wajane na kujisingizia kuwa watu wema kwa kusali sala ndefu. Kwa sababu hiyo mtapata adhabu kali.] (Taz Marko 12:40). 15“Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnasafiri baharini na nchi kavu ili kumpata mtu mmoja afuate dini yenu. Mnapompata, mnamfanya astahili maradufu kwenda katika moto wa Jehanamu kuliko nyinyi wenyewe. 16“Ole wenu viongozi vipofu! Nyinyi mwasema ati mtu akiapa kwa hekalu, kiapo hicho si kitu; lakini akiapa kwa dhahabu ya hekalu, kiapo hicho kinamshika. 17Enyi vipofu wapumbavu! Kipi kilicho cha maana zaidi: Dhahabu au hekalu linalofanya hiyo dhahabu kuwa takatifu? 18Tena mwasema ati mtu akiapa kwa madhabahu si kitu; lakini akiapa kwa zawadi iliyowekwa juu ya madhabahu, kiapo hicho humshika. 19Enyi vipofu! Ni kipi kilicho cha maana zaidi: Ile zawadi, au madhabahu ambayo hufanya hiyo zawadi kuwa takatifu? 20Anayeapa kwa madhabahu ameapa kwa hiyo madhabahu, na kwa chochote kilichowekwa juu yake. 21Na anayeapa kwa hekalu ameapa kwa hilo hekalu na pia kwa yule akaaye ndani yake. 22Na anayeapa kwa mbingu ameapa kwa kiti cha enzi cha Mungu, na kwa huyo aketiye juu yake. 23Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnatoza watu sehemu moja ya kumi, hata juu ya majani yenye harufu nzuri, bizari na jira, na huku mnaacha mambo muhimu ya sheria kama vile haki, huruma na imani. Haya ndio hasa mliyopaswa kuyazingatia bila kusahau yale mengine. 24Viongozi vipofu! Mnatoa nzi katika kinywaji, lakini mnameza ngamia! 25“Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnasafisha kikombe na bakuli kwa nje, lakini ndani mnaacha kumejaa vitu mlivyopata kwa unyanganyi na uchoyo. 26Mfarisayo kipofu! Kisafishe kikombe ndani kwanza na nje kutakuwa safi pia. 27“Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mko kama makaburi yaliyopakwa chokaa ambayo kwa nje yanaonekana kuwa mazuri, lakini ndani yamejaa mifupa ya maiti na kila namna ya uchafu. 28Hali kadhalika nyinyi mnaonekana na watu kwa nje kuwa wema, lakini kwa ndani mmejaa unafiki na uovu.

 Adhabu inakuja 
(Luka 11:47-51) 
29“Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnajenga makaburi ya manabii na kuyapamba makaburi ya watu wema. 30Mwasema: ‘Kama sisi tungaliishi nyakati za wazee wetu hatungalishirikiana nao katika mauaji ya manabii!’ 31Hivyo mnathibitisha nyinyi wenyewe kwamba nyinyi ni watoto wa watu waliowaua manabii. 32Haya, kamilisheni ile kazi wazee wenu waliyoianza! 33Enyi kizazi cha nyoka wenye sumu! Mnawezaje kuiepa hukumu ya moto wa Jehanamu? 34Ndio maana mimi ninawapelekea nyinyi manabii, watu wenye hekima na waalimu; mtawaua na kuwasulubisha baadhi yao, na wengine mtawapiga viboko katika masunagogi yenu na kuwasaka katika kila mji. 35Hivyo lawama yote itawapateni kwa ajili ya damu yote ya watu wema iliyomwagwa juu ya ardhi. Naam, tangu kumwagwa damu ya Abeli ambaye hakuwa na hatia, mpaka ile ya Zakaria, mwana wa Barakia, ambaye mlimuua hekaluni kati ya patakatifu na madhabahu. 36Nawaambieni kweli, kizazi hiki kitapata adhabu kwa sababu ya mambo haya. 

Jinsi Yesu alivyoupenda mji wa Yerusalemu
 (Luka 13:34-35) 
37“Yerusalemu! Ee Yerusalemu! Unawaua manabii na kuwapiga mawe wale waliotumwa kwako. Mara ngapi nimejaribu kuwakusanya watoto wako kwangu, kama vile kuku anavyokusanya vifaranga vyake chini ya mabawa yake, lakini hukutaka. 38Haya basi, nyumba yako itaachwa mahame. 39Taz Zab 118:26 Nakuambia, hutaniona tena mpaka wakati utakaposema: ‘Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana.’”

Mathayo23;1-39

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: