Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Haleluyah ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii Si kwamba sisi tumetenda mema sana wala si kwa nguvu zetu si kwa utashi wetu wala si kwa akili zetu si kwamba sisi ni wazuri mno si kwa uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii Ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu....
Tumshukuru Mungu wetu katika yote... |
Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu Sifa na Utukufu tunakurudshia Mungu wetu....!!
Kweli mimi Mwenyezi-Mungu nasema, nitawashambulia manabii wanaoropoka maneno yao wenyewe na kusema, ‘Mwenyezi-Mungu asema’. Yeremia 23:31 Tazama jana imepita ee Mungu wetu leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza, tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea Jehovah usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona
Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona....
Naam, mimi Mwenyezi-Mungu nasema kuwa nitawashambulia manabii wanaotabiri ndoto zao za uongo kwa watu wangu, na kuwapotosha kwa uongo wao na kuropoka kwao. Mimi sikuwatuma wala kuwaamuru waende; kwa hiyo hawatawafaa watu hao. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Yeremia 23:32 Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe
Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu, watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia sauti yako na kuitii Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...
Mwenyezi-Mungu aliniambia: “Mtu yeyote, awe nabii au kuhani, akikuuliza: ‘Uko wapi mzigo anaotubebesha Mwenyezi-Mungu?’ Wewe utawaambia: ‘Nyinyi ndio mzigo kwa Mwenyezi-Mungu naye atawatupa mbali.’ Yeremia 23:33 Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu kila mmoja na mahitaji yake Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako wakasimamie Neno lako nalo likawaweke huru Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele Amina...!!
Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea kama inavyompendeza yeye.... Nawapenda. |
|
|
|
|
|
|
Mpango wa kumwua Yesu
(Mat 26:1-5; Luka 22:1-2; Yoh 11:45-53)
1Ilikuwa siku mbili tu kabla ya sikukuu ya Pasaka na ya mikate isiyotiwa chachu. Makuhani wakuu na waalimu wa sheria walikuwa wakitafuta njia ya kumtia Yesu nguvuni kwa hila, wamuue. 2Lakini walisema, “Tusimtie nguvuni wakati wa sikukuu, watu wasije wakafanya ghasia.”
Yesu anapakwa marashi
(Mat 26:6-13; Yoh 12:1-8)
3Yesu alikuwa Bethania, nyumbani kwa Simoni Mkoma. Alipokuwa mezani kula chakula, mama mmoja aliyekuwa na chupa ya alabasta yenye marashi ya nardo safi ya thamani kubwa alikuja, akaivunja hiyo chupa, akammiminia Yesu marashi hayo kichwani. 4Baadhi ya watu waliokuwa hapo walikasirika, wakajisemea, “Kwa nini kupoteza ovyo marashi haya? 5Yangaliweza kuuzwa kwa fedha kiasi cha dinari 300, wakapewa maskini!” Wakamkemea huyo mama.
6Lakini Yesu akawaambia, “Mwacheni; kwa nini mnamsumbua? Amenitendea jambo jema. 7Maskini mnao daima pamoja nanyi; mnaweza kuwasaidia wakati wowote mnaopenda. Lakini mimi sitakuwapo pamoja nanyi daima. 8Yeye amefanya alivyoweza; ameupaka mwili wangu marashi kuutayarisha kwa mazishi. 9Nawaambieni kweli, popote ulimwenguni Habari Njema itakapohubiriwa, kitendo hiki alichofanya kitatajwa kwa kumkumbuka yeye.”
Yuda anakubali kumsaliti Yesu
(Mat 26:14-16; Luka 22:3-6)
10Kisha Yuda Iskarioti, mmoja wa wale kumi na wawili, alikwenda kwa makuhani wakuu ili kumsaliti Yesu. 11Makuhani wakuu waliposikia habari hizo, walifurahi, wakamwahidi kumpa fedha. Basi, Yuda akaanza kutafuta nafasi ya kumsaliti.
Maandalizi ya Pasaka
(Mat 26:17-25; Luka 22:7-14,21-23; Yoh 13:21-30)
12Siku ya kwanza ya sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, wakati ambapo mwanakondoo wa Pasaka huchinjwa, wanafunzi wake walimwuliza, “Wataka tukuandalie wapi karamu ya Pasaka?”
13Basi Yesu akawatuma wawili wa wanafunzi wake akiwaambia, “Nendeni mjini, na humo mtakutana na mwanamume mmoja anayebeba mtungi wa maji. Mfuateni 14mpaka katika nyumba atakayoingia, mkamwambie mwenye nyumba, ‘Mwalimu anasema: Wapi chumba changu ambamo nitakula Pasaka pamoja na wanafunzi wangu?’ 15Naye atawaonesha chumba kikubwa ghorofani kilichotayarishwa na kupambwa. Tuandalieni humo.”
16Wanafunzi wakaondoka, wakaenda mjini, wakakuta kila kitu sawa kama Yesu alivyokuwa amewaambia. Wakaandaa karamu ya Pasaka. 17Ilipokuwa jioni, Yesu alifika pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili. 18Taz Zab 41:9 Walipokuwa mezani wakila, Yesu alisema, “Kweli nawaambieni, mmoja wenu anayekula pamoja nami, atanisaliti.” 19Hapo wanafunzi wake wakaanza kuhuzunika, wakamwuliza mmojammoja, “Je, ni mimi?” 20Yesu akawaambia, “Ni mmoja wenu nyinyi kumi na wawili, anayechovya mkate pamoja nami katika bakuli. 21Kweli Mwana wa Mtu anakwenda zake kama Maandiko Matakatifu yanavyosema juu yake; lakini, ole wake mtu yule anayemsaliti Mwana wa Mtu! Ingalikuwa afadhali kwa mtu huyo kama hangalizaliwa!”
Karamu ya Bwana
(Mat 26:26-30; Luka 22:14-20; 1Kor 11:23-25)
22Walipokuwa wanakula, Yesu alitwaa mkate, akashukuru, akaumega na kuwapa wanafunzi wake akisema, “Twaeni; huu ni mwili wangu.” 23Kisha akatwaa kikombe cha divai, akamshukuru Mungu, akawapa; wote wakanywa kutoka kikombe hicho. 24Akawaambia, “Hii ni damu yangu inayothibitisha agano la Mungu, damu inayomwagwa kwa ajili ya watu wengi. 25Kweli nawaambieni, sitakunywa tena divai ya zabibu mpaka siku ile nitakapoinywa upya katika ufalme wa Mungu.” 26Kisha wakaimba wimbo, wakaondoka, wakaenda katika mlima wa Mizeituni.
Yesu anabashiri kwamba Petro atamkana
(Mat 26:31-35; Luka 22:31-34; Yoh 13:36-38)
27Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Nyinyi nyote mtakuwa na mashaka nami; maana Maandiko Matakatifu yasema:
‘Nitampiga mchungaji,
nao kondoo watatawanyika.’
28Lakini nikisha fufuka, nitawatangulieni kule Galilaya.” 29Petro akamwambia “Hata kama wote watakuwa na mashaka nawe na kukuacha, mimi sitakukana kamwe!” 30Yesu akamwambia, “Kweli nakuambia, usiku huu, kabla jogoo hajawika mara mbili, utanikana mara tatu.” 31Lakini Petro akasisitiza, “Hata kama ni lazima nife pamoja nawe, sitakuacha kamwe.” Wanafunzi wote pia wakasema vivyo hivyo.
Yesu anasali bustanini Gethsemane
(Mat 26:35-46; Luka 22:39-46)
32Basi, wakafika katika bustani iliyoitwa Gethsemane. Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kaeni hapa wakati mimi nasali.” 33Kisha akawachukua Petro, Yakobo na Yohane; akaanza kufadhaika sana na kuhangaika. 34Akawaambia, “Nina huzuni kubwa moyoni hata karibu kufa. Kaeni hapa na kukesha.” 35Akaenda mbele kidogo, akajitupa chini kifudifudi, akasali kwamba, kama ingewezekana, asiipitie saa hiyo ya mateso. 36Akasema, “Baba yangu, kwako mambo yote yanawezekana. Uniondolee kikombe hiki; lakini isiwe kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe.”
37Kisha akarudi kwa wanafunzi wale watatu, akawakuta wamelala. Basi, akamwuliza Petro, “Simoni, je, umelala? Hukuweza kukesha hata saa moja?” 38Kisha akawaambia, “Kesheni na kusali ili msije mkaingia katika majaribu. Roho inataka, lakini mwili ni dhaifu.”
39Akaenda kusali tena akirudia maneno yaleyale. 40Kisha akarudi tena, akawakuta wamelala. Macho yao yalikuwa yamebanwa na usingizi. Hawakujua la kumjibu.
41Alipowajia mara ya tatu aliwaambia, “Mnalala bado na kupumzika? Sasa imetosha! Saa imefika! Mwana wa Mtu anakabidhiwa kwa watu waovu. 42Amkeni, twende zetu. Tazameni, yule atakayenisaliti amekaribia.”
Yesu anatiwa nguvuni
(Mat 26:47-56; Luka 22:47-53; Yoh 18:3-12)
43Yesu alipokuwa bado anasema, Yuda, mmoja wa wale kumi na wawili, akafika pamoja na umati wa watu wenye mapanga na marungu. Watu hao walikuwa wametumwa na makuhani wakuu, waalimu wa sheria na wazee. 44Msaliti Yuda alikuwa amewapa ishara: “Yule nitakayembusu ndiye; mkamateni na kumpeleka chini ya ulinzi.”
45Yuda alipofika tu, alimwendea Yesu moja kwa moja, akamwambia, “Mwalimu!” Kisha akambusu. 46Basi, hao watu wakamkamata Yesu, wakamtia nguvuni. 47Mmoja wa wale waliokuwa wamesimama hapo pamoja na Yesu, akachomoa upanga wake, akampiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio. 48Yesu akawaambia, “Je, mmekuja na mapanga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyanganyi? 49Kila siku nilikuwa pamoja nanyi nikifundisha hekaluni, wala hamkunikamata. Lakini sasa lazima Maandiko Matakatifu yatimie.”
50Hapo wanafunzi wote wakamwacha, wakakimbia.
51Kulikuwa na kijana mmoja aliyekuwa anamfuata Yesu akiwa amevaa shuka. Nao wakajaribu kumkamata. 52Lakini yeye akaponyoka, akaiachilia ile shuka, akakimbia uchi.
Yesu mbele ya Baraza la wazee
(Mat 26:57-68; Luka 22:54-55,63-71; Yoh 18:13-14,19-24)
53Basi, wakampeleka Yesu kwa kuhani mkuu ambapo makuhani wakuu wote, wazee na waalimu wa sheria walikuwa wamekutanika. 54Petro alimfuata Yesu kwa mbali, akaingia ndani ya ua wa kuhani mkuu, akaketi pamoja na walinzi akiota moto. 55Makuhani wakuu na Baraza lote wakatafuta ushahidi wa kumshtaki Yesu wapate kumwua, lakini hawakuupata.
56Watu wengi walitoa ushahidi wa uongo juu ya Yesu, lakini ushahidi wao haukupatana. 57Kisha wengine walisimama, wakatoa ushahidi wa uongo wakisema: 58“Tulimsikia mtu huyu akisema, ‘Nitaliharibu hekalu hili lililojengwa kwa mikono, na kwa siku tatu nitajenga lingine lisilojengwa kwa mikono.’” 59Lakini hata hivyo, ushahidi wao haukupatana.
60Basi, kuhani mkuu akasimama katikati yao, akamwuliza Yesu, “Je, hujibu neno? Watu hawa wanashuhudia nini dhidi yako?” 61Lakini yeye akakaa kimya; hakusema hata neno moja. Kuhani mkuu akamwuliza tena, “Je, wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu Mtukufu?” 62Yesu akajibu, “Naam, mimi ndiye. Tena, mtamwona Mwana wa Mtu amekaa upande wa kulia wa yule Bwana Mwenye Nguvu, akija katika mawingu ya mbinguni.” 63Hapo kuhani mkuu akararua joho lake, akasema, “Tuna haja gani tena ya mashahidi? 64Mmesikia kufuru yake! Nyinyi mwaonaje?” Wote wakaamua kwamba anastahili kuuawa.
65Basi, baadhi yao wakaanza kumtemea mate, wakamfunika uso, wakampiga na kumwambia, “Bashiri ni nani amekupiga!” Hata watumishi wakamchukua, wakampiga makofi.
Petro anamkana Yesu
(Mat 26:69-75; Luka 22:56-62; Yoh 18:15-18,25-27)
66Petro alipokuwa bado chini uani, mmoja wa watumishi wa kike wa kuhani mkuu alikuja. 67Alipomwona Petro akiota moto, alimtazama, akamwambia, “Hata wewe ulikuwa pamoja na Yesu Mnazareti.” 68Lakini Petro akakana, “Sijui, wala sielewi unayosema!” Kisha Petro akaondoka, akaenda nje uani. Hapo jogoo akawika. 69Yule mtumishi alipomwona tena Petro, akaanza tena kuwaambia watu waliokuwa wamesimama hapo, “Mtu huyu ni mmoja wao.” 70Petro akakana tena. Baadaye kidogo, watu waliokuwa wamesimama hapo wakamwambia Petro, “Hakika wewe ni mmoja wao, maana wewe ni Mgalilaya.” 71Lakini Petro akaanza kulaani na kuapa akisema, “Mimi simjui mtu huyu mnayesema habari zake.” 72Hapo jogoo akawika mara ya pili. Basi, Petro akakumbuka jinsi Yesu alivyokuwa amemwambia: “Kabla jogoo hajawika mara mbili, utanikana mara tatu.” Petro akabubujika machozi.
Marko14;1-72
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe
No comments:
Post a Comment