Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday, 4 November 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Luka 15...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,
afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..


Lakini kama mmoja wenu ametindikiwa hekima, basi, anapaswa kumwomba Mungu ambaye atampatia; kwani Mungu huwapa wote kwa wingi na kwa ukarimu.

Yakobo 1:5

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Lakini anapaswa kuomba kwa imani bila mashaka yoyote. Mtu aliye na mashaka ni kama mawimbi ya bahari ambayo husukumwa na kutupwatupwa na upepo.

Yakobo 1:6

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu 
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 

katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...



 7,8Kwa hiyo mtu aliye na mashaka, mwenye nia mbili na asiye na msimamo katika mwenendo wake wote, asidhani ya kwamba atapata chochote kile kutoka kwa Bwana.

Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!



Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.



 Mfano wa kondoo aliyepotea

(Mat 18:12-14)
1Siku moja, watozaushuru na wenye dhambi wengi walikwenda kumsikiliza Yesu. 2Mafarisayo na waalimu wa sheria wakaanza kunungunika: “Mtazameni mtu huyu! Anawakaribisha wenye dhambi, na tena anakula nao.” 3Yesu akawajibu kwa mfano: 4“Hivi, mmoja wenu akiwa na kondoo 100, akigundua kwamba mmoja wao amepotea, atafanya nini? Atawaacha wale tisini na tisa mbugani, na kwenda kumtafuta yule aliyepotea mpaka ampate. 5Akimpata, atambeba mabegani kwa furaha. 6Anapofika nyumbani, atawaita rafiki zake na kuwaambia, ‘Furahini pamoja nami, kwa sababu nimempata yule kondoo wangu aliyepotea.’ 7Kadhalika nawaambieni, ndivyo kutakavyokuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya kutubu kwa mwenye dhambi mmoja, kuliko kwa ajili ya watu tisini na tisa wanaojiona kuwa wema, wasiohitaji kutubu.
Sarafu iliyopotea
8“Au mwaonaje? Tuseme mwanamke fulani ana sarafu kumi za fedha, akipoteza moja, atafanya nini? Atawasha taa, ataifagia nyumba na kuitafuta kwa uangalifu mpaka aipate. 9Akiipata, atawaita rafiki na jirani zake na kusema, ‘Furahini pamoja nami, kwa sababu nimeipata ile sarafu yangu iliyopotea.’ 10Kadhalika nawaambieni, ndivyo watakavyofurahi malaika wa Mungu kwa sababu ya mwenye dhambi mmoja anayetubu.”
Mfano wa mwana mpotevu
11Yesu akaendelea kusema, “Kulikuwa na mtu mmoja mwenye watoto wawili wa kiume. 12Yule mdogo alimwambia baba yake: ‘Baba, nipe urithi wangu.’ Naye akawagawia mali yake. 13Baada ya siku chache, yule mdogo aliuza urithi wake, akasafiri na fedha aliyopata, akaenda nchi ya mbali ambako aliitumia ovyo. 14Alipomaliza kutumia kila kitu, kukatokea njaa kali katika nchi ile, naye akaanza kuhangaika. 15Akaomba kazi kwa mwananchi mmoja wa huko naye akampeleka shambani mwake kulisha nguruwe. 16Alitamani kula maganda waliyokula wale nguruwe, ila hakuna mtu aliyempa kitu. 17Alipoanza kupata akili, akafikiri: ‘Mbona kuna wafanyakazi wengi wa baba yangu wanaokula na kusaza, nami ninakufa njaa? 18Nitarudi kwa baba yangu na kumwambia: Baba, nimemkosea Mungu, na nimekukosea wewe pia. 19Sistahili hata kuitwa mwanao. Nifanye kama mmoja wa wafanyakazi wako.’ 20Basi, akaanza safari ya kurudi kwa baba yake. Alipokuwa bado yu mbali, baba yake alimwona, na kwa moyo wa huruma alimkimbilia, akamkumbatia na kumbusu.
21“Mwanae akamwambia: ‘Baba, nimemkosea Mungu, na nimekukosea wewe pia. Sistahili hata kuitwa mwanao.’ 22Lakini baba yake akawaambia watumishi wake: ‘Haraka! Leteni nguo nzuri mkamvike! Mvisheni pete na viatu! 23Mchinjeni ndama mnono; tule na kusherehekea! 24Kwa sababu huyu mwanangu; alikuwa amekufa, kumbe yu hai; alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana.’ Wakaanza kufanya sherehe.
25“Wakati huo kaka yake alikuwa bado shambani. Alipokuwa akirudi na kukaribia nyumbani, akasikia vifijo na ngoma. 26Akamwita mmoja wa watumishi, akamwuliza: ‘Kuna nini?’ 27Huyo mtumishi akamwambia: ‘Ndugu yako amerudi nyumbani, na baba yako amemchinjia ndama mnono kwa kuwa amempata akiwa salama salimini.’ 28Huyo kijana mkubwa akawaka hasira hata akakataa kuingia nyumbani. Baba yake akatoka nje na kumsihi aingie. 29Lakini yeye akamjibu: ‘Kumbuka! Miaka yote nimekutumikia, sijavunja amri yako hata mara moja. Umenipa nini? Hujanipa hata mwanambuzi mmoja nikafanye sherehe pamoja na rafiki zangu! 30Lakini mtoto wako huyu aliyekula mali yako pamoja na makahaba, mara tu alipokuja umemchinjia yule ndama mnono.’ 31Baba yake akamjibu: ‘Mwanangu, wewe uko pamoja nami siku zote, na kila nilicho nacho ni chako. 32Ilitubidi kufanya sherehe na kufurahi, kwa sababu huyu ndugu yako alikuwa amekufa, kumbe yu mzima; alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana.’”

Luka15;1-32
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: