|
Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Tumshukuru Mungu katika yote....
Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana Mungu wa walio hai,Mungu mwenye huruma,Mungu wa upendo Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo... Asante kwa wema na fadhili zako kwetu Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!
|
“Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtapata; bisheni mlango, nanyi mtafunguliwa. Maana, yeyote aombaye hupewa, atafutaye hupata, na abishaye mlango hufunguliwa.
Mathayo 7:7-8 Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako, Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....
Je, kuna yeyote miongoni mwenu ambaye mtoto wake akimwomba mkate, atampa jiwe? Au je, akimwomba samaki, atampa nyoka? Mathayo 7:9-10 Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...
Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu, Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii.. Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako siku zote za maisha yetu... Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....
Kama basi nyinyi, ingawa ni waovu, mwajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, hakika Baba yenu wa mbinguni atafanya zaidi: Atawapa mema wale wanaomwomba. “Yote mnayotaka watu wawatendee nyinyi, watendeeni wao vivyo hivyo. Hii ndiyo maana ya sheria ya Mose na mafundisho ya manabii. Mathayo 7:11-12 Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu kila mmoja na mahitaji yake Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru... Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele... Amina...!!
Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake... Nawapenda. |
Sadaka ya mama mjane
(Marko 12:41-44)
1Yesu alitazama kwa makini, akawaona matajiri walivyokuwa wanatia sadaka zao katika hazina ya hekalu, 2akamwona pia mama mmoja mjane akitumbukiza humo sarafu mbili ndogo. 3Basi, akasema, “Nawaambieni kweli, mama huyu mjane maskini ametia katika hazina kiasi kikubwa kuliko walichotia wote. 4Kwa maana, wengine wote wametoa sadaka zao kutokana na ziada ya mali zao, lakini huyu mama, ingawa ni maskini, ametoa kila kitu alichohitaji kwa kuishi.”
Yesu anatabiri kuharibiwa kwa hekalu
(Mat 24:1-2; Marko 13:1-2)
5Baadhi ya wanafunzi walikuwa wanazungumza juu ya hekalu, jinsi lilivyopambwa kwa mawe ya thamani, pamoja na sadaka zilizotolewa kwa Mungu. Yesu akasema, 6“Haya yote mnayoyaona – zitakuja siku ambapo hakuna hata jiwe moja litakalosalia juu ya lingine; kila kitu kitaharibiwa.”
Taabu na mateso
(Mat 24:3-14; Marko 13:3-13)
7Basi, wakamwuliza, “Mwalimu, mambo hayo yatatokea lini? Na ni ishara gani zitakazoonesha kwamba karibu mambo hayo yatokee?”
8Yesu akawajibu, “Jihadharini, msije mkadanganyika. Maana wengi watatokea na kulitumia jina langu, kila mmoja akidai kwamba yeye ni mimi, na kwamba wakati ule umekaribia. Lakini nyinyi msiwafuate! 9Basi, mtakaposikia habari za vita na misukosuko, msitishike; maana ni lazima hayo yatokee kwanza, lakini mwisho wa yote, bado.”
10Halafu akaendelea kusema: “Taifa moja litapigana na taifa lingine, na ufalme mmoja utapigana na ufalme mwingine. 11Kila mahali kutakuwa na mitetemeko mikubwa ya ardhi, njaa na tauni. Kutakuwa na vituko vya kutisha na ishara kubwa angani. 12Lakini kabla ya kutokea hayo yote, watawatieni nguvuni, watawatesa na kuwapelekeni katika masunagogi na kuwatia gerezani; mtapelekwa mbele ya wafalme na watawala kwa ajili ya jina langu, 13mpate kunishuhudia kwao. 14Muwe na msimamo huu mioyoni mwenu: Hakuna kufikiria kabla ya wakati juu ya jinsi mtakavyojitetea, 15kwa sababu mimi mwenyewe nitawapeni ufasaha wa maneno na hekima, hata maadui zenu hawataweza kustahimili wala kupinga. 16Wazazi wenu, ndugu, jamaa na rafiki zenu watawasaliti nyinyi; na baadhi yenu mtauawa. 17Watu wote watawachukieni nyinyi kwa sababu ya jina langu. 18Lakini, hata unywele mmoja wa vichwa vyenu hautapotea. 19Kwa uvumilivu wenu, mtayaokoa maisha yenu.
Yesu anatabiri kuharibiwa kwa mji wa Yerusalemu
(Mat 24:15-21; Marko 13:14-19)
20“Mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, basi jueni ya kwamba wakati umefika ambapo mji huo utaharibiwa. 21Hapo, walioko Yudea wakimbilie milimani; wale walio mjini watoke; na wale walio mashambani wasirudi mjini. 22Kwa maana siku hizo ni siku za adhabu, ili yote yaliyoandikwa yatimie. 23Ole wao waja wazito na wanyonyeshao siku hizo! Kwa maana kutakuwa na dhiki kubwa katika nchi, na hasira ya Mungu itawajia watu hawa. 24Wengine watauawa kwa upanga, wengine watachukuliwa mateka katika nchi zote; na mji wa Yerusalemu utakanyagwa na watu wa mataifa mengine, hadi nyakati zao zitakapotimia.
Kuja kwake Mwana wa Mtu
(Mat 24:29-31; Marko 13:24-27)
25“Kutakuwa na ishara katika jua na mwezi na nyota. Mataifa duniani yatakuwa na dhiki kwa sababu ya wasiwasi kutokana na mshindo wa mawimbi ya bahari. 26Watu watazirai kwa sababu ya woga, wakitazamia mambo yatakayoupata ulimwengu; kwa maana nguvu za mbingu zitatikiswa. 27Halafu, watamwona Mwana wa Mtu akija katika wingu, mwenye nguvu na utukufu mwingi. 28Wakati mambo hayo yatakapoanza kutukia, simameni na kuinua vichwa vyenu juu, kwa maana ukombozi wenu umekaribia.”
Mfano wa mtini
(Mat 24:32-35; Marko 13:28-31)
29Kisha akawaambia mfano: “Angalieni mtini na miti mingine yote. 30Mnapoona kwamba imeanza kuchipua majani, mwatambua kwamba majira ya mavuno yamekaribia. 31Vivyo hivyo, mtakapoona mambo hayo yanatendeka, mtatambua kwamba ufalme wa Mungu umekaribia. 32Kweli nawaambieni, kizazi hiki cha sasa hakitapita kabla ya hayo yote kutendeka. 33Mbingu na dunia zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
Lazima kuwa macho
34“Muwe macho, mioyo yenu isije ikalemewa na anasa, ulevi na shughuli za maisha haya. La sivyo, siku ile itawajieni ghafla. 35Kwa maana itawajia kama mtego wote wanaoishi duniani pote. 36Muwe waangalifu basi, na salini daima ili muweze kupata nguvu ya kupita salama katika mambo haya yote yatakayotokea, na kusimama mbele ya Mwana wa Mtu.”
37Wakati wa mchana, siku hizo, Yesu alikuwa akifundisha watu hekaluni; lakini usiku alikuwa akienda katika mlima wa Mizeituni na kukaa huko. 38Watu wote walikuwa wanakwenda hekaluni asubuhi na mapema, wapate kumsikiliza.
Luka21;1-38
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe
No comments:
Post a Comment