Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday, 31 December 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Matendo 11...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu...


Wamesema uongo juu ya Mwenyezi-Mungu wamesema: “Hatafanya kitu; hatutapatwa na uovu wowote; hatutashambuliwa wala kuona njaa. Manabii si kitu, ni upepo tu; maana neno lake Mungu halimo ndani yao.” Basi hayo na yawapate wao wenyewe!

Yeremia 5:12-13

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Kwa kuwa wao wamesema jambo hilo, sasa nitayafanya maneno niliyokupa wewe Yeremia kuwa moto. Watu hawa watakuwa kuni, na moto huo utawateketeza.

Yeremia 5:14

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


“Nami Mwenyezi-Mungu nasema juu yenu enyi Waisraeli: Mimi naleta taifa moja kutoka mbali, lije kuwashambulia. Taifa ambalo halishindiki, taifa ambalo ni la zamani, ambalo lugha yake hamuifahamu, wala hamwezi kuelewa wasemacho.

Yeremia 5:15

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...

Nawapenda.



 Taarifa ya Petro kwa kanisa la Yerusalemu

1Mitume na ndugu kule Yudea walisikia kwamba watu wa mataifa mengine pia walikuwa wamelipokea neno la Mungu. 2Basi, Petro aliporudi Yerusalemu, wale Wayahudi waumini waliopendelea watu wa mataifa mengine watahiriwe, walimlaumu wakisema: 3“Wewe umekwenda kukaa na watu wasiotahiriwa na hata umekula pamoja nao! 4Hapo Petro akawaeleza kinaganaga juu ya yale yaliyotendeka tangu mwanzo:
5“Siku moja nikiwa nasali mjini Yopa, niliona maono; niliona kitu kama shuka kubwa ikishushwa chini kutoka mbinguni ikiwa imeshikwa pembe zake nne, ikawekwa kando yangu. 6Nilichungulia ndani kwa makini nikaona wanyama wenye miguu minne, wanyama wa mwituni, wanyama watambaao na ndege wa angani. 7Kisha nikasikia sauti ikiniambia: ‘Petro amka, chinja, ule.’ 8Lakini mimi nikasema: ‘La, Bwana; maana chochote kilicho najisi au kichafu hakijapata kamwe kuingia kinywani mwangu.’ 9Ile sauti ikasikika tena kutoka mbinguni: ‘Usiviite najisi vitu ambavyo Mungu amevitakasa.’ 10Jambo hilo lilifanyika mara tatu, na mwishowe vyote vilirudishwa juu mbinguni. 11Ghafla, watu watatu waliokuwa wametumwa kwangu kutoka Kaisarea waliwasili kwenye nyumba nilimokuwa nakaa. 12Roho aliniambia niende pamoja nao bila kusita. Hawa ndugu sita waliandamana nami pia kwenda Kaisarea na huko tuliingia nyumbani mwa Kornelio. 13Yeye alitueleza jinsi alivyokuwa amemwona malaika amesimama nyumbani mwake na kumwambia: ‘Mtume mtu Yopa akamwite mtu mmoja aitwaye Simoni, kwa jina lingine Petro. 14Yeye atakuambia maneno ambayo kwayo wewe na jamaa yako yote mtaokolewa.’ 15Na nilipoanza tu kuongea, Roho Mtakatifu aliwashukia kama alivyotushukia sisi pale awali. 16Hapo nilikumbuka yale maneno Bwana aliyosema: ‘Yohane alibatiza kwa maji, lakini nyinyi mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.’ 17Basi, kama Mungu amewapa pia watu wa mataifa mengine kipawa kilekile alichotupa sisi tulipomwamini Bwana Yesu Kristo, je, mimi ni nani hata nijaribu kumpinga Mungu?” 18Waliposikia hayo, waliacha ubishi, wakamtukuza Mungu wakisema, “Mungu amewapa watu wa mataifa mengine nafasi ya kutubu wapate uhai!”
Kanisa la Antiokia
19Kutokana na mateso yaliyotokea wakati Stefano alipouawa, waumini walitawanyika. Wengine walikwenda mpaka Foinike, Kupro na Antiokia wakihubiri ule ujumbe kwa Wayahudi tu. 20Lakini baadhi ya waumini waliotoka Kupro na Kurene, walikwenda Antiokia wakautangaza huo ujumbe kwa watu wa mataifa mengine wakiwahubiria Habari Njema juu ya Bwana Yesu. 21Bwana aliwasaidia na idadi kubwa ya watu iliamini na kumgeukia Bwana. 22Habari ya jambo hilo ikasikika kwa lile kanisa la Yerusalemu. Hivyo wakamtuma Barnaba aende Antiokia. 23Alipofika huko na kuona jinsi Mungu alivyowaneemesha wale watu, alifurahi na kuwahimiza wote wadumu katika uaminifu wao kwa Bwana. 24Barnaba alikuwa mtu mwema na mwenye kujaa Roho Mtakatifu na imani. Kundi kubwa la watu lilivutwa kwa Bwana. 25Kisha, Barnaba alikwenda Tarso kumtafuta Saulo. 26Alipompata, alimleta Antiokia. Nao wote wawili walikaa na ile jumuiya ya kanisa kwa mwaka wote mzima wakifundisha kundi kubwa la watu. Huko Antiokia, ndiko kwa mara ya kwanza, wafuasi waliitwa Wakristo.
27Wakati huohuo, manabii kadhaa walikuja Antiokia kutoka Yerusalemu. 28Basi, mmoja wao aitwaye Agabo alisimama, na kwa uwezo wa Roho akabashiri kwamba kutakuwa na njaa kubwa katika nchi yote. (Njaa hiyo ilitokea wakati wa utawala wa Klaudio). 29Wale wanafunzi waliamua kila mmoja kwa kadiri ya uwezo wake apeleke chochote ili kuwasaidia wale ndugu waliokuwa wanaishi Yudea. 30Basi, wakafanya hivyo na kuwapa Barnaba na Saulo mchango huo wauwasilishe wao wenyewe kwa wazee wa kanisa.

Matendo11;1-30
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: