Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday, 15 January 2021

Kikombe Cha Asubuhi; Matendo 22...

 


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,
afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..


Nitayarudia kwa sauti maagizo yako yote uliyotoa. Nafurahi kufuata maamuzi yako, kuliko kuwa na utajiri mwingi.

Zaburi 119:13-14

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Nazitafakari kanuni zako, na kuzizingatia njia zako. Nayafurahia masharti yako; sitalisahau neno lako.

Zaburi 119:15-16

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono ye
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Unitendee mimi mtumishi wako kwa ukarimu, nipate kuishi na kushika neno lako. Uyafumbue macho yangu, niyaone maajabu ya sheria yako.

Zaburi 119:17-18

Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.



1“Ndugu zangu na akina baba, nisikilizeni sasa nikijitetea mbele yenu!” 2Waliposikia akiongea nao kwa Kiebrania wakazidi kukaa kimya zaidi kuliko hapo awali. Naye Paulo akaendelea kusema, 3“Mimi ni Myahudi, mzaliwa wa Tarso katika Kilikia. Lakini nililelewa papa hapa mjini Yerusalemu chini ya mkufunzi Gamalieli. Nilifundishwa kufuata kwa uthabiti sheria ya wazee wetu. Nilijitolea kwa moyo wote kwa Mungu kama nyinyi wenyewe mlivyo hivi leo. 4Niliwatesa hata kuwaua wale watu waliofuata njia hii. Niliwatia nguvuni wanaume kwa wanawake na kuwafunga gerezani. 5Kuhani mkuu na baraza lote la wazee wanaweza kushuhudia jambo hilo. Kutoka kwao nilipokea barua walioandikiwa wale ndugu Wayahudi waliokuwa huko Damasko. Nilikwenda Damasko ili niwatie nguvuni watu hao na kuwaleta wamefungwa mpaka Yerusalemu ili waadhibiwe.

Paulo anaongea juu ya kuongoka kwake
(Mate 9:1-19; 26:12-18)
6“Basi, nilipokuwa njiani karibu na kufika Damasko, yapata saa sita mchana, mwanga mkubwa kutoka mbinguni ulitokea ghafla ukaniangazia pande zote. 7Hapo nilianguka chini, nikasikia sauti ikiniambia: ‘Saulo, Saulo! Kwa nini unanitesa?’ 8Nami nikauliza, ‘Nani wewe, Bwana?’ Naye akaniambia, ‘Mimi ni Yesu wa Nazareti ambaye wewe unamtesa.’ 9Wale wenzangu waliuona ule mwanga lakini hawakusikia sauti ya yule aliyeongea nami. 10Basi, mimi nikauliza, ‘Nifanye nini Bwana?’ Naye Bwana akaniambia, ‘Simama, nenda Damasko na huko utaambiwa yote ambayo umepangiwa kufanya.’ 11Kutokana na ule mwanga mkali sikuweza kuona na hivyo iliwabidi wale wenzangu kuniongoza kwa kunishika mkono mpaka nikafika Damasko.
12“Huko kulikuwa na mtu mmoja aitwaye Anania, mtu mcha Mungu, mwenye kuitii sheria yetu na aliyeheshimika sana mbele ya Wayahudi waliokuwa wanaishi Damasko. 13Yeye alikuja kuniona, akasimama karibu nami, akasema, ‘Ndugu Saulo! Ona tena.’ Papo hapo nikaona tena, nikamwangalia. 14Halafu Anania akasema, ‘Mungu wa babu zetu amekuchagua upate kujua matakwa yake na kumwona yule mtumishi wake mwadilifu na kumsikia yeye mwenyewe akiongea. 15Kwa maana utamshuhudia kwa watu wote ukiwaambia yale uliyoyaona na kuyasikia. 16Sasa basi, ya nini kukawia zaidi? Simama, ubatizwe na kuondolewa dhambi zako kwa kuliungama jina lake.’
Wito wa Paulo kuwahubiria watu wa mataifa
17“Basi, nilirudi Yerusalemu, na nilipokuwa nikisali hekaluni, niliona maono. 18Nilimwona Bwana akiniambia, ‘Haraka! Ondoka Yerusalemu upesi kwa maana watu wa hapa hawataukubali ushuhuda wako juu yangu.’ 19Nami nikamjibu, ‘Bwana, wao wanajua wazi kwamba mimi ni yule aliyekuwa anapitapita katika masunagogi na kuwatia nguvuni na kuwapiga wale waliokuwa wanakuamini. 20Na kwamba wakati shahidi wako Stefano alipouawa, mimi binafsi nilikuwako pale nikakubaliana na kitendo hicho na kuyalinda makoti ya wale waliokuwa wanamuua.’ 21Naye Bwana akaniambia, ‘Nenda; nitakutuma mbali kwa mataifa mengine.’”
22Mpaka hapa, wale watu walikuwa wanamsikiliza, lakini aliposema maneno haya, walianza kusema kwa sauti kubwa, “Mwondoe duniani! Mtu wa namna hiyo hastahili kuishi.” 23Waliendelea kupayukapayuka huku wakitikisa makoti yao na kurusha vumbi angani. 24Mkuu wa jeshi aliwaamuru watu wake wampeleke Paulo ndani ya ngome, akawaambia wamchape viboko ili wapate kujua kisa cha Wayahudi kumpigia kelele. 25Lakini walipokwisha mfunga ili wamchape viboko, Paulo alimwuliza jemadari mmoja aliyesimama hapo, “Je, ni halali kwenu kumpiga viboko raia wa Roma kabla hajahukumiwa?” 26Yule jemadari aliposikia hayo, alimpasha habari mkuu wa jeshi akisema, “Unataka kufanya nini? Mtu huyu ni raia wa Roma!” 27Basi, mkuu wa jeshi alimwendea Paulo, akamwambia, “Niambie; je, wewe ni raia wa Roma?” Paulo akamjibu, “Naam.” 28Mkuu wa jeshi akasema, “Mimi nami nimekuwa raia wa Roma kwa kulipa gharama kubwa.” Paulo akasema, “Lakini mimi ni raia wa Roma kwa kuzaliwa.” 29Wale watu ambao walikuwa tayari kumchunguza Paulo walitoweka mara. Hata yule mkuu wa jeshi aliogopa alipojua kwamba Paulo ni raia wa Roma na kwamba alikuwa amekwisha mfunga minyororo.
Paulo mahakamani
30Kesho yake, mkuu wa jeshi alitaka kujua mashtaka kamili ambayo Wayahudi walikuwa wamemwekea Paulo. Hivyo, alimfungua Paulo minyororo, akaamuru makuhani wakuu na Baraza lote wafanye kikao. Kisha alimleta Paulo, akamsimamisha mbele ya Baraza.

Matendo22;1-30
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: