|
Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Tumshukuru Mungu wetu katika yote...
Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii Asante kwa pumzi/uzima, afya na kuwatayari kwa majukumu yetu
Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni Neema yako yatutosha Mungu wetu..
|
Mikono yako iliniumba na kuniunda; unijalie akili nijifunze amri zako. Wakuchao wataniona na kufurahi, maana tumaini langu liko katika neno lako.
Zaburi 119:73-74 Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza, tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti, Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....
Najua hukumu zako ni adili, ee Mwenyezi-Mungu, na kwamba umeniadhibu kwani wewe ni mwaminifu. Fadhili zako na zinipe faraja, kama ulivyoniahidi mimi mtumishi wako. Unionee huruma nipate kuishi, maana sheria yako ni furaha yangu. Zaburi 119:75-77 Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono ye Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe
Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu, watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia sauti yako na kuitii Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama inavyokupendeza wewe Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...
Wenye kiburi waaibike kwa maana wamenifanyia hila, lakini mimi nitazitafakari kanuni zako. Wote wakuchao na waje kwangu, wapate kuyajua maamuzi yako. Moyo wangu na uzingatie masharti yako, nisije nikaaibishwa. Zaburi 119:78-80 Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao Nuru yako ikaangaze katika maisha yao Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele Amina....!!!
Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana kwakuwanami/kunisoma Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea kama inavyompendeza yeye Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba ukae nanyi daima.... Nawapenda.
|
Hukumu ya Mungu
1Basi, rafiki, kama unawahukumu wengine, huwezi kamwe kujitetea, hata kama wewe ni nani. Kwa maana, kwa kuwahukumu wengine, unajilaani wewe mwenyewe kwa vile nawe unayafanya mambo yaleyale unayohukumu. 2Tunajua kwamba hukumu ya Mungu kwa wale wanaofanya mambo kama hayo ni hukumu ya haki. 3Lakini wewe rafiki unayewahukumu wale wanaofanya mambo kama hayo hali wewe pia unayafanya, je unadhani utaiepa hukumu ya Mungu? 4Au labda unaudharau wema wake mkuu, uvumilivu wake na saburi yake, bila kutambua kwamba wema wake huo una shabaha ya kukuongoza upate kutubu? 5Lakini unao ugumu na ukaidi wa moyo, na hivyo unajirundikia adhabu kwa siku ile ya ghadhabu wakati hukumu ya haki ya Mungu itakapodhihirishwa. 6Taz Zab 62:12 Siku hiyo Mungu atamlipa kila mmoja kufuatana na matendo yake. 7Wale wanaozingatia kutenda mema, kutafuta utukufu na heshima ya Mungu na kutokufa, watapata uhai wa milele. 8Lakini wale wengine wenye ubinafsi, wenye kukataa mambo ya haki na kufuata uovu, wataangukiwa na ghadhabu na hasira ya Mungu. 9Mateso na maumivu yatampata binadamu yeyote atendaye uovu. Yatawapata Wayahudi kwanza na watu wa mataifa mengine pia. 10Lakini Mungu atawapa utukufu, heshima na amani wale wanaotenda mema; Wayahudi kwanza, na watu wa mataifa mengine pia. 11Maana Mungu hambagui mtu yeyote.
12Wale wanaotenda dhambi bila kuijua sheria wataangamia ingawaje hawaijui sheria. Na wale wanaotenda dhambi wakiwa wanaijua sheria watahukumiwa kisheria. 13Maana sio wanaosikia sheria ndio walio waadilifu mbele ya Mungu, ila wenye kuitii sheria ndio watakaokubaliwa kuwa waadilifu. 14Mathalani: Watu wa mataifa mengine hawana sheria; lakini kila wanapotimiza matakwa ya sheria wakiongozwa na dhamiri zao, wao wenyewe wanakuwa kipimo cha sheria ingawa hawaijui sheria. 15Mwenendo wao unaonesha kwamba matakwa ya sheria yameandikwa mioyoni mwao. Dhamiri zao zinashuhudia pia jambo hilo, maana fikira zao mara nyingine huwashtaki, na mara nyingine huwatetea. 16Hivyo, kufuatana na hii Habari Njema ninayohubiri, ndivyo itakavyokuwa wakati Mungu atakapohukumu mambo ya siri ya binadamu kwa njia ya Yesu Kristo.
Wayahudi na sheria yao
17Na wewe, je? Wewe mwenyewe unajiita Myahudi; unaitumainia sheria na kujivunia kuwa wa Mungu; 18kwa njia ya sheria unajua matakwa ya Mungu na unaweza kuchagua jambo jema; 19wewe unajiona kuwa kiongozi wa vipofu na mwanga kwa wale walio gizani; 20unajiona kuwa mkufunzi wa wajinga na mwalimu wa wale wasiokomaa bado. Unayo katika sheria picha kamili ya elimu na ukweli. 21Basi, wewe unawafundisha wengine; kwa nini hujifundishi wewe mwenyewe? Unawahubiria wengine wasiibe, lakini kumbe wewe mwenyewe unaiba. 22Unasema: “Msizini,” na huku wewe unazini; unachukia sanamu za miungu hali wewe unajitajirisha kwa kuiba katika nyumba za miungu. 23Kwa kujigamba ati unayo sheria ya Mungu, je huoni kwamba kwa kuivunja sheria unamdharau Mungu? 24Kama vile Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Watu wa mataifa mengine wamelikufuru jina la Mungu kwa sababu yenu nyinyi Wayahudi!” 25Kutahiriwa kwako kutakuwa na maana kama ukiitii sheria. Lakini kama unaivunja sheria, basi, ni afadhali ungalibaki bila kutahiriwa. 26Kama mtu wa mataifa mengine ambaye hakutahiriwa akitimiza matakwa ya sheria, hakika atafikiriwa kana kwamba ametahiriwa. 27Watu wa mataifa mengine watakuhukumu wewe Myahudi kama ukiivunja sheria, ingawaje unayo maandishi ya sheria na umetahiriwa, hali wao wanaitii sheria ingawa hawakutahiriwa. 28Ndiyo kusema, si kila anayeonekana kwa nje kuwa Myahudi ni Myahudi wa kweli, wala mtu hawi Myahudi wa kweli ati kwa kuwa ametahiriwa kimwili. 29Myahudi wa kweli ni yule aliye Myahudi kwa ndani, yaani yule ambaye ametahiriwa moyoni. Hili ni jambo la Roho, na si jambo la maandishi ya sheria. Mtu wa namna hiyo anapata sifa, si kutoka kwa watu, bali kutoka kwa Mungu.
Waroma2;1-29
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe
No comments:
Post a Comment