Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday, 19 March 2021

Kikombe Cha Asubuhi: Kitabu cha 2Wakorintho....7

 


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,
afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..


Petro alikuwa bado anajaribu kuelewa yale maono, na hapo Roho akamwambia, “Sikiliza! Kuna watu watatu hapa, wanakutafuta. Shuka upesi na wala usisite kwenda pamoja nao kwa maana ni mimi niliyewatuma.”

Matendo 10:19-20


Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Basi, Petro akateremka chini, akawaambia hao watu, “Mimi ndiye mnayemtafuta. Kwa nini mmekuja?”

Matendo 10:21

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono ye
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Wao wakamjibu, “Jemadari Kornelio ambaye ni mtu mwema, mcha Mungu na mwenye kuheshimika mbele ya Wayahudi wote, ametutuma. Aliambiwa na malaika mtakatifu akualike nyumbani kwake ili asikilize chochote ulicho nacho cha kusema.”

Matendo 10:22

Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.


1Basi, wapenzi wangu, tukiwa tumepewa ahadi hizi zote, na tujitakase na chochote kiwezacho kuchafua miili na roho zetu, tuwe watakatifu kabisa na kuishi kwa kumcha Mungu.

Furaha ya Paulo
2Tunaomba mtupe nafasi mioyoni mwenu! Hatujamkosea mtu yeyote, hatujamdhuru wala kumdanganya mtu yeyote. 3Sisemi mambo haya kwa ajili ya kumhukumu mtu; maana, kama nilivyokwisha sema, nyinyi mko mioyoni mwetu, tufe pamoja, tuishi pamoja. 4Nina imani kubwa sana ninaposema nanyi; naona fahari kubwa juu yenu! Katika taabu zetu nimepata kitulizo kikubwa na kufurahi mno.
5Hata baada ya kufika Makedonia hatukuweza kupumzika. Kila upande tulikabiliwa na taabu: Nje ugomvi; ndani hofu. 6Lakini Mungu, mwenye kuwapa shime wanyonge, alitupa moyo sisi pia kwa kuja kwake Tito. 7Si tu kwa kule kuja kwake Tito, bali pia kwa sababu ya moyo mliompa nyinyi. Yeye ametuarifu jinsi mnavyotamani kuniona, jinsi mlivyo na huzuni, na mnavyotaka kunitetea. Jambo hili linanifurahisha sana.
8Maana, hata kama kwa barua yangu ile nimewahuzunisha, sioni sababu ya kujuta. Naam, naona kwamba barua hiyo iliwatia huzuni lakini kwa muda. 9Sasa nafurahi, si kwa sababu mmehuzunika, ila kwa kuwa huzuni yenu imewafanya mbadili nia zenu na kutubu. Mmehuzunishwa kadiri ya mpango wa Mungu, na kwa sababu hiyo hatukuwadhuru nyinyi kwa vyovyote. 10Kuwa na huzuni jinsi atakavyo Mungu husababisha badiliko la moyo, badiliko lenye kuleta wokovu; hivyo hakuna sababu ya kujuta. Lakini huzuni ya kidunia huleta kifo. 11Sasa mnaweza kuona matokeo ya kuona huzuni jinsi Mungu atakavyo: Nyinyi mmepata kuwa sasa watu wenye jitihada, wenye hoja, mnashtuka na kuogopa, mna bidii na mko tayari kuona kwamba haki yatekelezwa. Nyinyi mmethibitisha kwa kila njia kwamba hamna hatia kuhusu jambo hili.
12Hivyo, ingawa niliandika ile barua, haikuwa kwa ajili ya yule aliyekosa, au kwa ajili ya yule aliyekosewa. Niliandika kusudi ionekane wazi mbele ya Mungu jinsi mlivyo na bidii kwa ajili yetu. 13Ndiyo maana sisi tulifarijika sana.
Siyo kwamba tulifarijika tu, ila pia Tito alitufurahisha kwa furaha aliyokuwa nayo kutokana na jinsi mlivyomchangamsha moyo. 14Mimi nimewasifu sana mbele yake, na katika jambo hilo sikudanganyika. Tumewaambieni ukweli daima, na kule kuwasifia nyinyi mbele ya Tito kumekuwa jambo la ukweli tupu. 15Hivyo upendo wake wa moyo kwenu nyinyi unaongezeka zaidi akikumbuka jinsi nyinyi nyote mlivyo tayari kutii, na jinsi mlivyomkaribisha kwa hofu nyingi na kutetemeka. 16Nafurahi sana kwamba naweza kuwategemea nyinyi kabisa katika kila jambo.

2Wakorintho7;1-16
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: