|
|
Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Tunamshukuru Mungu kwa kutupa kibali cha kupitia kitabu cha "Filemoni" Ni matumaini yangu kuna mengi tumejifunza/kufaidika na kutupa mwanga/kuelewa kwenye kitabu hiki...
Leo tunapokwenda anza kupitia Kitabu cha"Waebrania" tunamuomba Mungu wetu akatupe kibali,macho ya rohoni na akili ya kuelewa katika kujifunza NENO lake... Ee Mungu tunaomba ukatuongoze...!! Tumshukuru Mungu wetu katika yote...
Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana Mungu wa walio hai,Mungu mwenye huruma,Mungu wa upendo Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!
Hii ndiyo baraka ambayo Mose, mtu wa Mungu aliwatakia Waisraeli kabla ya kufariki kwake. Alisema: Mwenyezi-Mungu alikuja kutoka mlima Sinai, alitutokea kutoka mlima Seiri; aliiangaza kutoka mlima Parani. Alitokea kati ya maelfu ya malaika, na moto uwakao katika mkono wake wa kulia. Kumbukumbu la Sheria 33:1-2 Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako, Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona...
Mwenyezi-Mungu aliwapenda watu wake; na huwalinda watakatifu wake wote. Hivyo, malaika wake walifuata nyayo zake, na kupata maagizo kutoka kwake. Kumbukumbu la Sheria 33:3 Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu, Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii.. Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako siku zote za maisha yetu... Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....
Mose alituamuru tutii sheria; kitu cha thamani kuu cha taifa letu. Mwenyezi-Mungu akawa mfalme wa Israeli, wakati viongozi wao walipokutana, na makabila yote yalipokusanyika. Kumbukumbu la Sheria 33:4-5 Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu kila mmoja na mahitaji yake Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru... Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele... Amina...!!
Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami, Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake... Nawapenda. |
Mungu anasema kwa njia ya Mwanae
1Hapo zamani, Mungu alisema na babu zetu mara nyingi kwa namna nyingi kwa njia ya manabii, 2lakini siku hizi za mwisho, amesema nasi kwa njia ya Mwanae. Yeye ndiye ambaye kwa njia yake Mungu aliumba ulimwengu, akamteua avimiliki vitu vyote. 3Yeye ni mngao wa utukufu wa Mungu, na mfano kamili wa hali ya Mungu mwenyewe, akiutegemeza ulimwengu kwa neno lake lenye nguvu. Baada ya kuwatakasa binadamu dhambi zao, ameketi huko juu mbinguni, upande wa kulia wa Mungu Mkuu.
Ukuu wa Mwana wa Mungu
4Mwana ni mkuu kuliko malaika, kama vile jina alilopewa na Mungu ni kuu kuliko jina lao. 5Taz Zab 2:7 Maana Mungu hakumwambia kamwe hata mmoja wa malaika wake:
“Wewe ni Mwanangu;
mimi leo nimekuwa Baba yako.”
Wala hakusema juu ya malaika yeyote:
“Mimi nitakuwa Baba yake,
naye atakuwa Mwanangu.”
6Lakini Mungu alipokuwa anamtuma Mwanae, mzaliwa wa kwanza, ulimwenguni alisema:
“Malaika wote wa Mungu na wamwabudu.”
7 Taz Zab 104:4 Lakini kuhusu malaika, alisema:
“Amewafanya malaika wake kuwa upepo,
na wahudumu wake ndimi za moto.”
8 Taz Zab 45:6-7 Lakini kuhusu Mwana, Mungu alisema:
“Kiti chako cha enzi, ee Mungu, chadumu milele na milele!
Wewe wawatawala watu wako kwa haki.
9Wewe wapenda uadilifu na kuchukia uovu.
Ndiyo maana Mungu, Mungu wako, amekuweka wakfu
na kukumiminia furaha kubwa kuliko wenzako.”
10 Taz Zab 102:25-27 Na tena:
“Bwana, wewe uliumba dunia hapo mwanzo,
mbingu ni kazi ya mikono yako.
11Hizo zitatoweka, lakini wewe wabaki daima,
zote zitachakaa kama vazi.
12Utazikunjakunja kama koti,
nazo zitabadilishwa kama vazi.
Lakini wewe ni yuleyule daima,
na maisha yako hayatakoma.”
13 Taz Zab 110:1 Mungu hakumwambia kamwe hata mmoja wa malaika wake:
“Keti upande wangu wa kulia,
mpaka niwaweke adui zako chini ya miguu yako.”
14Malaika ni nini ila roho wanaomtumikia Mungu na ambao hutumwa kuwasaidia wale watakaopokea wokovu?
Waebrania1;1-14
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe