|
Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Haleluyah ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii Si kwamba sisi tumetenda mema sana wala si kwa nguvu zetu si kwa utashi wetu wala si kwa akili zetu si kwamba sisi ni wazuri mno si kwa uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii Ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu....
Tunamshukuru Mungu kwa kutupa kibali cha kupitia kitabu cha "1Timotheo" Ni matumaini yangu kuna mengi tumejifunza/kufaidika na kutupa mwanga/kuelewa kwenye kitabu hiki...
Leo tunapokwenda anza kupitia Kitabu cha"2Timotheo" tunamuomba Mungu wetu akatupe kibali,macho ya rohoni na akili ya kuelewa katika kujifunza NENO lake... Ee Mungu tunaomba ukatuongoze...!! Tumshukuru Mungu wetu katika yote...
Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana Mungu wa walio hai,Mungu mwenye huruma,Mungu wa upendo Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!
|
Wapenzi wangu, nawasihi nyinyi kama wageni na wakimbizi hapa duniani! Achaneni na tamaa za mwili ambazo hupingana na roho. Mwenendo wenu kati ya watu wasiomjua Mungu unapaswa kuwa mwema kabisa, ili hata watakapowasingizieni kwamba mnatenda mabaya, waweze kutambua matendo yenu mema na hivyo wamtukuze Mungu siku ya kuja kwake.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako, Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona...
Basi, jiwekeni chini ya mamlaka yote ya kibinadamu, kwa ajili ya Bwana: Utii kwa mfalme aliye mtawala mkuu, utii kwa wakuu wa mikoa ambao wameteuliwa naye kuwaadhibu wahalifu na kuwasifu watendao mema. 1 Petro 2:13-14 Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu, Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii.. Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako siku zote za maisha yetu... Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....
Maana Mungu anataka muweze kuyakomesha maneno ya kijinga ya watu wasio na akili kwa matendo mema mnayofanya. Ishini kama watu huru; lakini msiutumie uhuru wenu kuuficha ubaya, bali ishini kama watumishi wa Mungu. Waheshimuni watu wote, wapendeni ndugu zenu waamini, mcheni Mungu, mheshimuni mfalme. 1 Petro 2:15-17 Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu kila mmoja na mahitaji yake Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru... Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele... Amina...!!
Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami, Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake... Nawapenda. |
1Mimi Paulo, ambaye Mungu alitaka niwe mtume wa Kristo Yesu ili niutangaze ule uhai tulioahidiwa katika kuungana na Kristo Yesu, 2nakuandikia wewe mwanangu mpenzi Timotheo.
Nakutakia neema, huruma na amani kutoka kwa Mungu Baba na Kristo Yesu Bwana wetu.
Shukrani na maneno ya kutia moyo
3Ninamshukuru Mungu ambaye ninamtumikia kwa dhamiri safi kama walivyofanya wazee wangu; namshukuru kila ninapokukumbuka katika sala zangu usiku na mchana. 4Nakumbuka machozi yako na ninatamani sana kukuona, ili nijazwe furaha. 5Naikumbuka imani yako ya kweli, imani aliyokuwa nayo nyanya yako Loisi, na pia mama yako Eunike. Nina hakika kwamba wewe pia unayo. 6Ndio maana nakukumbusha ukiweke motomoto kile kipaji ulichopewa na Mungu wakati nilipokuwekea mikono yangu. 7Kwa maana Roho tuliyepewa na Mungu si wa kutufanya tuwe waoga; sivyo, ila ni Roho wa kutujalia upendo na nidhamu.
8Basi, usione haya kumshuhudia Bwana wetu, wala usione haya kwa sababu yangu mimi niliye mfungwa kwa ajili yake. Lakini shiriki katika mateso kwa ajili ya Habari Njema, kadiri ya nguvu unayopewa na Mungu. 9Yeye alituokoa, akatuita tuwe watu wake yeye mwenyewe, si kwa sababu ya mastahili ya matendo yetu, bali kwa sababu ya kusudi lake na neema yake. Alitujalia neema hiyo kwa ajili ya Kristo Yesu kabla ya wakati, 10lakini imefunuliwa kwetu sasa kwa kuja kwake Mwokozi wetu, Yesu Kristo. Yeye amekomesha nguvu za kifo, na kwa njia ya Habari Njema akadhihirisha uhai usio na kifo.
11Mimi nimechaguliwa niwe mtume na mwalimu kwa ajili ya kuhubiri Habari Njema, 12nami nateseka kwa mambo haya kwa sababu hiyo. Lakini niko bado timamu kabisa kwani namjua yule niliyemwamini, tena nina hakika kwamba yeye atakilinda salama kile alichonikabidhi, mpaka siku ile. 13Shika kwa makini mafundisho yale ya kweli niliyokufundisha na kubaki katika hiyo imani na huo upendo wetu katika kuungana na Kristo Yesu. 14Jambo lile bora ulilokabidhiwa lilinde kwa nguvu ya Roho Mtakatifu anayeishi ndani yetu.
15Kama unavyojua, watu wote mkoani Asia wameniacha, miongoni mwao wakiwa Fugelo na Hermogene. 16Bwana aihurumie jamaa ya Onesiforo, kwa sababu aliniburudisha rohoni mara nyingi, wala hakuona haya kwa kuwa nilikuwa kifungoni, 17ila mara tu alipofika Roma, alianza kunitafuta kwa bidii mpaka akanipata. 18Bwana amjalie kupata huruma ya Mungu katika siku ile! Nawe wajua vizuri mengi aliyonifanyia huko Efeso.
2Timotheo1;1-18
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe
No comments:
Post a Comment