Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday, 16 June 2021

Kikombe Cha Asubuhi; Kitabu cha Yakobo....2



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,
afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..

Baada ya siku kadhaa, Yesu alirudi Kafarnaumu, watu wakapata habari kwamba alikuwa nyumbani. Basi, wakaja watu wengi sana hata nafasi yoyote ikakosekana mlangoni. Yesu alikuwa akiwahubiria ujumbe wake,

Marko 2:1-2

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono ye
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe..

wakati mtu mmoja aliyepooza alipoletwa kwake akiwa amechukuliwa na watu wanne. Kwa sababu ya huo umati wa watu, hawakuweza kumpeleka karibu na Yesu. Basi, wakatoboa sehemu ya paa iliyokuwa juu ya mahali alipokuwa Yesu. Walipokwisha pata nafasi, wakamteremsha huyo mtu akiwa amelala juu ya mkeka.

Marko 2:3-4


Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...

Yesu alipoona imani yao, akamwambia huyo mtu aliyepooza, “Mwanangu, umesamehewa dhambi zako.” Baadhi ya waalimu wa sheria waliokuwa wameketi hapo wakawaza mioyoni mwao,

Marko 2:5-6

Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.


 Onyo kuhusu ubaguzi

1Ndugu zangu, mkiwa mnamwamini Bwana Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwabague watu kamwe. 2Tuseme mtu mmoja ambaye amevaa pete ya dhahabu na mavazi nadhifu anaingia katika mkutano wenu, na papo hapo akaingia mtu maskini aliyevaa mavazi machafu. 3Ikiwa mtamstahi zaidi yule aliyevaa mavazi ya kuvutia na kumwambia: “Keti hapa mahali pazuri,” na kumwambia yule maskini: “Wewe, simama huko,” au “Keti hapa sakafuni miguuni pangu,” 4je, huo si ubaguzi kati yenu? Je, na huo uamuzi wenu haujatokana na fikira mbaya?
5Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni! Mungu amechagua watu ambao ni maskini katika ulimwengu huu ili wapate kuwa matajiri katika imani na kupokea ufalme aliowaahidia wale wanaompenda. 6Lakini nyinyi mnawadharau watu maskini! Je, matajiri si ndio wanaowakandamiza na kuwapeleka mahakamani? 7Je, si haohao wanaolitukana hilo jina lenu zuri mlilopewa?
8Kama mnaitimiza ile sheria ya ufalme kama ilivyoandikwa katika Maandiko Matakatifu: “Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe”, mtakuwa mnafanya vema kabisa. 9Lakini mkiwabagua watu, basi, mwatenda dhambi, nayo sheria inawahukumu nyinyi kuwa mna hatia. 10Anayevunja amri mojawapo ya sheria, atakuwa na hatia ya kuivunja sheria yote. 11Maana yuleyule aliyesema: “Usizini,” alisema pia “Usiue.” Kwa hiyo, hata ikiwa hukuzini, lakini umeua, wewe umeivunja sheria. 12Basi, semeni na kutenda kama watu watakaohukumiwa kwa sheria iletayo uhuru. 13Maana, Mungu hatakuwa na huruma atakapomhukumu mtu asiyekuwa na huruma. Lakini huruma hushinda hukumu.
Imani na matendo
14Ndugu zangu, kuna faida gani mtu kusema ana imani, lakini haonyeshi kwa vitendo? Je, hiyo imani yawezaje kumwokoa? 15Tuseme kaka au dada hana nguo au chakula. 16Yafaa kitu gani nyinyi kuwaambia hao: “Nendeni salama mkaote moto na kushiba,” bila kuwapatia mahitaji yao ya maisha? 17Vivyo hivyo, imani peke yake bila matendo imekufa.
18Lakini mtu anaweza kusema: “Wewe unayo imani, mimi ninayo matendo!” Haya! Nioneshe jinsi mtu anavyoweza kuwa na imani bila matendo, nami nitakuonesha imani yangu kwa matendo yangu. 19Je, wewe unaamini kwamba yuko Mungu mmoja? Sawa! Lakini hata pepo huamini hilo, na hutetemeka kwa hofu. 20Mpumbavu wee! Je, wataka kuoneshwa kwamba imani bila matendo imekufa? 21Je, Abrahamu babu yetu alipataje kukubaliwa kuwa mwadilifu? Kwa matendo yake, wakati alipomtoa tambiko mwanawe Isaka juu ya madhabahu. 22Waona, basi, kwamba imani yake iliandamana na matendo yake; imani yake ilikamilishwa kwa matendo yake. 23Hivyo yakatimia yale Maandiko Matakatifu yasemayo: “Abrahamu alimwamini Mungu, na kwa imani yake akakubaliwa kuwa mtu mwadilifu; na hivyo Abrahamu akaitwa rafiki ya Mungu.” 24Mnaona, basi, kwamba mtu hukubaliwa kuwa mwadilifu kwa matendo yake, na si kwa imani peke yake.
25Ilikuwa vivyo hivyo kuhusu yule malaya Rahabu; yeye alikubaliwa kuwa mwadilifu kwa sababu aliwapokea wale wapelelezi na kuwasaidia waende zao kwa kupitia njia nyingine.
26Basi, kama vile mwili bila roho umekufa, vivyo hivyo imani bila matendo imekufa.
Yakobo2;1-26
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: