Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday, 11 June 2021

Kikombe Cha Asubuhi; Kitabu cha Waebrania....12


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu...


Ndipo Mwenyezi-Mungu akaipenda nchi yake akawahurumia watu wake. Alisikiliza, akajibu sala zao; akasema, “Sasa nitawapeni tena nafaka, sitawafanya mdharauliwe tena na mataifa.

Yoeli 2:18-19

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Nitawaondoa hao adui watokao kaskazini, nitawafukuza mpaka jangwani; askari wa mbele nitawatupa katika Bahari ya Chumvi na wale wa nyuma katika Bahari ya Mediteranea. Watatoa uvundo na harufu mbaya, hao ambao wamefanya maovu makubwa.

Yoeli 2:20

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....

“Usiogope, ewe nchi, bali furahi na kushangilia, maana Mwenyezi-Mungu ametenda makuu. Msiogope, enyi wanyama. malisho ya nyikani yamekuwa mazuri, miti inazaa matunda yake, mizabibu na mitini zinazaa kwa wingi.

Yoeli 2:21-22

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,
Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.



 Bwana atufunza kuwa na nidhamu

1Sisi tunalo kundi hili kubwa la mashahidi mbele yetu. Kwa hiyo tuondoe kila kizuizi kinachotuzuia, na dhambi ile inayotungangania. Tupige mbio kwa uvumilivu katika mashindano yaliyowekwa mbele yetu. 2Tumwelekee Yesu ambaye ndiye aliyeianzisha imani yetu na ambaye ataikamilisha. Kwa ajili ya furaha iliyokuwa inamngojea, yeye alivumilia kifo msalabani, bila kuijali aibu yake, na sasa anaketi upande wa kulia wa kiti cha enzi cha Mungu.
3Fikirini juu ya mambo yaliyompata Yesu, jinsi alivyostahimili upinzani mkubwa kwa watu wenye dhambi. Basi, msife moyo, wala msikate tamaa. 4Maana katika kupambana na dhambi, nyinyi hamjapigana mpaka kiasi cha kumwaga damu yenu. 5Je, mmesahau yale maneno ya kutia moyo ambayo Mungu anawataja nyinyi kuwa wanawe?
“Mwanangu, usidharau adhabu ya Bwana,
wala usife moyo anapokukanya.
6Maana Bwana humpa nidhamu kila anayempenda,
humwadhibu kila anayekubali kuwa mwanawe.”
7Vumilieni adhabu kwani ni mafundisho; Mungu huwatendea nyinyi kama wanawe. Maana ni mwana gani asiyeadhibiwa na baba yake? 8Lakini msipoadhibiwa kama wana wengine, basi, nyinyi si wanawe, bali ni wana haramu. 9Zaidi ya hayo, sisi tunawaheshimu wazazi wetu waliotuzaa hata wanapotuadhibu. Basi, tunapaswa kumtii zaidi Baba yetu wa kiroho ili tupate kuishi. 10Wazazi wetu hapa duniani walituadhibu kwa muda, kama wao wenyewe walivyoona kuwa vema; lakini Mungu anatuadhibu kwa ajili ya faida yetu wenyewe, tupate kuushiriki utakatifu wake. 11Kuadhibiwa si jambo la kufurahisha bali la kuhuzunisha. Lakini wale waliofunzwa kuwa na nidhamu mwishowe watavuna tuzo la amani kutoka katika maisha adili.
Mafundisho na maonyo
12Basi, inueni mikono yenu inayolegea na kuimarisha magoti yenu yaliyo dhaifu. 13Endeleeni kutembea katika njia iliyonyoka, ili kile kilicholemaa kisiumizwe, bali kiponywe.
14Jitahidini kuishi kwa amani na watu wote. Ishini maisha ya utakatifu, kwa sababu hakuna mtu atakayemwona Bwana bila ya maisha kama hayo. 15Jitahidini sana mtu yeyote asije akapoteza neema ya Mungu. Muwe waangalifu ili mti mchungu usizuke kati yenu na kuwaua wengi kwa sumu yake. 16Jihadharini ili miongoni mwenu pasiwe na mtu mwasherati au mtu asiyemcha Mungu kama Esau, aliyeuza haki yake ya mzaliwa wa kwanza kwa mlo mmoja. 17Nyinyi mnafahamu kwamba hata alipotaka kuipata tena ile baraka iliyokuwa yake, alikataliwa, maana hakupata tena nafasi ya kutubu, ingawa aliitafuta kwa machozi.
18Nyinyi hamkuwasili mlimani Sinai, ambao unaweza kushikika kama walivyofanya watu wa Israeli; hamkufika kwenye moto uwakao, penye giza, tufani, 19mvumo wa tarumbeta na sauti ya maneno. Wale waliosikia sauti hiyo waliomba wasisikie tena neno lingine, 20kwani hawakuweza kustahimili amri iliyotolewa: “Atakayegusa mlima huu, hata kama ni mnyama, atapigwa mawe.” 21Hayo yote yalionekana ya kutisha mno, hata Mose akasema, “Naogopa na kutetemeka.”
22Lakini nyinyi mmefika katika mlima wa Siyoni, kwenye mji wa Mungu aliye hai. Mmefika Yerusalemu, mji wa mbinguni, ambapo wamekusanyika malaika kwa maelfu. 23Mmefika kwenye kusanyiko kubwa la wazaliwa wa kwanza wa Mungu, ambao majina yao yameandikwa mbinguni. Mnasimama mbele ya Mungu aliye hakimu wa wote, na mbele ya roho za watu waadilifu waliofanywa wakamilifu. 24Mmefika kwa Yesu ambaye ni mpatanishi katika agano jipya, na ambaye damu yake iliyomwagika inasema mambo mema kuliko ile ya Abeli.
25Basi, jihadharini msije mkakataa kumsikiliza huyo anayesema nanyi. Kama wale waliokataa kumsikiliza yule aliyewaonya hapa duniani hawakuokoka, sisi tutawezaje kuokoka kama tukikataa kumsikiliza yule anayetuonya kutoka mbinguni? 26Wakati ule sauti ilitetemesha nchi, lakini sasa ameahidi: “Nitatetemesha nchi tena, lakini si nchi tu bali pia mbingu.” 27Neno hili: “Tena” linatuonesha kwamba vitu vyote vilivyoumbwa vitatetemeshwa na kutoweka ili vibaki vile visivyotetemeshwa.
28Sisi basi, na tushukuru, kwani tunapokea ufalme usiotikisika. Tuwe na shukrani na kumwabudu Mungu kwa namna itakayompendeza, kwa ibada na hofu; 29maana Mungu wetu kweli ni moto mkali unaoteketeza.
Waebrania12;1-29
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: