Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Tumshukuru Mungu wetu katika yote...
Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii Asante kwa pumzi/uzima, afya na kuwatayari kwa majukumu yetu
Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni Neema yako yatutosha Mungu wetu..
Ndipo niliposema: “Niko tayari; ninayotakiwa kufanya yameandikwa katika kitabu cha sheria; kutimiza matakwa yako, ee Mungu wangu ni furaha yangu, sheria yako naishika kwa moyo wangu wote!” Zaburi 40:7-8 Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza, tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti, Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona.... Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono ye Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe.. |
Nimesimulia habari njema za ukombozi, mbele ya kusanyiko kubwa la watu. Kama ujuavyo ee Mwenyezi-Mungu, mimi sikujizuia kuitangaza. Sikuuficha moyoni mwangu ukombozi ulionijalia, nimetangaza daima kuwa wewe ni mwokozi mwaminifu; sikulificha kusanyiko kubwa la watu fadhili zako na uaminifu wako. Zaburi 40:9-10
Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu, watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia sauti yako na kuitii Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama inavyokupendeza wewe Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...
Ee Mwenyezi-Mungu, usininyime huruma yako! Fadhili zako na uaminifu wako vinihifadhi daima. Zaburi 40:11 Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao Nuru yako ikaangaze katika maisha yao Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele Amina....!!!
Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana kwakuwanami/kunisoma Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea kama inavyompendeza yeye Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba ukae nanyi daima.... Nawapenda. |
|
|
|
|
|
|
Watoto wa Mungu
1Oneni, basi, jinsi Baba alivyotupenda mno hata tunaitwa watoto wa Mungu! Na kweli, ndivyo tulivyo. Ndiyo maana ulimwengu haututambui sisi, kwani haumjui Mungu. 2Wapenzi wangu, sisi ni watoto wa Mungu sasa, lakini bado haijaonekana wazi jinsi tutakavyokuwa. Lakini tunajua kwamba, wakati Kristo atakapotokea, tutafanana naye kwani tutamwona vile alivyo. 3Basi, kila mtu aliye na tumaini hili katika Kristo, hujiweka safi kama vile Kristo alivyo safi kabisa.
4Kila mtu atendaye dhambi anavunja sheria ya Mungu, maana dhambi ni uvunjaji wa sheria. 5Mnajua kwamba Kristo alikuja kuziondoa dhambi zetu, na kwamba kwake hamna dhambi yoyote. 6Basi, kila aishiye katika muungano na Kristo hatendi dhambi; lakini kila mtu atendaye dhambi hakupata kamwe kumwona wala kumjua Kristo. 7Basi, watoto wangu, msikubali kupotoshwa na mtu yeyote. Mtu atendaye matendo maadilifu ni mwadilifu kama vile Kristo alivyo mwadilifu kabisa. 8Lakini atendaye dhambi ni wa Ibilisi, maana Ibilisi ametenda dhambi tangu mwanzo. Lakini Mwana wa Mungu alikuja duniani kuiharibu kazi ya Ibilisi.
9Kila aliye mtoto wa Mungu hatendi dhambi, maana anayo hali ya kimungu ndani yake; hawezi kutenda dhambi kwa sababu yeye ni mtoto wa Mungu. 10Lakini yeyote asiyetenda mambo maadilifu, au asiyempenda ndugu yake, huyo si mtoto wa Mungu. Hiyo ndiyo tofauti iliyoko kati ya watoto wa Mungu na watoto wa Ibilisi.
Pendaneni
11Na, ujumbe mliousikia tangu mwanzo ndio huu: Tunapaswa kupendana! 12Tusiwe kama Kaini ambaye, kwa kuongozwa na yule Mwovu, alimuua ndugu yake. Na, kwa nini alimuua? Kwa sababu matendo yake yalikuwa maovu, lakini yale ya ndugu yake yalikuwa mema!
13Basi, ndugu zangu, msishangae kama ulimwengu unawachukia nyinyi. 14Sisi tunajua kwamba tumekwisha pita kutoka katika kifo na kuingia katika uhai kwa sababu tunawapenda ndugu zetu. Mtu asiye na upendo hubaki katika kifo. 15Kila anayemchukia ndugu yake ni muuaji; nanyi mnajua kwamba muuaji yeyote yule hana uhai wa milele ndani yake. 16Sisi tumepata kujua upendo ni nini, kwani Kristo aliyatoa maisha yake kwa ajili yetu. Nasi vilevile tunapaswa kuyatoa maisha yetu kwa ajili ya ndugu zetu. 17Basi, mtu akiwa na mali za hapa duniani, halafu akamwona ndugu yake ana shida, lakini akawa na moyo mgumu bila kumwonea huruma, anawezaje kusema kwamba anampenda Mungu? 18Watoto wangu, upendo wetu usiwe maneno matupu, bali uwe upendo wa kweli na wa vitendo.
Uthabiti wetu mbele ya Mungu
19Hivyo ndivyo tuwezavyo kuwa na hakika kwamba sisi ni watu wa ukweli; na hatutakuwa na wasiwasi mbele ya Mungu. 20Kwa maana, hata kama dhamiri zetu zatuhukumu, twajua kwamba Mungu ni mkuu kuliko dhamiri, na kwamba yeye ajua kila kitu. 21Wapenzi wangu, kama dhamiri zetu hazina lawama juu yetu, basi, twaweza kuwa na uthabiti mbele ya Mungu, 22na kupokea kwake chochote tunachoomba, maana tunazitii amri zake na kufanya yale yanayompendeza. 23Na, amri yake ndiyo hii: Kumwamini Mwanae Yesu Kristo, na kupendana kama alivyotuamuru. 24Anayezitii amri za Mungu anaishi katika muungano na Mungu na Mungu anaishi katika muungano naye. Kwa njia ya Roho ambaye Mungu ametujalia, sisi twajua kwamba Mungu anaishi katika muungano nasi.
1Yohane3;1-24
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe
No comments:
Post a Comment