Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday, 16 July 2021

Kikombe Cha Asubuhi; Kitabu cha Ufunuo....3


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu...

Kwa imani Abrahamu alimtoa tambiko mwanawe Isaka wakati Mungu alipomjaribu. Huyo Abrahamu ndiye aliyekuwa amepokea ahadi ya Mungu, lakini, hata hivyo, alikubali kumtoa tambiko mwanawe wa pekee,

Waebrania 11:17

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

ingawa Mungu alikuwa amemwambia: “Wazawa wako watatokana na Isaka.” Abrahamu aliamini kwamba Mungu anaweza kuwafufua wafu; na kwa namna fulani kweli Abrahamu alimpata tena mwanawe kutoka kwa wafu.

Waebrania 11:18-19

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....

Kwa imani Isaka aliwabariki Yakobo na Esau, wapate baraka zitakazokuja baadaye. Kwa imani Yakobo alipokuwa karibu kufa, aliwabariki kila mmoja wa wana wa Yosefu, akamwabudu Mungu akiegemea kichwa cha ile fimbo yake.

Waebrania 11:20-21

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,
Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.


Ujumbe kwa Sarde
1“Kwa malaika wa kanisa la Sarde andika:
“Mimi niliye na roho saba za Mungu na nyota saba, nasema hivi: Nayajua mambo yako yote; najua unajulikana kuwa na uhai kumbe umekufa! 2Amka! Imarisha chochote chema kilichokubakia kabla nacho hakijatoweka kabisa. Maana, mpaka sasa, sijayaona matendo yako kuwa ni makamilifu mbele ya Mungu wangu. 3Kumbuka, basi, yale uliyofundishwa na jinsi ulivyoyasikia, uyatii na kutubu. Usipokesha nitakujia ghafla kama mwizi, na wala hutaijua saa nitakapokujia. 4Lakini wako wachache huko Sarde ambao hawakuyachafua mavazi yao. Hao wanastahili kutembea pamoja nami wamevaa mavazi meupe.
5 Taz Zab 69:28 “Mshindi atavikwa hivyo kwa mavazi meupe. Nami sitalifuta jina lake kutoka katika kitabu cha uhai; tena nitamkiri kwamba ni wangu mbele ya Baba yangu na mbele ya malaika wake.
6“Aliye na masikio, basi, na ayasikie yale Roho anayoyaambia makanisa!
Ujumbe kwa Filadelfia
7“Kwa malaika wa kanisa la Filadelfia andika hivi:
“Mimi niliye mtakatifu na wa kweli, ambaye nina ule ufunguo wa Daudi na ambaye hufungua na hakuna awezaye kufunga, hufunga na hakuna awezaye kufungua. 8Nayajua mambo yako yote! Sasa, nimefungua mbele yako mlango ambao hakuna mtu awezaye kuufunga; najua kwamba ingawa huna nguvu sana, hata hivyo, umelitii neno langu wala hukulikana jina langu. 9Sikiliza! Nitawapeleka kwako watu wa kundi lake Shetani, watu ambao hujisema kuwa ni Wayahudi, kumbe sivyo, ila wanasema uongo. Naam, nitawapeleka kwako na kuwafanya wapige magoti mbele yako, wapate kujua kwamba nimekupenda wewe. 10Kwa kuwa wewe umezingatia neno langu la kuwa na uvumilivu thabiti, mimi nitakutegemeza salama wakati ule wa dhiki inayoujia ulimwengu mzima, kuwajaribu wote wanaoishi duniani. 11Naja kwako upesi! Shikilia kwa nguvu ulicho nacho sasa, ili usije ukanyang'anywa na mtu yeyote taji yako.
12“Mshindi nitamfanya awe nguzo katika hekalu la Mungu wangu, na hatatoka humo kamwe. Pia nitaandika juu yake jina la Mungu wangu na jina la mji wa Mungu wangu, yaani Yerusalemu mpya, mji ambao utashuka kutoka juu mbinguni kwa Mungu wangu. Tena nitaandika juu yake jina langu jipya.
13“Aliye na masikio, basi, na ayasikie yale Roho anayoyaambia makanisa!
Ujumbe kwa Laodikea
14“Kwa malaika wa kanisa la Laodikea andika hivi:
“Mimi niitwaye Amina, shahidi mwaminifu na wa kweli, ambaye ni chanzo cha viumbe vyote alivyoumba Mungu nasema hivi. 15Nayajua mambo yako yote! Najua kwamba wewe si baridi wala si moto. Afadhali ungekuwa kimojawapo: Baridi au moto. 16Basi, kwa kuwa hali yako ni vuguvugu, si baridi wala si moto, nitakutapika! 17Wewe unajisema, ‘Mimi ni tajiri; ninajitosheleza, sina haja ya kitu chochote;’ kumbe, hujui kwamba wewe ni mnyonge, unahitaji kuhurumiwa, maskini, kipofu tena uko uchi! 18Nakushauri ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto upate kuwa tajiri kweli. Tena afadhali ununue pia vazi jeupe, uvae na kufunika aibu ya uchi wako. Nunua pia mafuta ukapake machoni pako upate kuona. 19Mimi ndiye mwenye kumwonya na kumrudi yeyote ninayempenda. Kwa hiyo uwe na bidii na kutubu. 20Sikiliza! Mimi nasimama mlangoni na kubisha hodi. Mtu akisikia sauti yangu na kufungua mlango, nitaingia nyumbani kwake na kula chakula pamoja naye, naye atakula pamoja nami.
21“Mshindi nitamjalia kuketi pamoja nami juu ya kiti changu cha enzi, kama vile mimi mwenyewe nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu juu ya kiti chake cha enzi.

22“Aliye na masikio, basi, na ayasikie yale Roho anayoyaambia makanisa!” 

Ufunuo3;1-22

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: