Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday, 21 July 2021

Kikombe Cha Asubuhi; Kitabu cha Ufunuo....6


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu...

Kwa imani kuta za mji wa Yeriko zilianguka watu wa Israeli walipokwisha zunguka kuta hizo kwa siku saba. Kwa imani Rahabu aliyekuwa malaya hakuangamia pamoja na wale waliomwasi Mungu, kwa sababu aliwakaribisha wale wapelelezi.

Waebrania 11:30-31

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Basi, niseme nini zaidi? Wakati hauniruhusu kueleza juu ya Gideoni, Baraki, Samsoni, Yeftha, Daudi, Samueli na manabii. Kwa imani hawa wote walipigana vita na wafalme, wakashinda. Walitenda mambo adili, wakapokea yale aliyoahidi Mungu. Walifunga vinywa vya simba,

Waebrania 11:32-33

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....

walizima mioto mikali, waliepuka kuuawa kwa upanga, walikuwa dhaifu lakini walipata nguvu. Walikuwa hodari katika vita, wakashinda majeshi ya kigeni. Na, wanawake walioamini walirudishiwa wafu wao wakiwa wamefufuliwa. Baadhi yao walikataa kufunguliwa, wakateswa mpaka kufa ili wapate kufufuliwa na kuingia katika maisha bora zaidi.

Waebrania 11:34-35

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,
Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.



 Mwanakondoo anaivunja mihuri

1Kisha, nikamwona Mwanakondoo anavunja mhuri mmojawapo wa ile mihuri saba. Nikasikia mmoja wa wale viumbe hai wanne akisema kwa sauti kama ya ngurumo, “Njoo!” 2Mimi nikatazama, na kumbe palikuwa na farasi mmoja mweupe hapo. Na mpandafarasi wake alikuwa na upinde, akapewa na taji. Basi, akatoka kama mshindi, aendelee kushinda.
3Kisha, Mwanakondoo akavunja mhuri wa pili. Nikamsikia yule kiumbe hai wa pili akisema, “Njoo!” 4Nami nikatazama na kumbe palikuwapo farasi mwingine hapo, mwekundu. Mpandafarasi wake alikabidhiwa jukumu la kuondoa amani duniani, watu wauane, naye akapewa upanga mkubwa.
5Kisha Mwanakondoo akavunja mhuri wa tatu. Nikamsikia yule kiumbe hai wa tatu akisema, “Njoo!” Nikatazama na kumbe palikuwapo farasi mmoja hapo, mweusi. Mpandafarasi wake alikuwa na vipimo viwili vya kupimia uzito mkononi mwake. 6Nikasikia kitu kama sauti itokayo kwa wale viumbe hai wanne. Nayo ilisema, “Kibaba kimoja cha unga wa ngano kwa kiasi cha fedha denari moja, na vibaba vitatu vya shayiri kwa denari moja. Lakini usiharibu mafuta wala divai!”
7Kisha, Mwanakondoo akavunja mhuri wa nne. Nikamsikia yule kiumbe hai wa nne akisema, “Njoo!” 8Nami nikatazama, na kumbe alikuwapo farasi mmoja hapo, rangi yake kijivu. Na jina la mpandafarasi wake lilikuwa Kifo, na Kuzimu alimfuata nyuma. Hao walipewa mamlaka juu ya robo moja ya dunia, wawaue watu kwa upanga, njaa, tauni na kwa wanyama wakali wa dunia.
9Kisha, Mwanakondoo akavunja mhuri wa tano. Nikaona pale chini ya madhabahu ya kufukizia ubani roho za wale waliouawa kwa sababu ya ujumbe wa Mungu, na kwa sababu ya ushuhuda waliotoa. 10Basi, wakalia kwa sauti kubwa: “Ee Bwana, uliye mtakatifu na mwaminifu, mpaka lini utakawia kulipiza kisasi kwa wakazi wote wa dunia kwa ajili ya kuuawa kwetu?” 11Wakapewa kila mmoja vazi refu jeupe, wakaambiwa wazidi kusubiri kwa muda mfupi, mpaka itakapotimia idadi ya watumishi wenzao na ndugu ambao watauawa kama wao wenyewe walivyouawa.
12Kisha nikatazama, na wakati Mwanakondoo alipouvunja mhuri wa sita, kukawa na tetemeko kubwa la ardhi; jua likawa jeusi kama gunia la manyoya; mwezi wote ukawa mwekundu kama damu; 13nazo nyota za mbingu zikaanguka juu ya ardhi kama matunda ya mtini yasiyokomaa yaangukavyo wakati mti wake unapotikiswa na upepo mkali. 14Anga likatoweka kama vile karatasi inavyokunjwakunjwa; milima yote na visima vyote vikaondolewa mahali pake. 15Kisha, wafalme wa duniani, wakuu, majemadari, matajiri, wenye nguvu, kila mtumwa na mtu huru, wakajificha mapangoni na kwenye miamba milimani. 16Wakaiambia hiyo milima na hayo majabali, “Tuangukieni, mkatufiche mbali na yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na mbali na ghadhabu ya Mwanakondoo! 17Maana siku maalumu ya ghadhabu yao imefika. Nani awezaye kuikabili?”
Ufunuo6;1-17
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: