Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Tunamshukuru Mungu kwa kutupa kibali cha kupitia kitabu cha "Yuda" Ni matumaini yangu kuna mengi tumejifunza/kufaidika na kutupa mwanga/kuelewa kwenye kitabu hiki...
Leo tunapokwenda anza kupitia Kitabu cha"Ufunuo" tunamuomba Mungu wetu akatupe kibali,macho ya rohoni na akili ya kuelewa katika kujifunza NENO lake... Ee Mungu tunaomba ukatuongoze...!! Tumshukuru Mungu wetu katika yote...
Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana Mungu wa walio hai,Mungu mwenye huruma,Mungu wa upendo Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!
|
Kwa imani Noa alionywa na Mungu juu ya mambo ya baadaye ambayo hayakuwa yameonekana bado. Alimtii Mungu, akajenga ile safina ambamo aliokolewa yeye pamoja na jamaa yake. Kutokana na hayo ulimwengu ulihukumiwa, naye Noa akapokea uadilifu unaotokana na imani. Waebrania 11:7 Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako, Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona...
Kwa imani Abrahamu alimtii Mungu alipoitwa aende katika nchi ambayo Mungu angempa iwe yake. Ingawa hakujua alikokuwa anakwenda, Abrahamu alihama. Waebrania 11:8 Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu, Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii.. Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako siku zote za maisha yetu... Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....
Kwa imani aliishi kama mgeni katika nchi aliyoahidiwa na Mungu. Aliishi huko katika hema kama walivyoishi Isaka na Yakobo, ambao pia walishiriki ahadi ileile. Waebrania 11:9 Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu kila mmoja na mahitaji yake Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru... Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele... Amina...!!
Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami, Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake... Nawapenda. |
|
|
|
|
1Huu ni ufunuo aliotoa Yesu Kristo, ambao Mungu alimpa awaoneshe watumishi wake mambo ambayo yanapaswa kutukia karibuni. Kristo alimtuma malaika wake amjulishe mtumishi wake Yohane mambo hayo. 2Naye Yohane ameshuhudia yote aliyoyaona kuhusu ujumbe wa Mungu na ushahidi wa Yesu Kristo. 3Heri yake mtu anayesoma kitabu hiki chenye maneno ya ujumbe wa kinabii; na heri yao wanaosikia na kushika yaliyoandikwa humu, maana wakati wa mambo haya umekaribia.
Salamu kwa makanisa saba
4Mimi Yohane nayaandikia makanisa saba yaliyoko Asia. Nawatakieni neema na amani kutoka kwake yeye aliyeko, aliyekuwako na anayekuja; na kutoka kwa roho saba walio mbele ya kiti chake cha enzi, 5Taz Zab 89:27 na kutoka kwa Yesu Kristo, shahidi mwaminifu, wa kwanza kufufuliwa kutoka kwa wafu, na ambaye ni mtawala wa wafalme wa dunia.
Yeye anatupenda, na kwa damu yake ametufungua kutoka vifungo vya dhambi zetu, 6akatufanya sisi kuwa ufalme wa makuhani, tumtumikie Mungu, Baba yake. Kwake Yesu Kristo uwe utukufu na nguvu, milele na milele! Amina.
7Tazama! Anakuja na mawingu!
Kila mtu atamwona, na hata wale waliomtoboa.
Makabila yote duniani yataomboleza juu yake.
Naam! Amina.
8“Mimi ni Alfa na Omega,” asema Bwana Mungu Mwenye Nguvu1:8 Bwana Mungu…Nguvu: Jina la sifa la Mungu sasa linatumika kumtaja Yesu., aliyeko, aliyekuwako na anayekuja.
Njozi ya Mwana wa Mtu
9Mimi ni Yohane, ndugu yenu, ambaye kwa kuungana na Yesu, nashiriki pamoja nanyi mateso na ufalme wake na uvumilivu thabiti. Mimi nilikuwa katika kisiwa kiitwacho Patmo kwa sababu ya kuhubiri neno la Mungu na kumshuhudia Yesu. 10Basi, wakati mmoja, siku ya Bwana, nilikumbwa na Roho, nikasikia nyuma yangu sauti kubwa kama sauti ya tarumbeta. 11Nayo ilisema, “Andika katika kitabu yale unayoyaona, ukipeleke kwa makanisa haya saba: Efeso, Smurna, Pergamumu, Thuatira, Sarde, Filadelfia na Laodikea.”
12Basi, nikageuka nimwone huyo aliyesema nami, nikaona vinara vya taa saba vya dhahabu, 13na katikati yake kulikuwa na kitu kama Mwana wa Mtu1:13 Mwana wa Mtu: Msemo aliotumia Yesu kujitaja yeye mwenyewe., naye alikuwa amevaa kanzu ndefu na mkanda wa dhahabu kifuani. 14Nywele zake zilikuwa nyeupe kama pamba nyeupe, kama theluji; macho yake yalimetameta kama moto; 15miguu yake kama shaba iliyong'arishwa iliyosafishwa katika tanuri ya moto, na sauti yake ilikuwa kama sauti ya poromoko la maji. 16Katika mkono wake wa kulia alikuwa na nyota saba, na kinywani mwake mlitoka upanga wenye makali kuwili. Uso wake uling'aa kama jua kali kabisa.
17Basi, nilipomwona tu, nilianguka mbele ya miguu yake kama maiti. Lakini yeye akaweka mkono wake wa kulia juu yangu, akasema, “Usiogope! Mimi ni wa kwanza na wa mwisho. 18Mimi ni yeye aliye hai! Nilikuwa nimekufa, lakini, tazama, sasa ni hai milele na milele. Ninazo funguo za kifo na kuzimu. 19Basi, sasa andika mambo haya unayoyaona, mambo yanayotukia sasa na yale yatakayotukia baadaye. 20Siri ya nyota zile saba ulizoziona katika mkono wangu wa kulia na siri ya vile vinara saba vya taa vya dhahabu, ni hii: Zile nyota saba ni malaika wa makanisa; na vile vinara saba vya taa vya dhahabu ni makanisa saba.
Ufunuo1;1-20
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe
No comments:
Post a Comment