|
Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Tunamshukuru Mungu kwa kutupa kibali cha kupitia Vitabu cha VYOTE katika "BIBLIA" Ni matumaini yangu kuna mengi tumejifunza/kufaidika na kutupa mwanga/kuelewa kwenye Vitabu hivi...
Leo tunapokwenda Kumalizia /kupitia Kitabu cha MWISHO"Ufunuo22" tunamuomba Mungu wetu akatupe kibali,macho ya rohoni na akili ya kuelewa katika kujifunza NENO lake... Ee Mungu tunaomba ukatuongoze...!! Tumshukuru Mungu wetu katika yote...
Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana Mungu wa walio hai,Mungu mwenye huruma,Mungu wa upendo Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!
|
“Ufalme wa mbinguni unafanana na mtu mwenye shamba la mizabibu, ambaye alitoka asubuhi na mapema kuwaajiri wafanyakazi katika shamba lake. Akapatana nao kuwalipa fedha denari moja kwa siku, kisha akawapeleka katika shamba lake la mizabibu. Mathayo 20:1-2 Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako, Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona...
Akatoka mnamo saa tatu asubuhi, akaona watu wengine wamesimama sokoni, hawana kazi. Akawaambia, ‘Nendeni nanyi mkafanye kazi katika shamba la mizabibu, nami nitawapeni haki yenu.’ Mathayo 20:3-4 Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu, Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii.. Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako siku zote za maisha yetu... Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....
Basi, wakaenda. Huyo mwenye shamba akatoka tena mnamo saa sita na saa tisa, akafanya vivyo hivyo. Hata mnamo saa kumi na moja jioni, akatoka tena; akakuta watu wengine wamesimama pale sokoni. Basi, akawauliza, ‘Mbona mmesimama hapa mchana kutwa bila kazi?’ Wakamjibu: ‘Kwa sababu hakuna mtu aliyetuajiri.’ Naye akawaambia, ‘Nendeni nanyi mkafanye kazi katika shamba la mizabibu.’ Mathayo 20:5-7 Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu kila mmoja na mahitaji yake Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru... Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele... Amina...!!
Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami, Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake... Nawapenda. |
|
|
|
|
|
1Kisha malaika akanionesha mto wa maji ya uhai maangavu kama kioo, yakitoka kwenye kiti cha enzi cha Mungu na Mwanakondoo. 2Mto huo ulitiririka kupitia katikati ya barabara kuu ya mji. Kandokando ya mto huo kulikuwa na mti wa uhai unaozaa matunda mara kumi na mbili kwa mwaka, yaani kila mwezi; na majani yake ni dawa ya kuwaponya watu wa mataifa. 3Hapana kitu chochote kilicholaaniwa kitakachokuwa katika mji huo.
Kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwanakondoo kitakuwa katika mji huo, na watumishi wake watamwabudu. 4Watauona uso wake, na jina lake litaandikwa juu ya paji za nyuso zao. 5Usiku hautakuwako tena, wala hawatahitaji mwanga wa taa au wa jua, maana Bwana Mungu atawaangazia, nao watatawala milele na milele.
Kuja kwa Yesu
6Kisha malaika akaniambia, “Maneno haya ni ya kweli na ya kuaminika. Bwana Mungu ambaye huwapa manabii Roho wake, alimtuma malaika wake awaoneshe watumishi wake mambo ambayo lazima yatukie punde.
7“Sikiliza! Naja upesi. Heri yake anayeyazingatia maneno ya unabii yaliyo katika kitabu hiki.”
8Mimi Yohane, niliyaona na kusikia mambo haya. Nilipokwisha sikia na kuona, nikajitupa chini mbele ya miguu ya huyo malaika aliyenionesha mambo hayo, nikataka kumwabudu. 9Lakini yeye akaniambia, “Acha! Mimi ni mtumishi tu kama wewe na ndugu zako manabii na wote wanaoyatii maagizo yaliyomo katika kitabu hiki. Mwabudu Mungu!” 10Tena akaniambia, “Usiyafiche kama siri maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki, maana wakati wa kutimizwa kwake umekaribia. 11Kwa sasa anayetenda mabaya na aendelee kutenda mabaya, na aliye mchafu aendelee kuwa mchafu. Mwenye kutenda mema na azidi kutenda mema, na aliye mtakatifu na azidi kuwa mtakatifu.”
12 Taz Zab 28:4 “Sikiliza!” Asema Yesu, “Naja upesi pamoja na tuzo nitakalompa kila mmoja kufuatana na matendo yake. 13Mimi ni Alfa na Omega, wa kwanza na wa mwisho, mwanzo na mwisho.”
14Heri yao wale wanaoosha mavazi yao, wapate kuwa na haki ya kula tunda la mti wa uhai, na haki ya kuingia mjini kwa kupitia milango yake. 15Lakini mbwa, wachawi, wazinzi, wauaji, waabudu sanamu na wote wanaopenda kusema uongo, watakaa nje ya mji.
16“Mimi, Yesu, nimemtuma malaika wangu awathibitishieni mambo haya katika makanisa. Mimi ni mzawa wa ukoo wa Daudi. Mimi ni nyota angavu ya asubuhi!”
17Roho na Bibi arusi waseme, “Njoo!” Kila mtu asikiaye hili, na aseme, “Njoo!” Aliye na kiu na aje; anayependa, na achukue maji ya uhai bila malipo.
Hatima
18Mimi Yohane nawapa onyo wote wanaosikia maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki: Mtu yeyote akiongeza chochote katika mambo haya, Mungu atamwongezea mabaa yaliyoandikwa katika kitabu hiki. 19Na mtu yeyote akipunguza chochote katika maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki, Mungu atamnyang'anya sehemu yake katika ule mti wa uhai, na sehemu yake katika mji mtakatifu, ambavyo vimeelezwa katika kitabu hiki. 20Naye anayetoa ushahidi wake juu ya mambo haya asema: “Kweli naja upesi.”
Amina. Njoo Bwana Yesu!
21Nawatakieni nyote neema ya Bwana Yesu. Amina.
Ufunuo22;1-21
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe
MWISHO.
No comments:
Post a Comment