Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 25 May 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Kutoka 40- Mwisho wa kitabu cha Kutoka...

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tumshukuru Mungu wetu....

Mungu wetu, Baba yetu, Muumba wetu, Muumba Mbingu na Nchi na Vyote vilivyomo ni mali yako..Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..!
Yahweh.!Jehovah..!El shaddai..!Muweza wa yote, Alfa na Omega,Wewe ni Mwanzo na wewe ni mwisho,Hakuna kama wewe..!!


Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako.
Asante kwa ulinzi wako na kutuamsha salama..

Asante kwakutuchagua tena  na umetupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii..
Si kwa nguvu zetu wala Akili zetu,si kwamba sisi ni wema sana,si kwamba sisi wazuri mno..hapana ni kwa Neema/Rehema zako sisi kuiona leo hii...
Tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,kujishusha na kujiachilia mikononi mwako Mfalme wa Amani ..
Tunaomba utusamehe pale tulipokwenda kinyume nawe kwa kuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua,kutojua..
Baba wa mbinguni tunaomba nasi utupe Neema ya kuweza kuwasamehe waliotukosea..
Utuepushe na majaribu Baba wa mbinguni na utuokoe na yule mwovu na kazi zake..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..
Mungu Baba tunaomba ukatutakase Miili yetu na Akili zetu tupate kutambua na kujitambua..

Tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo,vyombo vya usafiri, tutembeapo hatua zetu ziwe nawe Yahweh..Mungu wetu ukabariki Kazi zetu,Biashara,Masomo,vilaji/vinywaji na vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Mfalme wa Amani ukavitakase kwa Damu ya mwanao mpendwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo yeye aliteseka ili sisi tupate kupona..

Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaguse na mkono wako wenye nguvu na kuwaponya wote wanaopitia majaribu mbalimbali,shida/tabu,wafiwa ukawe mfariji wao,wagonjwa na wote walio katika vifungo mbalimbali Baba ukawafungue na kuwaokoa, wakapate kupona kimwili na kiroho pia,Baba ukaonekane kwenye shida zao wote wanaokuomba na kukulilia Mungu wetu ukawafute machozi yao..

Tunakushuru Mungu wetu kwa uwezo wako na kutupa Neema hii ya kuweza kusoma Neno Lako Baba wa Mbinguni..

leo tumemaliza kusoma Neno lako kwenye kitabu hiki..Baba wa mbinguni isiwe mwisho na iwe ndiyo mwanzo tukawe na Shauku ya kusoma Neno lako..
 Tunaomba utubariki na kutupa mwangaza zaidi kwenye neno lako..na tusomapo tuondoke na faida na tupate kuelewa na kulitunza likapate kutusaidia sisi na wengine..
Yesu anafafanua mfano wa mpanzi
(Mat 13:18-23; Luka 8:11-15)



Basi, Yesu akawauliza, “Je, nyinyi hamwelewi mfano huu? Mtawezaje basi, kuelewa mfano wowote? Mpanzi hupanda neno la Mungu. Watu wengine ni kama walio njiani ambapo neno lilipandwa. Lakini mara tu baada ya kulisikia, Shetani huja na kuliondoa neno hilo lililopandwa ndani yao. Watu wengine ni kama zile mbegu zilizopandwa penye mawe. Mara tu walisikiapo hilo neno hulipokea kwa furaha. Lakini haliwaingii na kuwa na mizizi ndani yao; huendelea kulizingatia kwa kitambo tu, na wakati taabu au udhalimu vinapotokea kwa sababu ya hilo neno, mara wanakata tamaa. Watu wengine ni kama zile mbegu zilizoanguka penye miti ya miiba. Huo ni mfano wa wale wanaosikia hilo neno, lakini wasiwasi wa ulimwengu huu, anasa za mali na tamaa za kila namna huwaingia na kulisonga hilo neno, nao hawazai matunda. Lakini wengine ni kama zile mbegu zilizopandwa katika udongo mzuri. Hawa hulisikia hilo neno, wakalipokea, wakazaa matunda: Wengine thelathini, wengine sitini na wengine mia.”

Mungu wetu ukatupe masikio tusikie na macho ya kuona.. Tukawe kama zile mbegu zilizopandwa kwenye udongo mzuri..
Tukawe barua njema na tukasomeke popote tutakapo pita sawasawa na mapenzi yako...


Mfano wa mbegu inayoota


Yesu akaendelea kusema, “Ufalme wa Mungu ni kama ifuatavyo. Mtu hupanda mbegu shambani. Usiku hulala, mchana yu macho na wakati huo mbegu zinaota na kukua; yeye hajui inavyofanyika. Udongo wenyewe huiwezesha mimea kukua na kuzaa matunda: Kwanza huchipua jani changa, kisha suke, na mwishowe nafaka ndani ya suke. Nafaka inapoiva, huyo mtu huanza kutumia mundu wake, maana wakati wa mavuno umefika.”
Mungu wetu ukatupe Neema ya kupanda  mbegu njema na tupate kukua kiimani/kiroho na kuvuna yaliyo mema..
 Mungu wetu tunapanda mbegu zako kwa wote wasioamini na wapate kujua wewe Mungu wetu na wema wako..Sifa na utukufu tunakurudishia wewe Daima..


Asante Mungu wetu katika yote.
Tunayaweka haya yote mikononi mwako tukiamini wewe ni Mungu wetu na Tumaini letu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na utukufu hata Milele..
Amina..!
Mungu wetu yu mwema sana wapendwa..

kwa uwezo wake na mapenzi yake kwetu leo tumemaliza kitabu hiki..
ninaimani kuna tuliokuwa nao sambamba tangu mwanzo..
Mungu aendele kukupa shauku ya kuendelea kusoma Neno lake..

haijalishi uko busy kiasi gani lakini huwezi kukosa muda kidogo kwa ajili yake yeye Mungu aliyekupa hiyo shughuli ya kukufanya ukawa Busy..
kusikiliza Neno kanisani tuu haitoshi lazima tujibidishe na kujipa msukumo wa kujisomea katika mazingira yoyote tunayopitia tuweke  Mungu kwanza..
Mungu aendelee kutufunulia na kutupa mwanga zaidi..
tunachokipanda kipate kumea/kukua vyema..
Asanteni sana kwakutembelea hapa..
Mungu awabariki na kuwapa Amani ya Moyo..
Nawapenda sana. 

Hema lasimikwa na kuwekwa wakfu

1Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, 2“Mnamo siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, utalisimika hema takatifu la mkutano. 3Ndani ya hema hilo utaweka lile sanduku la ushuhuda, kisha weka pazia mbele yake. 4Utaiingiza meza na kupanga vyombo vyake juu. Utaingiza kile kinara pia na kuziweka taa zake juu yake. 5Madhabahu ya dhahabu ya kufukizia ubani utaiweka mbele ya sanduku la ushuhuda, kisha utatundika pazia kwenye mlango wa hema takatifu. 6Ile madhabahu ya kuteketezea sadaka utaiweka mbele ya mlango wa hema takatifu la mkutano. 7Birika la kutawadhia utaliweka katikati ya hema la mkutano na madhabahu na kulijaza maji. 8Utazungushia ua na kutundika pazia penye lango lake.
9“Kisha, utaliweka wakfu hema takatifu pamoja na vyombo vyake vyote kwa kuvipaka yale mafuta ya kupaka, nalo litakuwa takatifu. 10Halafu, utaiweka wakfu madhabahu ya kuteketezea sadaka na vyombo vyake vyote kwa kuipaka mafuta, nayo itakuwa takatifu kabisa. 11Birika la kutawadhia na tako lake pia utaliweka wakfu kwa namna hiyohiyo.
12“Utamwita Aroni na wanawe waje mlangoni mwa hema la mkutano, kisha uwatawadhe. 13Mvike Aroni yale mavazi matakatifu; utampaka mafuta na kumweka wakfu, ili aweze kunitumikia kama kuhani. 14Waite wanawe na kuwavisha zile kanzu. 15Kisha uwapake mafuta kama ulivyompaka baba yao, ili nao pia wanitumikie kama makuhani. Kupakwa mafuta huku kutawaingiza katika ukuhani wa kudumu katika vizazi vyao vyote.”
16Basi, Mose alitekeleza kikamilifu kabisa maagizo yote ya Mwenyezi-Mungu.
17Mnamo siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza mwaka wa pili baada ya kutoka Misri, hema la mkutano lilisimikwa. 18Mose aliweka vikalio vyake, akainua mbao zake, akashikamanisha pau zake na kusimamisha nguzo zake. 19Alitandaza pazia juu ya hema takatifu na kuweka kifuniko cha hema juu yake, kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. 20Kisha alichukua vile vibao viwili vya mawe na kuviweka katika lile sanduku. Aliipitisha ile mipiko katika vikonyo vya sanduku na kukiweka kiti cha rehema juu yake. 21Kisha akaliweka lile sanduku la maamuzi ndani ya hema na kutundika pazia, na kwa namna hiyo akalisitiri sanduku la maamuzi, kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu.
22Aliweka meza ndani ya hema la mkutano, upande wa kaskazini, sehemu ya nje ya pazia, 23na juu yake akaipanga mikate iliyotolewa kwa Mwenyezi-Mungu, kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. 24Alikiweka kinara ndani ya hema la mkutano, upande wa kusini, mkabala wa meza. 25Humo, mbele ya Mwenyezi-Mungu, akaziwasha taa zake, kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. 26Aliiweka ile madhabahu ya dhahabu katika hema, mbele ya pazia, 27na kufukiza ubani wenye harufu nzuri juu yake, kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. 28Alitundika pazia kwenye mlango wa hema takatifu, 29akaweka hapo langoni mwa hema takatifu madhabahu ya sadaka za kuteketezwa, akatolea juu yake sadaka ya kuteketezwa na sadaka ya nafaka, kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. 30Aliliweka birika la kutawadhia katikati ya hema la mkutano na madhabahu, na kutia maji ya kutawadha. 31Mose, Aroni na wanawe, wote walinawa mikono na miguu yao humo. 32Kila walipoingia ndani ya hema au walipokaribia ile madhabahu, walinawa, kama Mose alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. 33Mwishowe Mose akatengeneza ua kulizunguka hema takatifu na madhabahu, na kuweka pazia kwenye lango la ua. Hivyo,
Mose akaikamilisha kazi yote.


Wingu juu ya hema la mkutano

34Kisha, lile wingu likalifunika lile hema la mkutano, na utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukalijaza hema. 35Mose alishindwa kuingia ndani ya hema la mkutano kwa sababu hilo wingu lilikaa juu yake, na utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukajaa humo. 36Katika safari zao zote Waisraeli hawakuanza safari kamwe isipokuwa wakati wingu hilo lilipoinuliwa kutoka juu ya hema. 37Kama wingu hilo halikuinuliwa wao hawakuanza safari; walingoja mpaka wakati lilipoinuliwa. 38Katika safari zao zote, Waisraeli waliweza kuliona lile wingu la Mwenyezi-Mungu juu ya hema wakati wa mchana na ule moto ukiwaka juu yake usiku.

Kutoka40;1-38

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Wednesday 24 May 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Kutoka 39...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tumshukuru Mngu wetu katika yote..
Mtakatifu.!Mtakatifu.!Mtakatifu.! Baba wa Mbinguni..Tunakushukuru na kukusifu daima..

Asante kwa wema na fadhili zako Mungu wetu, Asante kwa ulinzi wako na kutuamsha salama Mungu wetu..Asante kwa kutuchagua na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii..
Tunashuka mbele zako tukijinyenyekeza na kujiachilia mikononi mwako Yahweh..!
Tunaomba utusamehe pale tulipokwenda kinyume nawe Mungu wetu kwa kuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Nasi utupe Neema ya kuweza kuwasamehe waliotukosea..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..
Baba tunaiweka siku hii na maisha yetu mikononi mwako..Tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo,Vyombo vya usafiri,Tutembeapo hatua zetu ziwe nawe Jehovah..Ukabariki vilaji/vinywaji,Kazi zetu,Biashara,Masomo na vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Mfalme wa Amani ukavitakase kwa Damu ya mwanao Mpendwa Bwana wetu na mwokozi wetu Yesu Kristo yeye aliteseka ili sisi tupate kupona..
Ukatuokoe na yule mwovu na kazi zake..


Ukatutakase Miili yetu na Akili zetu ..tupate kutambua na kujitambua..

Ukatupe ufahamu, Busara na hekima,Utuwema na Upendo..
Kila mmoja akatumike sawasawa na karama uliyompa na akaijitoe kwa kazi yako Mungu wetu Sifa na utukufu ukurudie wewe Mungu wetu..
Mungu wetu ukaonekane tuwapo Kazini,Shuleni na katika yote tunayoenda kufanya
Tukawe chombo chema tukatumike sawasawa na mapenzi yako..

Wapendwa Ndugu zangu Mungu wetu yu Mwema sana na kupitia yeye tumebarikiwa vipaji/karama mbalimbali na nilichonacho mimi pengine wewe huna na ulichonacho wewe mimi sina au siwezi kufanya hivyo/hicho kitu..Yote hiyo ni makusudi yake ili kuwe na mgawanyiko wa kazi zake...
Tumuombe Mungu atuongoze katika kazi zake na kutupa moyo wa kuifanya hiyo kazi..hakuna kazi ndogo mbele za Mungu..

Kama wewe nimshonaji unaweza kushona hata vitambaa vya kutandika/kupambia Nyumba ya Mungu[Tabitha-Matendo 9:36-43],kama wewe ni mfagiaji kafagie na kusafisha Nyumba ya Mungu,kama wewe ni mpambaji Pamba Nyumba ya Mungu,kama wewe ni mpishi pika hata chai na unaweza kukusanya wawili watatu mkaongea Neno la Mungu na kusaidiana kutafakari kila mmoja ataondoka na kitu..Kama wewe una pesa hayaaa kunamahitaji mengi yanahitaji pesa Bariki wengine nawe uendelee kubarikiwa, Angalia nini kimepungua kwenye Nyumba za ibada au kwa watu wa Mungu ili uwasaidie na Mungu akuongezee zaidi ya hizo utakazo toa..
kwenye maisha haya ya kila siku kuna vitu vingi vya kufanya/kumfanyia Mungu ili watu wauone wema,Utukufu wa Mungu..
Kila mmoja afanye kwa nafasi yake aliyopewa na Mungu..nasi kwakubishana au kugombania kazi moja..Baraka za Mungu zipo na zinapatikana hata kama wewe si kiongozi Kanisani..Na silazima ukafanye kazi inayoonekana na watu wengi ili upate sifa hapa Duniani..Kazi yako inawezekana isionekane zaidi machoni mwa Wanadamu na hata ikaonekana haifai na wakaidharau..Lakini Mungu wetu Baba wa Mbinguni yeye akiibariki nawe utabarikiwa..Mungu alitupa bure nasi tukatumike na kujitoa sawasawa na mapenzi yake..Tukawe wakarimu na wanyenyekevu katika kujitoa kwetu..



Kumbukeni: “Apandaye kidogo huvuna kidogo; apandaye kwa wingi huvuna kwa wingi.” Kila mmoja, basi, na atoe kadiri alivyoamua, kwa moyo na wala si kwa huzuni au kwa kulazimishwa, maana Mungu humpenda yule mwenye kutoa kwa furaha. Mungu anaweza kuwapeni nyinyi zaidi ya yale mnayoyahitaji, mpate daima kuwa na kila kitu mnachohitaji, na hivyo mzidi kusaidia katika kila kazi njema. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Yeye hutoa kwa ukarimu, huwapa maskini; wema wake wadumu milele.” Na Mungu ampaye mkulima mbegu na mkate kwa chakula, atawapa nyinyi pia mbegu mnazohitaji, na atazifanya ziote, zikue na kuwapa mavuno mengi ya ukarimu wenu. Yeye atawatajirisha nyinyi daima kwa kila kitu, ili watu wapate kumshukuru Mungu kwa ajili ya zawadi zenu wanazozipokea kwa mikono yetu. Maana huduma hii takatifu mnayoifanya si kwamba itasaidia mahitaji ya watu wa Mungu tu, bali pia itasababisha watu wengi wamshukuru Mungu. Kutokana na uthibitisho unaooneshwa kwa huduma hii yetu, watu watamtukuza Mungu kwa sababu ya uaminifu wenu kwa Habari Njema ya Kristo mnayoiungama, na pia kwa sababu ya ukarimu mnaowapa wao na watu wote. Kwa hiyo watawaombea nyinyi kwa moyo kwa sababu ya neema ya pekee aliyowajalieni Mungu. Tumshukuru Mungu kwa ajili ya zawadi yake isiyo na kifani!

Tazama wenye shida/tabu,waliomagerezani pasipo na hatia,waliokatika vifungo vya mwovu,wagonjwa, wafiwa ukawe mfariji wao..waliokataliwa,waliokata tamaa,wenye hofu/mashaka,wanaougua rohoni,Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaguse na mkono wako wenye nguvu, UKawaponye na kuwaokoa.. wapate kupona kimwili na kiroho pia..Baba wa mbinguni ukaonekane kwenye mapito yao..

Tunaweka haya yote mikononi mwako Baba wa mbinguni..
kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na utukufu hata milele..

Amina..!
Asanteni wote kwakupita hapa..
Mungu akawabariki katika yote na akawape sawasawa na mapenzi yake..
Nawapenda.


Mavazi ya makuhani: Kizibao

(Kut 28:1-14)
1Kwa kutumia sufu ya rangi ya buluu, ya zambarau na nyekundu walifuma sare za kuvaa wakati wa kuhudumu mahali patakatifu. Walimshonea Aroni mavazi matakatifu kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.
2Walitengeneza kizibao kwa nyuzi za dhahabu, kwa sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kwa kitani safi iliyosokotwa. 3Waliifua dhahabu na kuikata katika nyuzi nyembamba ili kuzifuma pamoja na sufu ya rangi ya buluu, ya zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa kwa ustadi. 4Kizibao hicho kilivaliwa kwa kamba mbili mabegani zilizoshonewa kwenye ncha zake mbili. 5Mkanda uliofumwa kwa ustadi juu yake ili kuifungia ulikuwa kitu kimoja na kizibao hicho, na ulitengenezwa kwa vitu hivyohivyo: Dhahabu, sufu ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.
6Kisha waliandaa vito vya sardoniki na kuvipanga katika vijalizo vya dhahabu; navyo vilichorwa, kama mtu achoravyo mhuri, majina kumi na mawili ya wana wa Israeli. 7Waliviweka vito hivyo katika kanda za mabegani za kile kizibao ili kuwakilisha makabila kumi na mawili ya Israeli, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.

Kifuko cha kifuani

(Kut 28:15-30)

8Mafundi walitengeneza kifuko cha kifuani kama vile walivyokitengeneza kile kizibao, kwa dhahabu, kwa sufu ya rangi ya buluu, rangi zambarau na nyekundu, na kwa kitani safi iliyosokotwa. 9Kifuko hicho kilikuwa cha mraba, sentimita 22 kwa sentimita 22 nacho kilikunjwa. 10Kifuko hicho kilipambwa kwa safu nne za mawe ya thamani; safu ya kwanza ilikuwa ya akiki, topazi na almasi nyekundu; 11safu ya pili ilikuwa ya zumaridi, na johari ya rangi ya samawati na almasi; 12safu ya tatu ilikuwa ya yasintho, ya akiki nyekundu na amethisto; 13na safu ya nne ilikuwa ya zabarajadi, ya shohamu na yaspi; yote yalimiminiwa vijalizo vya dhahabu. 14Basi, palikuwa na mawe kumi na mawili yaliyochorwa majina kumi na mawili ya wana wa Israeli. Yalikuwa yamechorwa kama wachoravyo mhuri, kila moja limechorwa jina kuwakilisha makabila kumi na mawili. 15Walikitengenezea kile kifuko cha kifuani mikufu ya dhahabu safi. 16Walitengeneza vijalizo viwili vya dhahabu safi na pete mbili za dhahabu, na kuzitia pete hizo kwenye ncha mbili za juu za kifuko hicho. 17Mikufu hiyo miwili ya dhahabu waliifunga kwenye pete hizo za kifuko cha kifuani. 18Zile ncha mbili za mikufu ya dhahabu walizitia kwenye vile vijalizo viwili wakazishikamanisha na vile vipande viwili vya mabegani vya kizibao, upande wa mbele. 19Walitengeneza pete mbili za dhahabu, wakazitia penye ncha mbili za chini upande wa ndani wa kifuko hicho cha kifuani karibu na kizibao. 20Walitengeneza pete nyingine mbili za dhahabu na kuzitia mbele katika ncha za chini za vipande vya kizibao, mahali kinapoungana na ule mkanda uliofumwa kwa ustadi. 21Walifunga kifuko cha kifuani kwenye kizibao kwa kufunganisha pete zake na kizibao kwa kamba ya rangi ya buluu, ili kifuko hicho kisilegee ila kikalie ule mkanda uliofumwa kwa ustadi, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.

Mavazi mengine ya kikuhani

(Kut 28:31-43)

22Alitengeneza kanzu ya kuvaa ndani ya kizibao ya rangi ya buluu. 23Joho hilo lilikuwa na nafasi ya kupitishia kichwa katikati, nayo ilizungushiwa utepe uliofumwa ili isichanike. 24Kwenye upindo wa chini wa kanzu walifuma mapambo ya makomamanga ya rangi ya buluu, ya zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa. 25Kisha walitengeneza njuga za dhahabu, na kila baada ya komamanga walitia njuga kwenye upindo wa joho. 26Hivyo, njuga na komamanga vilifuatana kuuzunguka upindo wa joho hilo, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.
27Kisha wakawafumia Aroni na wanawe vizibao vya kitani safi, 28kilemba cha kitani safi, kofia za kitani safi, suruali za kitani safi iliyosokotwa, 29na mikanda ya kitani safi iliyosokotwa kwa sufu ya rangi ya buluu, ya zambarau na nyekundu na kuitarizi vizuri, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.
30Kisha walitengeneza pambo la dhahabu safi kwa ajili ya taji takatifu na kuchora juu yake kama wachoravyo mhuri, “Wakfu kwa Mwenyezi-Mungu.” 31Kisha wakalifunga mbele ya kile kilemba kwa ukanda wa rangi ya buluu, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.

Kukamilika kwa kazi

(Kut 35:10-19)

32Basi, kazi yote ya hema la mkutano ikamalizika. Waisraeli walifanya yote kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. 33Wakamletea Mose hema takatifu pamoja na vyombo vyake vyote, vikonyo vyake, mbao zake, pau zake, nguzo zake na vikalio vyake; 34kifuniko cha ngozi za kondoo dume na mbuzi kilichotiwa rangi nyekundu, pazia la mahali patakatifu, 35sanduku la agano, mipiko yake na kiti cha rehema; 36meza na vyombo vyake vyote, mikate iliyowekwa mbele ya Mungu; 37kinara cha taa cha dhahabu safi, taa zake, vyombo vyake vyote pamoja na mafuta kwa ajili ya taa hizo; 38madhabahu ya dhahabu; mafuta ya kupaka, ubani wenye harufu nzuri, na pazia la mlango wa hema; 39madhabahu ya shaba na wavu wake wa shaba, mipiko yake na vyombo vyake vyote; bakuli, birika na tako lake; 40vyandarua vya ua, nguzo zake na vikalio vyake; pazia la mlango wa ua, kamba zake na vigingi vyake; vyombo vyote vilivyohitajika katika huduma ya hema takatifu, yaani hema la mkutano; 41na mavazi yote yaliyofumwa vizuri kabisa kwa ajili ya huduma ya mahali patakatifu, yaani mavazi matakatifu ya kuhani Aroni, na ya wanawe kwa ajili ya huduma ya ukuhani. 42Waisraeli walifanya kila kitu kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. 43Mose alikagua kila kitu, akaridhika kwamba walikuwa wamefanya kila kitu kama Mwenyezi-Mungu alivyoamuru. Hivyo Mose akawabariki.


Kutoka39;1-43

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Tuesday 23 May 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Kutoka 38...

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Asante Baba wa mbinguni,Mungu wetu,Muumba wetu,Muumba Mbingu na Nchi na vyote vilivyomo,Baba wa Yatima,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..Yahweh..!Jehovah nissi..! Jehovah Jireh..! Jehovah Shammah..!Jehovah Rapha..!Jehovah Shalom..!El Shaddai..!!
Asante kwa ulinzi wako na kutuamsha salama..
Asante kwakutupa kibali cha kuendelea kuiona siku hii..

Tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza na kujiachilia mikononi mwako Mfalme wa Amani..
Tunaomba utusamehe pale tulipokwenda kinyume nawe Baba wa mbinguni..
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua Mungu wetu..
Tunaomba nasi utupe Neema ya kuweza kuwasamehe waliotukosea..
Utuepushe  majaribuni Baba wa Mbinguni na utuokoe na yule Mwovu na kazi zake..

Ututakase  Miili yetu na Akili zetu Yahweh kwa Damu ya Mwanao mpendwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote tupate kutambua/kujitambua na tukawe na kiasi..
Tunauweka Mji huu tunaoshi na Nchi hii yote mikononi mwako Baba wa Mbiguni. ukatuokoe na hatari zozote zilizopangwa na ukatamalaki na kutuatamia yahweh..!Utuokoe na njama,ukabila,udini na Amani ikatawale Jehovah..!Ukaibariki Nchi hii na watu wote tunaoshi hapa ukatufunike na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo..
Tunaiweka "MANCHESTER" Mikononi mwako Baba wa mbingu ukawe mfariji kwa waliopoteza wapendwa wao..Ukawaguse na mkono wako wenye nguvu na  kuwaponya wote waliojeruhiwa..Ukatupe uvumilivu na hekima katika wakati huu mgumu..Mungu wetu ukatupe ulinzi na ukawape mwanga,umakini na uelewa wote wanaofuatilia jambo hili..


Mwenyezi-Mungu asipoijenga nyumba, waijengao wanajisumbua bure. Mwenyezi-Mungu asipoulinda mji, waulindao wanakesha bure.

Asante kwakuwa wewe ni Mungu  unayeweza yote,Asante kwa uwepo wako,Asante kwa wema na Fadhili zako..
Asante kwa Kazi zetu,Biashara,Masomo..Tunaomba ukavibariki na kutubariki katika yote..Tumaini la kweli lipo kwako, Upendo wa kweli una wewe Baba wa Mbinguni, Faraja ina wewe,Amani inapatikana kwako, Wokovu una wewe,Furaha iko kwako Baba wa Mbinguni..

Tunayaweka haya yote mikononi mwako Tukishukuru na kuamini wewe ni Mungu wetu na vyote vinapatika kwako..
Kwakua ufalme ni wako nguvu na Utukufu hata milele..
Amina..!
Asanteni wote mnaotembelea hapa..
Mungu akawe nanyi Daima na akawape sawasawa na mapenzi yake..
Nawapenda.

Madhabahu ya kuteketezea tambiko na birika la shaba

(Kut 27:1-8; 30:18)

1Alitengeneza madhabahu kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa. Madhabahu hiyo ilikuwa ya mraba, mita mbili na robo kwa mita 2.25, na kimo chake mita 1.25. 2Katika kila pembe ya madhabahu hiyo alitengeneza upembe uliokuwa umeundwa kutokana na madhabahu yenyewe. Madhabahu hiyo yote aliipaka shaba. 3Alitengeneza pia vyombo vyote kwa ajili ya madhabahu: Vyungu, sepetu, mabirika, nyuma na visahani vya kuchukulia moto. Vyombo vyake vyote alivitengeneza kwa shaba. 4Alitengeneza wavu wa shaba, akautia chini ya ukingo wa madhabahu hadi katikati ya madhabahu. 5Katika pembe nne alitengeneza pete nne za kuibebea hiyo madhabahu. 6Alitengeneza mipiko ya mjohoro na kuipaka shaba. 7Aliitia ile mipiko katika zile pete zilizokuwa kando ya madhabahu ili kuibebea. Madhabahu hiyo iliyotengenezwa kwa mbao ilikuwa na mvungu ndani.

Ua wa hema la mkutano

(Kut 27:9-19)

8 Taz Kut 30:18 Kisha alitengeneza birika la shaba na tako lake la shaba; birika hilo lilitengenezwa kwa kutumia vioo vya shaba vya wanawake waliohudumu penye lango la hema la mkutano.
9Kisha alilitengenezea ua. Vyandarua vya upande wa kusini wa ua vilikuwa vya kitani safi iliyosokotwa na vyenye urefu wa mita 44; 10navyo vilishikiliwa na nguzo ishirini za shaba zenye vikalio ishirini vya shaba. Lakini kulabu za nguzo hizo na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha. 11Upande wa kaskazini urefu wa chandarua ulikuwa mita 44, na nguzo zake 20 za shaba, lakini kulabu za nguzo hizo na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha. 12Upande wa magharibi ulikuwa na chandarua chenye urefu wa mita 22, nguzo zake 10 na vikalio vyake 10. Kulabu za nguzo na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha. 13Upande wa mashariki, kulikokuwa na mlango, ulikuwa na upana wa mita 22. 14Chandarua cha kila upande wa mlango kilikuwa na upana wa mita 6.5, pamoja na nguzo tatu na vikalio vyake vitatu. 15Upande mwingine kadhalika ulikuwa na chandarua chenye upana wa mita 6.5, pamoja na nguzo tatu na vikalio vyake vitatu. 16Vyandarua vyote kuuzunguka ua vilikuwa vya kitani safi iliyosokotwa. 17Vikalio vyote vya nguzo vilikuwa vya shaba, lakini kulabu za nguzo hizo na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha. Matumba yake yalikuwa ya fedha; pia nguzo zake zote zilishikamanishwa kwa fito za fedha. 18Pazia la mlango wa ua lilitengenezwa kwa sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa, na kutariziwa vizuri; nalo lilikuwa na urefu wa mita 9 na kimo cha mita 2, kulingana na vyandarua vya ua. 19Pia nguzo zake zilikuwa nne na vikalio vinne vya shaba. Kulabu zake zilikuwa za fedha, hata nguzo zake na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha. 20Vigingi vyote vya hema na vya ua kandokando ya hema vilikuwa vya shaba.

Vyombo vya hema

21Ifuatayo ni orodha ya vifaa vilivyotumika katika kulijenga hema takatifu, yaani hema la agano. Orodha hii ilitayarishwa na Walawi kwa amri ya Mose, chini ya uongozi wa Ithamari, mwana wa kuhani Aroni.
22Bezaleli, mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda, alifanya kila kitu ambacho Mwenyezi-Mungu alimwamuru Mose. 23Alisaidiwa na Oholiabu mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani, fundi stadi wa kutia nakshi, kusanii michoro na kutarizi kwa nyuzi za sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu na kitani safi iliyosokotwa.
24Dhahabu yote waliyomtolea Mwenyezi-Mungu kwa ajili ya ujenzi wa hema takatifu ilikuwa na uzito wa kilo 877 na gramu 300 kulingana na vipimo vya hema takatifu. 25Fedha waliyochanga hao watu wa jumuiya waliohesabiwa ilikuwa ya uzito wa kilo 3,017 na gramu 750 kulingana na vipimo vya hema takatifu. 26Kila mtu aliyehesabiwa tangu umri wa miaka ishirini na moja na zaidi alitoa mchango wake wa fedha gramu 5; na wanaume wote waliohesabiwa walikuwa 603,550. 27Kilo 3,000 za fedha zilitumika kutengenezea vile vikalio 100 vya hema takatifu na lile pazia, yaani kilo 30 kwa kila kikalio. 28Zile kilo 17 na gramu 75 zilizosalia, zilitumika kutengenezea kulabu za nguzo na kuvipaka vichwa vya nguzo na kuitengenezea vitanzi. 29Jumla ya mchango wa shaba Waisraeli waliomtolea Mwenyezi-Mungu ilikuwa na uzito wa kilo 2124. 30Bezaleli aliitumia shaba hiyo kutengenezea vikalio vya mlango wa hema la mkutano, madhabahu ya shaba pamoja na wavu wake wa shaba, vyombo vyote vya madhabahu, 31vikalio vya ua uliolizunguka hema la mkutano na vya lango la ua, na vigingi vyote vya hema takatifu na vya ua.

Kutoka38;1-31

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Monday 22 May 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Kutoka 37...

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tumshukuru Mungu wetu katika roho na kweli..

Asante Baba yetu, Mungu wetu, Muumba wetu,Muumba Mbingu na Nchi na vyote vilivyomo, Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Asante kwa wema na fadhili zako, Asante kwa ulinzi wako usiku wote na umetuamsha salama..Asante kwa ulinzi wako siku zote..
Tazama Jana imepita Baba wa Mbingu, Leo ni siku Mpya na Kesho ni siku nyingine..
Asante kwa kutupa Kibali na kutuchagua kuendelea kuiona leo/wiki hii..
Si kwa uwezo wetu Baba wa mbinguni ni kwa Neema/Rehema zako tuu..
Tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza na kujiachilia mikononi mwako Mfalme wa Amani..
Tunaomba utusamehe pale tulipokwenda kinyume nawe Jehovah..!

kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua,kutojua..
Baba wa Mbinguni nasi ukatupe Neema ya kuweza kuwasamehe waliotukosea..
Mungu wetu ukatuokoe na yule mwovu na kazi zake zote ..
Ukatufunike na Kututakasa Miili yetu Na Akili zetu kwa Damu ya Mwanao mpendwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka ili sisi tupate kupona..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..
Mfalme wa Amani ukatawale Maisha yetu na ukabariki Kazi zetu, Biashara,Masomo,vilaji/vinywaji,Tuingiapo/tutokapo,vyombo vya usafiri na tutembeapo hatua zetu ziwe nawe Jehovah..!Baba wa Mbingu ukavitakase vyote tunavyoenda kugusa/kutumia kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo..
Tazama wenye Shida/tabu, wagonjwa,wafiwa,waliokata tamaa, waliokataliwa,wenyehofu/mashaka,waliopoteza matumaini..
Mfamle wa Amani, Mungu wetu tunaomba ukawaguse na mkono wako wenye nguvu,ukawaponye kiroho na kimwili pia,ukaonekane kwenye mapito/majaribu na magumu yao..


Mfalme wa Amani ukatawele Nyumba zetu,Ndoa zetu,familia zetu ..Eeh-Mungu wetu Ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia..
Tupate kutambua na kujitambua.. tukawe  chombo chema na tukatumike sawasawa na mapenzi yako..
Ukatuongoze katika maamuzi yetu, tukasimamie Neno lako, tukawe na hekima,Busara na tusiyumbishwe na Dunia hii yenye mambo mengi  na tukawe na kiasi..

Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwuliza, “Kwa nini unasema na watu kwa mifano?” Yesu akawajibu, “Nyinyi mmejaliwa kuzijua siri za ufalme wa mbinguni, lakini wao hawakujaliwa. Maana, aliye na kitu atapewa na kuzidishiwa; lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa. Ndio maana ninasema nao kwa mifano, kwa sababu wanatazama lakini hawaoni, wanasikiliza lakini hawasikii, wala hawaelewi. Kwao yametimia yale aliyosema nabii Isaya: ‘Kusikia mtasikia, lakini hamtaelewa. Kutazama mtatazama, lakini hamtaona. Maana akili za watu hawa zimepumbaa, wameyaziba masikio yao, wameyafumba macho yao. La sivyo, wangeona kwa macho yao, wangesikia kwa masikio yao, wangeelewa kwa akili zao, na kunigeukia, asema Bwana, nami ningewaponya.’ “Lakini heri yenu nyinyi, maana macho yenu yanaona na masikio yenu yanasikia. Kweli nawaambieni, manabii na watu wengi wema walitamani kuyaona yale mnayoyaona, wasiyaone, na kuyasikia yale mnayoyasikia, wasiyasikie.

Sifa na utukufu ni kwako daima..
Tunayaweka haya yote mikononi mwako..

kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata millele..
Amina..!
Asanteni sana wapendwa/waungwana mliopitia hapa/mnaoendelea kupitia hapa..Mungu aendelee kuwabariki katika safari yenu ya maisha..
msipungukiwe mahitaji yenu na Mungu akawape sawasawa na mapezni yake..
Nawapenda.

Kutengeneza sanduku la agano

(Kut 25:10-22)

1Bezaleli alitengeneza sanduku kwa mbao za mjohoro; urefu wake ulikuwa sentimita 110, upana sentimita 66, na kimo chake sentimita 66. 2Alilipaka dhahabu safi ndani na nje, na kulifanyia ukingo wa dhahabu pande zote. 3Kisha alitengeneza pete nne za dhahabu za kulibebea, akazitia kwenye pembe zake, kila pembe pete moja. 4Alitengeneza mipiko ya mjohoro na kuipaka dhahabu. 5Mipiko hiyo akaipitisha katika zile pete zilizo katika pande mbili za sanduku, kwa ajili ya kulibebea. 6Alitengeneza kiti cha rehema37:6 kiti cha rehema: Taz 25:17 cha dhahabu safi; urefu wake sentimita 110, na upana wake sentimita 66. 7Alitengeneza pia viumbe wenye mabawa wawili kwa kufua dhahabu kwenye miisho ya kifuniko hicho; 8kiumbe kimoja mwisho huu na kingine mwisho mwingine. Alitengeneza viumbe hivyo vyenye mabawa kwenye miisho ya kifuniko hicho, vikiwa kitu kimoja na kifuniko. 9Viumbe hivyo vilikuwa vimeelekeana, mabawa yao yamekunjuliwa kukifunika kifuniko cha sanduku; nyuso zao zilikielekea kifuniko cha sanduku.

Meza ya mikate ya dhabihu

(Kut 25:23-30)

10Vilevile alitengeneza meza ya mjohoro yenye urefu wa sentimita 88, upana sentimita 44, na kimo chake sentimita 66. 11Aliipaka dhahabu safi na kuitengenezea ukingo wa dhahabu. 12Aliizungushia mviringo wa ubao wenye upana wa milimita 75, na kuifanyia ukingo wa dhahabu. 13Aliitengenezea pete nne za dhahabu na kuzitia katika pembe zake nne mahali miguu ilipoishia. 14Pete hizo za kushikilia ile mipiko ya kulibebea ziliwekwa karibu na ule mviringo wa ubao. 15Alitengeneza mipiko miwili ya mjohoro ya kulibebea, akaipaka dhahabu. 16Alitengeneza vyombo vya dhahabu safi vya kuweka juu ya meza: Sahani zake na visahani kwa ajili ya ubani, na bilauri zake na bakuli kwa ajili ya tambiko za kinywaji.

Kinara cha taa

(Kut 25:31-40)

17Alitengeneza pia kinara cha taa kwa dhahabu safi. Tako lake, na ufito wa hicho kinara ulikuwa kitu kimoja pamoja na vikombe vyake, matumba yake na maua yake. 18Matawi sita yalitokeza kila upande wa ufito wake, matawi matatu upande mmoja na matawi matatu upande mwingine. 19Katika kila tawi kulikuwa na vikombe vitatu mfano wa maua ya mlozi, kila kimoja na tumba lake na ua lake. 20Na katika ufito kulikuwa na vikombe vinne mfano wa maua ya mlozi, pamoja na matumba yake na maua yake. 21Mahali pale palipotokezea jozi tatu za matawi chini ya kila jozi kulikuwa na tumba moja. 22Matumba hayo na matawi vilikuwa kitu kimoja na kinara hicho, na chote kilifuliwa kwa dhahabu safi. 23Alikitengenezea taa saba, koleo na visahani vyake kwa dhahabu safi. 24Alikitengeneza kinara hicho na vifaa vyake kwa kilo thelathini na tano za dhahabu.

Madhabahu ya kufukizia ubani

(Kut 30:1-5)

25Alitengeneza madhabahu ya kufukizia ubani kwa mbao za mjohoro. Madhabahu hiyo ilikuwa ya mraba, sentimita 45 kwa sentimita 45, na kimo chake sentimita 90. Pembe za madhabahu hiyo zilikuwa kitu kimoja na madhabahu yenyewe. 26Yote aliipaka dhahabu safi: Upande wake wa juu, pande zake za ubavuni na pembe zake; pia aliitengenezea ukingo wa dhahabu. 27Alitengeneza pete mbili za dhahabu chini ya ukingo kwenye pande mbili zinazokabiliana. Pete hizo zilitumika kushikilia mipiko ya kuibebea. 28Alifanya mipiko miwili ya mjohoro na kuipaka dhahabu.
29 Taz Kut 30:22-38 Alitengeneza mafuta matakatifu ya kupaka, na ubani safi wenye harufu nzuri uliochanganywa vizuri kama manukato.

Kutoka37;1-29

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Friday 19 May 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Kutoka 36...

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tumshukuru Mungu wetu ..
Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na Fadhili zako..
Asante kwakutulinda usiku wote na kutuamsha tukiwa salama..
Asante kwa siku hii mpya..Asante kwa kutupa kibali cha kuendelea kuiona..
Asante kwa uzima na Afya tulizonazo..Baba wa Mbinguni umetupa kwa Neema/ Rehema zako, sisi ni nani Baba mbele zako si kwanguvu zetu au kujua kwetu ni kwa mapenzi yako Yahweh..!

Tunashuka mbele zako Baba wa Mbinguni tukijinyenyekeza na kujiachilia mikononi mwako Jehovah..!!
Tunaomba utusamehe pale tulipo kwenda kinyume nawe Mungu wetu kwa kuwaza,kwakunena,kwakutenda, kwakujua/kutojua..
Mfalme wa Amani tunaomba nasi utupe Neema ya kuweza kuwasamehe waliotukosea..

Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote tupate kutambua/kujitambua na tukawe na kiasi..

Yahweh..! Tunaomba utupe Hekima, Busara,Upendo wa kweli,Huruma, tuweze kuwasaidia wenye kuhitaji .Tusiwe wenye kujisifu/kujivuna/kujitapa/kujikweza,wenye kiburi, tukawe salama moyoni , Tukawe barua njema na tukasomeke popote tutakapo pita, ikiwa kazini,ikiwa kanisani,ikiwa shuleni,ikiwa safarini na kwenye maisha yetu yote...Baba wa Mbinguni ukatuongoze na tukawe na kiasi,Tusaidiane,Tuchukuliane/Tuvumiliane,Tuheshimiane,Tuelimishane kwa Upendo na utaratibu na Tuombeane ..

Tuvumiliane na kusaidiana
Ndugu, kama mkimwona mtu fulani amekosea, basi, nyinyi mnaoongozwa na Roho mwonyeni mtu huyo ajirekebishe; lakini fanyeni hivyo kwa upole, mkiwa na tahadhari msije nanyi wenyewe mkajaribiwa. Saidianeni kubeba mizigo yenu na hivyo mtatimiza sheria ya Kristo. Mtu akijiona kuwa ni kitu, na kumbe si kitu, huyo anajidanganya mwenyewe. Lakini kila mmoja na aupime vizuri mwenendo wake mwenyewe. Ukiwa mwema, basi, anaweza kuona fahari juu ya alichofanya bila kuwa na sababu ya kujilinganisha na mtu mwingine. Maana kila mmoja anapaswa kuubeba mzigo wake mwenyewe. Mwenye kufundishwa neno la Mungu na amshirikishe mwalimu wake riziki zake. Msidanganyike; Mungu hafanyiwi dhihaka. Alichopanda mtu ndicho atakachovuna. Apandaye katika tamaa za kidunia, atavuna humo uharibifu; lakini akipanda katika Roho, atavuna kutoka kwa Roho uhai wa milele. Basi, tusichoke kutenda mema; maana tusipolegea tutavuna mavuno kwa wakati wake. Kwa hiyo, tukiwa bado na wakati, tuwatendee watu wote mema, na hasa ndugu wa imani yetu.


Asante kwakuwa wewe ni Mungu wetu  unatosha maishani.. 

Kwako wewe hakuna linaloshindikana..
Ukatubariki tuingiapo/tutokapo,Kazi zetu,Biashara,Masomo,vilaji/vinywaji,vyombo vya usafiri na tutembeapo hatua zetu ziwe nawe Jehovah.!
Vyote tunavyoenda kugusa kutumia Baba wa Mbinguni tunaomba ukavitakase na Damu ya mwanao mpendwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo yeye aliteseka ili sisi tuapate kupona..
Mungu wetu ukatutakase Miili yetu na Akili zetu na ukatufunike na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo..
Tunayaweka haya yote mikononi mwako..

Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!
Asanteni wapendwa mnaotembelea hapa..Mungu aendelee kuwabariki na kuwatendea sawasawa na mapenzi yake..
Nawapenda.



1“Bezaleli na Oholiabu, pamoja na kila mwanamume ambaye Mwenyezi-Mungu amemjalia uwezo na akili ya kujua namna ya kufanya kazi zote katika ujenzi wa hema takatifu, atafanya kazi kulingana na yote ambayo Mwenyezi-Mungu aliamuru.”

Matoleo kwa wingi
2Mose alimwita Bezaleli na Oholiabu na kila mtu ambaye alikuwa amejaliwa ujuzi na Mwenyezi-Mungu, na kila mtu ambaye moyo wake ulimsukuma kufanya kazi kwa hiari. 3Hao wakapokea kutoka kwa Mose vitu vyote vilivyotolewa na Waisraeli kwa hiari kwa ajili ya kazi ya hema takatifu. Watu waliendelea kumletea michango yao ya hiari kila asubuhi. 4Watu wote wenye ujuzi waliokuwa wanafanya kazi za kila namna za kujenga hema la mkutano walitoka, kila mmoja katika kazi yake, wakamwendea 5Mose na kumwambia, “Watu wameleta vitu vingi zaidi ya vile vinavyohitajiwa kwa kazi aliyotuagiza Mwenyezi-Mungu tuifanye.” 6Basi, Mose akaagiza: “Mtu yeyote, awe mwanamume au mwanamke, asilete mchango zaidi kwa ajili ya hema takatifu.” Watu wakazuiwa kuleta vitu, 7maana vile walivyokuwa wameleta vilitosha kwa kazi hiyo na kubaki.

Kutengeneza hema takatifu

(Kut 26:1-37)
8Wanaume wote wenye ujuzi walitengeneza hema takatifu kwa mapazia kumi ya kitani safi iliyosokotwa, na kwa sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kuyatarizi viumbe wenye mabawa. 9Urefu wa kila pazia ulikuwa mita 12 na upana mita 2. Mapazia yote yalikuwa ya kipimo kimoja.
10Aliyaunga36:10 Aliyaunga: Hapa, Kiebrania ni umoja, yaani huenda ikawa anayeongoza kazi hiyo ni Mose. mapazia matano kufanya kipande kimoja na kufanya vivyo hivyo na yale mengine matano. 11Alitengeneza vitanzi vya buluu upindoni mwa pazia la mwisho la kipande cha kwanza, na vitanzi vingine katika pazia la mwisho la kipande cha pili. 12Alitia vitanzi hamsini katika pazia la kwanza la kipande cha kwanza, na vitanzi hamsini kwenye utepe wa pazia la pili; vitanzi vyote vilielekeana. 13Kisha alitengeneza vifungo hamsini vya dhahabu ili kuunganishia vile vipande viwili vya mapazia; hivyo, hema likawa kitu kimoja.
14Kisha alitengeneza pia kifuniko cha hema kwa mapazia kumi na moja ya manyoya ya mbuzi. 15Kila pazia lilikuwa na urefu wa mita 13, na upana wa mita 2. Mapazia yote 11 yalikuwa ya kipimo kilekile. 16Basi, akayaunganisha mapazia matano pamoja, na mapazia sita pamoja. 17Kisha alifanya vitanzi hamsini upindoni mwa pazia la mwisho la kipande cha kwanza, na vitanzi hamsini upindoni mwa kipande cha pili. 18Halafu akatengeneza vifungo hamsini vya shaba ili kuunganishia vile vipande viwili vya mapazia, na hivyo kufanya pazia moja la hema. 19Kisha alitengeneza kifuniko cha ngozi laini ya kondoo dume, na juu yake kifuniko kingine cha ngozi laini ya mbuzi.
20Halafu akalitengenezea hema mbao za mjohoro za kusimama wima. 21Kila ubao ulikuwa na urefu wa mita 4 na upana wa sentimita 66. 22Kila ubao ulikuwa na ndimi mbili za kuunganishia. Mbao zote za hema alizifanyia ndimi. 23Mbao hizo za hema zilitengenezwa hivi: Mbao ishirini upande wa kusini, 24na vikalio arubaini vya fedha chini ya hizo mbao 20; vikalio viwili chini ya kila ubao ili kushikilia zile ndimi zake mbili. 25Na upande wa pili, yaani kaskazini mwa hema, alitengeneza pia mbao ishirini, 26na vikalio vyake arubaini vya fedha; vikalio viwili chini ya kila ubao. 27Upande wa nyuma, yaani magharibi mwa hema, alitengeneza mbao sita. 28Alitengeneza pia mbao mbili kwa ajili ya pembe za hema upande wake wa nyuma. 29Mbao hizo mbili za pembeni ziliachana chini lakini zilishikamanishwa kwenye pete ya kwanza. Mbao mbili kwa ajili ya hizo pembe mbili zilitengenezwa namna hiyo. 30Hivyo kulikuwa na mbao nane na vikalio vyake vya fedha kumi na sita, vikalio viwili chini ya kila ubao.
31Alitengeneza pia pau za mjohoro: Pau tano kwa ajili ya mbao za upande mmoja wa hema, 32pau tano kwa ajili ya upande wa pili wa hema, na pau tano kwa ajili ya mbao za upande wa nyuma wa hema, ulio magharibi. 33Alitengeneza upau wa katikati uliofika nusu ya jengo la hema ambao ulipenya katikati kutoka mwisho hadi mwisho. 34Mbao zote alizipaka dhahabu, akazitengeneza na pete za dhahabu za kushikilia pau hizo ambazo pia alizipaka dhahabu.
35Alitengeneza pazia la nyuzi za rangi ya buluu, zambarau na nyekundu na kitani safi iliyosokotwa. Pazia hilo lilitariziwa viumbe wenye mabawa kwa ustadi. 36Alitengeneza nguzo nne za mjohoro, akazipaka dhahabu na kuzitilia kulabu za dhahabu. Vilevile alizifanyia vikalio vinne vya fedha. 37Kadhalika, kwa ajili ya mlango wa hema, alitengeneza pazia kwa nyuzi za rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa, nalo pazia lilitariziwa vizuri, 38na nguzo zake tano zikiwa na kulabu. Matumba yake na vifungo vyake alivipaka dhahabu, lakini vikalio vyake vitano vilikuwa vya shaba.

Kutoka36;1-38

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Thursday 18 May 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Kutoka 35...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Haleluyah..!! Mungu wetu yu mwema sana..
Asante Baba wa Mbinguni kwa kutuamsha salama na kutupa Kibali cha kuendelea kuiona leo hii..
Si kwa uwezo wetu wala nguvu zetu, si kwamba sisi ni wema sana na wazuri mno zaidi ya wengine walioshindwa kuamka leo hii..
Ni kwa Neema/Rehema zako tuu Mungu wetu..
Tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza na kujiachilia mikononi mwako Mfalme wa Amani..
Tunaomba utusamehe pale tulipokwenda kinyume nawe..kwa kuwaza,kwakunena, kwakutenda, kwakujua/kutojua..

Tunaomba nasi utupe Neema ya kuweza kuwasamehe waliotukosea..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..


Tazama Jana imepita Baba wa Mbinguni Leo ni siku mpya na Kesho ni siku nyingine..
Tunaomba ukaibariki siku hii..
 Utulinde  na ukatuokoe na yule mwovu na kazi zake ..


Ukatutakase Miili yetu na Akili zetu kwa Damu ya Mwanao mpendwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti..


  Tunaomba ukabariki kazi zetu,Biashara, Masomo na ukabariki Vilaji/vinywaji,kuingia/kutoka kwetu, vyombo vya usafiri na tutembeapo hatua zetu ziwe nawe Yahweh..na vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba wa mbinguni ukavitakase na kuvifunika kwa Damu Ya Bwana we Yesu Kristo...


Tazama wenye shida/tabu Baba wa mbinguni, wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali, wagonjwa, wafiwa ukawe mfariji wao,waliokwenye vifungo mbalimbali Jehovah.. tunaomba ukawaguse na mkono wako wenye nguvu, wakapate uponyaji na wasipungukiwe katika mahitaji yao na ukawape sawasawa na mapenzi yako..

Jehovah tuwaweka watoto wetu wanaondelea na mitihani na wanaojiandaa na mitihani, Yahweh ukawape ufahamu  na uelewa,wapate  kukumbuka yote waliyofundishwa..
 Baba ukawaongoze katika makuzi yao na maisha yao, ukawaokoe na vishawishi na kufuata mkumbo..wakujue Mungu na kufuata njia iliyo njema..wakue kimwili, kimo na kiimani pia..


Yesu anawabariki watoto wadogo
(Mat 19:13-15; Luka 18:15-17)
Watu walimletea Yesu watoto wadogo ili awaguse, lakini wanafunzi wakawakemea. Yesu alipoona hivyo, alikasirika akawaambia, “Waacheni hao watoto waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana ufalme wa Mungu ni kwa ajili ya watu walio kama watoto hawa. Nawaambieni kweli, mtu yeyote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hataingia humo.” Kisha akawapokea watoto hao, akawawekea mikono, akawabariki.
Asante kwa sababu wewe ni Mungu wetu na Mlinzi wetu Mkuu, Asante kwa wema na fadhili zako, Asante kwa ridhiki zetu, Asante kwa yote Jehovah..!Maisha yetu yapo nawe Mfalme wa Amani, Upendo upo kwako Yahweh..!Ufalme wa Mbinguni una wewe Baba wa Mbinguni, Amani ipo kwako, Furaha na Ushindi  vipo nawe Jehovah nissi..!Tumaini la kweli lipo kwako Yahweh..Sifa na utukufu tunakurudishia wewe..
Tunashukuru na kuamini wewe ni Mungu wetu unayetosha..
Amina..!
Asanteni wote mnaopita hapa Mungu aendelee kuwabariki na kuwatendea sawasawa na mapenzi yake..

Nawapenda.


Kanuni za Sabato

1Mose alikusanya jumuiya yote ya Waisraeli, akawaambia, “Haya ndiyo mambo ambayo Mwenyezi-Mungu amewaamuru muyafanye: 2Taz Kut 20:8-11; 23:12; 31:15; 34:21; Lawi 23:3; Kumb 5:1-14 Kwa siku sita mtafanya kazi zenu; lakini siku ya saba ni Sabato siku ya mapumziko ambayo ni wakfu kwa Mwenyezi-Mungu. Yeyote atakayefanya kazi siku hiyo lazima auawe. 3Msiwashe hata moto katika makao yenu siku ya Sabato.”

Matoleo kwa ajili ya hema takatifu
(Kut 25:1-9)

4Mose aliiambia jumuiya yote ya Waisraeli, “Hili ndilo jambo ambalo Mwenyezi-Mungu amewaamuru mlifanye: 5Mtatoa katika mali zenu mchango wa kumpa Mwenyezi-Mungu. Kila mtu mwenye moyo mwema atamletea Mwenyezi-Mungu mchango: Dhahabu, fedha, shaba; 6sufu ya buluu, ya zambarau na nyekundu; kitani safi iliyosokotwa; manyoya ya mbuzi; 7ngozi za kondoo dume zilizotiwa rangi nyekundu, ngozi za mbuzi; mbao za mjohoro, 8mafuta kwa ajili ya taa, viungo kwa ajili ya mafuta ya kupaka na kwa ajili ya ubani wenye harufu nzuri; 9vito vya sardoniki na vito vingine kwa ajili ya mapambo ya kizibao na kifuko cha kifuani.

Vifaa vya hema takatifu
(Kut 39:32-43)

10“Kila mtu mwenye ujuzi wa kazi fulani miongoni mwenu atakuja kufanya vitu vyote alivyoamuru Mwenyezi-Mungu: 11Kutengeneza hema takatifu, kifuniko chake na pazia lake, kulabu zake, pau zake, vikalio vyake; 12sanduku la agano pamoja na mipiko yake, kiti cha rehema, pazia la mahali patakatifu sana; 13meza na mipiko yake pamoja na vyombo vyake vyote, mikate iliyowekwa mbele ya Mwenyezi-Mungu; 14vinara vya taa pamoja na vyombo vyake vyote, taa zake na mafuta yake; 15madhabahu ya ubani na mipiko yake, mafuta ya kupaka na ubani wenye harufu nzuri, pazia la mlango wa hema takatifu; 16madhabahu ya sadaka za kuteketezwa pamoja na wavu wa shaba, mipiko yake pamoja na vyombo vyake vyote, birika na tako lake; 17vyandarua vya ua, nguzo zake na vikalio vyake, pazia la mlango wa ua; 18vigingi vya hema takatifu na vya ua pamoja na kamba zake; 19mavazi yaliyofumwa vizuri kabisa kwa ajili ya huduma ya mahali patakatifu, yaani mavazi matakatifu ya kuhani Aroni na ya wanawe, kwa ajili ya huduma yao ya ukuhani.”

Watu wanaleta matoleo yao

20Basi, jumuiya yote ya Waisraeli ikaondoka mbele ya Mose. 21Kila mtu aliyevutwa na kusukumwa moyoni mwake alimtolea Mungu mchango wake kwa ajili ya hema la mkutano, huduma zake zote na mavazi yake matakatifu. 22Hivyo wote wenye moyo mkarimu, wanaume kwa wanawake, wakaleta vipini, pete za mhuri, vikuku na kila aina ya vyombo vya dhahabu; kila mtu akamtolea Mwenyezi-Mungu kitu cha dhahabu. 23Kila mtu alileta chochote alichokuwa nacho kama vile sufu ya rangi ya buluu zambarau na nyekundu, au kitani safi, au manyoya ya mbuzi au ngozi ya kondoo iliyotiwa rangi nyekundu. 24Kila mtu aliyeweza kutoa fedha au shaba aliileta kwa Mwenyezi-Mungu kama toleo lake. Tena mtu yeyote aliyekuwa na mbao za mjohoro alileta pia. 25Wanawake wote waliokuwa na ujuzi wa kufuma walileta vitu walivyofuma kwa sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu na kitani safi iliyosokotwa. 26Na wanawake wote waliokuwa na ujuzi walisokota manyoya ya mbuzi. 27Viongozi walileta vito vya rangi na mawe mengine kwa ajili ya kizibao na kifuko cha kifuani; 28walileta pia viungo na mafuta kwa ajili ya taa, mafuta ya kupaka na ubani wenye harufu nzuri. 29Waisraeli wote, wanaume kwa wanawake, ambao walivutwa moyoni mwao kuleta chochote kwa ajili ya kazi ambayo Mwenyezi-Mungu alikuwa amemwagiza Mose ifanyike, walileta vitu hivyo kwa hiari, kama mchango wa kumpa Mwenyezi-Mungu.

Mafundi kwa ajili ya hema la mkutano
(Kut 31:1-11)

30Mose aliwaambia Waisraeli; “Tazameni! Mwenyezi-Mungu amemteua Bezaleli, mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda. 31Amemjaza roho yake, amempa ujuzi, akili, maarifa na ufundi, 32abuni michoro ya sanaa na kufanya kazi za kufua dhahabu, fedha na shaba; 33achonge mawe ya kupambia na mbao kwa ajili ya kazi nyingine zote za kifundi. 34Pia amemwongoza yeye na Oholiabu, mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani wawafundishe wengine. 35Amewapa ujuzi wa kufanya kila kazi ya ufundi au ifanywayo na watu wa sanaa au mafundi wa kutarizi kwa sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu na kitani safi iliyosokotwa, kwa kutumia ufundi wowote wa msanii.

Kutoka35;1-35

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Wednesday 17 May 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Kutoka 34...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tumshukuru Mungu wetu...

Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na Fadhili zako, Asante kwa ulinzi wako na kutuamsha salama, Asante kwa kutupa Kibali cha kuendelea kuiona siku hii..
Tunakuja mbele zako Mungu wetu tukijinyenyekeza na kujiachilia mikononi mwako..
Tunaomba utusamehe pale tulipokwenda kinyume nawe kwa kuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Baba Mungu tunaomba nasi utupe Neema ya kuweza kuwasamehe walio tukosea..
Roho mtakatifu akatuongoze tupate kutambua na kujitambua na tuwe na kiasi..
Baba tunaomba utulinde na kutuokoa na yule mwovu na kazi zake zote..ukatutakase Miili yetu na Akili zetu na utufunike na Damu ya mwanao mpendwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka ili sisi tupate kupona..

Tunajua kwamba kila aliye mtoto wa Mungu hatendi dhambi, kwa sababu Mwana wa Mungu humlinda salama, na yule Mwovu hawezi kumdhuru. Tunajua kwamba sisi ni wake Mungu ingawa ulimwengu wote unatawaliwa na yule Mwovu. Twajua pia kwamba Mwana wa Mungu amekuja, akatupa elimu ili tumjue Mungu wa kweli; tuishi katika muungano na Mungu wa kweli – katika muungano na Mwanae, Yesu Kristo. Huyu ndiye Mungu wa kweli, na huu ndio uhai wa milele. Watoto wangu, epukaneni na sanamu za miungu!

Asante Mungu wetu kwa Upendo wako kwetu ,Nasi ukatupe moyo wa upendo kwa wengine, tukawe na upendo wa kweli..

Wapenzi wangu, tupendane, maana upendo hutoka kwa Mungu. Kila mtu aliye na upendo ni mtoto wa Mungu, na anamjua Mungu. Mtu asiye na upendo hamjui Mungu, maana Mungu ni upendo. Na Mungu alionesha upendo wake kwetu kwa kumtuma Mwanae wa pekee ulimwenguni, ili tuwe na uhai kwa njia yake. Hivi ndivyo upendo ulivyo: Si kwamba sisi tulikuwa tumempenda Mungu kwanza, bali kwamba yeye alitupenda hata akamtuma Mwanae awe sadaka ya kutuondolea dhambi zetu. Wapenzi wangu, ikiwa Mungu alitupenda hivyo, basi, nasi tunapaswa kupendana.

Asante kwa ridhiki zetu Baba wa Mbinguni tunaomba ukazibariki nasi tuweze kuwabariki wengine wenye kuhitaji..
Asante kwa kazi zetu,Biashara,Masomo tunaviweka mikononi mwako Baba wa mbinguni tunaomba ukabariki na kutuongoza vyema..
Mfalme wa Amani ukabariki tuingiapo/tutokapo, vilaji/vinywaji,vyombo vya usafiri na tutembeapo hatua zetu ziwe nawe Yahweh..!
Vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Jehovah..! Ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo..
Mfalme wa Amani tazama wenye shida/tabu, wagonjwa, wafiwa ukawe mfariji wao,waliokwenye vifungo mbalimbali, wanaopitia magumu/majaribu yoyote Mungu wetu, Baba yetu, Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo.. Tunaomba ukawaguse na mkono wako wenye nguvu na uponyaji..wakapate kupona kimwili na kiroho pia..ukaonekane kwenye mapito yao Baba..
Maisha yetu yapo mikononi mwako Baba wa Mbinguni hatuna Mungu mwingine, hakuna wa kuabudiwa ila ni wewe tuu Mfalme wa Amani.. wewe ni mwanzo na wewe ni mwisho, wewe ni Alfa na Omega..Sifa na utukufu ni wako Jehovah Jireh...!!

Tunayaweka haya yote mikononi mwako, Tunashukuru na kukuabudu Mungu wetu..
Amina..!!

Asanteni kwakutembelea hapa..
Mungu aendelee kuwabariki na kubariki kazi zenu na familia zenu..

Awape sawasawa na mapenzi yake..
Nawapenda.

Vibao vipya vya agano

(Kumb 10:1-5)

1Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Chonga vibao viwili vya mawe kama vile vya kwanza, nami nitayaandika maneno yale yaliyokuwa katika vile vibao vya kwanza ulivyovivunja. 2Uwe tayari kesho asubuhi, uje kukutana nami mlimani Sinai. 3Mtu yeyote asije pamoja nawe, wala asionekane popote mlimani; wala kondoo au ng'ombe wasilishwe karibu yake.” 4Basi, Mose akachonga vibao viwili vya mawe kama vile vya kwanza. Akaondoka asubuhi na mapema, akapanda mlimani Sinai, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru, akiwa na vile vibao viwili vya mawe mikononi mwake. 5Mwenyezi-Mungu akashuka katika wingu, akasimama pamoja na Mose, akalitaja jina lake, “Mwenyezi-Mungu.” 6Taz Kut 20:5-6; Hes 14:18; Kumb 5:9-10; 7:9-10 Kisha Mwenyezi-Mungu akapita mbele ya Mose akitangaza tena, “Mwenyezi-Mungu; mimi Mwenyezi-Mungu, ni Mungu mwenye huruma na neema; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa fadhili na uaminifu. 7Mimi nawafadhili maelfu,34:7 maelfu: Au Maelfu ya vizazi. nikiwasamehe uovu, makosa na dhambi; lakini kwa vyovyote vile sitaacha kumwadhibu mwenye hatia; nawapatiliza watoto na wajukuu uovu wa baba na babu zao, hata kizazi cha tatu na nne.”
8Mose akainama chini mara, akamwabudu Mungu. 9Kisha akasema, “Ee Bwana wangu, kwa vile umenijalia fadhili mbele zako, nakuomba uende pamoja nasi. Watu hawa ni wenye vichwa vigumu, lakini utusamehe uovu wetu na dhambi yetu, utupokee kama watu wako mwenyewe.”

Agano lafanywa upya

(Kut 23:14-19; Kumb 7:1-5; 16:1-17)

10Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Sasa ninafanya agano na watu wako. Nitatenda maajabu mbele yao ambayo hayajapata kutendwa duniani kote, wala katika taifa lolote. Na watu wote mnaoishi kati yao wataona matendo yangu makuu. Maana nitafanya jambo la ajabu kwa ajili yako.
11“Shikeni amri ninazowapa leo. Nitawafukuza mbele yenu Waamori, Wakanaani, Wahiti, Waperizi, Wahivi na Wayebusi. 12Jihadharini msije mkafanya agano na wakazi wa nchi mnayoiendea, maana hilo litakuwa mtego miongoni mwenu. 13Taz Kumb 16:21 Lakini mtazibomoa madhabahu zao na kuzivunja nguzo zao za ibada na sanamu zao za Ashera.34:13 Ashera: Mungu wa kike aliyeabudiwa na wananchi wa Kanaani. 14Msiabudu mungu yeyote mwingine, maana mimi Mwenyezi-Mungu najulikana kwa jina: ‘Mwenye Wivu,’ mimi ni Mungu mwenye wivu. 15Msifanye mikataba yoyote na wakazi wa nchi hiyo, maana watakapoiabudu miungu yao ya uongo na kuitambikia, watawaalikeni, nanyi mtashawishiwa kula vyakula wanavyoitambikia miungu yao, 16nao wavulana wenu wakaoa binti zao, na hao binti wanaoabudu miungu yao, wakawashawishi wavulana wenu kufuata miungu yao.
17 Taz Kut 20:4; Lawi 19:4; Kumb 5:8; 27:15 “Msijifanyie miungu ya uongo ya chuma.
18 Taz Kut 12:14-20; Lawi 23:6-8; Hes 28:16-25 “Mtaiadhimisha sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu. Kwa muda wa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu wakati uliopangwa katika mwezi wa Abibu,34:18 mwezi wa Abibu: Ni kati ya Machi na Aprili katika kalenda yetu. kama nilivyowaamuru, kwa sababu katika mwezi huo wa Abibu mlitoka Misri. 19Taz Kut 13:2 Kila mzaliwa wa kwanza wa kiume ni wangu, pamoja na wazaliwa wa kwanza wa kiume wa wanyama wako wote, wa ng'ombe na wa kondoo. 20Mzaliwa wa kwanza wa punda utamkomboa kwa kunitolea kondoo. Kama hutamkomboa utamvunja shingo. Watoto wenu wote wa kiume ambao ni wazaliwa wa kwanza mtawakomboa. Mtu yeyote asije mbele yangu mikono mitupu.
21“Siku sita mtafanya kazi zenu, lakini siku ya saba mtapumzika, hata ikiwa ni wakati wa kulima au kuvuna. 22Taz Kut 23:16 Mtaadhimisha sikukuu ya majuma34:22 majuma: Au Pentekoste. mwanzoni mwa majira ya mavuno ya ngano, na sikukuu ya kukusanya mavuno mwishoni mwa mwaka. 23Mara tatu kwa mwaka wanaume wote watakusanyika mbele yangu mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. 24Nitayafukuza mataifa mengine mbele yenu na kuipanua mipaka yenu. Hakuna mtu yeyote atakayeitamani nchi yenu wakati mnapokusanyika kuniabudu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu mara tatu kila mwaka.
25“Msinitolee damu ya tambiko yangu pamoja na chachu; wala tambiko ya sikukuu ya Pasaka isibakizwe mpaka asubuhi.
26 Taz Kumb 24:21; 26:2 “Mazao ya kwanza ya ardhi yako utayaleta nyumbani kwangu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako.
“Usimchemshe mwanakondoo au mwanambuzi katika maziwa ya mama yake.”
27Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Andika maneno haya, maana kulingana na maneno haya, ninafanya agano nawe na watu wa Israeli.” 28Mose alikaa huko mlimani pamoja na Mwenyezi-Mungu siku arubaini, mchana na usiku; hakula chakula wala kunywa maji. Aliandika maneno yote ya agano na zile amri kumi.

Mose anashuka kutoka mlimani Sinai

29 Taz 2Kor 3:7-16 Mose alipokuwa anashuka mlimani Sinai akiwa na vile vibao viwili vyenye maneno ya agano mikononi mwake, hakujua kuwa uso wake ulikuwa unangaa kwa sababu alikuwa ameongea na Mwenyezi-Mungu. 30Aroni na watu Waisraeli wote walipomwona waliogopa kumkaribia, kwani uso wake ulikuwa unangaa. 31Lakini Mose alimwita Aroni na viongozi wa jumuiya ya Waisraeli waende karibu naye, kisha akazungumza nao. 32Baadaye Waisraeli wote wakaja karibu naye, naye akawapa amri zote ambazo Mwenyezi-Mungu alimpa kule mlimani Sinai. 33Mose alipomaliza kuzungumza na watu aliufunika uso wake kwa kitambaa. 34Lakini ikawa kwamba kila mara Mose alipokwenda kuongea na Mwenyezi-Mungu katika hema la mkutano, alikiondoa kile kitambaa mpaka alipotoka nje. Na alipotoka nje aliwaambia Waisraeli mambo yote aliyoamriwa, 35nao Waisraeli waliuona uso wake unangaa. Ndipo Mose alipoufunika tena uso wake kwa kitambaa mpaka alipokwenda kuongea na Mwenyezi-Mungu.

Kutoka34;1-35

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.