Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Wapendwa/Waungwana tunamshukuru Mungu kwa kutuwezesha kumaliza kupitia/kusoma kitabu cha "YOSHUA" Natumaini tumejifunza na kuongeza kitu... Leo tunaanza kitabu cha "WAAMUZI"Tunaomba Mungu akatuongoze vyema katika kusoma na tukaelewe na kufuata yaliyomo na tukasimamie Neno lake na likawe msaada kwetu na kwa wengine.. Ee Mungu tusaidie tukawe na kiu/shauku ya kusoma zaidi na kuzingatia
Kama ukiwapa ndugu wote maagizo haya, utakuwa mtumishi mwema wa Kristo Yesu, ukijiendeleza kiroho kwa maneno ya imani na mafundisho ya kweli ambayo wewe umeyafuata. Lakini achana na hadithi zile zisizo za kidini na ambazo hazina maana. Jizoeshe kuishi maisha ya uchaji wa Mungu. Mazoezi ya mwili yana faida yake, lakini mazoezi ya kiroho yana faida za kila namna, maana yanatuahidia uhai katika maisha ya sasa, na pia hayo yanayokuja. Usemi huo ni wa kusadikika kabisa na unastahili kukubaliwa. Sisi tunajitahidi na kufanya kazi kwa bidii kwani tumemwekea tumaini letu Mungu aliye hai ambaye ni Mwokozi wa watu wote, na hasa wale wanaoamini. Wape maagizo hayo na mafundisho hayo. Usikubali mtu yeyote akudharau kwa sababu wewe ni kijana, lakini jitahidi uwe mfano kwa wanaoamini: Katika usemi wako, mwenendo wako, upendo, imani na maisha safi. Tumia wakati wako na juhudi yako katika kusoma hadharani Maandiko Matakatifu, kuhubiri na kufundisha, mpaka nitakapokuja. Usiache kukitumia kile kipaji cha Kristo ndani yako ulichopewa kwa maneno ya manabii na kwa kuwekewa mikono na wazee. Fikiri kwa makini juu ya hayo yote na kuyatekeleza kusudi maendeleo yako yaonekane na wote. Angalia sana mambo yako mwenyewe na mafundisho yako. Endelea kufanya hayo, maana ukifanya hivyo, utajiokoa mwenyewe na wale wanaokusikiliza.
Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana tunamshukuru katika yote... Asante Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu,Muumba wa Mbingu Nchi na vyote vilivyomo,vinavyoonekana na visivyoonekana.. Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Mungu wa wote walio hai.. Muweza wa yote,Baba wa upendo,Mungu wenye huruma,Mponyaji Jehovah Jireh,Jehovah Nissi,Jehovah Rapha,Jehovah Raah,Jehovah Shammah,Jehovah Shalom,Emanueli-Mungu pamoja nasi.. Unastahili Sifa,Unastahili kutukuzwa,Unastahili kuabudiwa, Unastahili kuhimidiwa,Unastahili ee Baba...!Unatosha Mungu wetu..
Basi, ikiwa mmefufuka pamoja na Kristo, panieni mambo ya juu, kule Kristo aliko, ameketi upande wa kulia wa Mungu. Muwe na hamu ya mambo ya huko juu, na siyo mambo ya hapa duniani. Maana nyinyi mmekufa na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu. Uhai wenu halisi ni Kristo, na wakati atakapotokea ndipo nanyi pia mtakapotokea pamoja naye katika utukufu.
Asante kwa kwa ulinzi wako wakati wote Mungu wetu.. Asante kwa kutuchagua na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari katika majukumu yetu..
Tunakuja mbele zako Mungu wetu tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu.. Tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua.. Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea.. Mungu wetu tunaomba utuepushe katika majaribu Baba utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote.. Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Mungu wetu tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona.. Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu,Baba ukatupe ubunifu,maarifa katika kufanya/kutenda nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako,Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo,Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji.. Tusipungukiwe katika mahitaji yetu,Jehovah ukatupe sawasawa na mapenzi yako...
Basi, ueni chochote kilicho ndani yenu ambacho ni cha kidunia: Uasherati, uchafu, shauku, tamaa mbaya na uchu (ambao ni sawa na kuabudu sanamu). Kwa sababu ya mambo hayo hasira ya Mungu huwajia wote wanaomwasi. Wakati mmoja nyinyi pia mliishi kufuatana na mambo hayo, mlipotawaliwa nayo. Lakini sasa mnapaswa kuachana na mambo haya yote: Hasira, tamaa na uovu; kufuru au maneno yasiyofaa yasitoke kamwe vinywani mwenu. Msiambiane uongo, kwani nyinyi mmekwisha vua ule utu wa kale pamoja na matendo yake yote, mkavaa utu mpya. Huu unaendelea kurekebishwa na Mungu, Muumba wake, kadiri ya mfano wake, ili mpate kumjua Mungu kwa ukamilifu. Katika hali hii, hakuna tena tofauti kati ya Mgiriki na Myahudi, aliyetahiriwa na asiyetahiriwa, msomi na asiye msomi, mtumwa na mtu aliye huru. Kristo ni kila kitu, na yumo katika yote. Nyinyi ni watu wake Mungu; yeye aliwapenda na kuwateua. Kwa hiyo, basi, vaeni moyo wa huruma, wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu. Vumilianeni na kusameheana iwapo mmoja wenu analo jambo lolote dhidi ya mwenzake. Mnapaswa kusameheana kama Bwana alivyowasamehe nyinyi. Zaidi ya hayo yote, zingatieni upendo, kwani upendo huunganisha kila kitu katika umoja ulio kamili. Nayo amani ya Kristo itawale mioyoni mwenu; maana kwa ajili hiyo nyinyi mmeitwa katika mwili huo mmoja. Tena muwe na shukrani! Ujumbe wa Kristo na ukae ndani yenu pamoja na utajiri wake wote. Fundishaneni na kushauriana kwa hekima yote. Imbeni Zaburi, nyimbo na tenzi za kiroho; mwimbieni Mungu mioyoni mwenu kwa shukrani. Na, kila mfanyacho kwa neno au tendo, fanyeni vyote kwa jina la Bwana Yesu na kumshukuru Mungu Baba kwa njia yake.
Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka,Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki Baba tunaomba ukatubariki na ukatupe neema ya kusimamia Neno lako,amri na sheria zako siku zote za maisha yetu.. Ukatufanye chombo chema Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe.. Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..
Lakini wewe, mtu wa Mungu, jiepushe na mambo hayo. Zingatia uadilifu, uchaji wa Mungu, imani, upendo, subira na unyenyekevu. Piga mbio kadiri uwezavyo katika shindano la mbio za imani, ukajipatie tuzo la uhai wa milele uliloitiwa wakati ulipokiri imani yako mbele ya mashahidi wengi. Mbele ya Mungu anayevipa vitu vyote uhai, na mbele ya Yesu Kristo aliyetoa ushahidi na kukiri ukweli mbele ya Pontio Pilato, nakuamuru ushike maagizo yako na kuyatii kwa uaminifu mpaka siku ile atakapotokea Bwana wetu Yesu Kristo. Kutokea kwake kutafanyika wakati ufaao uliopangwa na Mungu mwenye heri na aliye Mtawala pekee, Mfalme wa wafalme, na Bwana wa mabwana. Yeye peke yake anaishi milele katika mwanga usioweza kukaribiwa na mtu. Hakuna mtu aliyepata kumwona au awezaye kumwona. Kwake iwe heshima na uwezo wa milele! Amina. Waamuru watu walio matajiri katika mambo ya maisha ya sasa, wasijivune, wasiweke tumaini lao katika mali isiyoweza kutegemewa; bali wamtegemee Mungu, ambaye kwa ukarimu hutupatia vitu vyote tuvifurahie. Waamuru watende mema, wawe matajiri katika matendo mema, na wawe wakarimu na walio tayari kuwashirikisha wengine mali zao. Kwa namna hiyo watajiwekea hazina ambayo itakuwa kwao msingi imara kwa wakati ujao. Hapo wataweza kujipatia uhai ambao ni uhai wa kweli. Timotheo, tunza salama yote yale uliyokabidhiwa. Jiepushe na majadiliano ya kidunia na ubishi wa kipumbavu juu ya kile wanachokiita watu wengine “Elimu.” Maana wengine wamejidai kuwa na hiyo elimu, na matokeo yake wamepoteza imani. Nawatakieni nyote neema!
Mungu wetu ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu wagonjwa,ukawape uponyaji,wenye njaa ukawape chakula na ukabariki mashamba yao wakapate mavuno mengi na wakawe na akiba,waliokatika magumu/majaribu Baba wa Mbinguni tunaomba ukawavushe salama,waliokatika vifungo mbalimbali Mungu wetu tunaomba ukawafungue na ukawape wote neema ya kujiombea,kufuata njia zako ukawaweke huru na Nuru yako ikaangaze katika maisha yao.. Wafiwa ukawe mfariji wao.. Kwa imani tunayaweka haya yote mikononi mwako Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu Hata Milele.. Amina..!
Asanteni sana wapendwa katika Bwana kwa kuwa nami Mungu aendelee kuwabariki na Upendo wa Kristo Amani na furaha iwe nanyi Daima.. Nawapenda.
|