Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday, 5 February 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Samueli 5...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana...

 Ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii..
Si kwamba sisi ni wema sana wala si kwa nguvu zetu,si kwa uwezo wetu wala si kwa utashi wetu,si kwamba sisi ni wazuri mno wala si kwa akili zetu..
Ni kwa neema/rehema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii..
Tumshukuru Mungu wetu kwa wema na fadhili zake kwetu...
Tumsifu Mungu na kumtukuza daima..
Unastahili sifa na kutukuzwa Mungu wetu,Unastahili kuabudiwa Baba wa Mbinguni,Unastahili kuhimidiwa Yahweh,Unatosha Jehovah..
Neema yako yatutosha Mungu wetu,Mtendo yako ni makuu sana,Mtendo yako ni ya ajabu Mungu wetu..!!


Mimi Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, nawaandikia nyinyi watu wa Mungu huko Efeso, mlio waaminifu katika kuungana na Kristo Yesu. Nawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo. Atukuzwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Maana, katika kuungana na Kristo ametubariki kwa kutujalia zawadi zote za kiroho mbinguni. Kabla ya kuumbwa ulimwengu, Mungu alituteua tuwe wake katika kuungana na Kristo ili tuwe watakatifu na bila hitilafu mbele yake. Kwa sababu ya upendo wake, Mungu alikuwa ameazimia tangu zamani kutuleta kwake kama watoto wake kwa njia ya Yesu Kristo. Ndivyo alivyopenda na kunuia. Basi, tumsifu Mungu kwa sababu ya neema yake tukufu ambayo ametujalia katika Mwanae mpenzi!



Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako....
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Baba wa Mbinguni tunaomba utuepushe katika majaribu 
Yahweh utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Mungu wetu utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona...



Maana kwa damu yake Kristo sisi tunakombolewa, yaani dhambi zetu zinaondolewa. Ndivyo ulivyo ukuu wa neema yake aliyotukirimia bila kipimo! Kwa hekima na ujuzi wake wote Mungu alitekeleza kile alichonuia, akatujulisha mpango wake uliofichika, ambao alikuwa ameazimia kuutekeleza kwa njia ya Kristo. Mpango huo ambao angeutimiza wakati utimiapo ni kukusanya pamoja viumbe vyote, kila kitu mbinguni na duniani, chini ya Kristo. Katika kuungana na Kristo, sisi tumerithishwa wokovu kama tulivyopangiwa kadiri ya azimio lake Mungu atekelezaye kila kitu kulingana na uamuzi na matakwa yake. Basi, sisi tuliotangulia kumtumainia Kristo tunapaswa kuusifu utukufu wa Mungu! Nanyi pia watu wa mataifa mengine, mliusikia ujumbe wa kweli yaani Habari Njema iliyowaletea wokovu, mkamwamini Kristo; naye Mungu, ili kuonesha kuwa nyinyi ni wake, akawapiga mhuri kwa kuwapeni yule Roho Mtakatifu aliyetuahidia. Huyu Roho ni dhamana ya kupata yote yale Mungu aliyowaahidia watu wake, na jambo hili latuhakikishia kwamba Mungu atawakomboa kabisa wote walio wake. Tuusifu utukufu wake!



Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Yahweh tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Mungu wetu nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Jehovah tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Baba wa Mbinguni tunaomba nasi ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Jehovah ukatupe kama inavyokupendeza wewe..


Mafalme wa amani tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Mungu wetu tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh ukatamalaki na kutuatamia,Mungu wetu ukatubariki tuingiapo/tutokapo Yahweh ukabariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba wa Mbinguni tunaomna ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo..
Jehovah tukawe salama moyoni Mungu wetu ukatupe macho ya rohoni na masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Mungu wetu tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako Yahweh kusimamia Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu..
Jehovah ukatupe hekima,busara,amani,utuwema,fadhili.huruma na tukatende yote yanayokupendeza wewe..
Yahweh ukatuokoe na choyo,kiburi,unafiki,ubinafsi,ugombanishi,makwazo na vyote vinavyokwenda kinyume nawe..
Jehovah ukaonekane katika maisha yetu,Mungu wetu ukawe nasi popote tupitapo Jehovah na ikajulikane kwamba upo Baba wa mbinguni..
amani ikatawale na upendo ukadumu kati yetu..
Ukatufanye chombo chema Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..



Kwa sababu hiyo, tangu niliposikia juu ya imani yenu kwa Bwana Yesu, na mapendo yenu kwa watu wote wa Mungu, sijaacha kamwe kumshukuru Mungu kwa ajili yenu. Ninawakumbuka katika sala zangu, ili Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba mtukufu, awajalieni Roho wake atakayewapa hekima na kuwafunulieni Mungu mpate kumjua. Namwomba Mungu aifunue mioyo yenu iweze kuuona mwanga wake, mpate kutambua lile tumaini alilowaitieni na utukufu mkuu wa zawadi alizowawekea watu wake, mpate kutambua jinsi uwezo wake ulivyo mkuu mno kwa ajili yetu sisi tunaoamini. Uwezo huo unaofanya kazi ndani yetu ni sawa na nguvu ile kuu mno aliyomfufua nayo Kristo kutoka kwa wafu, akamketisha upande wake wa kulia mbinguni. Huko, Kristo anatawala juu ya kila tawala, mamlaka, enzi na ukuu; anatawala juu ya kila cheo kiwezacho kutajwa katika ulimwengu huu na katika ulimwengu ujao. Mungu ameweka vitu vyote chini ya miguu yake, akamkabidhi kwa kanisa akiwa mkuu wa vitu vyote. Kanisa ni mwili wa Kristo, na ukamilifu wake yeye anayekamilisha vitu vyote kila mahali.


Yahweh tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu wenye shida/tabu,wagonjwa,wenye njaa,wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,walio kata tamaa,walio kataliwa,wenye hofu na mashaka,waliokatika vifungo vya yule mwovu,walio magerezani pasipo na hatia,walioanguka/potea na wote waliokwenda kinyume nawe na wakatubu na kukurudia Mungu wetu ukawaokoe na kuwaongoza
Baba wa Mbinguni ukawasamehe na kuwainua,Mungu wetu ukawaponye na kuwapa chakula,Yahweh ukawape neema ya kujiombea na kufuata njia zako nazo ziwaweke huru,Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Yahweh ukaonekane katika maisha yao Mungu wetu tunaomba ukapokee na kusikia kuomba kwetu,Yahweh tunaomba ukajibu maombi/sala zetu na  ukawatendee sawasawa na mapenzi yako..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami/kunisoma
Mungu aendelee kuwabariki na kuwatendea kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo ikawe nanyi daima..
Nawapenda.


Daudi awa mfalme wa Israeli na Yuda

(1Nya 11:1-9; 14:1-7)

1Kisha makabila yote ya Israeli yalimwendea Daudi huko Hebroni, na kumwambia, “Tazama, sisi ni mwili na damu yako. 2Hapo awali, Shauli alipokuwa mfalme wetu wewe ndiwe uliyewaongoza Waisraeli vitani, na Mwenyezi-Mungu alikuambia ‘Utakuwa mchungaji wa watu wangu Israeli na utakuwa mkuu juu ya Israeli.’” 3Basi, wazee wote wa Israeli wakamwendea mfalme Daudi huko Hebroni; naye akafanya agano nao mbele ya Mwenyezi-Mungu, halafu wakampaka Daudi mafuta awe mfalme wa Israeli. 4Daudi alikuwa na umri wa miaka thelathini alipoanza kutawala, na alitawala kwa muda wa miaka arubaini. 5Huko Hebroni, alitawala watu wa Yuda kwa muda wa miaka saba na miezi sita, na huko Yerusalemu alitawala watu wa Israeli pamoja na Yuda kwa muda wa miaka thelathini na mitatu.
6Baadaye mfalme na watu wake walikwenda Yerusalemu kuwashambulia Wayebusi waliokuwa wenyeji wa nchi hiyo. Lakini wao wakamwambia, “Hutaingia mjini humu, kwani vipofu na vilema watakufukuzia mbali.” Walimwambia hivyo kwani walifikiri kuwa Daudi asingeweza kuingia mjini humo. 7Hata hivyo, mfalme Daudi aliiteka ngome ya Siyoni, yaani mji wa Daudi.
8Siku hiyo, Daudi alisema, “Mtu yeyote atakayewapiga Wayebusi na apitie kwenye mfereji wa maji ili kuwashambulia vilema na vipofu ambao roho yangu inawachukia.” Ndio maana watu husema, “Vipofu na vilema hawataingia nyumbani.”5:8 makala ya Kiebrania si dhahiri.
9Daudi alikaa kwenye ngome hiyo, nao mji akauita, “Mji wa Daudi.” Daudi aliujenga mji kuuzunguka, akianzia Milo5:9 Milo: Sehemu iliyojazwa na mfalme Daudi mjini Yerusalemu mahali ambapo hekalu lilijengwa. kuelekea ndani. 10Naye Daudi akazidi kuwa maarufu zaidi kwa sababu Mwenyezi-Mungu, Mungu wa majeshi, alikuwa pamoja naye.
11Kisha, mfalme Hiramu wa Tiro alituma wajumbe kwa Daudi; alimpelekea pia mierezi, maseremala na waashi ambao walimjengea Daudi ikulu. 12Hivyo, Daudi akatambua kwamba Mwenyezi-Mungu amemwimarisha awe mfalme wa Israeli, na kwamba ameukuza ufalme wake kwa ajili ya watu wake wa Israeli.
13Daudi alijitwalia masuria na wake zaidi wa huko mjini Yerusalemu baada ya kutoka Hebroni. Hao, wakamzalia watoto zaidi wa kiume na wa kike. 14Yafuatayo ndiyo majina ya watoto wa kiume, wake zake waliomzalia huko Yerusalemu: Shamua, Shobabu, Nathani, Solomoni, 15Ibhari, Elishua, Nefegi, Yafia, 16Elishama, Eliada na Elifeleti.

Ushindi juu ya Wafilisti

(1Nya 14:8-17)

17Wafilisti waliposikia kwamba Daudi amepakwa mafuta kuwa mfalme wa Israeli, wote walitoka kwenda kumtafuta, lakini yeye alipata habari, akaingia ndani ya ngome. 18Wafilisti walifika na kujitawanya kwenye Bonde la Refaimu. 19Basi, Daudi alimwuliza Mwenyezi-Mungu shauri, “Je, niende kuwashambulia Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwangu?” Naye Mwenyezi-Mungu akamwambia Daudi, “Nenda, maana hakika nitawatia Wafilisti mikononi mwako.” 20Basi, Daudi akafika Baal-perasimu, na kuwashinda Wafilisti; halafu akasema, “Mwenyezi-Mungu amepita katikati ya adui zangu kama mafuriko ya maji yaendayo kasi.” Kwa hiyo mahali hapo pakaitwa Baal-perasimu.5:20 Baal-perasimu: Kiebrania maana yake, “Bwana apitaye katikati”. 21Wafilisti waliziacha sanamu zao za miungu mahali hapo, naye Daudi na watu wake wakazichukua.
22Kwa mara ya pili, Wafilisti walifika tena na kujitawanya kwenye bonde la Refaimu. 23Daudi alipomwomba Mwenyezi-Mungu shauri, Mwenyezi-Mungu alimwambia, “Usiwashambulie kutoka hapa ulipo, bali zunguka na kuwashambulia kutoka mkabala wa miti na miforosadi. 24Na mara mtakaposikia vishindo vya gwaride kwenye vilele vya miforosadi hiyo, hapo jipe moyo kwani nitakuwa nimetoka ili kukutangulia kulipiga jeshi la Wafilisti.” 25Daudi alifanya kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu, naye akawapiga Wafilisti kutoka Geba hadi Gezeri.



2Samweli5;1-25

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Friday, 2 February 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Samueli 4...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu kwa mema mengi aliyotutendea..

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wenye nguvu,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Mungu wa walio hai,Baba wa Yatima,Mungu wa Wajane
Mponyaji wetu,Muweza wa yote,Baba wa Baraka,Mungu wa upendo,
Mungu wa faraja,Alfa na Omega,Hakuna linaloshindikana mbele zako  Mungu wetu,Neema yako yatutosha ee Mungu wetu...!!


Mungu ainuka, na maadui zake watawanyika; wanaomchukia wakimbia mbali naye! Kama moshi unavyopeperushwa na upepo, ndivyo anavyowapeperusha; kama nta inavyoyeyuka karibu na moto, ndivyo waovu wanavyoangamia mbele ya Mungu! Lakini waadilifu hufurahi ajapo Mungu, hushangilia na kuimba kwa furaha. Mwimbieni Mungu, lisifuni jina lake; mtengenezeeni njia yake apandaye mawinguni. Jina lake ni Mwenyezi-Mungu; furahini mbele yake. Mungu akaaye mahali pake patakatifu, ni Baba wa yatima na mlinzi wa wajane.

Asante kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante kwa uwepo wako Mungu wetu..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu..
Sifa na Utukufu tunakurudishia wewe Baba wa Mbinguni..

Mungu huwapa fukara makao ya kudumu, huwafungua wafungwa na kuwapa fanaka. Lakini waasi wataishi katika nchi kame. Ee Mungu, ulipowaongoza watu wako, uliposafiri kule jangwani, dunia ilitetemeka, mbingu zilitiririsha mvua; kwa kuweko kwako, Mungu wa Sinai, naam, kwa kuweko kwako, Mungu wa Israeli! Ee Mungu, uliinyeshea nchi mvua nyingi, uliiburudisha nchi yako ilipokuwa imechakaa. Watu wako wakapata humo makao; ukawaruzuku maskini kwa wema wako. Bwana alitoa amri, nao wanawake wengi wakatangaza habari: “Wafalme na majeshi yao wanakimbia ovyo!” Kina mama majumbani waligawana nyara, ingawa walibaki mazizini: Sanamu za njiwa wa madini ya fedha, na mabawa yao yanangaa kwa dhahabu. Mungu Mwenye Nguvu alipowatawanya wafalme huko, theluji ilianguka juu ya mlima Salmoni. Ewe mlima mrefu, mlima wa Bashani, ewe mlima wa vilele vingi, mlima wa Bashani! Mbona unauonea kijicho mlima aliochagua Mungu akae juu yake? Mwenyezi-Mungu atakaa huko milele! Akiwa na msafara mkubwa, maelfu na maelfu ya magari ya kukokotwa, Bwana anakuja patakatifuni pake kutoka Sinai. Anapanda juu akichukua mateka; anapokea zawadi kutoka kwa watu, hata kutoka kwa watu walioasi; Mwenyezi-Mungu apate kukaa huko. Mwenyezi-Mungu asifiwe siku kwa siku! Yeye hutubebea mizigo yetu; yeye ndiye Mungu wa wokovu wetu. Mungu wetu ni Mungu mwenye kutuokoa; Bwana Mungu pekee ndiye aokoaye katika kifo. Mungu ataviponda vichwa vya maadui zake, naam, vichwa vya wanaoshikilia njia mbaya. Bwana alisema: “Nitawarudisha maadui kutoka Bashani; nitawarudisha kutoka vilindi vya bahari, uoshe miguu katika damu ya maadui zako, nao mbwa wako wale shibe yao.” Ee Mungu, misafara yako ya ushindi yaonekana; misafara ya Mungu wangu, mfalme wangu, hadi patakatifu pake! Mbele waimbaji, nyuma wanamuziki, katikati wasichana wanavumisha vigoma. “Msifuni Mungu katika jumuiya kubwa ya watu. Msifuni Mwenyezi-Mungu, enyi wazawa wa Israeli!” Kwanza ni Benyamini, mdogo wa wote; kisha viongozi wa Yuda na kundi lao, halafu wakuu wa Zebuluni na Naftali. Onesha, ee Mungu, nguvu yako kuu; enzi yako uliyotumia kwa ajili yetu, kutoka hekaluni mwako, Yerusalemu, ambapo wafalme watakujia na zawadi zao. Uwakemee wale wanyama wakaao bwawani, kundi la mabeberu na fahali, mpaka mataifa hayo yakupe heshima na kodi. Uwatawanye hao watu wenye kupenda vita! Mabalozi watakuja kutoka Misri, Waethiopia watamletea Mungu mali zao. Enyi falme za dunia, mwimbieni Mungu, mwimbieni Bwana nyimbo za sifa; mwimbieni yeye apitaye katika mbingu, mbingu za kale na kale. Msikilizeni akinguruma kwa kishindo. Itambueni nguvu kuu ya Mungu; yeye atawala juu ya Israeli, enzi yake yafika katika mbingu. Mungu ni wa kutisha patakatifuni pake, naam, yeye ni Mungu wa Israeli! Huwapa watu wake nguvu na enzi. Asifiwe Mungu!


Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako..
Jehovaha tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Mungu wetu tunaomba utuepushe katika majaribu Yahweh utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..

Mungu wetu tnaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Yahweh tunaomba utupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Mungu wetu nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Jehovah tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Baba wa Mbinguni tunaomba tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Jehovah ukatupe kama inavyokupemdeza wewe..

Mfalme wa amani tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Yahweh tunaomba amani yako ikatawale katika nyumba/ndoa zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Mungu wetu tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatamalaki na kutuatamia
Yahweh ukatuongoze tuingiapo/tutokapo Mungu wetu ukavibariki  vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Jehovah tunaomba ukavitakase na ukavifunike kwa Damu Ya Mwanao mpendwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo,Mungu wetu ukatupe akili ya kutambua/kujitambua Jehovah
tunaomba tukawe salama moyoni Baba wa Mbinguni ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Mungu wetu ukatupe neema ya kufuata njia zako Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu..
Yahweh Nuru yako ikaangze katika maisha yetu Jehovah ukaonekane katika maisha yetu na popote tupitapo ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni..
Mungu wetu ukatufanye chombo chema Yahweh nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..


Basi, acheni uovu wote; uongo, unafiki, wivu na maneno ya kashfa visiweko tena. Kama vile watoto wachanga wanavyotamani maziwa, nanyi pia mnapaswa kuwa na hamu ya maziwa halisi ya kiroho, ili kwa nguvu yake mpate kukua na kukombolewa. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Mmegundua kwamba Bwana ni mwema.” Basi, mwendeeni Bwana! Yeye ndiye jiwe hai lililokataliwa na watu; lakini mbele ya Mungu ni jiwe teule na la thamani kubwa. Mwendeeni yeye kama mawe hai mkajengeke na kuwa nyumba ya kiroho ambamo mtatumikia kama makuhani watakatifu, kutolea tambiko za kiroho zenye kumpendeza Mungu kwa njia ya Yesu Kristo. Maana Maandiko Matakatifu yasema: “Tazama! Naweka jiwe huko Siyoni, jiwe la msingi, teule na la thamani. Mtu atakayemwamini huyo hataaibishwa.” Kwenu nyinyi mnaoamini, jiwe hilo ni la thamani kubwa; lakini kwa wale wasioamini, “Jiwe walilolikataa waashi, sasa limekuwa jiwe kuu la msingi.” Tena Maandiko yasema: “Jiwe hilo ni jiwe la kujikwaa, mwamba wa kuwaangusha watu.” Watu hujikwaa kwa sababu hawauamini ule ujumbe; na ndivyo walivyopangiwa tangu mwanzo. Lakini nyinyi ni ukoo mteule, makuhani wa Mfalme, taifa takatifu; watu wake Mungu mwenyewe, mlioteuliwa kutangaza matendo makuu ya Mungu aliyewaiteni kutoka gizani, akawaingizeni katika mwanga wake mkuu. Wakati mmoja nyinyi hamkuwa watu wa Mungu, lakini sasa nyinyi ni watu wake; wakati mmoja hamkupewa huruma ya Mungu, lakini sasa mmepokea huruma.

Yahweh tazama wenye shida/tabu , Wagonjwa, wenye njaa,walio katika vifungo vya yule mwovu,waliokataliwa,waliokata tamaa,wenye hofu na mashaka,walio magerezani pasipo na hatia,wafiwa na wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali..
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
Yahweh tunaomba ukawaponye na kuwasimamisha tena,Baba wa mbinguni ukawape chakula,Jehovah ukawavushe salama na kuwaokoa
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,Baba wa Mbinguni ukaonekane katika shida zao,Mungu wetu ukawasamehe,ukawabariki,ukawatakase na kuwafunika kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo,Mungu wetu ukasikie kuomba kwetu Baba wa Mbinguni ukapokee sala/maombi yetu
Yahweh ukajibu na kuwatendea sawasawa na mapenzi yako..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!!!

Wapendwa katika Bwana asanteni sana kwakuwa nami/kunisoma
Mungu mwenye nguvu na akawabariki na kuwatendea sawasawa na mapenzi yake..
Nawapenda.

Ishboshethi anauawa
1Ishboshethi mwana wa Shauli, aliposikia kwamba Abneri ameuawa huko Hebroni, alivunjika moyo na watu wote wa Israeli walifadhaika. 2Ishboshethi mwana wa Shauli, alikuwa na watu wawili waliokuwa viongozi wa kikosi cha uvamizi; mmoja aliitwa Baana na mwingine Rekabu. Hao walikuwa wana wa Rimoni, mtu wa kabila la Benyamini kutoka mji wa Be-erothi, (kwa maana Be-erothi pia ulikuwa mali ya kabila la Benyamini). 3Wakazi wa Be-erothi walikimbilia Gitaimu, na wameishi huko kama wageni hadi leo.
4Yonathani mwana wa Shauli, alikuwa na mtoto aliyelemaa miguu yake yote miwili. Mtoto huyo aliitwa Mefiboshethi. Mefiboshethi alikuwa na umri wa miaka mitano habari za kifo cha Shauli na Yonathani ziliposikika kutoka Yezreeli. Yaya aliyekuwa anamtunza aliposikia kuwa Shauli na Yonathani wameuawa huko Yezreeli, alimchukua Mefiboshethi akakimbia naye. Lakini alipokuwa anakimbia kwa haraka mtoto huyo alianguka, naye akalemaa.
5Rekabu na Baana wana wa Rimoni Mbeerothi, wakaenda nyumbani kwa Ishboshethi. Walifika huko adhuhuri, Ishboshethi alipokuwa anapumzika nyumbani kwake. 6,7Waliingia nyumbani wakijifanya kana kwamba wanataka kuchukua ngano, wakamkuta Ishboshethi amelala kitandani mwake ndani ya chumba chake cha kulala, wakamchoma mkuki tumboni. Baada ya kumwua hivyo hao ndugu wawili walimkata kichwa wakatoroka wakiwa wamekichukua. Walipitia njia ya Araba, wakasafiri usiku kucha. 8Halafu walichukua kichwa cha Ishboshethi na kumpelekea Daudi huko Hebroni. Nao wakamwambia mfalme Daudi, “Hiki ni kichwa cha Ishboshethi mwana wa Shauli ambaye ni adui yako, aliyekuwa anataka kuyaangamiza maisha yako. Mwenyezi-Mungu leo amekulipizia kisasi dhidi ya Shauli na wazawa wake.”
9Lakini Daudi akamjibu Rekabu na Baana, nduguye, wana wa Rimoni, Mbeerothi,. “Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, kwamba yeye ameyakomboa maisha yangu kutokana na kila adui. 10Yule mtu aliyekuja kuniambia kuwa Shauli amekufa, akidhani kuwa ananiletea habari njema, nilimkamata na kumwua huko. Hivyo ikawa ndiyo zawadi niliyompa kutokana na taarifa yake. 11Je, mtu mwovu anapomuua mtu mwadilifu akiwa kitandani, nyumbani kwake, je, si haki kwangu kumlipiza kwa sababu ya kumwaga damu kwa kumwulia mbali toka duniani?” 12Daudi akawaamuru vijana wake, nao wakawaua. Wakawakata mikono yao na miguu yao. Halafu wakawatundika mtini kando ya bwawa huko Hebroni. Lakini walikichukua kichwa cha Ishboshethi na kukizika katika kaburi la Abneri huko Hebroni.


2Samweli4;1-12

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Thursday, 1 February 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Samueli 3...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana..
Tumshukuru Mungu katika yote..

Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima na kuwa tayari kwa majukumu yetu..

Utukuzwe ee Mungu wetu,Usifiwe Baba wa Mbinguni,Uhimidiwe Jehovah,
Uabudiwe Yahweh,Unatosha ee Mfalme wa amani,Matendo yako ni makuu mno,Matendo yako ni ya ajabu,Neema yako yatutosha Mungu wetu..!!

Nitajivuna basi, ingawa haifai! Lakini sasa nitasema juu ya maono na ufunuo alivyonijalia Bwana. Namjua mtu mmoja Mkristo, ambaye miaka kumi na minne iliyopita alinyakuliwa mpaka katika mbingu ya tatu. (Sijui kama alikuwa huko kwa mwili au kwa roho; Mungu ajua). Narudia: Najua kwamba mtu huyo alinyakuliwa mpaka peponi. (Lakini sijui kama alikuwa huko kwa mwili au kwa roho; Mungu ajua). Huko akasikia mambo ya siri ambayo binadamu hastahili kuyatamka. Basi, nitajivunia juu ya mtu wa namna hiyo, na si juu yangu mimi binafsi, isipokuwa tu juu ya udhaifu wangu. Kama ningetaka kujivuna singekuwa mpumbavu hata kidogo, maana ningekuwa nasema ukweli tupu. Lakini sitajivuna; sipendi mtu anifikirie zaidi ya vile anavyoona na kusikia kutoka kwangu. Lakini, kusudi mambo haya makuu niliyofunuliwa yasinifanye nilewe majivuno, nilipewa maumivu mwilini kama mwiba, mjumbe wa Shetani mwenye kunipiga, nisijivune kupita kiasi. Nilimsihi Bwana mara tatu kuhusu jambo hili ili linitoke. Lakini akaniambia: “Neema yangu inatosha kwa ajili yako; maana uwezo wangu hukamilishwa zaidi katika udhaifu.” Basi, ni radhi kabisa kujivunia udhaifu wangu ili uwezo wake Kristo ukae juu yangu. Kwa hiyo nakubali kwa radhi udhaifu, dharau, taabu, udhalimu na mateso, kwa ajili ya Kristo; maana ninapokuwa dhaifu, ndipo ninapokuwa na nguvu.

Mungu wetu tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako..
Baba wa Mbinguni tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Jehovah tunaomba utuepushe katika majaribu Baba wa Mbinguni utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote
Mungu wetu tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Yahweh utufunike kwa Damu ya Bwana na mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..


Nimekuwa kama mpumbavu, lakini nyinyi mmenilazimisha kuwa hivyo. Nyinyi ndio mngalipaswa kunisifu. Maana, ingawa mimi si kitu, kwa vyovyote, mimi si mdogo kuliko hao “mitume wakuu.” Miujiza na maajabu yaoneshayo wazi kwamba mimi ni mtume yalifanyika miongoni mwenu kwa uvumilivu wote. Je, mlipungukiwa nini zaidi kuliko makanisa mengine, isipokuwa tu kwamba mimi kwa upande wangu sikuwasumbueni kupata msaada wenu? Samahani kwa kuwakoseeni haki hiyo! Sasa niko tayari kabisa kuja kwenu mara ya tatu, na sitawasumbua. Maana ninachotafuta si mali zenu, bali ni nyinyi wenyewe. Ni kawaida ya wazazi kuwawekea watoto wao akiba, na si watoto kuwawekea wazazi wao. Mimi ni radhi kabisa kutumia nilicho nacho, na hata kujitolea mimi mwenyewe kabisa, kwa faida ya roho zenu. Je, mtanipenda kidogo ati kwa kuwa mimi nawapenda nyinyi mno?
Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu Mungu wetu tunaomba ukatupe ubunifu katika utendaji Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Mungu Baba tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako Yahweh tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Jehovah tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Yahweh ukabariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Mungu wetu tunaomba ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo..
Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika maisha yetu
Baba wa Mbinguni tukawe salama moyoni,Upendo kati yetu na ukadumu,Furaha,fadhili na utu wema vikawe nasi..
Baba wa Mbinguni ukatuepushe na roho za kiburi,majivuno,makwazo,kisasi,choyo,unafiki na yote yasiyokupendeza wewe,Yahweh ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia sauti yako
na kuitii,Tukanene sawasawa na mapenzi yako,Mungu wetu ukatupe neema ya kufuata njia zako Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu..
Jehovah ukaonekane katika maisha yetu Yahweh Nuru yako ikaangaze
Mungu wetu ukaonekane popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni..
Ukatufanye chombo chema Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..


Basi, mtakubali kwamba sikuwa mzigo kwenu. Lakini labda mtu mwingine atasema: “Kwa vile Paulo ni mwerevu, amewafanyieni ulaghai.” Je, mimi niliwanyonyeni kwa njia ya mjumbe yeyote niliyemtuma kwenu? Mimi nilimwita Tito, nikamtuma kwenu na ndugu yetu mwingine. Je, Tito aliwanyonyeni? Je, hamjui kwamba sisi tumekuwa tukiongozwa na roho yuleyule, na mwenendo wetu ni mmoja? Labda mnafikiri kwamba mpaka sasa tumekuwa tukijitetea wenyewe mbele yenu! Lakini, tunasema mambo haya mbele ya Mungu, tukiwa tumeungana na Kristo. Mambo hayo yote, wapenzi wangu, ni kwa ajili ya kuwajenga nyinyi. Naogopa, huenda nitakapokuja kwenu nitawakuta katika hali nisiyopenda, nami itanilazimu kuwa katika hali msiyoipenda. Naogopa huenda kukawa na ugomvi, wivu, uhasama, ubishi, masengenyo, kunongona, majivuno na fujo kati yenu. Naogopa huenda hapo nitakapokuja safari ijayo Mungu wangu atanifanya niaibike mbele yenu, nami nitaomboleza kwa ajili ya wengi wa wale waliotenda dhambi lakini hawakujuta huo uchafu, tamaa zao mbaya na uzinzi waliokuwa wamefanya.
Asante kwa neema na uponyaji wako Mungu wetu..
Asante kwa matendo yako makuu kwetu Mungu wetu
Asante kwa baraka zako na kufungua milango ya kheri kwa watoto wako waliokuomba na ukawajibu Baba wa Mbinguni.
Tunarudisha shukrani tunakusifu na kukushukuru daima kwa mema mengi uliyotutendea,Mkono wako wenye nguvu umewagusa watoto wako Yahweh umeonekana katika shida/tabu zao Baba walikuita ukawasikia Mungu wetu wakakuomba ukawapa kwa wakati uliyo faa,Yahweh sifa na utukufu tunakurudishia wewe..
Mungu wetu tunaomba ukawatendee na wengine wanaohitaji msaada wako,wenye kukuomba kwa bidii na imani..
Mungu wetu ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe Yahweh Nuru yako ikaangaze katika maisha yao,Jehovah ukawape neema ya kujiombea na kufuata njia zako nazo ziwaweke huru,Utukufu una wewe ee Baba wa Mbinguni,amani inapatikana kwako Mungu wetu,Furaha ipo nawe Jehovah..
Jehovah tunaomba ukasikie sala/maombi yetu Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo kwakuwa nami
Mungu wetu wenye nguvu na kubariki akawatendee kama inavyompendeza yeye,Amani ya Kristo iwe nanyi daima..
Nawapenda.



1Kulikuwa na vita vya muda mrefu kati ya watu walioiunga mkono jamaa ya Shauli, na wale walioiunga mkono jamaa ya Daudi. Lakini Daudi alizidi kupata nguvu zaidi na zaidi, ambapo upande wa Shauli ulizidi kudhoofika zaidi na zaidi.

Watoto wa kiume wa Daudi

2Watoto wa kiume aliozaliwa Daudi huko Hebroni walikuwa: Amnoni, mzaliwa wake wa kwanza, mama yake alikuwa Ahinoamu kutoka Yezreeli; 3Kileabu, mzaliwa wake wa pili, mama yake alikuwa Abigaili, mjane wa Nabali kutoka Karmeli; Absalomu, mzaliwa wake wa tatu, mama yake alikuwa Maaka, bintiye Talmai mfalme wa Geshuri; 4Adoniya, mzaliwa wake wa nne, mama yake alikuwa Hagithi; Shefatia, mzaliwa wake wa tano, mama yake alikuwa Abitali, 5na Ithreamu, mzaliwa wake wa sita, mama yake alikuwa Egla, mke wake Daudi. Daudi alizaliwa wana hawa wote alipokuwa huko Hebroni.

Abneri ajiunga na Daudi

6Kadiri vita vilivyoendelea kati ya jamaa ya Daudi na ile ya Shauli, Abneri alizidi kujiimarisha katika jamaa ya Shauli.
7Shauli alikuwa na suria mmoja aitwaye Rispa, binti Aya. Basi, wakati mmoja, Ishboshethi akamwuliza Abneri, “Kwa nini umelala na suria wa baba yangu?” 8Abneri alikasirika sana kutokana na maneno ya Ishboshethi, akasema: “Je, unafikiri mimi naweza kumsaliti Shauli? Je, unafikiri kuwa mimi naitumikia jamaa ya Yuda? Tazama, mimi nimekuwa mtiifu kwa jamaa ya baba yako Shauli, ndugu zake, rafiki zake na sijakutia mikononi mwa Daudi hadi leo. Hata hivyo, leo hii unaniona kuwa mwenye hatia kwa ajili ya mwanamke. 9Mungu aniue ikiwa sitatekeleza yote ambayo Mwenyezi-Mungu alimwapia Daudi. 10Mwenyezi-Mungu alimwapia Daudi kuwa atauhamisha ufalme kutoka jamaa ya Shauli na kumpa yeye. Naye atatawala Israeli na Yuda kutoka Dani hadi Beer-sheba.” 11Ishboshethi hakuweza kusema neno, kwa kuwa alikuwa anamwogopa Abneri.
12Basi, Abneri akatuma wajumbe kwa Daudi, huko Hebroni3:12 Hebroni: Au Mahali alipokuwa. wakamwambie, “Je, nchi hii ni mali ya nani? Fanya agano na mimi, nami nitakusaidia kuifanya Israeli yote iwe chini yako.” 13Daudi akamjibu, “Vema, nitafanya agano nawe. Lakini ninakutaka jambo moja kwamba kabla hujaniona sharti kwanza uniletee Mikali binti wa Shauli. Hapo utaniona.” 14Daudi pia alituma wajumbe kwa Ishboshethi mwana wa Shauli akisema, “Nirudishie mke wangu Mikali ambaye nilimwoa kwa magovi 100 ya Wafilisti.” 15Basi, Ishboshethi alituma watu wakamchukue Mikali kutoka kwa mumewe, Paltieli mwana wa Laishi. 16Lakini Paltieli akaenda pamoja na mkewe huku analia njia nzima mpaka huko Bahurimu. Abneri akamwambia Paltieli, “Rudi nyumbani.” Naye akarudi.
17Abneri alifanya mashauri na wazee wa Israeli, akawaambia, “Kwa muda fulani uliopita mmekuwa mkitaka Daudi awe mfalme wenu. 18Sasa, lileteni jambo hilo hadharani kwa sababu Mwenyezi-Mungu alimwahidi hivi Daudi, ‘Kwa mkono wako wewe Daudi mtumishi wangu, nitawaokoa watu wangu wa Israeli kutoka kwa Wafilisti na kutoka kwa adui zao wengine.’” 19Abneri pia akazungumza na Wabenyamini, kisha akaenda mpaka Hebroni kumwambia Daudi kuhusu yale ambayo watu wote wa Israeli na kabila lote la Benyamini walipatana kutenda. 20Abneri alipomwendea Daudi, alikuwa na watu ishirini, Daudi aliwafanyia karamu. 21Abneri akamwambia Daudi, “Mimi sasa nitakwenda na kukuletea watu wote wa Israeli, wewe bwana wangu mfalme. Watakuja na kufanya agano nawe, ili uwe mfalme wao, nawe utawatawala wote kama upendavyo.” Daudi akamuaga Abneri aende zake, naye akaondoka kwa amani.

Abneri anauawa

22Baadaye, Yoabu na baadhi ya watu wa Daudi walirudi kutoka mashambulio, wakaleta nyara nyingi. Lakini Abneri hakuwa pamoja na Daudi huko Hebroni kwani Daudi alikuwa amemuaga aende zake, naye akaondoka kwa amani. 23Yoabu aliporudi akiwa na jeshi lake lote alilokuwa nalo, aliambiwa kwamba Abneri mwana wa Neri, alikuwa amekuja kumwona mfalme Daudi, naye amemuaga aende zake, naye ameondoka kwa amani. 24Yoabu alimwendea mfalme na kumwambia, “Sasa umefanya nini? Tazama Abneri alikuja kwako, kwa nini umemwacha aende? 25Je, unajua kuwa Abneri mwana wa Neri alikuja kukudanganya? Alikuja ili ajue mienendo yako na yale unayoyafanya.”
26Yoabu alipotoka kuzungumza na Daudi, alituma wajumbe wakamlete Abneri, nao wakamkuta kwenye kisima cha Sira na kumrudisha, lakini Daudi hakujua jambo hilo. 27Abneri aliporudi Hebroni, Yoabu alimchukua kando kwenye lango kana kwamba anataka kuzungumza naye kwa faragha. Hapo Yoabu akamkata Abneri tumboni kwa sababu Abneri alikuwa amemuua Asaheli ndugu yake, na Abneri akafa. 28Baadaye Daudi aliposikia habari hizo alisema, “Mimi na ufalme wangu hatuna hatia mbele ya Mwenyezi-Mungu kuhusu damu ya Abneri mwana wa Neri. 29Lawama ya mauaji hayo yawe juu ya kichwa cha Yoabu na jamaa yote ya baba yake! Jamaa ya Yoabu daima isikose mtu mwenye ugonjwa wa kisonono, au ugonjwa wa ukoma, au anayetembea kwa magogo au kuuawa kwa upanga, au mwenye kukosa chakula!” 30Yoabu na ndugu yake Abishai walimuua Abneri kwa kuwa alikuwa amemuua ndugu yao Asaheli wakati wa vita huko Gibeoni. 31Kisha, mfalme Daudi akamwambia Yoabu na wale wote waliokuwa pamoja naye, wararue mavazi yao, wavae mavazi ya gunia ili wamwombolezee Abneri. Wakati wa mazishi hayo, mfalme Daudi alitembea nyuma ya jeneza. 32Abneri alizikwa huko Hebroni na mfalme aliomboleza kwa sauti akiwa kando ya kaburi, pia watu wengine wote walifanya vivyo hivyo. 33Mfalme alimwombolezea Abneri akisema,
“Je, ilikuwaje Abneri akafa kama mpumbavu?
34Mikono yako haikufungwa
na miguu yako haikutiwa pingu.
Amekufa kama mtu aliyeuawa na waovu!”
Na watu wote walimlilia tena. 35Kisha, watu wote walikwenda kumshawishi Daudi ale mkate wakati ulipokuwa bado mchana. Lakini Daudi aliapa akawaambia, “Mungu na aniue ikiwa nitaonja mkate au kitu chochote hadi jua litakapotua.” 36Watu wote waliyaona mambo hayo, nao walipendezwa; kama vile kila kitu alichofanya mfalme kilivyowapendeza. 37Hivyo, siku ile, Waisraeli wote walielewa kwamba haikuwa nia ya mfalme Daudi kumuua Abneri mwana wa Neri. 38Mfalme Daudi aliwaambia watumishi wake, “Je, hamjui kuwa leo mtu mkuu na mashuhuri amefariki katika Israeli? 39Ijapokuwa mmenipaka mafuta ili niwe mfalme, lakini leo mimi ni mnyonge. Hawa wana wa Seruya ni wakatili kupita kiasi. Mwenyezi-Mungu na awaadhibu waovu hawa sawasawa na uovu wao.”

2Samweli3;1-39

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Wednesday, 31 January 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Samueli 2...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Mungu wetu yu mwema sana tumshukuru katika yote..

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Muweza wa yote,Alfa na Omega,Mungu wa walio hai,Mungu wenye nguvu
Mungu mwenye huruma,Mungu anayetenda,anayejibu,Mponyaji wetu
Matendo yako ni makuu mno,Matendo yako ni ya ajabu
hakuna kama wewe ee Baba wa Mbinguni,Neema yako yatutosha Mfalme wa amani..!!

Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu..
Sifa na Utukufu tunakurudishia ee Mungu wetu..!!

Siku moja, watozaushuru na wenye dhambi wengi walikwenda kumsikiliza Yesu. Mafarisayo na waalimu wa sheria wakaanza kunungunika: “Mtazameni mtu huyu! Anawakaribisha wenye dhambi, na tena anakula nao.” Yesu akawajibu kwa mfano: “Hivi, mmoja wenu akiwa na kondoo 100, akigundua kwamba mmoja wao amepotea, atafanya nini? Atawaacha wale tisini na tisa mbugani, na kwenda kumtafuta yule aliyepotea mpaka ampate. Akimpata, atambeba mabegani kwa furaha. Anapofika nyumbani, atawaita rafiki zake na kuwaambia, ‘Furahini pamoja nami, kwa sababu nimempata yule kondoo wangu aliyepotea.’ Kadhalika nawaambieni, ndivyo kutakavyokuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya kutubu kwa mwenye dhambi mmoja, kuliko kwa ajili ya watu tisini na tisa wanaojiona kuwa wema, wasiohitaji kutubu.

Tunakuja mbele zako ee Mungu wetu tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Baba wa Mbinguni..
Yahweh tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Mfalme wa amani nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote walio tukosea..
Jehovah tunaomba utuepushe katika majaribu Yahweh tunaomba utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote
Baba wa Mbinguni tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Jehovah tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,Yeyye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..

“Au mwaonaje? Tuseme mwanamke fulani ana sarafu kumi za fedha, akipoteza moja, atafanya nini? Atawasha taa, ataifagia nyumba na kuitafuta kwa uangalifu mpaka aipate. Akiipata, atawaita rafiki na jirani zake na kusema, ‘Furahini pamoja nami, kwa sababu nimeipata ile sarafu yangu iliyopotea.’ Kadhalika nawaambieni, ndivyo watakavyofurahi malaika wa Mungu kwa sababu ya mwenye dhambi mmoja anayetubu.”

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Yahweh tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Mungu wetu tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Baba wa Mbinguni tunaomba tusipungukiwe katika mahitaji yetu Yahweh ukatupe kama inavyokupendeza wewe..

Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Yahweh tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Mungu wetu tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Jehovah tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Yahweh ukavibariki  vyote tunavyoenda kugusa/kutumia,Mungu wetu ukavitakase na kuvifunika  kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo...
Mungu wetu tunaomba Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Baba wa Mbinguni ukaonekane katika maisha yetu
Yahweh ukaonekane popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni..
Jehovah tukawe salama moyoni Yahweh ukatupe macho ya kuona masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Mungu wetu ukatupe neema ya kufuata njia zako Baba wa Mbinguni tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu
Yahweh ukatufanye chombo chema Jehovah tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Yesu akaendelea kusema, “Kulikuwa na mtu mmoja mwenye watoto wawili wa kiume. Yule mdogo alimwambia baba yake: ‘Baba, nipe urithi wangu.’ Naye akawagawia mali yake. Baada ya siku chache, yule mdogo aliuza urithi wake, akasafiri na fedha aliyopata, akaenda nchi ya mbali ambako aliitumia ovyo. Alipomaliza kutumia kila kitu, kukatokea njaa kali katika nchi ile, naye akaanza kuhangaika. Akaomba kazi kwa mwananchi mmoja wa huko naye akampeleka shambani mwake kulisha nguruwe. Alitamani kula maganda waliyokula wale nguruwe, ila hakuna mtu aliyempa kitu. Alipoanza kupata akili, akafikiri: ‘Mbona kuna wafanyakazi wengi wa baba yangu wanaokula na kusaza, nami ninakufa njaa? Nitarudi kwa baba yangu na kumwambia: Baba, nimemkosea Mungu, na nimekukosea wewe pia. Sistahili hata kuitwa mwanao. Nifanye kama mmoja wa wafanyakazi wako.’ Basi, akaanza safari ya kurudi kwa baba yake. Alipokuwa bado yu mbali, baba yake alimwona, na kwa moyo wa huruma alimkimbilia, akamkumbatia na kumbusu. “Mwanae akamwambia: ‘Baba, nimemkosea Mungu, na nimekukosea wewe pia. Sistahili hata kuitwa mwanao.’ Lakini baba yake akawaambia watumishi wake: ‘Haraka! Leteni nguo nzuri mkamvike! Mvisheni pete na viatu! Mchinjeni ndama mnono; tule na kusherehekea! Kwa sababu huyu mwanangu; alikuwa amekufa, kumbe yu hai; alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana.’ Wakaanza kufanya sherehe. “Wakati huo kaka yake alikuwa bado shambani. Alipokuwa akirudi na kukaribia nyumbani, akasikia vifijo na ngoma. Akamwita mmoja wa watumishi, akamwuliza: ‘Kuna nini?’ Huyo mtumishi akamwambia: ‘Ndugu yako amerudi nyumbani, na baba yako amemchinjia ndama mnono kwa kuwa amempata akiwa salama salimini.’ Huyo kijana mkubwa akawaka hasira hata akakataa kuingia nyumbani. Baba yake akatoka nje na kumsihi aingie. Lakini yeye akamjibu: ‘Kumbuka! Miaka yote nimekutumikia, sijavunja amri yako hata mara moja. Umenipa nini? Hujanipa hata mwanambuzi mmoja nikafanye sherehe pamoja na rafiki zangu! Lakini mtoto wako huyu aliyekula mali yako pamoja na makahaba, mara tu alipokuja umemchinjia yule ndama mnono.’ Baba yake akamjibu: ‘Mwanangu, wewe uko pamoja nami siku zote, na kila nilicho nacho ni chako. Ilitubidi kufanya sherehe na kufurahi, kwa sababu huyu ndugu yako alikuwa amekufa, kumbe yu mzima; alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana.’”

Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu wenye shida/tabu,Mungu wetu ukawape macho ya rohoni wanaokutafuta kwa bidii na imani,Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea na kufuata njia zako,Yahweh ukawaamshe na kuwasimamisha waliopotea..
Mungu wetu ukawasamehe wote waliokwenda kinyume nawe 
na wameamua kukurudia/kutubu na kukutafuta wewe..
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao,Neema yako ikawe nao,amani ikatawale katika maisha yao,furaha na baraka ziwafuate..
Mungu wetu ukawaongoze na kuwalinda,Baba wa Mbinguni ukawatendee sawasawa na mapenzi yako..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!!

Wapendwa katika Bwana asanteni sana kwa kuwa nami/kunisoma
Mungu aendelee kuwalinda na kuwabariki katika yote ..
Pendo lenu likadumu na Mungu akawatendee sawasawa na mapenzi yake
Nawapenda.





Daudi anafanywa mfalme wa Yuda

1Baada ya mambo haya, Daudi alimwomba Mwenyezi-Mungu shauri, akasema, “Je, niende kwenye mji mmojawapo wa miji ya Yuda?” Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Nenda!” Daudi akamwuliza, “Niende mji upi?” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Nenda kwenye mji wa Hebroni.” 2Hivyo, Daudi alikwenda Hebroni, pamoja na wake zake wawili, Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili, mjane wa Nabali, kutoka mji wa Karmeli. 3Aliwachukua watu wake, kila mtu akiwa pamoja na jamaa yake; nao wakafanya makao yao katika miji iliyokuwa kandokando ya Hebroni.
4Watu wa Yuda walimwendea Daudi huko Hebroni wakampaka mafuta awe mfalme wao.
Daudi aliposikia kuwa watu wa Yabesh-gileadi ndio waliomzika Shauli, 5aliwatuma watu huko Yabesh-gileadi na ujumbe: “Mwenyezi-Mungu na awabariki kwa maana mlionesha utii wenu kwa Shauli, bwana wenu, kwa kumzika. 6Sasa, Mwenyezi-Mungu awafadhili na kuwa mwaminifu kwenu. Nami nitawatendea mema kutokana na jambo mlilolitenda. 7Lakini muwe imara na mashujaa. Shauli, bwana wenu, amekufa, na watu wa Yuda wamenipaka mafuta niwe mfalme wao.”

Ishboshethi anafanywa mfalme wa Israeli

8Abneri mwana wa Neri, kamanda wa jeshi la Shauli alikuwa amemchukua Ishboshethi mwana wa Shauli na kumpeleka huko Mahanaimu. 9Huko, Abneri akamtawaza Ishboshethi kuwa mfalme wa nchi ya Gileadi, Ashuru,2:9 Ashuru; au Asheri. Yezreeli, Efraimu na Benyamini na Israeli yote.
10Ishboshethi alikuwa na umri wa miaka arubaini alipoanza kuitawala Israeli, naye alitawala kwa muda wa miaka miwili. Lakini kabila la Yuda lilimfuata Daudi. 11Daudi alikuwa mfalme wa kabila la Yuda kwa muda wa miaka saba na nusu, makao yake yalikuwa huko Hebroni.

Vita kati ya watu wa Israeli na watu wa Yuda

12Abneri mwana wa Neri, pamoja na maofisa wa Ishboshethi, mwana wa Shauli, waliondoka Mahanaimu na kwenda Gibeoni. 13Yoabu mwana wa Seruya na watumishi wengine wa Daudi, nao walitoka na kukutana na Abneri na watu aliokuwa nao kwenye bwawa lililoko huko Gibeoni. Kikosi kimoja upande mmoja wa bwawa na kingine upande mwingine. 14Abneri akamwambia Yoabu, “Waruhusu vijana wapambane mbele yetu!” Yoabu akamjibu, “Sawa.” 15Ndipo vijana ishirini na wanne wakatolewa: Upande wa kabila la Benyamini na Ishboshethi mwana wa Shauli, vijana kumi na wawili; na upande wa Daudi vijana kumi na wawili.
16Kila mmoja alimkamata adui yake kichwani, akamchoma mpinzani wake upanga, hivyo wote wawili wakaanguka chini, wamekufa. Hivyo, mahali hapo pakaitwa Helkath-hazurimu.2:16 Helhath-hazurimu: Maana yake ni mashamba ya mapanga. Mahali hapo pako huko Gibeoni. 17Vita vya siku hiyo vilikuwa vikali. Abneri na watu wa Israeli walipigwa vibaya na watu wa Daudi. 18Wana watatu wa Seruya: Yoabu, Abishai na Asaheli walikuwapo hapo. Asaheli alikuwa na mbio kama paa. 19Asaheli alimfuatia Abneri moja kwa moja bila kugeuka kulia wala kushoto. 20Abneri alipoangalia nyuma na kumwona Asaheli, alimwambia, “Je, ni wewe Asaheli?” Yeye akamjibu, “Naam, ni mimi.” 21Abneri akamwambia, “Geukia kulia au kushoto, umkamate kijana mmoja na kuchukua nyara zake.” Lakini Asaheli hakuacha kumfuatia. 22Abneri akamwambia Asaheli mara ya pili, “Acha kunifuatia. Kwa nini nikuue? Nitawezaje kuonana na kaka yako Yoabu?” 23Lakini Asaheli alikataa. Hivyo Abneri akampiga mkuki tumboni kinyumenyume,2:23 Hivyo … kinyumenyume: Makala ya Kiebrania si dhahiri. na mkuki huo ukatokeza mgongoni kwa Asaheli. Asaheli akaanguka chini, na kufa papo hapo. Watu wote waliofika mahali alipofia Asaheli, walisimama kimya. 24Lakini Yoabu na Abishai walimfuatia Abneri. Jua lilipokuwa linatua, wakafika kwenye mlima wa Ama, ulioko mashariki ya Gia, katika barabara iendayo jangwa la Gibeoni. 25Watu wa kabila la Benyamini wakajikusanya pamoja wakawa nyuma ya Abneri, hivyo wakaunda kikosi chao; nao wakasimama juu ya mlima. 26Kisha Abneri akamwita Yoabu, “Je, tutapigana siku zote? Je, huoni kwamba mwisho utakuwa mchungu? Je, utaendelea kwa muda gani bila kuwashawishi watu wako waache kuwaandama ndugu zao?” 27Yoabu akamwambia, “Naapa kwa Mungu aliye hai, kwamba kama hungesema jambo hilo, hakika watu wangu wangeendelea kuwaandama ndugu zao hadi kesho asubuhi.” 28Hivyo, Yoabu akapiga tarumbeta na watu wakaacha kuwafuatia watu wa Israeli, wala hawakupigana zaidi. 29Abneri na watu wake walipita bonde la Araba usiku kucha. Wakavuka mto Yordani, wakatembea mchana kutwa hadi Mahanaimu. 30Yoabu aliporudi kutoka kumfuatia Abneri, aliwakusanya watu wake wote, akagundua kuwa watumishi kumi na tisa wa Daudi walikosekana, licha ya Asaheli. 31Lakini watumishi wa Daudi walikuwa wamewaua watu 360 kutoka kabila la Benyamini pamoja na watu wa Abneri. 32Yoabu na watu wake waliuchukua mwili wa Asaheli, wakauzika kwenye kaburi la baba yake, lililoko huko Bethlehemu. Yoabu na watu wake walitembea usiku kucha, na kulipokucha wakafika mjini Hebroni.

2Samweli2;1-32

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.