Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 3 April 2018

Kikombe Cha Asubuhi ;1 Wafalme 21...




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana...
Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Mungu mwenye nguvu,Mungu wa walio hai,Mungu mwenye huruma
Mungu mwenye kuponya,Mungu mwenye kubariki,Mungu mwenye kusamehe
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo.....!!

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea
kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majuku yetu
Sifa na Utukufu tunakurudishia Mungu wetu...

Walipokuwa wakiwaambia hayo, Yesu mwenyewe akasimama kati yao, akawaambia “Amani iwe nanyi.” Wakashtuka na kushikwa na hofu wakidhani wameona mzimu. Lakini yeye akawaambia, “Kwa nini mnafadhaika? Mbona mnakuwa na mashaka mioyoni mwenu? Angalieni mikono na miguu yangu, ya kwamba ni mimi mwenyewe. Nipapaseni mkaone, maana mzimu hauna mwili na mifupa kama mnionavyo.”


Mungu wetu tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na 
kujiachilia mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
Kwakuwaza,Kwakunena,Kwakutenda,Kwakujua/kutojua
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote
waliotukosea
Jehovah usitutie katika majaribu Baba wa Mbinguni tunaomba
utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Jehovah tunaomba 
utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona...


Baada ya kusema hayo, akawaonesha mikono na miguu. Wakiwa bado katika hali ya kutosadiki kwa sababu ya furaha yao, na wakiwa wanastaajabu, akawauliza, “Mnacho chakula chochote hapa?” Wakampa kipande cha samaki wa kuokwa. Akakichukua, akala, wote wakimwona. Halafu akawaambia, “Hii ndiyo maana ya maneno niliyowaambia nilipokuwa pamoja nanyi: Kwamba ilikuwa lazima kukamilisha yote yaliyoandikwa juu yangu katika sheria ya Mose na katika vitabu vya manabii na katika kitabu cha Zaburi.” Kisha, akaziangazia akili zao ili wapate kuelewa Maandiko Matakatifu. Akawaambia, “Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na siku ya tatu atafufuka kutoka kwa wafu, na kwamba ni lazima, kwa jina lake, mataifa yote kuanzia Yerusalemu, yahubiriwe kwamba watu wanapaswa kutubu na kusamehewa dhambi. Nyinyi ni mashahidi wa mambo hayo. Nami mwenyewe nitawapelekeeni yule ambaye Baba aliahidi kumtuma, lakini ngojeni huku mjini mpaka mtakapopewa ile nguvu itokayo juu.”


Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Jehovah tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Yahweh nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Jehovah ukatupe
kama inavyokupendeza wewe...

Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika nyumba/ndoa zetu,Mungu wetu tunaomba ukabariki watoto,wazazi wetu,familia/ndugu
na wote wanaotuzunguka
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Mungu wetu tunaomba ukatamalaki na kutuatamia,Jehovah tukawe
salama rohoni,Baba wa Mbinguni tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Yahweh tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda
kugusa/kutumia Mungu wetu tunaomba ukavitakase na kuvifunika kwa
Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo....
Mungu wetu tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako Baba wa Mbinguni tukasiamamie neno lako amri na sheria zako siku zote za 
maisha yetu Jehovah neema yako na Nuru yako ikaangaze katika
maisha yetu,Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Yahweh na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni..
Mungu wetu tukawe barua njema na tukatumike kama
 inavyokupendeza wewe..
Roho mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi ....

Kisha akawaongoza nje ya mji hadi Bethania, akainua mikono yake juu, akawabariki. Alipokuwa anawabariki, akawaacha; akachukuliwa mbinguni. Wao wakamwabudu, kisha wakarudi Yerusalemu wakiwa na furaha kubwa: Wakakaa muda wote hekaluni wakimsifu Mungu.


Baba wa Mbinguni tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,
wagonjwa,wenye njaa,walio kataliwa,waliokata tamaa,wenye hofu na mashaka,walio katika magumu/majaribu mbalimbali,walio katika
vifungo vya yule mwovu,walio magerezani pasipo 
na hatia waliokwama
kibiashara,wanaotafuta kazi,waliokwama kimasomo,walioumizwa
mioyo,walioelemewa na mizigo mizito Mungu wetu tunaomba ukawatue na ukawapumzishe,Yahweh tunaomba ukawaponye kimwili na kiroho pia
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawatendee kila mmoja na hitaji lake
Mungu wetu ukawavushe na kuwakoa,Yahweh ukaonekane katika 
maisha yao,Mungu wetu ukawape ubunifu na maarifa,Jehovah ukabariki
mashamba yao na kazi zao,Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe Baba wa Mbinguni ukawape neema
ya kujiombea na kufuata njia zako nazo ziwaweke huru...
Ee Baba tunaomba ukasikie kuomba kwetu Mungu wetu ukapokee
na kujibu sala/maombi yetu Mungu wetu ukatende sawasawa
 na mapenzi yako..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwanami/kunisoma
Mungu wetu aendelee kuwabariki na kuwatendea kama
inavyompendeza yeye....
Nawapenda.



Kisa cha shamba la Nabothi

1Nabothi, mwenyeji wa Yezreeli, alikuwa na shamba lake la mizabibu huko Yezreeli, karibu na ikulu ya Ahabu, mfalme wa Samaria. 2Basi, siku moja, Ahabu akamwambia Nabothi, “Nipe shamba lako la mizabibu nilifanye shamba la mboga, kwa sababu liko karibu na nyumba yangu. Nitakupa shamba lingine zuri zaidi, au ukitaka, nitakulipa thamani yake, fedha taslimu.” 3Lakini, Nabothi akamjibu, “Jambo la kukupa wewe urithi nilioupata kwa wazee wangu, Mwenyezi-Mungu na apishe mbali.” 4Hapo, Ahabu akaenda zake nyumbani amejaa chuki na huzuni nyingi, kwa sababu Nabothi, mwenyeji wa Yezreeli, alimwambia kwamba hatampa kile alichorithi kutoka kwa wazee wake. Basi, akajilaza kitandani, akauficha uso wake na kususia chakula.
5Yezebeli, mkewe, akamwendea na kumwuliza, “Mbona umejaa huzuni moyoni hata kula huli?” 6Naye akamwambia, “Kwa sababu nilizungumza na Nabothi, mwenyeji wa Yezreeli, nikamtaka aniuzie shamba lake la mizabibu, ama akipenda nimpe shamba lingine badala ya hilo. Lakini yeye akaniambia, ‘Sitakupa shamba langu la mizabibu.’” 7Hapo, Yezebeli, mkewe, akamwambia, “Anayetawala Israeli ni nani? Si ni wewe? Amka, ule na uchangamke; mimi binafsi nitakupa shamba la mizabibu la Nabothi, Myezreeli.”
8Basi, Yezebeli akaandika barua kadha kwa jina la Ahabu na kuzipiga mhuri wa mfalme. Kisha akapeleka barua hizo kwa wazee na watu mashuhuri walioishi na Nabothi huko mjini. 9Barua zenyewe ziliandikwa hivi: “Pigeni mbiu ya mfungo, mkutane na kumpa Nabothi mahali pa heshima kati ya watu. 10Kisha, tafuteni walaghai wawili wamkabili na kumshtaki wakisema: ‘Wewe umemwapiza Mungu na mfalme.’ Kisha mtoeni nje, mkamuue kwa kumpiga mawe!”
11Basi, wakazi wenzake Nabothi, wazee na watu mashuhuri wa mji wa Yezreeli, wakafanya kama Yezebeli alivyowaagiza. Kwa mujibu wa barua aliyowapelekea, 12wakapiga mbiu ya mfungo, wakakutana na kumweka Nabothi mahali pa heshima kati ya watu. 13Wale walaghai wawili wakaketi kumkabili Nabothi, kisha wakamshtaki hadharani wakisema, “Nabothi amemwapiza Mungu na mfalme.” Basi, Nabothi akatolewa nje ya mji, akauawa kwa kupigwa mawe. 14Kisha, Yezebeli akapelekewa habari kwamba Nabothi amekwisha uawa kwa kupigwa mawe.
15Mara tu Yezebeli alipopata habari kwamba Nabothi amekwisha uawa kwa kupigwa mawe, akamwambia Ahabu, “Inuka! Nenda ukamiliki lile shamba la mizabibu la Nabothi, Myezreeli, ambalo alikataa kukuuzia. Nabothi hayuko hai tena; amekwisha fariki.” 16Mara tu Ahabu aliposikia Nabothi amekwisha fariki, aliinuka kwenda kulimiliki shamba la mizabibu la Nabothi.

Nabii Elia anamkaripia Ahabu

17Basi, neno la Mwenyezi-Mungu likamjia nabii Elia wa Tishbe: 18“Inuka uende kukutana na Ahabu mfalme wa Israeli, ambaye yuko Samaria. Utamkuta katika shamba la mizabibu la Nabothi, akilimiliki. 19Mwambie, Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Umeua na kumiliki pia?’ Mwambie Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Mahali pale mbwa walipoiramba damu ya Nabothi, ndipo watakapoilamba damu yako.’”
20Basi, Ahabu alipomwona Elia, akasema, “Ewe adui yangu, umenifuma?” Elia akamjibu, “Naam! Nimekufuma, kwa sababu wewe umenuia kabisa kutenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu. 21Haya! Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Hakika, nitakuletea maangamizi. Nitakuzoa wewe na kufutilia mbali kila mwanamume wa ukoo wako katika Israeli, awe mtumwa au huru. 22Jamaa yako nitaifanya kama jamaa ya Yeroboamu, mwana wa Nebati, na kama jamaa ya Baasha mwana wa Ahiya, kwa sababu umeiwasha hasira yangu na kuwafanya watu wa Israeli watende dhambi.’ 23Tena, Mwenyezi-Mungu asema hivi juu ya Yezebeli: ‘Mbwa wataula mwili wa Yezebeli humuhumu mjini Yezreeli. 24Naam, yeyote wa jamaa yake atakayefia mjini, mbwa watamla; na yeyote atakayefia shambani, ndege wa angani watamla.’”
25(Hakuna mtu aliyenuia kutenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu kama Ahabu, ambaye alishawishiwa na Yezebeli, mkewe. 26Alitenda machukizo kwa kuabudu sanamu za miungu kama walivyofanya Waamori ambao hapo awali Mwenyezi-Mungu aliwafukuza mbele ya watu wa Israeli). 27Lakini, Ahabu aliposikia maneno hayo, alirarua nguo zake, akajivalia gunia peke yake, akafunga, akawa analala na gunia, na kwenda huko na huko kwa huzuni. 28Basi, ujumbe huu wa Mwenyezi-Mungu ukamjia Elia wa Tishbe: 29“Umeona jinsi Ahabu alivyojinyenyekesha mbele yangu? Basi, kwa kuwa amejinyenyekesha, sitaleta yale maangamizi akiwa hai, lakini nyakati za utawala wa mwanawe nitaiangamiza jamaa yake Ahabu.”



1Wafalme21;1-29


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Monday 2 April 2018

Kikombe Cha Asubuhi ;1 Wafalme 20...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana...
Ni siku/wiki/mwezi mwingine tena Mungu wetu ametuchagua
na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii...
Si kwa uwezo wetu wala si kwa nguvu zetu si kwa akili zetu
wala si kwaujuwaji wetu si kwa utashi wetu si kwamba sisi tumetenda mema sana ni kwa neema/rehema
zake ni Kwa mapenzi yake Mungu wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii
Tumshukuru Mungu wetu katika yote....

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima na kuwa tari ya kwa majukumu yetu
Utukuzwe ee Mungu wetu,Unasthili sifa Baba wa Mbinguni,
Unastahili kuabudiwa Yahweh,Unastahili kuhimidiwa Jehovah
hakuna kama wewe Mungu wetu,Matendo yako ni makuu mno,
Matendo yako yanatisha,Matendo yako ni ya ajabu Baba wa Mbinguni
Neema yako yatutosha ee Mungu wetu...




Jumapili, alfajiri na mapema, wale wanawake walikwenda kaburini wakichukua yale manukato waliyotayarisha. Walikuta lile jiwe limevingirishwa mbali na kaburi. Walipoingia ndani, hawakuuona mwili wa Bwana Yesu. Walipokuwa bado wanashangaa juu ya jambo hilo, mara watu wawili waliovaa mavazi yenye kungaa sana, wakasimama karibu nao. Hao wanawake wakaingiwa na hofu, wakainama chini. Ndipo wale watu wakawaambia, “Kwa nini mnamtafuta aliye hai kati ya wafu? Hayuko hapa; amefufuka. Kumbukeni aliyowaambieni alipokuwa kule Galilaya: ‘Ni lazima Mwana wa Mtu atolewe kwa watu waovu, nao watamsulubisha na siku ya tatu atafufuka.’”

Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishuhsa na 
kujiachilia mikononi mwako Mumgu wetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utusamehe dhambi zetu zote 
tulizozifanya kwa kuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale
wote waliotukosea..
Mungu wetu usitutie katika majaribu Baba wa Mbinguni utuokoe
na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh ututakase miili yetu na akili zetu Jehovah utufunike
kwa Damu ya Bwana na  Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona,kwakupigwa kwakwe
sisi tumepona....


Hapo hao wanawake wakayakumbuka maneno yake, wakarudi kutoka kaburini, wakawapa mitume wale kumi na mmoja na wafuasi wengine habari za mambo hayo yote. Hao waliotoa habari hizo kwa mitume ni: Maria Magdalene, Yoana na Maria mama wa Yakobo, pamoja na wanawake wengine walioandamana nao. Mitume waliyachukua maneno hayo kama yasiyo na msingi, hivyo hawakuamini. Lakini Petro alitoka, akaenda mbio hadi kaburini. Alipoinama kuchungulia ndani, akaiona tu ile sanda. Akarudi nyumbani huku akiwa anashangaa juu ya hayo yaliyotokea.


Jehovah tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Mungu wetu tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Yahweh nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye
kuhitaji
Mungu wetu tusipungukiwe katika mahitaji yetu Jehovah ukatupe
kama inavyokupendeza wewe...


Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi
wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Yahweh  ukavitakase na kuvifunika kwa Damu Ya Bwana wetu Yesu Kristo
Jehovah tunaomba utubariki tuingiapo/tutokapo Mungu wetu ukatamalaki
na kutuatami,Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni Jehovah tunaomba
ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia sauti yako na kuitii
Mungu wetu ukatupe neema ya kufuata njia zako Yahweh tukasimamie
Neno lako,amri na sheria zako siku zote za maisha yetu
Yahweh ukaonekane katika maisha yetu Mungu wetu popote tupitapo
na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni
Yahweh tukanene yaliyo yako Mungu wetu ukatupe hekima,busara,
amani na upendo ukadumu kati yetu..
Mungu wetu ukatufanye chombo chema Jehovah nasi tukatumike
kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....



Siku hiyohiyo, wawili kati ya wafuasi wake Yesu wakawa wanakwenda katika kijiji kimoja kiitwacho Emau, umbali wa kilomita kumi na moja kutoka Yerusalemu. Wakawa wanazungumza juu ya hayo yote yaliyotukia. Walipokuwa wakizungumza na kujadiliana, Yesu mwenyewe akatokea, akatembea pamoja nao. Walimwona kwa macho, lakini hawakumtambua. Akawauliza, “Mnazungumza nini huku mnatembea?” Nao wakasimama kimya, nyuso zao wamezikunja kwa huzuni. Mmoja, aitwaye Kleopa, akamjibu, “Je, wewe ni mgeni peke yako Yerusalemu ambaye hujui yaliyotukia huko siku hizi?” Naye akawajibu, “Mambo gani?” Wao wakamjibu, “Mambo yaliyompata Yesu wa Nazareti. Yeye alikuwa nabii mwenye uwezo wa kutenda na kufundisha mbele ya Mungu na mbele ya watu wote. Makuhani na watawala wetu walimtoa ahukumiwe kufa, wakamsulubisha. Lakini sisi tulitumaini kwamba yeye ndiye angeikomboa Israeli. Zaidi ya hayo yote, leo ni siku ya tatu tangu mambo hayo yalipotendeka. Tena, wanawake wengine wa kwetu wametushtua. Walikwenda kaburini mapema asubuhi, wasiukute mwili wake. Wakarudi wakasema kwamba walitokewa na malaika waliowaambia kwamba alikuwa hai. Wengine wetu walikwenda kaburini wakashuhudia yale waliyosema hao wanawake; ila yeye hawakumwona.” Kisha Yesu akawaambia, “Mbona mu wapumbavu kiasi hicho na mioyo yenu ni mizito hivyo kusadiki yote yaliyonenwa na manabii? Je, haikumpasa Kristo kuteswa, na hivyo aingie katika utukufu wake?” Akawafafanulia mambo yote yaliyomhusu yeye katika Maandiko Matakatifu kuanzia Mose hadi manabii wote. Walipokikaribia kile kijiji walichokuwa wanakiendea, Yesu akafanya kana kwamba anaendelea na safari; lakini wao wakamsihi wakisema, “Kaa pamoja nasi, maana kunakuchwa, na usiku unakaribia.” Basi, akaingia kijijini, akakaa pamoja nao. Alipoketi kula chakula pamoja nao, akachukua mkate, akaubariki, akaumega, akawapa. Mara macho yao yakafumbuliwa, wakamtambua; lakini yeye akatoweka kati yao. Basi, wakaambiana, “Je, mioyo yetu haikuwa inawaka ndani yetu wakati alipokuwa anatufafanulia Maandiko Matakatifu kule njiani?” Wakaondoka saa ileile, wakarudi Yerusalemu; wakawakuta wale mitume kumi na mmoja na wale wengine waliokuwa pamoja nao wamekusanyika wakisema, “Hakika Bwana amefufuka, amemtokea Simoni.” Basi, hao wafuasi wawili wakawajulisha yale yaliyowapata njiani, na jinsi walivyomtambua katika kumega mkate.




Baba wa Mbinguni tazama watoto wako wanaokutafuta kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu kila
mmoja na hitaji lake,Yahweh ukaonekane katika shida zao Mungu wetu
ukawape neema ya kujiombea,kufuta njia zako nazo ziwaweke huru
Yahweh ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe Jehovah
ukawaponye kimwili na kiroho pia,Baba wa Mbinguni neema
yako na Nuru yako ikaangaze katika maisha yao...
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina..!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu wetu mwenye nguvu akawabariki na kuwatendea
sawasawa na mapenzi yake
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba 
ukawe nayi daima...

Nawapenda.


Vita kati ya Ashuru na Israeli
1Ben-hadadi mfalme wa Aramu, alikusanya jeshi lake lote; aliungwa mkono na wafalme wengine thelathini na wawili pamoja na farasi na magari yao ya kukokotwa. Aliuendea mji wa Samaria akauzingira na kuushambulia. 2Kisha, akatuma wajumbe wake mjini kwa mfalme Ahabu wa Israeli, wakamwambia, “Mfalme Ben-hadadi asema hivi: 3‘Fedha na dhahabu yako yote ni mali yangu; wake zako warembo na watoto wako pia ni wangu.’” 4Naye mfalme wa Israeli akajibu, “Bwana wangu mfalme, ulivyosema ni sawa: Mimi ni wako, na vyote nilivyo navyo ni vyako.”
5Baadaye, wajumbe hao wakamrudia tena Ahabu, wakamwambia, “Mfalme Ben-hadadi asema hivi: ‘Nilikutumia ujumbe unipe dhahabu, fedha, wake zako pamoja na watoto wako. 6Sasa, kesho wakati kama huu, nitatuma watumishi wangu waje kuisaka ikulu na nyumba za watumishi wako, wachukue kila kitu unachothamini.’” 7Ndipo Ahabu mfalme wa Israeli, akawaita viongozi wote wa nchi, akawaambia, “Sasa, oneni jinsi jamaa huyu anavyotaka kututaabisha! Ametuma ujumbe kwamba anataka wake zangu, watoto wangu, dhahabu na fedha yangu. Nami sikumkatalia!” 8Wazee na watu wote wakamwambia, “Usimjali wala usikubali.”
9Basi, Ahabu akawaambia wajumbe wa Ben-hadadi, “Mwambieni bwana wangu mfalme hivi: ‘Niko radhi kutimiza matakwa yako ya kwanza, lakini haya ya pili sikubali hata kidogo.’” Hapo, wajumbe hao wakaenda zao na kumhabarisha tena mfalme Ben-hadadi. 10Ben-hadadi akamtumia Ahabu ujumbe huu: “Miungu na waniulie mbali, nakuapia, ikiwa huko Samaria kutabakia mavumbi ya kutosha gao moja kwa kila mmoja wa watu wangu wengi!” 11Mfalme Ahabu wa Israeli akajibu, “Mwambieni mfalme Ben-hadadi kwamba shujaa hujisifu baada ya vita, si kabla!” 12Ben-hadadi alipokea ujumbe huu wa Ahabu wakati yeye na wafalme waliomwunga mkono walipokuwa mahemani mwao wanakunywa. Basi, akayaweka majeshi yake katika hali ya tahadhari, kuushambulia mji.
13Wakati huohuo, nabii mmoja akamwendea Ahabu, mfalme wa Israeli, akamwambia, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Unaona wingi wa majeshi haya? Leo hii nitawatia mikononi mwako, nawe utatambua kwamba mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.’” 14Naye Ahabu akauliza, “Kwa msaada wa nani?” Nabii akasema, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Kwa msaada wa vijana wanaotumikia jeshi chini ya wakuu wa wilaya.’” Naye mfalme akauliza, “Ni nani atakayeanza kupigana?” Nabii akajibu, “Wewe!”
15Basi, mfalme Ahabu akakagua vijana waliotumikia jeshi chini ya wakuu wa wilaya, jumla yao watu 232. Kisha akakagua jeshi la Israeli, wanajeshi 7,000.
16Basi, mnamo adhuhuri, wakati Ben-hadadi na wale wafalme wenzake thelathini na wawili waliomwunga mkono walipokuwa mahemani mwao wakinywa na kulewa, mashambulizi yakaanza. 17Wale vijana waliotumikia jeshi chini ya wakuu wa wilaya, wakatangulia. Wakati huo, Ben-hadadi alikuwa amekwisha peleka askari wa doria, nao wakampa habari kwamba kulikuwa na kundi la watu waliokuja kutoka Samaria. 18Ben-hadadi akawaambia, “Wakamateni wakiwa hai. Hata kama wanakuja kwa vita au kwa amani.”
19Basi, wale vijana waliotumikia jeshi chini ya wakuu wa wilaya, wakaongoza mashambulizi, huku, nyuma yao, wanafuata wanajeshi wa Israeli. 20Kila mmoja wao akamuua adui mmoja. Watu wa Aramu wakatimua mbio, nao askari wa Israeli wakawafuatilia; lakini Ben-hadadi, mfalme wa Aramu, akiwa amepanda farasi, akatoroka na baadhi ya askari wapandafarasi. 21Basi, mfalme wa Israeli akashinda vita, akateka farasi na magari ya kukokotwa mengi, na kuwaua watu wa Aramu kwa wingi.
22Kisha, yule nabii akamwendea mfalme wa Israeli, akamwambia, “Jiandae upya ufikirie vizuri la kufanya. Mwakani, mfalme wa Aramu atakuja kupambana nawe tena.”

Waaramu wanawashambulia tena watu wa Israeli

23Watumishi wa mfalme Ben-hadadi walimshauri hivi: “Miungu ya Waisraeli ni miungu ya milimani; ndiyo maana tulishindwa. Lakini, bila shaka tutawashinda kama tukipigana nao mahali tambarare. 24Sasa, wastaafishe wale wafalme thelathini na wawili na mahali pao uweke majemadari. 25Unda jeshi kama lilelile ulilopoteza, farasi na magari ya kukokotwa kama yale uliyopoteza. Kisha, tutapigana nao mahali tambarare na bila shaka tutawazidi nguvu.” Mfalme Ben-hadadi akasikia ushauri wao, akafanya hivyo.
26Mara baada ya majira ya baridi, mfalme Ben-hadadi aliwakusanya watu wake, akaenda mjini Afeka kupigana na watu wa Israeli. 27Nao watu wa Israeli walikusanywa na kupewa silaha, wakaenda kuwakabili Waaramu. Watu wa Israeli walipiga kambi, wakaonekana kama vikundi vidogovidogo vya mbuzi, lakini Waaramu walitapakaa kote nchini.
28Ndipo, mtu mmoja wa Mungu akamkaribia mfalme wa Israeli, akamwambia, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Kwa kuwa Waaramu wamesema kwamba mimi Mwenyezi-Mungu ni Mungu wa milimani wala si Mungu wa nchi tambarare, nitakupa ushindi dhidi ya jeshi hili kubwa, nawe utatambua kwamba mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.’”
29Watu wa Israeli na Waaramu walipiga kambi kwa muda wa siku saba, wakikabiliana; siku ya saba, mapigano yakaanza. Siku hiyohiyo, watu wa Israeli wakaua askari wa miguu 100,000. 30Waliosalia, walikimbilia mjini Afeka. Huko, kuta za mji ziliwaangukia na kuwaua watu 27,000 waliobakia. Ben-hadadi pia alikimbia na kujificha katika chumba fulani cha ndani, mjini. 31Watumishi wake wakamwendea wakamwambia, “Tumesikia kwamba wafalme wa Israeli ni watu wenye huruma. Basi, turuhusu tujifunge magunia viunoni na kamba shingoni, tumwendee mfalme wa Israeli. Huenda atayasalimisha maisha yako.” 32Basi, wakajifunga magunia viunoni na kamba shingoni mwao, wakamwendea mfalme wa Israeli, wakamwambia, “Mtumishi wako, Ben-hadadi, anakusihi akisema ‘Tafadhali uniache nipate kuishi.’ Ahabu akasema, ‘Kumbe anaishi bado? Yeye ni ndugu yangu.’” 33Watumishi wa Ben-hadadi walikuwa wanategea ishara yoyote ile ya bahati njema, basi Ahabu aliposema hivyo, wao wakadakia wakasema, “Naam, Ben-hadadi ni ndugu yako!” Ahabu akawaambia, “Nendeni mkamlete kwangu.”
Basi, Ben-hadadi alipomjia, Ahabu akamtaka aketi naye katika gari lake la kukokotwa. 34Kisha, Ben-hadadi akamwambia, “Miji yote ambayo baba yangu alimnyanganya baba yako, nitakurudishia. Unaweza kuanzisha masoko huko Damasko kama alivyofanya baba yangu huko Samaria.” Ahabu akajibu, “Nitakuachilia kwa masharti hayo.” Hapo, akafanya mkataba naye na kumwacha huru.

Nabii amlaani Ahabu

35Kwa amri ya Mwenyezi-Mungu, mmojawapo wa wanafunzi wa manabii, akamwambia mwenzake, “Nipige, tafadhali.” Lakini mwenzake akakataa kumpiga. 36Naye akamwambia, “Kwa kuwa umekataa kutii amri ya Mwenyezi-Mungu, basi, mara tu utakapoachana nami, simba atakuua.” Na kweli, mara tu alipoachana naye, akakutana na simba, akamuua.
37Kisha, huyo mwanafunzi akamkuta mtu mwingine, akamwambia, “Nipige tafadhali.” Mtu huyo akampiga na kumjeruhi. 38Basi, nabii akaondoka, akaenda akakaa kando ya njia, kumngojea mfalme wa Israeli, huku amejifunga kitambaa usoni, asitambulike. 39Mfalme alipokuwa anapita, nabii akamlilia akisema, “Bwana, mimi mtumishi wako nilikuwa mstari wa mbele vitani; akaja askari mmoja, akaniletea mateka mmoja na kuniambia, ‘Mlinde mtu huyu; akitoroka utalipa kwa maisha yako wewe binafsi, au kwa vipande 3,000 vya fedha.’ 40Lakini nilipokuwa nikishughulikashughulika, mtu huyo akatoroka.” Mfalme wa Israeli akamwambia, “Ndivyo itakavyokuwa hukumu yako; umejihukumu mwenyewe.”
41Hapo, nabii akaondoa harakaharaka kitambaa usoni mwake, naye mfalme akamtambua kuwa mmoja wa manabii. 42Basi, nabii akamwambia mfalme, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Kwa kuwa umemwachilia mtu ambaye niliamuru auawe akuponyoke, basi, maisha yake utalipa kwa maisha yako, na watu wake kwa watu wako.’” 43Basi, mfalme wa Israeli akaenda zake nyumbani Samaria, amejaa chuki na huzuni nyingi.



1Wafalme20;1-43


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Thursday 29 March 2018

Kikombe Cha Asubuhi ;1 Wafalme 19...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana
Tumshukuru katika yote...

Mungu wetu,Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Mungu mwenye nguvu,Mungu wa walio hai,Mungu mwenye huruma
Mungu wa Abraham,Isaka na Yakobo..
Yahweh..!Jehovah..!Adonai..!El him..! El Qanna..!El Olam..!El Elyon..!El Shaddai..!
Emanuel-Mungu pamoja nasi...!!

Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha 
kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!


Huu ndio ushahidi Yohane alioutoa wakati viongozi wa Wayahudi kule Yerusalemu walipowatuma makuhani na Walawi, wamwulize: “Wewe u nani?” Yohane hakukataa kujibu swali hilo, bali alisema waziwazi, “Mimi siye Kristo.” Hapo wakamwuliza, “Basi, wewe ni nani? Je, wewe ni Elia?” Yohane akajibu, “La, mimi siye.” Wakamwuliza, “Je, wewe ni yule nabii?” Yohane akawajibu, “La!” Nao wakamwuliza, “Basi, wewe ni nani? Wasema nini juu yako mwenyewe? Tuambie, ili tuwapelekee jibu wale waliotutuma.” Yohane akawajibu, “Mimi ndiye yule ambaye nabii Isaya alisema habari zake: ‘Sauti ya mtu anaita jangwani: Nyosheni njia ya Bwana.’”


Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale
wote waliotukosea
Mungu wetu usitutie majaribuni Baba wa Mbinguni tunaomba
utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote
Nguvu za giza,nguvu za mapepo,nguvu za mizimu,nguvu za 
mpinga Kristo zishindwe katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni
utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu  Yesu Kristo wa 
Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona...



Hao watu walikuwa wametumwa na Mafarisayo. Basi, wakamwuliza Yohane, “Kama wewe si Masiha, wala Elia, wala yule nabii, mbona wabatiza?” Yohane akawajibu, “Mimi nabatiza kwa maji, lakini yuko mmoja kati yenu, msiyemjua bado. Huyo anakuja baada yangu, lakini mimi sistahili hata kumfungua kamba za viatu vyake.” Mambo haya yalifanyika huko Bethania, ngambo ya mto Yordani ambako Yohane alikuwa anabatiza.

Jehovah tunaomba ukabarikiki kazi za mikono yetu
Mungu wetu tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Yahweh nasi tutakatende sawasawa na mapenzi yako
Mungu wetu tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza 
kuwabariki wenye kuhitaji
Jehovah tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu
 ukatupe kama inavyokupendeza wewe....


Mungu wetu tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia Baba wa Mbinguni tunaomba
utubariki tuingiapo/tutokapo Jehovah tunaomba ukabariki vyote
tunavyoenda kugusa/kutumia Mungu wetu ukavitakase na kuvifunika
kwa Damu ya Bwana wetu Yesu kristo
Yahweh tukawe salama rohoni Mungu wetu ukatupe macho ya kuona
na masikio ya kusikia sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote
 za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo
na ikajaulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni
Neema na Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu,amani ikatawale,
Upendo ukadumu kati yetu..
Ukaatufanye chombo chema Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi.....


Kesho yake, Yohane alimwona Yesu akimjia, akasema, “Huyu ndiye Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu! Huyu ndiye niliyeongea juu yake niliposema: ‘Baada yangu anakuja mtu mmoja aliye mkuu zaidi kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa!’ Mimi mwenyewe sikumfahamu, lakini nimekuja kubatiza kwa maji ili watu wa Israeli wapate kumjua.” Yohane alishuhudia hivi: “Nilimwona Roho akishuka kama njiwa kutoka mbinguni na kutua juu yake. Mimi sikumjua, lakini yule aliyenituma kubatiza watu kwa maji alikuwa ameniambia: ‘Mtu yule utakayemwona Roho akimshukia kutoka mbinguni na kukaa juu yake, huyo ndiye anayebatiza kwa Roho Mtakatifu.’ Mimi nimeona na nimeshuhudia kwamba huyu ndiye Mwana wa Mungu.”

Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako Wagonjwa Baba tunaomba ukawaponye na ukawape imani na uvumilivu wanao wauguza
tazama wenye njaa Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki mashamba yao
kazi zao ,Biashara zao Mungu wetu ukawape ubunifu na maarifa katika
utendaji wao wakapate chakula cha kutosha kuweka akiba na
kusadia wengine..
Yahweh tunaomba ukawaguse kwa mkonoi wako wenye nguvu
wote wenye shida/tabu,walio kataliwa,waliokata tamaa,walio katika
vifungo vya yule mwovu,walio magerezani pasipo na hatia
wenye hofu na mashaka,wanaopitia magumu majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawavushe salama Yahweh tunaomba ukawaweke
huru na haki ikatendeke Jehovah ukawafungue na kuwaokoa
Mungu wetu ukawaponye kiroho na kimwili pia Baba wa Mbinguni
ukamguse kila mmoja na hitaji lake Yahweh wakawe salama rohoni
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yao
Yahweh ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Jehovah ukawape neema ya kujiombea na kufuata njia zako
Mungu wetu ukawabariki na kuwatendea sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina..!!

Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana kwakuwanami/kunisoma
Baba wa Mbinguni akawabariki,Roho Mtakatifu akawaongeze
katika yote,msipungukiwe katika mahitaji yenu Mungu Baba akawape
sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.

Elia mlimani Horebu

1Mfalme Ahabu alimsimulia mkewe Yezebeli mambo yote aliyofanya Elia na jinsi alivyowaua manabii wa Baali kwa upanga. 2Yezebeli akatuma mjumbe kwa Elia amwambie: “Miungu waniulie mbali, nakuapia, ikiwa saa hizi kesho sitakuwa nimekufanya kama mmoja wa hao manabii.” 3Elia akakimbilia mjini Beer-sheba mkoani Yuda, alikomwacha mtumishi wake, 4naye akatembea mwendo wa siku nzima kuingia jangwani. Basi, akafika, akaketi chini ya mti mmoja, mretemu. Hapo, akaomba afe, akisema, “Imetosha! Siwezi tena. Ee Mwenyezi-Mungu, sasa utoe uhai wangu. Mimi si bora kuliko wazee wangu.”
5Basi, Elia akalala chini ya mti huo, akashikwa na usingizi. Punde, malaika akaja, akamgusa na kumwambia, “Amka ule.” 6Elia alipotazama, akaona mkate uliookwa juu ya makaa, na chupa ya maji karibu na kichwa chake. Basi, akala, akanywa, akalala tena. 7Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamjia tena mara ya pili, akamgusa na kumwambia, “Amka ule, la sivyo safari itakuwa ngumu mno kwako.” 8Elia akaamka, akala na kunywa. Kisha akatembea kwa nguvu ya chakula hicho mwendo wa siku arubaini, mchana na usiku, mpaka Horebu, mlima wa Mungu.
9Huko, akafika penye pango, akakaa humo. Mara neno la Mwenyezi-Mungu likamjia: “Elia! Unafanya nini hapa?” 10Naye akasema, “Naona uchungu na wivu, ewe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa majeshi, kwa sababu watu wa Israeli wamevunja agano lako, wakazibomoa madhabahu zako na kuwaua manabii wako kwa upanga; ni mimi tu niliyebaki, nami pia wananiwinda, waniue!”
11Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Nenda ukasimame mlimani, mbele yangu mimi Mwenyezi-Mungu.” Basi, Mwenyezi-Mungu akapita na kuuvumisha upepo mkali ambao uliporomosha milima na kuvunja miamba. Lakini Mwenyezi-Mungu hakuwemo katika upepo huo. Upepo ukapita, kukawa na tetemeko la ardhi. Lakini Mwenyezi-Mungu hakuwemo katika tetemeko la ardhi. 12Tetemeko likapita, kukawa na moto. Lakini Mwenyezi-Mungu hakuwemo katika moto huo. Baada ya moto, pakatokea sauti ndogo, tulivu. 13Basi, Elia aliposikia sauti hiyo, alijifunika uso kwa joho lake, akatoka na kusimama mlangoni mwa pango. Hapo, akasikia sauti, “Elia! Unafanya nini hapa?” 14Naye akasema, “Naona uchungu na wivu, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa majeshi, kwa sababu watu wa Israeli wamevunja agano lako, wakazibomoa madhabahu zako na kuwaua manabii wako kwa upanga; ni mimi tu niliyebaki, nami pia wananiwinda waniue!”
15Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Rudi kwa kupitia njia ya jangwani mpaka Damasko. Utakapofika, mpake Hazaeli mafuta awe mfalme wa Aramu. 16Naye Yehu, mwana wa Nimshi, mpake mafuta awe mfalme wa Israeli. Elisha, mwana wa Shafati, wa Abel-mehola, utampaka mafuta awe nabii mahali pako. 17Basi, yeyote atakayenusurika upanga wa Hazaeli, Yehu atamuua, na yeyote atakayenusurika upanga wa Yehu, Elisha atamuua. 18Lakini, nitaacha hai watu 7,000 nchini Israeli, ambao hawajamwinamia Baali, wala kuibusu sanamu yake.”

Elisha anaitwa kuwa nabii

19Elia akaondoka, akamkuta Elisha, mwana wa Shafati, analima. Hapo, palikuwa na jozi kumi na mbili za ng'ombe wanalima, na jozi ya Elisha ilikuwa ya nyuma kabisa. Basi, Elia akavua joho lake na kumtupia. 20Hapo, Elisha akawaacha ng'ombe wake, akamfuata Elia mbio na kumwambia, “Niruhusu kwanza niende kumpa baba yangu na mama yangu busu la kwaheri, kisha nikufuate.” Elia akamjibu, “Nenda! Kwani nimekuzuia?”19:20 “Nenda! Kwani nimekuzuia?” au “Nenda, urudi upesi kwa kuwa jambo nililokutendea ni la maana.”
21Basi, Elisha akamwacha Elia, akairudia jozi yake ya ng'ombe, akawachinja ng'ombe hao na kuwapika akitumia miti ya nira kama kuni, akawapa watu, wakala. Kisha akaondoka, akamfuata Elia na kuwa mtumishi wake.



1Wafalme19;1-21


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.