Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 20 April 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Wafalme 12......




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Mungu wetu yu mwema sana tumshukuru katika yote...

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea
kuiona leo hii
Asante kwa uwepo wako,pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa makujukumu yetu
Utukuzwe ee Mungu wetu,hakuna kama wewe Baba wa Mbinguni
Neema yako yatutosha ee Mungu wetu
Sifa na Utukufu  tunakurudishia wewe Baba wa Mbinguni..!!


Mimi Paulo, mtume wa Yesu Kristo kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu na Yesu Kristo tumaini letu, nakuandikia Timotheo mwanangu halisi katika imani. Nakutakia neema, huruma na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Kristo Yesu Bwana wetu. Napenda ukae huko Efeso, kama nilivyokuomba nilipokuwa ninakwenda Makedonia. Wako watu fulani huko wanaofundisha mafundisho ya uongo. Wakomeshe watu hao. Waambie waachane na zile hadithi tupu na orodha ndefu za mababu, ambazo huleta tu ubishi, wala haviwajengi watu katika mpango ujulikanao kwa imani. Shabaha ya amri hii ni kuhimiza mapendo yatokayo katika moyo safi, dhamiri njema, na imani ya kweli.

Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
 na kujiachilia mikononi mwako ee Mungu wetu
Jehovah tunaomba utusamehe makosa yetu yote tuliyoyafanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza
kuwasamehe wale wote waliotukosea
Mungu wetu utuepushe katika majaribu Yahweh utuokoe na
 yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike na damu ya Bwana na Mwokozi wetu
Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Watu wengine wamepotoka na kugeukia majadiliano yasiyo na maana. Wanapenda kuwa waalimu wa sheria, lakini hawaelewi maneno yao wenyewe au mambo wanayosisitiza. Twajua kwamba sheria ni njema, kama ikitumiwa ipasavyo. Lakini tunapaswa kukumbuka kwamba sheria haziwekwi kwa ajili ya watu wema, bali kwa ajili ya wahalifu na wasiotii, wasiomcha Mungu na wenye dhambi, watu wasio na dini na wa kidunia, watu wanaowaua baba na mama zao, au wauaji wowote wale; sheria imewekwa kwa ajili ya waasherati, wafiraji, wezi wa watu, waongo na wanaoapa uongo au wanaofanya chochote ambacho ni kinyume cha mafundisho sahihi. Mafundisho hayo hupatikana katika injili ya Mungu mtukufu na mwenye heri ambayo mimi nimekabidhiwa niihubiri.

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Yahweh nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Jehovah tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu 
tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi
wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Jehovah tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Yahweh tunaomba ukatamalaki na kutuatamia
Mungu wetu tukawe salama rohoni Baba wa Mbinguni tunaomba
ukatupe macho ya kuona na  masikio ya kusikia sauti yako na kuitii
Jehovah tunaomba ukatupe neema ya kutambua mema na mabaya
Yahweh tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako Baba wa Mbinguni
tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Yahweh ukaonekane katika maisha yetu Jehovah popote tupitapo
na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni
Mungu wetu ukatufanye chombo chema Baba wa Mbinguni
nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Namshukuru Bwana wetu Yesu Kristo aliyenipa nguvu kwa ajili ya kazi yangu. Namshukuru kwa kuniona mimi kuwa ni mwaminifu, akaniteua nimtumikie, ingawa pale awali mimi nilimtukana na kumtesa na kumdhulumu. Lakini Mungu alinionea huruma, kwa sababu sikuwa na imani bado, na hivyo sikujua nilichokuwa ninafanya. Lakini Bwana wetu alinijalia neema yake kwa wingi, akanipa imani na upendo katika kuungana na Kristo Yesu. Usemi huu ni wa kuaminika, na tena unafaa kukubaliwa kabisa: Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuwaokoa wenye dhambi. Nami ni mkosefu zaidi kuliko hao wote, lakini Mungu alinionea huruma, ili Kristo aoneshe uvumilivu wake wote kwangu mimi, kama mfano kwa wale wote ambao baadaye watamwamini na kupokea uhai wa milele. Kwake yeye aliye Mfalme wa milele, asiyekufa, asiyeonekana na aliye Mungu pekee – kwake viwe heshima na utukufu milele na milele! Amina. Mwanangu Timotheo, nakukabidhi amri hii kufuatana na maneno ya unabii yaliyosemwa zamani juu yako. Yatumie maneno hayo yawe silaha yako katika kupigana vita vizuri, na ushike imani yako na dhamiri njema. Watu wengine hawakusikiliza dhamiri zao na hivyo wakaiharibu imani yao. Miongoni mwao ni Humenayo na Aleksanda ambao nimewakabidhi kwa Shetani, ili wafundishwe wasimtukane Mungu.

Mungu wetu tazama watoto wako wanaokutafuta/kukuomba kwa bidii na imani
Yahweh tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
Jehovah tunaomba ukawatendee kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukasikie kulia kwao Mungu wetu
tunaomba ukawafute machozi yao
Yahweh ukaonekane katika mapito/majaribu yao
Mungu wetu tunaomba ukawaponye kimwili na kiroho pia
Jehovah tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawape neema ya ujiombea,kufuata
njia zako na kusimamia Neno lako nalo likawaweke huru
Nuru yako ikaangze katika maisha yao,amani ikatawale upendo
ukadumu kati yao...
Ee Baba tunaomba ukasikie kuomba kwetu Mungu wetu ukapokee sala/maombi yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami/kunisoma
Mungu mwenye nguvu na baraka akawabariki na kuwatendea
sawasawa na mapenzi yake
Amani,furaha na upendo vikadumu kati yetu...
Nawapenda.


Mfalme Yoashi wa Yuda

(2Nya 24:1-16)

1Katika mwaka wa saba wa enzi ya mfalme Yehu wa Israeli Yoashi alianza kutawala Yuda huko Yerusalemu, naye akatawala kwa muda wa miaka arubaini huko Yerusalemu. Mama yake alikuwa Sibia, kutoka Beer-sheba. 2Wakati wa maisha yake yote alitenda mema mbele ya Mwenyezi-Mungu, kwa sababu kuhani Yehoyada alikuwa akimfundisha. 3Hata hivyo, mahali pa juu pa kuabudia miungu hapakuharibiwa, na watu waliendelea kutambika na kufukiza ubani huko.
4Yoashi akaita makuhani na kuwaamuru, akisema, “Fedha yote inayoletwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu ikiwa imetokana na uuzaji wa vitu vitakatifu, fedha ya kila mtu kadiri alivyoandikiwa, na fedha ambayo mtu huvutwa kuitoa kwa hiari katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, 5makuhani wazipokee kutoka kwa kila mtu; nao warekebishe nyumba popote panapohitajika marekebisho.”
6Lakini hata baada ya miaka ishirini na mitatu ya mfalme Yoashi makuhani walikuwa bado hawajafanya marekebisho yoyote ya nyumba. 7Kwa hiyo mfalme Yoashi alimwita kuhani Yehoyada na makuhani wengine na kuwauliza, “Mbona hamrekebishi nyumba? Basi, msichukue fedha kutoka kwa watu mnaowatumikia, bali mtazileta, ili nyumba irekebishwe.” 8Makuhani wakakubali wasipokee fedha tena kutoka kwa watu na pia wakaahidi kutofanya marekebisho ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu.
9Yehoyada akachukua sanduku na kutoboa tundu kwenye kifuniko chake, kisha akaliweka kwenye madhabahu upande wa kulia, mtu anapoingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Nao makuhani waliokuwa katika zamu langoni waliweka fedha zote zilizoletwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. 10Kila walipoona kuwa mna fedha nyingi sandukuni, katibu wa mfalme na kuhani mkuu waliingia na kuhesabu na kuzifunga katika vifurushi fedha zote zilizopatikana katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. 11Kisha baada ya kuzipima waliwapa wafanyakazi waliosimamia nyumba ya Mwenyezi-Mungu, nao wakawalipa maseremala na wajenzi, waliorekebisha nyumba ya Mwenyezi-Mungu; 12pia waashi na wakata-mawe, zikatumiwa kununulia mbao na mawe yaliyochongwa ili kufanyia marekebisho nyumba ya Mwenyezi-Mungu na kutimiza mahitaji mengine yote ya marekebisho ya nyumba. 13Lakini pesa hizo hazikutumiwa kwa kulipia utengenezaji wa mabirika ya fedha, mikasi ya kukatia tambi za mishumaa, mabakuli, tarumbeta, wala kwa vyombo vingine vyovyote vya dhahabu au vya fedha. 14Zote zilitumiwa kwa kuwalipa wafanyakazi waliozitumia kufanya marekebisho ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. 15Wafanyakazi waliosimamia kazi hii walikuwa waaminifu kabisa, kwa hiyo hapakuwa na haja ya kuwataka watoe hesabu ya matumizi ya fedha hizo. 16Fedha zilizotolewa kuwa sadaka za hatia na sadaka za kuondoa dhambi hazikuingizwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu; hizo zilikuwa ni mali ya makuhani.
17Wakati huo Hazaeli mfalme wa Aramu akaushambulia mji wa Gathi na kuuteka. Lakini Hazaeli alipoelekea Yerusalemu ili aushambulie, 18Yoashi mfalme wa Yuda alichukua sadaka zote zilizowekwa wakfu na babu zake wafalme wa Yuda: Yehoshafati, Yehoramu na Ahazia, na kuongeza zile zake, pamoja na dhahabu yote iliyokuwa katika hazina ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu na katika ikulu, akazituma kwa Hazaeli mfalme wa Aramu. Naye Hazaeli akatoka Yerusalemu.
19Matendo mengine yote ya mfalme Yoashi yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Yuda.
20Maofisa wake walikula njama dhidi yake, wakamuulia katika nyumba ya Milo kwenye barabara inayoelekea Sila. 21Waliomuua ni Yozakari mwana wa Shimeathi na Yehozabadi mwana wa Shomeri watumishi wake. Halafu walimzika katika makaburi ya kifalme katika mji wa Daudi; naye Amazia, mwanawe, akatawala mahali pake.


2Wafalme12;1-21


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.



Thursday 19 April 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Wafalme 11......




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana
Tumshukuru Mungu wetu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Mungu mwenye nguvu,Mungu wa walio hai,Mungu wa Abrahamu,Isaka
na Yakobo,Baba wa Yatima,Mume wa Wajane,Baba wa Upendo,Baba wa baraka,Baba wa huruma,Mungu mwenye kusamehe..
Matendo yako ni makuu mno,Mtendo yako ni ya ajabu,Matendo yako yanatisha,Neema yako yatutosha ee Mungu wetu...!!

Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea
kuiona leo hii
Asante kwa uwepo wako,pumzi/uzima,afya na kuwa tayari 
kwa majukumu yetu
Utukuzwe ee Mungu wetu...
Sifa na Utukufu tunakurudishia wewe Baba wa Mbinguni!!



Sasa yahusu kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo na kukusanywa kwetu pamoja, tukae naye. Ndugu, tunawaombeni sana msifadhaike upesi moyoni, na wala msitiwe wasiwasi kwa sababu ya madai kwamba siku ya Bwana imekwisha fika. Labda inadhaniwa kwamba jambo hili limetokana na uaguzi fulani, mahubiri au barua inayosemekana kuwa imetoka kwetu. Msikubali kudanganywa na mtu yeyote kwa namna yoyote ile. Maana siku hiyo haitakuja mpaka kwanza ule uasi utokee na yule Mwovu aonekane, ambaye mwisho wake ni kuangamizwa kabisa. Yeye hujikuza yeye mwenyewe juu ya kila kitu wanachokiona watu kuwa ni mungu, au wanachokiabudu; hata ataingia na kuketi ndani ya hekalu la Mungu akijidai kuwa Mungu.


Mungu wetu tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
Kwakuwaza,Kwakunena,Kwakutenda,Kwakujua/Kutojua
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale
wote waliotukosea
Yahweh usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuokoe na yule
mwovu kazi zake zote
Baba wa Mbinguni tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Yahweh utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo
wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona...

Je, hamkumbuki kwamba niliwaambieni haya yote wakati nilipokuwa pamoja nanyi? Lakini kuna kitu kinachomzuia sasa, nanyi mwakijua kitu hicho. Basi, huyo Mwovu ataonekana wakati wake ufaao. Hata hivyo, Mwovu huyo aliyefichika anafanya kazi sasa, lakini hataonekana mpaka yule anayemzuia aondolewe. Hapo ndipo Mwovu atakapotokea; lakini Bwana Yesu anapokuja atamuua kwa pumzi ya kinywa chake na kumwangamiza kwa mngao wa kuja kwake. Huyo Mwovu atakuja na nguvu za Shetani na kufanya kila namna ya miujiza na maajabu ya uongo, na kutumia udanganyifu wa kila namna kwa wale walio katika mkumbo wa kupotea. Hao watapotea kwa sababu hawakuupokea na kuupenda ule ukweli ili waokolewe. Ndiyo maana Mungu amewaweka chini ya nguvu ya upotovu, wauamini uongo. Matokeo yake ni kwamba wote wasioamini ukweli, bali wanafurahia dhambi, watahukumiwa.

Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Mungu wetu nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Jehovah tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Jehovah ukatupe kama inavyokupendeza wewe....

Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,
familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Jehovah tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Mungu wetu tunaomba ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo..
Mungu wetu tunaomba ukatamalaki na kutuatamia,Baba wa Mbinguni
tukawe salama rohoni Yahweh tunaomba ukatupe macho ya kuona na 
masikio ya kusikia sauti sauti yako na kuitii..
Jehovah tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako Yahweh
tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu
Baba wa Mbinguni ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo
na ikajulikane kwamba upo Mungu wetu
Yahweh ukatupe hekima,busara,utu wema  na upendo ukadumu kati yetu
Ukatufanye chombo chema Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe...
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Tunapaswa kumshukuru Mungu daima kwa ajili yenu nyinyi ndugu, nyinyi mnaopendwa na Bwana, kwa maana Mungu amewateua tangu mwanzo mpate kuokolewa kwa nguvu ya Roho, mfanywe watu wake watakatifu kwa imani yenu katika ukweli. Mungu aliwaitieni jambo hili kwa njia ya Habari Njema tuliyowahubirieni; aliwaiteni mpate kupokea sehemu yenu katika utukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo. Basi, ndugu, simameni imara na kuzingatia yale mafundisho tuliyowafundisheni kwa mahubiri yetu na barua yetu. Tunamwomba Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe na Mungu Baba yetu ambaye alitupenda na kwa neema yake akatujalia faraja ya milele na tumaini jema, aifariji mioyo yenu na kuwaimarisheni ili muweze daima kutenda na kusema yaliyo mema.

Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,wenye shida/tabu,wagonjwa,wenye njaa,
waliokataliwa,waliokata tamaa,wenye hofu na mashaka,walio katika
vifungo vya yule mwovu,walio magerezani pasipo na hatia na wengine
wote kulingana na mahitaji yao...
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawatendee kila mmoja na hitaji lake
Yahweh tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Jehovah tunaomba ukawaponye kimwili na kiroho pia
Baba wa Mbinguni ukawaokoe na kuwaweka huru
Jehovah ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Mungu wetu ukabariki mashamba/kazi zao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawape neema ya kujiombea
kufuata njia zako na kusimamia Neno lako nalo likawaweke huru
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao,amani ikatawale kati yao
Ee Baba wa Mbinguni tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako...
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki katika yote yampendezayo
Upendo wa Mungu ukawe nanyi daima...
Nawapenda.


Malkia Athalia wa Yuda

(2Nya 22:10-23:15)

1Mara Athalia, mamake mfalme Ahazia, alipoona kuwa mwanawe ameuawa, alitoka, akaangamiza jamii yote ya kifalme. 2Lakini Yehosheba binti ya mfalme Yoramu, dada yake Ahazia, alimchukua kwa siri Yoashi mwana wa Ahazia, kutoka miongoni mwa wana wa mfalme waliokuwa karibu kuuawa. Alimficha11:2 Kiebrania hakina “alimficha”. yeye pamoja na yaya wake katika chumba cha kulala. Hivyo walimficha ili Athalia asimwone na kumwua. 3Yoashi alikaa naye kwa muda wa miaka sita akiwa amefichwa ndani ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, wakati Athalia alipokuwa akitawala nchi.
4Lakini katika mwaka wa saba Yehoyada alituma ujumbe na kuwakusanya makapteni wa Wakari na walinzi; akaamuru wamjie katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, naye akafanya nao mapatano na kuwaapisha humo katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Halafu akawaonesha Yoashi mwana wa mfalme Ahazia. 5Kisha akatoa amri: “Mtafanya hivi: Mtakapokuja kushika zamu siku ya Sabato, theluthi moja italinda ikulu; 6theluthi nyingine ikiwa kwenye lango la Suri na theluthi nyingine ikiwa kwenye lango nyuma ya walinzi. Hivyo ndivyo mtakavyolinda ikulu ili isivunjwe. 7Yale makundi mawili ambayo humaliza zamu yao siku ya Sabato yatashika zamu katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu kumlinda mfalme. 8Mtamzunguka mfalme, kila mtu na silaha yake mkononi na mtu yeyote atakayethubutu kuwakaribia lazima auawe. Lazima mkae na mfalme, awe anatoka au anakaa.”
9Makapteni walitii amri zote alizotoa kuhani Yehoyada. Kila ofisa akawachukua watu wake wote, wale waliokuwa wamemaliza zamu na wale waliokuwa wanaingia kushika zamu siku ya Sabato, basi wakamwendea kuhani Yehoyada. 10Kisha kuhani akawapa makapteni mikuki na ngao zilizokuwa mali ya mfalme Daudi, na ambazo zilikuwa zimewekwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, 11nao walinzi walisimama kuanzia upande wa kusini wa nyumba mpaka upande wa kaskazini wa nyumba na kuzunguka madhabahu na nyumba ili kumzunguka mfalme;11:11 kumzunguka mfalme: Makala ya Kiebrania si dhahiri. kila mtu akiwa ameshika mkuki wake mkononi. 12Halafu akamtoa nje mwana wa mfalme, akamvika taji kichwani, na kumpa ule ushuhuda; wakamtawaza na kumpaka mafuta; wakapiga makofi na kusema, “Aishi mfalme!”
13Naye Athalia aliposikia sauti za walinzi pamoja na za watu wengine, aliwaendea hao watu waliokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. 14Alipochungulia akamwona mfalme mpya amesimama karibu na nguzo kwenye lango la hekalu, kama ilivyokuwa desturi, huku makapteni na wapiga tarumbeta wakiwa kando ya mfalme; na wakazi wote wakishangilia na kupiga tarumbeta; ndipo aliporarua nguo zake na kusema kwa sauti kubwa, “Uhaini! Uhaini!”
15Kisha kuhani Yehoyada akaamuru makapteni wa jeshi akisema; “Mtoeni nje katikati ya askari, na ueni mtu yeyote atakayemfuata.” Kwa sababu kuhani alisema, “Asiuawe katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.” 16Basi, wakamkamata, wakampeleka na kumpitisha kwenye Lango la Farasi kuelekea ikulu, naye akauawa huko.

Mabadiliko ya Yehoyada

(2Nya 23:16-21)

17Kisha Yehoyada akafanya agano kati ya Mwenyezi-Mungu na mfalme na watu kwamba watakuwa watu wa Mwenyezi-Mungu; kadhalika alifanya agano kati ya mfalme na watu. 18Halafu wakazi wote wakaenda kwenye nyumba ya Baali na kuibomoa, wakavunja madhabahu pamoja na sanamu zake, hata wakamuua Matani, kuhani wa Baali mbele ya madhabahu. Kuhani Yehoyada akaweka walinzi kulinda nyumba ya Mwenyezi-Mungu. 19Aliwachukua makapteni, Wakari na wakazi wote; nao wakamsindikiza mfalme kutoka nyumba ya Mwenyezi-Mungu wakapitia katika lango la walinzi mpaka ikulu. Naye akakikalia kiti cha enzi. 20Kwa hiyo, wakazi wote walijawa furaha; na mji wote ulikuwa mtulivu, baada ya Athalia kuuawa kwa upanga katika ikulu.
21 11:21 Kiebrania: 12:1. Yoashi alianza kutawala Yuda akiwa na umri wa miaka saba.



2Wafalme11;1-21


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Wednesday 18 April 2018

MAKAMU WA RAIS AKUTANA NA WATANZANIA NA WAINGEREZA ,LONDON


Picha na Habari za Freddy Macha

Ulikuwa mkutano mfupi uliokusudia kutoa shukrani kwa wafadhili na Watanzania London wanaosaidia nyumbani. Fadhila hupitia Jumuiya ya Waingereza na Watanzania (BTS) na kitengo chake cha TDT = shirika la Mfuko wa Maendeleo Tanzania. BTS ilianzishwa mwaka 1975, na mlezi wake sasa hivi ni Rais mstaafu Ali Mwinyi.

BTS ilimkaribisha Makamu wa Rais Mheshimiwa Suluhu Samia, aliyekuja London wiki hii kudhuruia mkutano wa Viongozi wa Jumuiya ya Madola.

Kawaida viongozi hutegemewa hotuba ndefu zenye maelezo yanayochosha masikio.

Mhe Suluhu alitua chuo kikuu cha lugha za Afrika na Mashariki ya Kati (SOAS) akasalimiana na kupeana mikono na wananchi wa pande zote mbili. Hiyo tu ilitosha kuonesha imani yake kwa wananchi wachapa kazi wa pande hizi mbili.

 Makamu wa Rais Mhe Suluhu Samia akizungumza na Dk Mohammed Hamza, kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Uingereza




 Balozi wetu Uingereza, Dk Asha Rose Migiro akiwa na Kaimu Balozi Uingereza Tanzania, Mhe Marc Thayre


 Mwenyekiti wa Jumuiya Ya Uingereza na Tanzania – BTS. Dk Andrew Coulson aliyefungua na kufunga kikao cha Brunei Gallery, SOAS.




 Baadhi ya Watanzania waliohudhuria. Kutoka kushoto, Kiondo Wilkins, Dk Alex Paurine, Simon Mzuwanda na Joe Warioba.

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Wafalme 10......




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...
Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea
kuiona leo hii
Asante kwa uwepo wako,pumzi/uzima,afya na kuwa tayari 
kwa majukumu yetu
Utukuzwe ee Mungu wetu,Usifiwe Baba wa Mbinguni,
Uabudiwe Yahweh,Uhimidiwe Jehovah..!!
Sifa na Utukufu tunakurudishia wewe Baba wa Mbinguni!!




Kwa sababu hiyo nilizuiwa mara nyingi kuja kwenu. Lakini maadamu sasa nimemaliza kazi yangu pande hizi, na kwa kuwa kwa miaka mingi nimekuwa na nia kubwa ya kuja kwenu, natumaini kufanya hivyo sasa. Ningependa kuwaoneni nikiwa safarini kwenda Spania na kupata msaada wenu kwa safari hiyo baada ya kufurahia kuwa kwa muda pamoja nanyi. Lakini, kwa sasa nakwenda kuwahudumia watu wa Mungu kule Yerusalemu.

Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
Kwakuwaza,Kwakunena,Kwakutenda,Kwakujua/Kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Jehovah usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuoke na yule
mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi
wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi
tupate kupona...

Maana makanisa ya Makedonia na Akaya yemeamua kutoa mchango wao kuwasaidia watu wa Mungu walio maskini huko Yerusalemu. Wao wenyewe wameamua kufanya hivyo; lakini, kwa kweli, hilo ni jukumu lao kwa hao. Maana, ikiwa watu wa mataifa mengine wameshiriki baraka za kiroho za Wayahudi, wanapaswa nao pia kuwahudumia Wayahudi katika mahitaji yao ya kidunia. Nitakapokwisha tekeleza kazi hiyo na kuwakabidhi mchango huo uliokusanywa kwa ajili yao, nitawatembeleeni nyinyi nikiwa safarini kwenda Spania.

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Jehovah tunaomba ukatupe maarifa na ubunifu katika utendaji
Yahweh nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji,Jehovah tunaomba tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe  kama inavyokupendeza wewe...

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi
wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba utubariki tuingiapo/tutokapo Mungu wetu
tunaomba ukabariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana
wetu Yesu Kristo
Mungu wetu tunaomba ukatamalaki na kutuatamia
Yahweh tukawe salama rohoni Jehovah tunaomba ukatupe macho
ya kuona na masikio ya kuisikia sauti yako na kuitii
Jehovah tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Baba wa Mbinguni tukasimamie Neno lako amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu..
Ukatupe neema ya kutambua mema na mabaya

Neema yako na Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
upendo ukadumnu kati yetu
Ukatufanye chombo chema Mungu wetu nasi tukatumike
kama inavyokupendeza wewe...
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Najua ya kuwa nikija kwenu nitawaletea wingi wa baraka za Kristo. Basi, ndugu zangu, nawasihi kwa Bwana wetu Yesu Kristo na kwa upendo uletwao na Roho, mniunge mkono kwa kuniombea kwa Mungu. Ombeni nipate kutoka salama miongoni mwa wale wasioamini walioko Uyahudi, nayo huduma yangu huko Yerusalemu ipate kukubaliwa na watu wa Mungu walioko huko. Hivyo, Mungu akipenda, nitaweza kuja kwenu na moyo wa furaha, nikapumzike pamoja nanyi. Mungu aliye chanzo cha amani na awe nanyi nyote! Amina!


Mungu wetu tazama watoto wako wanaokutafuta lwa bidii/imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
Yahweh ukawatendee kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Jehovah ukawape neema ya kufuata njia zako Mungu wetu ukawape
macho ya rohoni Yahweh ukawape neema ya kusimamia Neno lako
nalo likawaweke huru...
Amani na neema ikawafutae nuru ikaangazwe katika maisha yao
Ee Baba ukasikie kulia kwao Mungu wetu tunaomba ukawafute machozi
yao Jehovah ukasikie na ukapokee sala/maombi yetu
Baba wa Mbinguni ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina..!!

Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana kwakuwa nami/kunisoma
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea sawasawa na mapenzi
yake,Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
vikawe nanyi daima...
Nawapenda.



Wazawa wa Ahabu wauawa

1Katika mji wa Samaria kulikuwa na wana sabini wa Ahabu. Yehu akaandika barua na kuzituma kwa watawala wa mji,10:1 Baadhi ya tafsiri za kale; Kiebrania: Yezreeli. kwa viongozi na kwa walinzi wa wana wa Ahabu. Barua yenyewe ilisema hivi:
2“Kwa kuwa mnao miongoni mwenu wana wa mfalme, kadhalika mnao farasi na magari, silaha na miji ya ngome, 3mchagueni na kumtawaza mwenye uwezo zaidi kati ya wana wa mfalme; halafu mpige vita kwa ajili ya ukoo wa mfalme.”
4Watawala wa Samaria waliogopa sana na kusema, “Tunawezaje kumpiga Yehu hali mfalme Yoramu na mfalme Ahazia hawakuweza?” 5Kwa hiyo ofisa mkuu wa nyumba ya mfalme na ofisa mkuu wa mji, wakishirikiana na viongozi wengine na walinzi, wakampelekea Yehu ujumbe huu: “Sisi tu watumwa wako, na tuko tayari kufanya lolote unalosema. Lakini hatutamtawaza mtu yeyote kuwa mfalme; fanya unavyoona vyema.” 6Yehu akawaandikia barua nyingine akiwaambia: “Ikiwa kweli mko tayari kufuata maagizo yangu, leteni hapa Yezreeli vichwa vya wana wa bwana wenu; nivipate kesho wakati kama huu.”
Wana sabini wa mfalme Ahabu waliishi kwa viongozi wa Samaria, ambao walikuwa walezi wao. 7Basi, barua ilipowafikia waliwachukua hao wana wa mfalme na kuwakata wote sabini. Waliweka vichwa vyao vikapuni na kumpelekea Yehu huko Yezreeli.
8Kisha mtumishi mmoja akamwendea na kusema, “Vichwa vya wana wa mfalme vimekwisha letwa.” Ndipo akaamuru, “Viwekwe chini katika mafungu mawili kwenye lango la mji; halafu viache vikae huko mpaka asubuhi.” 9Asubuhi yake akatoka, akasimama na kuwaambia watu wote, “Nyinyi ni waadilifu, angalia mimi nilikula njama dhidi ya bwana wangu na kumuua. Lakini ni nani aliyewaua hawa wote? 10Jueni ya kwamba maneno yote aliyosema Mwenyezi-Mungu kuhusu jamaa ya Ahabu yametimia. Mwenyezi-Mungu ameyafanya hayo aliyosema kwa njia ya mtumishi wake Elia.” 11Ndipo Yehu akaua jamaa yote ya Ahabu iliyokuwa inakaa Yezreeli, pamoja na maofisa wake na marafiki na makuhani wake; hakumwacha mtu yeyote.
Jamaa za Ahazia wauawa
12Baadaye Yehu aliondoka Yezreeli, akaelekea Samaria. Akiwa njiani mahali panapoitwa “Kambi ya Wachungaji,” 13alikutana na jamaa za marehemu Ahazia mfalme wa Yuda akawauliza, “Nyinyi ni kina nani?” Wakamjibu, “Sisi ni jamaa za Ahazia. Tumeteremka huku kuwatembelea wana wa mfalme na wana wa malkia.” 14Kisha akasema, “Wakamateni wakiwa hai.” Wakawakamata watu arubaini na wawili, wakawaulia karibu na kisima cha “Kambi ya Wachungaji.” Hakuna aliyebaki hata mmoja. 15Yehu akatoka tena na alipofika njiani akakutana na Yehonadabu mwana wa Rekabu; Yehu akamsalimu, kisha akamwambia “Wewe una mawazo sawa na yangu? Je, utajiunga nami na kunisaidia?” Yehonadabu akamjibu, “Naam, nitajiunga nawe:”
Yehu akasema, “Basi, nipe mkono wako.” Wakashikana mikono na Yehu akampandisha garini mwake. 16Akamwambia, “Fuatana nami ili ujionee jinsi nilivyo mwaminifu kwa Mwenyezi-Mungu.” Basi, wakasafiri pamoja garini mwake. 17Walipofika Samaria, Yehu aliua jamaa yote ya Ahabu bila kumwacha hata mmoja wao. Ikawa sawa kama Mwenyezi-Mungu alivyomwambia Elia itakavyokuwa.
Wafuasi wa Baali wauawa
18Yehu akawakusanya watu wa Samaria na kuwaambia, “Mfalme Ahabu alimtumikia Baali kidogo tu, lakini mimi nitamtumikia zaidi. 19Waite manabii wote wa Baali, wafuasi wake wote na makuhani. Ni sharti kila mmoja afike, kwani nataka kumtolea Baali tambiko kubwa, na yeyote atakayekosa kufika atauawa.” Hiyo ilikuwa ni njama ya Yehu ili apate kuwaua wafuasi wa Baali. 20Yehu akaamuru: “Alika mkutano mkubwa wa ibada ya Baali!” Tangazo likatolewa, 21na Yehu akapeleka habari katika nchi yote ya Israeli ili wafuasi wote wa Baali wahudhurie kila mmoja. Wakaja wote na kujaa katika hekalu la Baali kutoka pembe moja mpaka nyingine. 22Ndipo Yehu akamwagiza aliyesimamia mavazi matakatifu akisema, “Toa mavazi hayo na kuwapa watu waliohudhuria ibada.” Msimamizi akatoa mavazi hayo, akawapa. 23Halafu Yehu akaingia katika hekalu la Baali akifuatana na Yehonadabu na kuwaambia waliokuwa hekaluni, “Hakikisheni kwamba waliomo hekaluni ni wale wamwabuduo Baali tu, na kwamba hakuna mtu yeyote anayemwabudu Mwenyezi-Mungu. 24Kisha akaingia pamoja na Yehonadabu kumtolea Baali matambiko na tambiko za kuteketezwa. Yehu alikuwa ameweka watu themanini nje ya hekalu na kuwapa maagizo haya: ‘Waueni watu hawa wote. Yeyote atakayemwacha hata mmoja wao atoroke atalipa kwa maisha yake!’”
25Mara Yehu alipomaliza kutoa tambiko ya kuteketezwa, aliwaambia walinzi na maofisa, “Ingieni mkawaue wote. Msimwache hata mmoja atoroke!” Wakaingia na panga zao tayari na kuwaua wote, kisha wakatoa maiti zao nje. Ndipo wakaingia chumba cha ndani cha hekalu, 26na kutoa nguzo takatifu na kuiteketeza kwa moto. 27Wakaharibu nguzo pamoja na hekalu; wakaligeuza hekalu kuwa choo; na hivyo ndivyo ilivyo mpaka hivi leo.
28Hivyo ndivyo Yehu alivyofuta ibada za Baali katika Israeli. 29Lakini alifuata dhambi ya Yeroboamu mwana wa Nebati ya kuwaongoza Waisraeli watende dhambi. Aliweka sanamu za ndama wa dhahabu huko Betheli na Dani. 30Mwenyezi-Mungu akamwambia Yehu, “Umewatendea wazawa wa Ahabu yale yote niliyotaka uwatendee. Kwa hiyo nimekuahidi kuwa wazawa wako hadi kizazi cha nne watatawala Israeli.” 31Lakini Yehu hakutii sheria za Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa moyo wake wote. Badala yake, alifuata mfano wa Yeroboamu aliyewapotosha watu wa Israeli wakatenda dhambi.
Kifo cha Yehu
32Wakati huo Mwenyezi-Mungu alianza kupunguza eneo la nchi ya Israeli. Mfalme Hazaeli wa Aramu akashinda nchi yote ya Israeli, 33kutoka upande wa mashariki ya mto Yordani, na nchi za Gileadi, Gadi, Reubeni na Manase na kutoka Aroeri ulioko kwenye bonde la Arnoni, kwenye nchi za Gileadi na Bashani.
34Matendo mengine yote ya Yehu na vitendo vyake vya ushujaa yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli. 35Akafariki na kuzikwa Samaria. Mwanae Yehoahazi akatawala mahali pake. 36Yehu alitawala Israeli akiwa Samaria kwa miaka ishirini na minane.




2Wafalme10;1-37


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Tuesday 17 April 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Wafalme 9......



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...
Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu mwenye nguvu,Mungu mwenye huruma
,Mungu mwenye kuponya,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Muweza wa yote Alfa na Omega...!!

Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea
kuiona leo hii
Asante kwa uwepo wako,pumzi/uzima,afya na kuwa tayari 
kwa majukumu yetu
Neema yako yatutosha ee Mungu wetu...!!


Sisi tulio imara katika imani tunapaswa kuwasaidia wale walio dhaifu wayakabili matatizo yao. Tusijipendelee sisi wenyewe tu. Kila mmoja wetu anapaswa kumpendeza jirani yake kwa wema ili huyo apate kujijenga katika imani. Maana Kristo hakujipendelea mwenyewe; ila alikuwa kama yasemavyo Maandiko: “Kashfa zote walizokutolea wewe zimenipata mimi.” Maana, yote yaliyoandikwa yameandikwa kwa ajili ya kutufundisha sisi ili kutokana na saburi na faraja tupewayo na hayo Maandiko Matakatifu tupate kuwa na matumaini. Mungu aliye msingi wa saburi na faraja yote, awajalieni nyinyi kuwa na msimamo mmoja kufuatana na mfano wake Kristo Yesu, ili nyinyi nyote, kwa nia moja na sauti moja, mumtukuze Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo.

Tazama jana imepita  ee Mungu wetu leo ni siku mpya Baba wa Mbinguni
na kesho ni siku nyingine Jehovah....
Mungu wetu tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na 
kujiachilia mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba utusamehe makosa yetu yote tuliyoyafanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote
waliotukosea
Jehovah usitutie majaribuni Mungu wetu utuokoe na yule mwovu na kazi
zake zote
Baba wa Mbinguni tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Yahweh tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu
Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Basi, karibishaneni kwa ajili ya utukufu wa Mungu kama naye Kristo alivyowakaribisheni. Maana, nawaambieni Kristo aliwatumikia Wayahudi apate kuonesha uaminifu wa Mungu, na zile ahadi Mungu alizowapa babu zetu zipate kutimia; ili nao watu wa mataifa mengine wapate kumtukuza Mungu kwa sababu ya huruma yake. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Kwa hiyo nitakusifu miongoni mwa watu wa mataifa. Nitaziimba sifa za jina lako.” Tena Maandiko yasema: “Furahini, enyi watu wa mataifa; furahini pamoja na watu wake.” Na tena: “Enyi mataifa yote, msifuni Bwana; enyi watu wote, msifuni.” Tena Isaya asema: “Atatokea chipukizi katika ukoo wa Yese, naye atawatawala watu wa mataifa; nao watamtumainia.” Basi, Mungu aliye msingi wa matumaini, awajazeni furaha yote na amani kutokana na imani yenu; tumaini lenu lipate kuongezeka kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.

Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Mungu wetu tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Mungu wetu tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Yahweh nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji
Mungu wetu tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni
ukatupe kama inavyokupendeza wewe...

Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu
Familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Mungu wetu tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Jehovah ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu tunaomba ukatamalaki na kutuatamia
Yahweh tukawe salama rohoni Baba wa Mbinguni ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia sauti yako na kuitii
Jehovah tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu
Mungu wetu ukatupe neema ya kutambua mema na mabaya
Baba wa Mbinguni ukaonekane katika maisha yetu neema yako na Nuru
yako ikaangaze katika maisha yetu,hekima,busara vikawe nasi  upendo
ukadumu kati yetu....
Ukatufanye chombo chema Mungu wetu nasi tukatumike kama 
inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Ndugu zangu, mimi binafsi nina hakika kwamba nyinyi pia mmejaa wema, elimu yote, na mnaweza kushauriana nyinyi kwa nyinyi. Lakini nimewaandikia hapa na pale katika barua hii bila woga, nipate kuwakumbusheni juu ya mambo fulani. Nimefanya hivyo kwa sababu ya neema aliyonijalia Mungu ya kuwa mtumishi wa Yesu Kristo kwa watu wa mataifa. Ni jukumu langu la kikuhani kuihubiri Habari Njema ya Mungu ili watu wa mataifa mengine wapate kuwa tambiko inayokubaliwa na Mungu, tambiko iliyotakaswa na Roho Mtakatifu. Kwa hiyo, nikiwa nimeungana na Kristo Yesu, naweza kujivunia huduma yangu kwa ajili ya Mungu. Sithubutu kusema kitu kingine chochote isipokuwa tu kile ambacho Kristo Yesu amekifanya kwa kunitumia mimi ili watu wa mataifa wapate kutii. Amefanya hivyo kwa maneno na vitendo, kwa nguvu ya miujiza na maajabu, na kwa nguvu ya Roho wa Mungu. Basi, kwa kusafiri kila mahali, tangu kule Yerusalemu mpaka Iluriko, nimeihubiri kikamilifu Habari Njema ya Kristo. Nia yangu imekuwa daima kuihubiri Habari Njema popote pale ambapo jina la Kristo halijapata kusikika, nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Watu wote ambao hawakuambiwa habari zake wataona; nao wale ambao hawajapata kusikia, wataelewa.”

Baba wa Mbinguni tazama wenye shida/tabu,wagonjwa,wenye njaa,
wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,waliokatika vifungo vya
yule mwovu,walio magerezani pasipo na hatia,walio kataliwa,
walio kata tamaa,wenye hofu na mashaka,walioumizwa rohoni,
waliokwama kibiashara,waliokwama kielimu...
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Jehovah tunaomba ukawaponye na kuwaokoa,Mungu wetu ukawaweke huru na haki ikatendeke ,Baba wa Mbinguni ukabariki mashamba,biashara na kazi  zao
Yahweh tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Jehovah tunaomba ukawape neema ya kujiombea na kufuata njiza zako
nazo zikawaweke huru
Neema na nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Ee Mungu wetu tunaomba ukasikie na ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami/
kunisoma Mungu aendelee kuwabariki na kuwatendea kama inavyompendeza yeye,Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na Upendo
wa Mungu Baba vikawe nanyi daima....
Nawapenda. 
  

Yehu atawazwa kuwa mfalme wa Israeli

1Wakati huohuo nabii Elisha alimwita mmoja wa wanafunzi wa manabii, akamwambia, “Jitayarishe kwenda Ramothi katika Gileadi. Chukua chupa hii ya mafuta 2na utakapofika huko, mtafute Yehu mwana wa Yehoshafati na mjukuu wa Nimshi. Mchukue kando chumbani mbali na wenzake, 3kisha chukua chupa hii ya mafuta, ummiminie kichwani na kumwambia, ‘Mwenyezi-Mungu asema hivi: Nimekupaka mafuta kuwa mfalme wa Israeli.’ Kisha fungua mlango na kuondoka upesi utakavyoweza.”
4Basi, Nabii huyo kijana akaenda Ramothi Gileadi. 5Alipofika aliwakuta makamanda wa jeshi mkutanoni. Akasema “Nina ujumbe wako, kamanda.”
Yehu akamwuliza, “Ni nani kati yetu unayemwambia?” Akamjibu, “Wewe, kamanda.” 6Ndipo wote wawili wakaingia chumba cha ndani na huko nabii akamtia Yehu mafuta kichwani na kumwambia, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema, ‘Nakupaka mafuta uwe mfalme juu ya watu wangu Israeli. 7Nawe utaipiga jamaa ya bwana wako Ahabu ili nimlipize kisasi Yezebeli damu ya watumishi wangu manabii na ya watumishi wangu wote. 8Utafanya hivyo kwa sababu jamaa yote ya Ahabu itaangamia; pia nitamkatilia mbali kila mwanamume wa jamaa ya Ahabu awe mtumwa au mtu huru. 9Jamaa yake itakuwa kama jamaa ya Yeroboamu mwana wa Nebati na ya Baasha mwana wa Ahiya. 10Yezebeli hatazikwa na mtu, maiti yake italiwa na mbwa katika nchi ya Yezreeli.’” Baada ya kusema hayo, nabii akaondoka chumbani na kukimbia.
11Yehu aliporudi kwa wenzake, mmoja wao alimwuliza, “Kuna shida yoyote? Mwendawazimu huyu alitaka nini kwako?” Yehu akawajibu, “Mnajua alichotaka.” 12Nao wakamwambia, “Hiyo si kweli! Tuambie alilosema!” Akawaambia, “Aliniambia kwamba Mwenyezi-Mungu amesema, ‘Nimekutawaza kuwa mfalme wa Israeli.’”
13Mara moja makamanda wenzake wakavua mavazi yao, wakayarundika pamoja kwenye ngazi ili asimame juu yake, wakapiga tarumbeta na kupaza sauti, “Yehu ni mfalme!”

Mfalme Yoramu wa Israeli auawa

14Yehu mwana wa Yehoshafati, ambaye pia alikuwa mjukuu wa Nimshi, alikula njama dhidi ya Yoramu. Yoramu na watu wote wa Israeli walikuwa Ramoth-gileadi kulinda zamu dhidi ya mfalme Hazaeli wa Aramu. 15Lakini mfalme Yoramu alikuwa amerudi Yezreeli ili apone majeraha aliyopata wakati wa kupigana vitani na mfalme Hazaeli wa Aramu. Yehu aliwaambia maofisa wenzake; “Ikiwa mtakubaliana nami, mtu yeyote asitoke Ramothi kwenda Yezreeli kupeleka habari hizi.” 16Ndipo akapanda gari lake na kuelekea Yezreeli. Yoramu alikuwa bado hajapona, na Ahazia mfalme wa Yuda alikuwa amemtembelea.
17Mlinzi aliyekuwa kwa zamu juu ya mnara wa Yezreeli akasema, “Naona watu wakija na gari!” Yoramu akajibu, “Chagua mpandafarasi mmoja, umtume ili akutane nao, awaulize ‘Kuna amani?’” 18Basi, mjumbe huyo alipokwenda alikutana na Yehu na kumwambia, “Mfalme anauliza: Kuna amani?” Yehu akajibu, “Kwa nini unauliza kuhusu amani? Wewe geuka ufuatane nami!” Mlinzi juu ya mnara akasema, “Mjumbe amewafikia, lakini harudi.” 19Ndipo mjumbe wa pili akatumwa, ambaye pia alimwuliza Yehu swali hilohilo. Yehu akamwambia vivyo hivyo, “Kwa nini unauliza kuhusu amani? Wewe geuka ufuatane nami!” 20Kwa mara nyingine tena mlinzi akasema “Mjumbe amewafikia lakini harudi.” Halafu akaongeza, “Uendeshaji wa gari ni kama wa Yehu mwana wa Nimshi; kwa sababu yeye huendesha kwa kasi.”
21Basi, Yoramu mfalme wa Israeli akaamuru akisema, “Tayarisha gari.” Nao walitayarisha gari lake. Kisha Yoramu mfalme wa Israeli na Ahazia mfalme wa Yuda waliondoka kila mmoja akipanda gari lake, wakaenda kukutana na Yehu. Walimkuta katika uwanja wa Nabothi Myezreeli. 22Ikawa Yoramu, alipomwona Yehu, alimwuliza, “Je, kuna amani, Yehu?” Yehu akamjibu, “Amani gani, wakati makahaba na wachawi wa Yezebeli ni wengi?” 23Yoramu aligeuza gari lake na kuondoka, huku akimwambia Ahazia, “Huu ni uhaini Ahazia!” 24Yehu akatwaa upinde wake na kutupa mshale ambao ulipenya mabega ya Yoramu na kuchoma moyo wake, naye akafa papo hapo garini mwake. 25Yehu akamwambia msaidizi wake Bidkari, “Chukua hiyo maiti yake uitupe katika shamba hilo la Nabothi Myezreeli. Kwa maana, kumbuka wewe na mimi tulipokuwa tumepanda farasi wetu nyuma ya baba yake Ahabu, jinsi Mwenyezi-Mungu alivyonena maneno haya dhidi yake. 26Mwenyezi-Mungu alisema, ‘Kwa ile damu ya Nabothi na kwa damu ya wanawe niliyoona jana naapa kwamba nitakulipiza kisasi katika shamba hilo.’ Kwa hiyo, chukua maiti ya Yoramu uitupe katika shamba la Nabothi kama alivyosema Mwenyezi-Mungu.”

Mfalme Ahazia wa Yuda auawa

27Ahazia mfalme wa Yuda alipoona yaliyotukia alikimbia akielekea Nyumba ya Bustani, huku akifuatwa na Yehu. Yehu akawaamuru watu wake, “Muueni naye pia!” Nao wakampiga mshale akiwa garini kwenye njia ya kupanda Guri karibu na mji wa Ibleamu. Halafu alikimbilia Megido na kufia huko. 28Maofisa wake wakaichukua maiti yake ndani ya gari lake na kuipeleka Yerusalemu; na huko akazikwa katika makaburi ya kifalme katika mji wa Daudi.
29Ahazia alianza kutawala juu ya Yuda katika mwaka wa kumi na moja wa enzi ya Yoramu mwana wa Ahabu.

Malkia Yezebeli auawa

30Yehu alipofika Yezreeli, Yezebeli alikuwa amekwisha pata habari za mambo yaliyotokea. Alijipaka rangi machoni na kupanga nywele zake, ndipo akaenda dirishani na kuangalia chini. 31Yehu alipokuwa akiingia langoni Yezebeli alisema, “Unakuja kwa amani, ewe Zimri! Wewe unayewaua mabwana zako?” 32Yehu akaangalia juu na kusema “Ni nani aliye upande wangu?” Maofisa wawili au watatu wakatokeza vichwa vyao kumwangalia kutoka dirishani, 33naye Yehu akawaambia, “Mtupe chini!” Wakamtupa chini na damu yake ikatapakaa juu ya ukuta na kwenye farasi. Yehu akapitisha farasi na gari lake juu ya maiti yake 34na kuingia katika jumba la kifalme, na huko akala na kunywa. Halafu akaamuru: “Mzikeni mwanamke huyo aliyelaaniwa; kwa kuwa ni binti mfalme.” 35Ndipo walipokwenda kumzika; lakini hawakuona chochote isipokuwa fuvu la kichwa, mifupa ya mikono na miguu. 36Kisha walirudi na kumpasha Yehu habari hizi, naye akasema, “Hivi ndivyo Mwenyezi-Mungu alivyotabiri kupitia kwa mtumishi wake Elia Mtishbi akisema, ‘Mbwa wataula mwili wa Yezebeli katika nchi ya Yezreeli. 37Maiti yake Yezebeli itakuwa kama mavi shambani katika nchi ya Yezreeli, hivyo kwamba hakuna atakayeweza kumtambua.’”




2Wafalme9;1-37


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.