Maombolezo
(Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Yungiyungi. Zaburi ya Daudi)
1Uniokoe, ee Mungu;
maji yamenifika shingoni.
2Ninazama ndani ya matope makuu,
hamna hata mahali pa kuweka miguu.
Nimetumbukia kwenye kilindi cha maji,
nachukuliwa na mawimbi.
3Niko hoi kwa kupiga yowe,
na koo langu limekauka.
Macho yangu yamefifia,
nikikungojea ewe Mungu wangu.
4 Taz Zab 35:19; Yoh 15:25 Watu wengi kuliko nywele zangu ndio wanichukiao bure.
Wana nguvu sana hao wanaotaka kuniua,
hao wanaonishambulia kwa mambo ya uongo.
Je, nirudishe kitu ambacho sikuiba?
5Ee Mungu, waujua upumbavu wangu;
makosa yangu hayakufichika kwako.
6Wanaokutumainia wasiaibishwe kwa sababu yangu,
ee Bwana Mwenyezi-Mungu wa majeshi;
wanaokutafuta, wasione fedheha kwa sababu yangu
ee Mungu wa Israeli.
7Kwa ajili yako nimefedheheshwa,
aibu imefunika uso wangu.
8Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu,
kaka na dada zangu hawanitambui.
9 Taz Yoh 2:17; Rom 15:3 Upendo wangu kwa nyumba yako unanimaliza.
Kashfa zote wanazokutolea wewe zimenipata mimi.
10Nilipojinyenyekesha kwa kufunga,
watu walinilaumu.
11Nilipovaa vazi la gunia kuomboleza,
wao walinidharau.
12Watu wananisengenya mabarabarani;
walevi wanatunga nyimbo juu yangu.
13Lakini mimi nakuomba wewe, ee Mwenyezi-Mungu;
nikubalie ombi langu wakati unaopenda, ee Mungu.
Kwa wingi wa fadhili zako unijibu.
Wewe ni mkombozi wa kuaminika.
14Kwa msaada wako amini uniokoe
nisizame katika matope;
uniokoe na hao wanaonichukia,
unisalimishe kutoka vilindi vya maji.
15Usiniache nikumbwe na mkondo wa maji,
au nizame kwenye kilindi
au nimezwe na kifo.
16Unijibu, ee Mwenyezi-Mungu,
kwa wema na fadhili zako;
unielekee kwa wingi wa huruma yako.
17Usimfiche mtumishi wako uso wako;
unijibu haraka, maana niko hatarini.
18Unijie karibu na kunikomboa,
uniokoe na maadui zangu wengi.
19Wewe wajua ninavyotukanwa,
wajua aibu na kashfa ninazopata;
na maadui zangu wote wewe wawajua.
20Kashfa zimeuvunja moyo wangu,
nami nimekata tamaa.
Nimetafuta kitulizo lakini sikupata,
wa kunifariji lakini sikumpata.
21 Taz Mat 27:48; Marko 15:36; Luka 23:36; Yoh 19:28-29 Walinipa sumu kuwa chakula,
na nilipokuwa na kiu wakanipa siki.
22 Taz Rom 11:9-10 Karamu zao na ziwe mtego kwao,
na sikukuu zao za sadaka ziwanase.
23Macho yao yatiwe giza wasiweze kuona,
uitetemeshe daima migongo yao.
24Uwamwagie hasira yako,
ghadhabu yako iwakumbe.
25 Taz Mate 1:20 Kambi zao ziachwe mahame,
asiishi yeyote katika mahema yao.
26Maana wanawatesa wale uliowaadhibu,
wanawaongezea majeraha wale uliowajeruhi.
27Uwaadhibu kwa kila uovu wao;
uwakatalie kabisa msamaha wako.
28 Taz Ufu 3:5; 13:8; 17:8 Uwafute katika kitabu cha walio hai,
wasiwemo katika orodha ya waadilifu.
29Lakini mimi mnyonge na mgonjwa;
uniinue juu, ee Mungu, uniokoe.
30Kwa wimbo nitalisifu jina la Mungu,
nitamtukuza kwa shukrani.
31Jambo hili litampendeza Mwenyezi-Mungu zaidi,
kuliko kumtolea tambiko ya ng'ombe,
kuliko kumtolea fahali mzimamzima.
32Wanyonge wataona hayo na kufurahi;
wanaomheshimu Mungu watapata moyo.
33Mwenyezi-Mungu huwasikiliza fukara;
hatawasahau kamwe watu wake wafungwa.
34Enyi mbingu na dunia msifuni Mungu;
bahari na vyote vilivyomo, msifuni.
35Maana Mungu atauokoa mji Siyoni,
na kuijenga tena miji ya Yuda.
Watu wake wataishi humo na kuimiliki;
36wazawa wa watumishi wake watairithi,
wale wanaopenda jina lake wataishi humo.
Zaburi69;1-36
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.