Mawaidha kwa vijana
1Mwanangu, usiyasahau mafundisho yangu,
bali kwa moyo wako uzishike amri zangu.
2Maana yatakupa wingi wa siku,
maisha marefu na fanaka kwa wingi.
3Utii na uaminifu visitengane nawe.
Vifunge shingoni mwako;
viandike moyoni mwako.
4 Taz Luka 2:52 Hivyo utakubalika na kusifika,
mbele ya Mungu na mbele ya wanadamu.
5Mtumaini Mwenyezi-Mungu kwa moyo wako wote,
wala usitegemee akili zako mwenyewe.
6Umtambue Mungu katika kila ufanyalo,
naye atazinyosha njia zako.
7 Taz Rom 12:16 Usijione wewe mwenyewe kuwa mwenye hekima;
mche Mwenyezi-Mungu na kujiepusha na uovu.
8Hiyo itakuwa dawa mwilini mwako,
na kiburudisho mifupani mwako.
9Mheshimu Mwenyezi-Mungu kwa mali yako,
na kwa malimbuko ya mazao yako yote.
10Hapo ghala zako zitajaa nafaka,
na mapipa yako yatafurika divai mpya.
11 Taz Yobu 5:17 Mwanangu, usidharau adhabu ya Mwenyezi-Mungu,
wala usiudhike kwa maonyo yake; Taz Ebr 12:5-6
12 Taz Ufu 3:19 maana Mwenyezi-Mungu humwonya yule ampendaye,
kama baba amwonyavyo mwanawe mpenzi.
13Heri mtu anayegundua hekima,
mtu yule anayepata ufahamu.
14Hekima ni bora kuliko fedha,
ina faida kuliko dhahabu.
15Hekima ina thamani kuliko johari,
hamna unachotamani kiwezacho kulingana nayo.
16Kwa mkono wake wa kulia Hekima atakupa maisha marefu;
kwa mkono wake wa kushoto atakupa mali na heshima.
17Njia zake ni za kupendeza,
zote zaelekea kwenye amani.
18Hekima ni mti wa uhai kwa wote wampatao;
wana heri wote wanaoshikamana naye.
19Kwa hekima Mwenyezi-Mungu aliweka misingi ya dunia,
kwa akili aliziimarisha mbingu.
20Kwa maarifa yake vilindi vilipasuka,
na mawingu yakadondosha umande.
21Mwanangu, zingatia hekima safi na busara;
usiviache vitoweke machoni pako,
22navyo vitakuwa uhai nafsini mwako,
na pambo zuri shingoni mwako.
23Hapo utaweza kwenda zako kwa usalama,
wala mguu wako hautajikwaa.
24Ukiketi hutakuwa na hofu;
ukilala utapata usingizi mtamu.
25Usiogope juu ya tishio la ghafla,
wala shambulio kutoka kwa waovu,
26Maana Mwenyezi-Mungu ndiye atakayekutegemeza;
atakuepusha usije ukanaswa mtegoni.
27Usimnyime mtu anayehitaji msaada,
ikiwa unao uwezo wa kufanya hivyo.
28Usimwambie jirani yako aende zake hadi kesho,
hali wewe waweza kumpa anachohitaji leo.
29Usipange maovu dhidi ya jirani yako,
anayeishi karibu nawe bila wasiwasi.
30Usigombane na mtu bila sababu
ikiwa hajakudhuru kwa lolote.
31Usimwonee wivu mtu mkatili,
wala usiige mwenendo wake.
32Maana waovu ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu;
lakini yeye huwafanya marafiki zake wale walio wanyofu.
33Mwenyezi-Mungu huapiza nyumba za waovu,
lakini huyabariki makao ya waadilifu.
34 Taz Yak 4:6; 1Pet 5:5 Yeye huwadharau wenye dharau,
lakini huwafadhili wanyenyekevu.
35Wenye hekima watavuna heshima,
lakini wapumbavu watapata fedheha.
Methali3;1-35
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.