Mfalme Hezekia anaugua
(2Fal 20:1-11; 2Nya 32:24-26)
1Wakati huo, mfalme Hezekia aliugua sana karibu kufa. Ndipo nabii Isaya mwana wa Amozi, akamwendea, akamwambia, “Hivi ndivyo anavyosema Mwenyezi-Mungu: Panga mambo yako sawasawa katika nyumba yako kwa kuwa utakufa, hutapona.”
2Hezekia akageukia upande wa ukuta na kumwomba Mwenyezi-Mungu, 3akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, nakusihi ukumbuke jinsi nilivyokutumikia kwa uaminifu na kwa moyo wangu wote, na kutenda yaliyo sawa mbele yako.” Hezekia akalia kwa uchungu sana.
4Kisha neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Isaya: 5“Nenda ukamwambie Hezekia, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa baba yako Daudi, anasema hivi: Nimesikia ombi lako na nimeyaona machozi yako. Basi, nakuongezea miaka kumi na mitano ya kuishi. 6Nitakuokoa wewe pamoja na mji huu mikononi mwa mfalme wa Ashuru na kuulinda.”
21Basi, Isaya akasema, “Chukueni andazi la tini mkaliweke kwenye jipu lake, apate kupona.”38:21-22 aya ya 21-22 zimehamishiwa hapa kuleta maana yake kamili katika simulizi hilo. 22Hezekia akauliza, “Ni ishara gani itakayonijulisha kwamba mimi nitakwenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu?” 7Isaya akamjibu, “Hii itakuwa ishara kwako kutoka kwa Mwenyezi-Mungu kwamba Mwenyezi-Mungu atafanya kama alivyoahidi. 8Nitafanya kivuli kwenye ngazi iliyojengwa na Ahazi, kirudi nyuma hatua kumi.” Nacho kivuli kikarudi nyuma hatua kumi.38:8 ngazi … hatua kumi … hatua kumi: Au Kwenye saa ya jua … hatua kumi … hatua kumi.
9Kisha mfalme Hezekia alipopona, akatunga wimbo huu wa shukrani:
10“Nilisema: Nikiwa mbichi kabisa,
inanibidi niage dunia.
Mimi nimepangiwa kwenda kuzimu
siku zote zilizonibakia.
11Nilisema sitamwona tena Mwenyezi-Mungu,
katika nchi ya walio hai;
wala sitamwona mtu yeyote tena,
miongoni mwa wakazi wa ulimwengu.
12Makao yangu yamengolewa kwangu,
kama hema la mchungaji;
kama, mfumanguo nimefungasha maisha yangu;
Mungu amenikatilia mbali;
kabla hata mwisho wa siku amenikomesha.38:12 maana ya aya hii katika Kiebrania si dhahiri.
13Usiku kucha nililia kuomba msaada;
kama simba, anavunjavunja mifupa yangu;
mchana na usiku ananikomesha.38:13 maana ya aya hii katika Kiebrania si dhahiri.
14“Ninalia kama mbayuwayu,
nasononeka kama njiwa.
Macho yangu yamefifia kwa kuangalia juu.
Ee Bwana, nateseka;
uwe wewe usalama wangu!
15Lakini niseme nini:
Yeye mwenyewe aliniambia,
naye mwenyewe ametenda hayo.
Usingizi wangu wote umenitoroka
kwa sababu ya uchungu moyoni mwangu.
16“Ee Bwana, Sisi twaishi kutokana na yote uliyotenda,
kwa hayo yote mimi binafsi pia ninaishi.38:16 aya hii maana ya Kiebrania si dhahiri.
Nirudishie afya, uniwezeshe kuishi.
17Nilipata mateso makali kwa faida yangu;
lakini umeyaokoa maisha yangu
kutoka shimo la uharibifu,
maana umezitupa dhambi zangu nyuma yako.
18Huko kuzimu mtu hawezi kukushukuru wewe;
waliokufa hawawezi kukushukuru wewe.
Wala washukao huko shimoni
hawawezi tena kutumainia uaminifu wako.
19Walio hai ndio wanaokushukuru,
kama na mimi ninavyofanya leo.
Kina baba huwajulisha watoto wao uaminifu wako.
20“Mwenyezi-Mungu ataniokoa.
Nasi tutamsifu kwa nyimbo za vinubi
siku zote za maisha yetu,
nyumbani kwake Mwenyezi-Mungu.”
Isaya38;1-20
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.