Mtumishi wa Mungu
1“Tazameni mtumishi wangu ninayemtegemeza;
mteule wangu ambaye moyo wangu umependezwa naye.
Nimeiweka roho yangu juu yake,
naye atayaletea mataifa haki.
2Hatalia wala hatapiga kelele,
wala hatapaza sauti yake barabarani.
3Mwanzi uliochubuka hatauvunja,
utambi ufukao moshi hatauzima;
ataleta haki kwa uaminifu.
4Yeye hatafifia wala kufa moyo,
hata atakapoimarisha haki duniani.
Watu wa mbali wanangojea mwongozo wake.”
Mwanga wa mataifa
5Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi-Mungu
aliyeziumba mbingu, akazitandaza kama hema,
yeye aliyeiunda nchi na vyote vilivyomo,
yeye awapaye watu waliomo pumzi,
na kuwajalia uhai wote waishio humo:
6“Mimi Mwenyezi-Mungu nimekuita kutenda haki,
nimekushika mkono na kukulinda.
Kwa njia yako nitaweka ahadi na watu wote,
wewe utakuwa mwanga wa mataifa.
7Utayafumbua macho ya vipofu,
utawatoa wafungwa gerezani,
waliokaa gizani utawaletea uhuru.
8Jina langu mimi ni Mwenyezi-Mungu;
utukufu wangu sitampa mwingine,
wala sifa zangu sanamu za miungu.
9Tazama, mambo niliyotabiri yametukia;
na sasa natangaza mambo mapya,
nakueleza hayo kabla hayajatukia.”
Wimbo wa sifa
10Mwimbieni Mwenyezi-Mungu wimbo mpya!
Dunia yote iimbe sifa zake:
Bahari na vyote vilivyomo,
nchi za mbali na wakazi wake;
11jangwa na miji yake yote ipaaze sauti,
vijiji vya wakazi wa Kedari vimsifu,
wakazi wa Sela waimbe kwa shangwe;
wapaaze sauti kutoka mlimani juu.
12Wote wakaao nchi za mbali,
na wamtukuze na kumsifu Mwenyezi-Mungu.
13Mwenyezi-Mungu ajitokeza kama shujaa;
kama askari vitani ajikakamua kupigana.
Anapaza sauti kubwa ya vita,
na kujionesha mwenye nguvu dhidi ya maadui zake.
Mungu aahidi kuwasaidia watu wake
14Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Kwa muda mrefu sasa nimenyamaza,
nimekaa kimya na kujizuia;
lakini sasa nitalia kama mama anayejifungua,
anayetweta pamoja na kuhema.
15Nitaharibu milima na vilima,
na majani yote nitayakausha.
Mito ya maji nitaigeuza kuwa nchi kavu,
na mabwawa ya maji nitayakausha.
16“Nitawaongoza vipofu katika njia wasiyoifahamu,
nitawaongoza katika njia ambazo hawazijui.
Mbele yao giza nitaligeuza kuwa mwanga,
na mahali pa kuparuza patakuwa laini.
Huo ndio mpango wangu wa kufanya,
nami nitautekeleza.
17Wote wanaotegemea sanamu za miungu,
wote wanaoziambia: Nyinyi ni miungu yetu;
watakomeshwa na kuaibishwa.
Waisraeli ni viziwi na vipofu
18“Sikilizeni enyi viziwi!
Tazameni enyi vipofu, mpate kuona!
19Nani aliye kipofu ila mtumishi wangu?
Nani aliye kiziwi kama mjumbe ninayemtuma?
Ni nani aliye kipofu kama huyu niliyemweka wakfu,
au kipofu kama mtumishi wa Mwenyezi-Mungu?
20Nyinyi mmeona mambo mengi,
lakini hamwelewi kitu.
Masikio yenu yako wazi,
lakini hamsikii kitu!”
21Mwenyezi-Mungu, kwa ajili ya uaminifu wake,
alipenda kukuza mwongozo wake na kuutukuza.
22Lakini hawa ni watu walioibiwa mali na kuporwa!
Wote wamenaswa mashimoni,
wamefungwa gerezani.
Wamekuwa kama mawindo bila mtu wa kuwaokoa,
wamekuwa nyara na hakuna asemaye, “Waokolewe!”
23Je, mtatega sikio kusikia kitu hiki?
Nani kati yenu atakayesikiliza vizuri yatakayotukia?
24Ni nani aliyewatia Waisraeli mikononi mwa adui zao?
Nani aliyewaacha wanyanganywe mali zao?
Ni Mwenyezi-Mungu ambaye tumemkosea!
Wazee wetu walikataa kuzifuata njia zake,
wala hawakuzitii amri zake.
25Kwa hiyo aliwamwagia hasira yake kali,
akawaacha wakumbane na vita vikali.
Hasira yake iliwawakia kila upande,
lakini wao hawakuelewa chochote;
iliwachoma, lakini hawakutilia jambo hilo maanani.
Isaya42;1-25
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.