Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 3 January 2018

Kikombe Cha Asubuhi ;1Samueli13...




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu..
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Utukuzwe Mungu wetu,Unastahili sifa,Unastahili kuabudiwa,unastahili kuhimidiwa,Neema yako yatutosha,Matendo yako ni makuu mno,Mtendo yako ni ya ajabu..!!


Dunia na vyote vilivyomo ni vyake Mwenyezi-Mungu; ulimwengu na wote waishio humo ni mali yake. Maana yeye aliweka misingi ya dunia juu ya bahari; aliisimika imara juu ya mito ya maji. Nani atakayepanda mlima wa Mwenyezi-Mungu? Nani atakayekaa katika hekalu lake takatifu? Ni mtu wa matendo mema na moyo safi, asiyeuelekeza moyo wake katika upuuzi, wala kuapa kwa uongo. Mtu huyo atapokea baraka kwa Mwenyezi-Mungu, na haki yake kwa Mungu mwokozi wake. Ndio hali ya kizazi cha watu wamtafutao yeye; naam, watu wamtafutao Mungu wa Yakobo. Fungukeni enyi milango; fungukeni enyi milango ya kale, ili Mfalme mtukufu aingie. Ni nani huyo Mfalme mtukufu? Ni Mwenyezi-Mungu, mwenye nguvu na uwezo; Mwenyezi-Mungu, mwenye uwezo vitani. Fungukeni enyi malango, fungukeni enyi milango ya kale, ili Mfalme mtukufu aingie. Ni nani huyo Mfalme mtukufu? Ni Mwenyezi-Mungu, wa majeshi, yeye ndiye Mfalme mtukufu.

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako..
Yahweh tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale
wote waliotukosea..
Jehovah tunaomba utuepushe katika majaribu,Yahweh utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Baba wa Mbinguni tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Mfalme wa amani utufunike kwa damu ya Bwana na Mwokozi wetu
Yesu Kristo wa Nazareti,Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu..
Baba wa Mbinguni ukatupe ubunifu na maarifa katika ufanyaji/utendaji
Yahweh nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako..
Jehovah tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji...
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbingubi ukatupe kama inavyokupendeza wewe..

Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale maisha yetu Yahweh tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Mungu Baba tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba uwepo wako katika kila jambo tunaloenda kufanya
Mungu wetu ukatutangulie na kutuongoza,Baba wa mbinguni ukatamalaki na kutuatamia,Yahweh ukaonekane popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni..
Jehovah ukatupe neema ya kufuata njia zako Baba wa Mbinguni tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu..
Yahweh tunaomba ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazareti vyote tunavyoenda kugusa,kutumia..
Mungu wetu ukatufanye chombo chema Yahweh nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..



Mwenyezi-Mungu ni mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu. Hunipumzisha kwenye malisho mabichi; huniongoza kando ya maji matulivu, na kuirudishia nafsi yangu nguvu mpya. Huniongoza katika njia sawa kwa hisani yake. Nijapopita katika bonde la giza kuu la kifo, sitaogopa hatari yoyote, maana wewe ee Mwenyezi-Mungu u pamoja nami; gongo lako na fimbo yako vyanilinda. Umeniandalia karamu mbele ya maadui zangu; umenipaka mafuta kichwani pangu; kikombe changu umekijaza mpaka kufurika. Kweli wema wako na fadhili zako zitakuwa pamoja nami, siku zote za maisha yangu; nami nitakaa nyumbani mwa Mwenyezi-Mungu milele.

Baba wa Mbinguni tunarusha shukrani na utukufu kwako kwa yote 
uliyotutendea..
Umeponya,umeokoa,umebariki,umefungua njia,umefariji
umetutendea mema mengi na umejibu sala/maombi yetu
umendelea kuwa msaada kwa wengi..
Mungu wetu ukaonekane kwa wengine pia wanaokutafuta kwa bidii na imani,ukawafute machozi yao,ukasikie kuomba kwao,ukawajibu na kuwatendea sawasawa na mapenzi yako..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!
Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba akaonekane katika maisha yenu,Amani ya Kristo
Yesu ikawe nayi Daima..
Nawapenda.

Vita dhidi ya Wafilisti

1Shauli alikuwa na umri wa miaka kadha wa kadha13:1 makala ya Kiebrania haina idadi ya miaka ya Shauli. alipoanza kutawala. Na alitawala Israeli kwa muda wa miaka … miwili.13:1 miwili: Hii si idadi kamili, kuna kasoro hapa. 2Shauli aliwachagua Waisraeli 3,000. Kati yao, 2,000 alikuwa nao huko Mikmashi na katika nchi ya milima ya Betheli. Elfu moja aliwaweka huko Gibea katika eneo la Benyamini. Hao aliwaweka chini ya mwanawe Yonathani. Watu wengine wote waliobakia, aliwarudisha, kila mtu nyumbani kwake. 3Yonathani alishinda kambi ya kijeshi ya13:3 kambi ya kijeshi ya: Au Kamanda wa Wafilisti huko Geba, na Wafilisti wote walisikia juu ya habari hizo. Hivyo Shauli alipiga tarumbeta katika nchi yote akatangaza, akisema, “Waebrania na wasikie.” 4Waisraeli wote waliposikia kuwa Shauli alikuwa ameishinda ngome ya kijeshi ya Wafilisti, na kwamba Wafilisti wanawachukia sana Waisraeli, waliitwa kwenda kuungana na Shauli huko Gilgali.
5Wafilisti walikuwa na magari 30,000, askari 6,000 wapandafarasi na kikosi cha askari wa miguu wengi kama mchanga wa pwani; wote walipanda juu na kupiga kambi yao huko Mikmashi, mashariki ya Beth-aveni.
6Waisraeli walipoona wako taabuni (maana walikuwa wanashambuliwa vikali), walianza kujificha. Wengine walijificha mapangoni, wengine mashimoni, wengine kwenye miamba, wengine kwenye makaburi na wengine kwenye visima. 7Wengine walivuka mto Yordani mpaka katika nchi ya Gadi na nchi ya Gileadi.
Lakini Shauli alikuwa bado huko Gilgali na watu wote walimfuata wakitetemeka. 8Shauli alimngoja Samueli kwa muda wa siku saba, kama Samueli alivyosema. Lakini Samueli hakuja huko Gilgali na watu walianza kumwacha Shauli.
9Basi, Shauli akawaambia watu, “Nileteeni sadaka yenu ya kuteketezwa na zile za amani.” Naye akatolea sadaka ya kuteketezwa.
10Mara tu alipokuwa anamaliza kutoa sadaka ya kuteketezwa, Samueli aliwasili. Shauli akatoka nje kwenda kumlaki Samueli na kumsalimia. 11Samueli akamwuliza, “Umefanya nini?” Shauli akamjibu, “Nilipoona watu wananiacha, na wewe hukuja, katika muda wa siku ulizosema, na tena nilipoona Wafilisti wamejipanga tayari kwa vita huko Mikmashi, 12nikawaza kwamba Wafilisti watakuja kunishambulia huko Gilgali. Tena nilikuwa bado sijaomba fadhili za Mwenyezi-Mungu. Ndipo nilipolazimika kutolea mimi mwenyewe sadaka ya kuteketezwa.”
13Samueli akamjibu Shauli, “Umefanya kipumbavu. Hukutii aliyokuamuru Mwenyezi-Mungu, Mungu wako. Kama ungetii, Mwenyezi-Mungu angeudumisha milele ufalme wako juu ya Israeli. 14Lakini sasa ufalme wako hautadumu kwa kuwa amri aliyokuamuru Mwenyezi-Mungu hukuitii. Mwenyezi-Mungu amejitafutia mtu mwingine ambaye atamtii kwa moyo wote, na huyo ndiye ambaye amemteua kuwa mtawala juu ya watu wake.”
15Samueli akaondoka kutoka Gilgali na kwenda huko Gibea katika nchi ya Benyamini.
Shauli alipowahesabu watu waliokuwa pamoja naye, aliona wako watu 600 tu. 16Shauli na Yonathani mwanawe pamoja na watu waliokuwa pamoja nao, walikaa huko Gibea katika nchi ya Benyamini na Wafilisti walipiga kambi huko Mikmashi. 17Wafilisti walitoka kwenye kambi yao kwenda kuwashambulia wakiwa wako katika vikosi vitatu. Kikosi kimoja kilielekea Ofra katika nchi ya Shuali. 18Kikosi kingine kilielekea Beth-horoni, na kikosi kingine kikageukia njia ielekeayo bonde la Seboimu, kuelekea jangwani.
19Wakati huo hapakuwepo na mhunzi yeyote katika nchi nzima ya Israeli, kwani Wafilisti walikusudia kuwazuia Waebrania wasije wakajitengenezea mapanga au mikuki. 20Kila Mwisraeli alilazimika kuwaendea Wafilisti kunoa wembe wa plau yake au sururu au shoka au mundu wa kuvunia. 21Waisraeli walikuwa wanalipa fedha theluthi mbili za shekeli kunoa wembe wa plau na sururu. Na bei ya kunoa shoka au kupata mchokoo ilikuwa theluthi moja ya shekeli. 22Kwa hiyo siku ya vita hakuna mtu miongoni mwa wote waliokuwa pamoja na Shauli na Yonathani aliyekuwa na upanga au mkuki isipokuwa Shauli na Yonathani mwanawe. 23Wafilisti walipeleka kikosi cha askari kwenda kulinda njia ya Mikmashi.


1Samweli13;1-23

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Tuesday 2 January 2018

Kikombe Cha Asubuhi ;1Samueli12...




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote..

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyo onekana
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Mungu mwenye nguvu
Mungu wa walio hai,Mungu mwenye huruma,Muweza wa yote
Hakuna kama wewe,Neema yako yatutosha..!!

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kwakuwa tayari kwa majukumu yetu
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii

Utukuzwe Baba wa Mbinguni,Usifiwe ee  Mungu wetu,Uabudiwe Jehovah
Uhimidiwe Yahweh,Mtendo yako ni makuu mno,Mtendo yako ni ya ajabu..
Sifa na Utukufu tunakurudishia Mungu wetu..!


Ukuu ni wako, ee Mwenyezi-Mungu, una nguvu, utukufu, ushindi na enzi. Vyote vilivyoko mbinguni na duniani ni vyako. Ee Mwenyezi-Mungu, ufalme ni wako, nawe umetukuzwa, u mkuu juu ya vitu vyote. Utajiri na heshima hutoka kwako, vyote wavitawala. Uwezo na nguvu vimo mkononi mwako, nawe wawakuza uwapendao, na huwaimarisha wote. Sasa ee Mungu wetu, tunakushukuru na kulisifu jina lako tukufu. “Lakini, mimi ni nani, na watu wangu ni nani, hata tuweze kukupa kitu? Kwa maana vitu vyote vyatoka kwako, tumekutolea vilivyo vyako wewe mwenyewe.

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Yahweh tunaomba utusamehe makosa yetu tuliyoyafanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea..
Mungu wetu tunaomba utuepushe katika majaribu Baba wa Mbinguni
tunaomba utuokoe na yule mwovu na Kazi zake zote...
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Jehovah
utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..

Ziko habari za kuaminika kwamba kuna uzinzi miongoni mwenu; tena ni uzinzi mbaya ambao haujapata kuwako hata kati ya watu wasiomjua Mungu. Nimeambiwa eti mmoja wenu anaishi na mke wa baba yake! Mnawezaje kujivuna? Ingekuwa afadhali kwenu kuomboleza, na huyo aliyefanya kitu hicho aondolewe miongoni mwenu. Nami, kwa upande wangu, ingawa kwa mwili niko mbali nanyi, hata hivyo kwa roho niko hapo pamoja nanyi: Na hivyo, kama vile nipo hapo, nimekwisha mhukumu huyo aliyefanya jambo hilo la aibu. Wakati mnapokusanyika pamoja kwa jina la Bwana Yesu, nami nikiwa pamoja nanyi kwa roho, basi, kwa uwezo wa Bwana wetu Yesu, mkabidhini mtu huyo kwa Shetani ili mwili wake uharibiwe na roho yake iweze kuokolewa siku ile ya Bwana. Majivuno yenu hayafai! Je, hamjui kwamba chachu kidogo huchachusha donge lote la unga? Jitakaseni, mkatupe mbali chachu ya kale ili mpate kuwa donge jipya lisilotiwa chachu kama mnavyopaswa kuwa; maana, Kristo, Pasaka yetu, amekwisha tolewa kuwa sadaka. Basi, tufanye karamu hiyo si kwa chachu ile ya kale, chachu ya ubaya na uovu, bali kwa mkate usiotiwa chachu, mkate wa usafi na kweli. Niliwaandikia katika barua yangu msishirikiane na wazinzi. Ukweli ni kwamba sikuwa na maana ya watu wote duniani walio wazinzi, wachoyo, walaghai na wenye kuabudu sanamu. Maana, ili kuwaepa hao wote ingewalazimu nyinyi kuihama dunia hii kabisa! Nilichoandika ni hiki: Msishirikiane na ndugu Mkristo aliye mzinzi, mchoyo, mwenye kuabudu sanamu, mchongezi, mlevi na mlaghai. Mtu wa namna hiyo, hata kula msile naye. Je, ni shauri langu kuwahukumu watu walio nje? Hao Mungu atawahukumu. Je, nyinyi hampaswi kuwahukumu wale walio katika jamii yenu nyinyi wenyewe? Mfukuzeni mbali nanyi huyo mwovu!

Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za kimono yetu
Mungu wetu tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika
Ufanyaji/utendaji Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Mungu wetu tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Yahweh ukatupe sawasawa na mapenzi yako....


Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika 
Maisha yetu,Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa
zetu,watoto,wazazi/walezi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Baba wa Mbinguni tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote 
tunavyovimiliki..
Yahweh tunaomba ukatuguse kwa mKono wako Wenye nguvu
Mungu wetu tukawe salama rohoni,Baba wa Mbinguni tunaomba
ukatamalaki na kutuatamia,Mungu wetu tunaomba utupe neema
ya kufuata njia zako Jehovah tukasimamie Neno lako amri na sheria
zako siku zote za maisha yetu..
Mfalme wa amani ukatupe macho ya rohoni Baba wa Mbinguni
ukatupe masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Yahweh  sema  nasi Baba wa Mbinguni ukaonekane popote tupitapo
na ikajulikane kwamba upo Mungu wetu..
Yahweh Nuru yako ikaangaze Katika Maisha yetu,furaha,amani,
utu wema,fadhili,mafanikio,ushindi na vyote vinavyokupendeza
wewe visipungue..
Baba wa Mbinguni utuepushe na kiburi,majivuno,ubinafsi,choyo,makwazo,
unafiki, masengenyo na yote yanayokwenda kinyume nawe..
Mungu wetu ukatufanye barua njema nasi tukasomeke kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..


Kisha mfalme Daudi akaingia ndani ya hema na kuketi mbele ya Mwenyezi-Mungu, halafu akaomba, “Mimi ni nani, ee Mwenyezi-Mungu, na nyumba yangu ni nini hata unitukuze hivi? Isitoshe, umenifanyia mengine zaidi: Umenitolea ahadi juu ya vizazi vyangu vijavyo ee Mwenyezi-Mungu! Nikuambie nini zaidi, mimi Daudi mtumishi wako, kwa kunitukuza hivyo? Wewe unanijua mimi mtumishi wako. Ee Mwenyezi-Mungu, kwa ajili ya mtumishi wako na kwa kufuatana na moyo wako mwenyewe, umeyatenda hayo makuu yote, ili yajulikane hayo matendo makuu yote. Hakuna mwingine kama wewe, ee Mwenyezi-Mungu, na yote tunayoyasikia yanathibitisha kwamba hakuna Mungu mwingine ila wewe. Tena ni watu gani duniani ambao wanaweza kulinganishwa na watu wako wa Israeli ambao peke yao Mungu wao alikwenda kuwakomboa ili wawe watu wake? Wewe ulijifanyia jina kwa kutenda mambo makubwa na ya ajabu hapo ulipoyafukuza mataifa mbele ya watu wako ambao uliwakomboa kutoka Misri. Hata umejifanyia watu wako wa Israeli kuwa watu wako milele; nawe ee Mwenyezi-Mungu, umekuwa Mungu wao. “Basi sasa, ewe Mwenyezi-Mungu, liimarishe milele neno lako ulilosema kunihusu mimi mtumishi wako na kuhusu jamaa yangu. Nalo jina lako litatukuzwa milele, nao watu watasema, ‘Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, ndiye Mungu wa Israeli!’ Na jamaa yangu, mimi Daudi mtumishi wako, itaimarika mbele yako. Maana ee Mungu wangu nimepata ujasiri kukuomba kwa sababu wewe, umenifunulia ukisema ya kwamba utanijengea nyumba. Sasa ee Mwenyezi-Mungu, wewe ndiwe Mungu, umeniahidi mimi mtumishi wako jambo hili jema; kwa hiyo nakuomba uibariki nyumba yangu, mimi mtumishi wako, ili idumu milele mbele yako; kwani unachobariki wewe, huwa kimebarikiwa milele.”
Yahweh tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
wenye shida/tabu
Mungu wetu tunaomba uponyaji kwa wagonjwa na ukawape uvumilivu wanaowauguza..
Jehovah tunaomba ukawavushe salama wale wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali..
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaweke huru wale walio katika vifungo
vya yule mwovu, Mungu wetu haki ikatendeke kwa walio magerezani
pasipo na hatia..
Yahweh ukawe tumaini kwa waliokata tamaa,walio kataliwa,wenye hofu na mashaka..
Mungu wetu tunaomba ukawe mfariji wa wafiwa na ukawaponye
wote  walio umizwa roho..
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe wale wote waliokwenda
kinyume nawe...
Jehovah ukawe msaada na ukawape chakula wenye njaa..
Baba wa Mbinguni tuyaweka haya mikononi mwako
Tukiamini wewe ni Mungu wetu hakuna lililogumu kwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!!

Asanteni sana wapendwa/waungwana kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na msipungukiwe katika
mahitaji yenu..
Baba wa Mbinguni akawape sawasawa na mapezni yake
Nawapenda.



Samueli anawahutubia Waisraeli

1Samueli akawaambia Waisraeli wote, “Yote mliyoniambia, nimeyasikiliza. Nimemtawaza mfalme juu yenu. 2Sasa, mnaye mfalme wa kuwaongoza. Kwa upande wangu, mimi ni mzee mwenye mvi, na watoto wangu wa kiume wako pamoja nanyi. Nimekuwa kiongozi wenu tangu nilipokuwa kijana mpaka sasa. 3Niko hapa, na kama nimefanya tendo lolote lile baya, basi, toeni ushahidi mbele ya Mwenyezi-Mungu na mbele ya mfalme wake mteule. Je, nimepora fahali au punda wa mtu yeyote? Je, nimempunja mtu yeyote? Je, nimemkandamiza mtu yeyote? Je, nimepokea rushwa kwa mtu yeyote ili kupotosha haki? Nami nitamrudishia chochote kile.” 4Watu wakamjibu, “Kamwe hujatudanganya, hujatukandamiza, wala hujachukua kitu chochote kwa mtu.” 5Samueli akajibu, “Mwenyezi-Mungu ni shahidi juu yenu, na mfalme wake mteule leo ni shahidi kuwa mmeniona sina hatia.” Wao wakajibu: “Yeye ni shahidi.” 6Samueli akawaambia, “Mwenyezi-Mungu ndiye aliyemteua Mose na Aroni na kuwatoa babu zenu nchini Misri. 7Sasa simameni papo hapo mlipo ili mimi na nyinyi tuhukumiwe mbele ya Mwenyezi-Mungu, nami nitawahutubia kuhusu matendo yake ya ajabu ambayo aliyatenda ili kuwaokoa nyinyi na babu zenu.
8“Yakobo na jamaa yake walipokwenda Misri, na Wamisri walipowakandamiza, babu zenu walimlilia Mwenyezi-Mungu; naye akawatuma Mose na Aroni ambao waliwatoa babu zenu nchini Misri na kuwafanya mkae katika nchi hii. 9Lakini wao walimsahau Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, naye akawatia mikononi mwa Sisera, kamanda wa jeshi la Hazori, na mikononi mwa Wafilisti na mikononi mwa mfalme wa Moabu. Mataifa hayo yalipigana na babu zenu na kuwashinda. 10Babu zenu wakamlilia Mwenyezi-Mungu, wakisema, ‘Tumefanya dhambi kwa sababu tumekuacha wewe Mwenyezi-Mungu, kwa kutumikia Mabaali na Maashtarothi. Tuokoe kutoka mikononi mwa adui zetu, nasi tutakutumikia’. 11Ndipo Mwenyezi-Mungu alipomtuma Yerubaali, na baadaye akamtuma Bedani,12:11 Bedani: Au Baraka. kisha Yeftha, na mwishowe akanituma mimi Samueli. Kila mmoja wetu aliwaokoa kutoka kwa adui zenu waliowazunguka, nanyi mkaishi kwa amani. 12Lakini mlipomwona mfalme Nahashi wa Waamoni amekuja kuwashambulia, mkamkataa Mwenyezi-Mungu ambaye ndiye Mfalme wenu, mkaniambia, ‘La! Mfalme ndiye atakayetutawala.’ 13Sasa, mfalme mliyejichagulia ndiye huyu hapa. Mlimwomba Mwenyezi-Mungu awape mfalme, naye amewapa. 14Kama mkimcha Mwenyezi-Mungu, na kumtumikia, na kusikiliza sauti yake bila kuiasi amri yake, kama nyinyi wenyewe pamoja na mfalme anayewatawala mkimfuata Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, basi mtafanikiwa. 15Lakini kama hamtasikiliza sauti ya Mwenyezi-Mungu, mkaasi amri yake, basi yeye atapambana nanyi pamoja na mfalme wenu.12:15 mfalme wenu: Makala ya Kiebrania: Baba zenu. 16Kwa hiyo basi, tulieni na kulitazama jambo hilo kubwa ambalo Mwenyezi-Mungu atatenda mbele yenu. 17Je, sasa si wakati wa kuvuna ngano? Lakini mimi nitamwomba Mwenyezi-Mungu alete radi na mvua, nanyi mtatambua na kuona kuwa uovu wenu mliotenda mbele ya Mwenyezi-Mungu kwa kujitakia mfalme, ni mkubwa.”
18Basi, Samueli akamwomba Mwenyezi-Mungu, naye akatuma radi na mvua katika siku hiyo. Watu wote wakamwogopa sana Mwenyezi-Mungu na Samueli. 19Hivyo wakamwambia Samueli, “Tafadhali utuombee sisi watumishi wako kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ili tusife; kwa sababu tumezidisha dhambi zetu kwa uovu huo wa kujitakia mfalme.”
20Samueli akawajibu, “Msiogope; ingawa mmefanya uovu huu, msiache kumfuata Mwenyezi-Mungu, ila mtumikieni kwa moyo wenu wote. 21Msiifuate miungu ya uongo isiyo na faida wala haiwezi kuwaokoa, maana ni ya uongo. 22Kwa heshima ya jina lake kuu, Mwenyezi-Mungu hatawatupa watu wake kwa sababu amependa kuwafanya nyinyi muwe watu wake. 23Tena kwa upande wangu haitatokea niache kuwaombea kwa Mwenyezi-Mungu; kufanya hivyo itakuwa kumkosea Mwenyezi-Mungu. Nitaendelea kuwafundisha njia njema na ya haki. 24Basi, nyinyi mcheni Mwenyezi-Mungu na kumtumikia kwa uaminifu kwa moyo wenu wote. Kumbukeni yale mambo makuu aliyowatendea. 25Lakini kama mkiendelea kutenda maovu, mtaangamia nyinyi wenyewe pamoja na mfalme wenu.”


1Samweli12;1-25

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Monday 1 January 2018

Kikombe Cha Asubuhi ;1Samueli11...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
ni Siku/wiki/mwaka mwingine tena Mungu wetu ametupa kibali cha kuendelea
kuiona siku hii...
Wangapi tulianza nao mwaka?nini tumempa Mungu?
ni wema gani tumetenda zaidi ya wengine?ni jambo gani zuri zaidi tumelifanya?
si kwamba sisi ni wazuri mno,si kwa nguvu zetu,wala si kwa utashi wetu,
si kwa akili zetu wala si kwa ujuaji wetu...
Ni kwa mapenzi yake Mungu wetu,ni kwa neema/rehema zake Baba wa Mbinguni 
sisi kuwa hivi tulivyo leo hii..

Kutoka kwangu mimi Paulo, mtumishi wa Kristo Yesu, na mtume niliyeteuliwa na kuitwa kwa ajili ya kuhubiri Habari Njema ya Mungu. Hapo kale, Mungu aliwaahidi watu hii Habari Njema kwa njia ya manabii wake katika Maandiko Matakatifu. Hii Habari Njema inamhusu Mwana wa Mungu, Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kuhusu ubinadamu wake, alikuwa mzawa wa Daudi; kuhusu utakatifu wake wa kimungu, alithibitishwa kwa uwezo mkuu kwamba ni Mwana wa Mungu kwa kufufuliwa kutoka kwa wafu. Kwa njia yake, mimi nimepewa neema ya kuwa mtume, ili kwa ajili yake niwaongoze watu wa mataifa yote wapate kuamini na kutii. Nyinyi ni miongoni mwa watu hao; mmeitwa muwe watu wake Yesu Kristo. Basi, nawaandikia nyinyi nyote mlioko Roma ambao Mungu anawapenda, akawateua muwe watu wake. Nawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.
Tunakushuru ee Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante kwa kutuchagua na kutupa nafasi ya kuendelea kuiona leo hii..
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari katika majukumu yetu..
Asante kwa mwaka uliopita na asante kwa mwaka huu tunaouanza..
Utukuzwe ee Mungu wetu,Usifiwe Baba wa Mbinguni..
Usifiwe Jehovah,Uhimidiwe Yahweh,Unatosha Mungu wetu..
Uabudiwe Mfalme wa amani,hakuna kama wewe Mungu wetu..
Mungu  mwenye nguvu,Baba wa Upendo,Baba wa huruma,Mponyaji wetu,
Kimbilio letu,Mungu wa walio hai,Mungu wa Yatima,Mungu wa wajane..
Alfa na Omega,wewe ni mwanzo na wewe ni mwisho..
Sifa na utukufu tunakurudishia ee Baba wa Mbinguni..!!



Awali ya yote, namshukuru Mungu wangu kwa njia ya Yesu Kristo kwa ajili yenu nyote, kwa sababu imani yenu inasikika duniani kote. Mungu, ambaye ninamtumikia kwa moyo wangu wote katika kuhubiri Habari Njema ya Mwanae, ni shahidi wangu kwamba ninawakumbukeni daima katika sala zangu. Namwomba Mungu akipenda, anipatie nafasi nzuri ya kuja kwenu sasa. Kwa maana ninatamani sana kuwaoneni ili nipate kuwagawieni zawadi ya kiroho na kuwaimarisha. Ndiyo kusema, tutaimarishana: Imani yenu itaniimarisha mimi, na yangu itawaimarisha nyinyi. Ndugu zangu, nataka mjue kwamba mara nyingi nilikusudia kuwatembeleeni, lakini mpaka sasa nimezuiwa. Ningependa kupata mafanikio mema kati yenu kama nilivyopata kati ya watu wa mataifa mengine. Ninalo jukumu kwa watu wote, waliostaarabika na wasiostaarabika, wenye elimu na wasio na elimu. Ndiyo maana ninatamani pia kuihubiri Habari Njema kwenu nyinyi mlioko huko Roma.
Mungu wetu tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia
mikononi mwako Jehovah..
Yahweh tunaomba utusamehe Dhabi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Mfalme wa amani nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale
wote waliotukosea.. 
Baba wa Mbinguni tunaomba utuepushe katika majaribu Mungu wetu utuokoe
na yule mwovu na Kazi zake zote..
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Mungu wetu utufunike
kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..



Sioni aibu kutangaza Habari Njema; yenyewe ni nguvu ya Mungu inayowaokoa wote wanaoamini: Wayahudi kwanza na wasio Wayahudi pia. Kwa maana Habari Njema inaonesha wazi jinsi Mungu anavyowakubali watu kuwa waadilifu; jambo hili hufanyika kwa imani, tangu mwanzo mpaka mwisho; kama ilivyoandikwa: “Mwadilifu kwa imani ataishi.”
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Yahweh tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika ufanyaji/utendaji
Mungu wetu nasi tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Yahweh tunayaweka Maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu
familia/ndugu na wote wanaotuzunguka...
Yahweh tunaomba Amani yako ikatawale,Upendo wetu ukadumu,tukawe salama moyoni,Baba wa Mbinguni ukatamalaki na kutuatamia,Mungu Baba ukawe mlinzi
wetu kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki,Yahweh ukaseme nasi,Baba wa Mbinguni
ukatupe macho ya rohoni,Jehovah ukatupe masikio ya kusikia sauti yako na kuitii
Mungu wetu neema yako yatutosha Baba wa Mbinguni ukatupe hekima,busara,
utu wema na utuepushe na kiburi,chuki,makwazo,unafiki na yote yanayokwenda kinyume nawe..
Yahweh tunaomba utupe neema ya kufuata njia zako,Mungu wetu tukasimamie
Neno lako amri na sheia zako siku zote za maisha yetu..
Mungu wetu ukataufanye chombo chema nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..


Ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni dhidi ya uasi na uovu wote wa binadamu ambao kwa njia zao mbaya wanaupinga ukweli usijulikane. Kwa maana, yote yanayoweza kujulikana juu ya Mungu ni wazi kwao; maana Mungu mwenyewe ameyadhihirisha. Tangu Mungu alipoumba ulimwengu, uwezo wake wa milele na uungu wake, ingawa havionekani kwa macho, vinafahamika wazi. Watu wanaweza kuyajua mambo hayo kutokana na vitu hivyo alivyoumba Mungu. Kwa hiyo hawana njia yoyote ya kujitetea! Ingawa wanajua kuna Mungu, lakini hawampi heshima anayostahili, wala hawamshukuru. Badala yake, fikira zao zimekuwa batili na akili zao tupu zimejaa giza. Wanajidai kuwa wenye hekima, kumbe ni wapumbavu. Wanaacha kumwabudu Mungu aishiye milele, na badala yake, wanaabudu sanamu zilizo mfano wa binadamu ambaye hufa, mfano wa wanyama, ndege, au wanyama watambaao. Kwa sababu hiyo, Mungu amewaacha wafuate tamaa mbaya za mioyo yao na kufanyiana mambo ya aibu kwa miili yao. Wanaubadili ukweli juu ya Mungu kwa uongo; wanaheshimu na kuabudu kiumbe badala ya Muumba mwenyewe, ambaye ndiye astahiliye sifa milele! Amina. Kwa hiyo, Mungu amewaacha wafuate tamaa mbaya. Hata wanawake wanabadili matumizi yanayopatana na maumbile. Nao wanaume hali kadhalika, wanaacha kufuata matumizi ya maumbile ya mume na mke, wakawakiana tamaa wao kwa wao. Wanaume wanafanyiana mambo ya aibu, na hivyo wanajiletea wenyewe adhabu wanayostahili kwa vitendo vyao viovu. Kwa vile watu walikataa kumtambua Mungu, Mungu amewaacha katika fikira zao potovu, wakafanya yale ambayo hawangestahili kufanya. Wamejaa kila aina ya uovu, dhuluma, ulafi na ufisadi. Wamejaa wivu, uuaji, ugomvi, udanganyifu na nia mbaya; husengenya, na kusingiziana; ni watu wa kuchukiza kwa Mungu, wafidhuli, wenye kiburi na majivuno; hodari sana katika kutenda mabaya, na hawawatii wazazi wao; hawana dhamiri, hawatimizi ahadi zao, hawana wema wala huruma kwa wengine. Wanajua kwamba sheria ya Mungu yasema kwamba watu wanaoishi mithili hiyo, wanastahili kifo. Zaidi ya hayo, siyo tu kwamba wanafanya mambo hayo wao wenyewe, bali hata huwapongeza wale wanaofanya mambo hayohayo.

Mungu wetu tazama wenye shida/tabu,Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye  nguvu wote walio katika mahangaiko..
Mungu wetu tunaomba ukawaponye wagonjwa na ukawape uvumilivu/nguvu
wanaowauguza,Yahweh tunaomba ukawavushe salama wale wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali Mungu wetu ukaonekane katika maisha yao..
Baba wa Mbinguni ukawe faraja kwa wafiwa Mungu wetu ukawe tumaini
kwa wote waliokata tamaa,waliokataliwa,wenye hofu na mashaka..
Yahweh tunaomba ukawalishe wenye njaa na ukabariki vyanzo vyao..
Jehovah tunaomba ukawasamehe wale wote waliokwenda kinyume nawe
Mungu wetu ukawainue walio anguka Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...

Yahweh Nuru yako ikaangaze katika maisha Yao..
Baba wa Mbinguni ukasikie kuomba kwetu..Yahweh ukapokee
sala/maombi yetu Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi
yako...
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina..!


Asanteni sana wapendwa/waungwana kwakuwa nami
Baba wa Upendo akawabariki na pendo lenu likadumu
Mungu mwenye nguvu akawaguse kwa mkono wake kila
jambo likatendeke sawasawa na mapenzi yake..
Nawapenda.



Shauli anawashinda Waamoni

1Kisha mfalme Nahashi wa Waamoni, alikwenda na kuuzingira mji wa Yabesh-gileadi. Wakazi wa mji wa Yabesh-gileadi wakamwambia Nahashi, “Fanya mapatano nasi, nasi tutakutumikia.” 2Lakini akawaambia, “Nitafanya mapatano nanyi kwa sharti moja kwamba nitamngoa kila mmoja wenu jicho lake la kulia; hivyo nitawaaibisha Waisraeli wote.” 3Wazee wa Yabeshi wakamwambia, “Tupe muda wa siku saba ili tuwatume wajumbe katika nchi yote ya Israeli. Kama hakuna mtu yeyote wa kutuokoa, tutajisalimisha wenyewe kwako.” 4Wale wajumbe walipofika mjini Gibea, alikoishi Shauli, wakaeleza habari hizo na watu wote wakaanza kulia kwa sauti.
5Sasa, Shauli alikuwa anatoka shambani akiwa na fahali wake, akauliza, “Watu wana nini? Kwa nini wanalia?” Wakamwambia habari waliyoleta wajumbe kutoka Yabeshi. 6Mara, Shauli aliposikia maneno hayo, roho ya Mungu ikamjia kwa nguvu, naye akawaka hasira kali. 7Akachukua fahali wawili akawakatakata vipandevipande, akatuma wajumbe wavipitishe kila mahali nchini Israeli wakisema, “Mtu yeyote ambaye hatamfuata Shauli na Samueli vitani, fahali wake watafanywa hivyo.” Hofu ikawaaingia Waisraeli kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu angeweza kufanya. Kwa hiyo, wote walitoka kwa pamoja. 8Shauli alipowapanga Waisraeli huko Bezeki akawa na watu 300,000 kutoka Israeli na 30,000 kutoka Yuda. 9Wakawaambia wale wajumbe waliorudi kutoka Yabeshi, “Waambieni hivi wakazi wa Yabesh-gileadi: Kesho, wakati jua linapokuwa kali, mtakuwa mmekombolewa.” Watu wa Yabeshi walipopata habari hizo walifurahi sana. 10Hivyo, wakamkejeli Nahashi wakimwambia, “Kesho tutajisalimisha kwako, nawe utatutendea lolote unaloona ni jema.”
11Kesho yake, Shauli aliwagawa watu katika vikosi vitatu. Wakati wa zamu ya asubuhi, wakaingia kwenye kambi ya adui, na kuwashambulia Waamoni. Kufikia adhuhuri adui wengi walikuwa wamekatiliwa mbali. Wale walionusurika walitawanyika ovyo, hata kusiwe kikundi chochote cha watu wawili pamoja.
12Ndipo Waisraeli wakamwambia Samueli, “Wako wapi wale watu waliosema Shauli asiwe mfalme juu yetu? Tuletee watu hao, nasi tutawaulia mbali.” 13Lakini Shauli akawaambia, “Hakuna mtu yeyote atakayeuawa leo, kwa kuwa katika siku hii, Mwenyezi-Mungu ameikomboa Israeli.”
14Samueli akawaambia, “Twendeni wote Gilgali na kwa mara nyingine tutamtangaza Shauli kuwa mfalme.” 15Watu wote wakaenda Gilgali, na walipofika huko, wakamtawaza Shauli kuwa mfalme mbele ya Mwenyezi-Mungu. Wakamtolea Mwenyezi-Mungu tambiko za amani hapo. Na Shauli pamoja na watu wote wa Israeli wakafurahi sana.

1Samweli11;1-15

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.




Friday 29 December 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;1Samueli10...




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Mungu wetu yu mwema sana ..
Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo 
hii..
Utukuzwe Mungu wetu,Usifiwe Baba wa Mbinguni,Uhimidiwe yahweh
Unastahili kuabudiwa Jehovah..
Matendo yako ni makuu sana,Mtendo yako ni ya ajabu mno,hakuna kama wewe ee Mungu wetu,Unatosha Baba wa Mbinguni..

Anayekaa chini ya ulinzi wa Mungu Mkuu, anayeishi chini ya kivuli cha Mungu Mwenye Nguvu, ataweza kumwambia Mwenyezi-Mungu: “Wewe ni kimbilio langu na ngome yangu; Mungu wangu, ninayekutumainia!” Hakika Mungu atakuokoa katika mtego; atakukinga na maradhi mabaya. Atakufunika kwa mabawa yake, utapata usalama kwake; mkono wake utakulinda na kukukinga. Huna haja ya kuogopa vitisho vya usiku, wala shambulio la ghafla mchana; huna haja ya kuogopa baa lizukalo usiku, wala maafa yanayotokea mchana. Hata watu elfu wakianguka karibu nawe, naam, elfu kumi kuliani mwako, lakini wewe baa halitakukaribia. Kwa macho yako mwenyewe utaangalia, na kuona jinsi watu waovu wanavyoadhibiwa. Wewe umemfanya Mwenyezi-Mungu kuwa kimbilio lako; naam, Mungu aliye juu kuwa kinga yako. Kwa hiyo, hutapatwa na maafa yoyote; nyumba yako haitakaribiwa na baa lolote. Maana Mungu atawaamuru malaika zake, wakulinde popote uendapo. Watakuchukua mikononi mwao, usije ukajikwaa kwenye jiwe. Utakanyaga simba na nyoka, utawaponda wana simba na majoka. Mungu asema: “Nitamwokoa yule anipendaye; nitamlinda anayenitambua! Akiniita, mimi nitamwitikia; akiwa taabuni nitakuwa naye; nitamwokoa na kumpa heshima. Nitamridhisha kwa maisha marefu, nitamjalia wokovu wangu.”
Mungu wetu Baba yetu,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Tunakuja mbele zako ee Yahweh..
Jehovah tunaomba utusamehe Dhabi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea..
Mungu Baba tunaomba utuepushe katika majaribu Yahweh tunaomba
utuokoe na yule mwovu na Kazi zake zote..
Mfalme wa amani tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Jehovah tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu
Yesu Kristo wa Nazareti..
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..

“Iwapo kuna njaa nchini, au tauni, ukame, ugonjwa wa mimea, nzige au viwavi; au ikiwa watu wako wamezingirwa na adui zao katika mji wao wowote ule; ikiwa kuna pigo lolote au ugonjwa wowote, tafadhali, usikie maombi yoyote yatakayoombwa na watu wako, Israeli, au yatakayoombwa na mtu yeyote au watu wako wote wa Israeli; kila mtu akijua taabu za moyoni mwake, akikuomba huku akinyosha mikono yake kuelekea kwenye nyumba hii. Basi, usikie huko kwako mbinguni, utoe msamaha na kuchukua hatua; pia umtendee kila mtu kadiri anavyostahili (kwani ni wewe tu ujuaye mawazo ya mioyo ya wanadamu wote); ili wakutii wakati wote wanapoishi katika nchi uliyowapa babu zetu. “Vivyo hivyo, wakati mgeni asiye mmoja wa watu wako Israeli akija kutoka nchi ya mbali kwa ajili ya jina lako (maana watu wa mataifa mengine watasikia sifa zako na kuhusu nguvu na uwezo wako), mtu huyo akija na kuomba katika nyumba hii, nakusihi umsikie kutoka huko mbinguni, na umjalie huyo mgeni yote atakayokuomba; kusudi watu wote ulimwenguni wapate kujua jina lako na kukutii kama wafanyavyo watu wako, Israeli, na wapate kufahamu kwamba nyumba hii ambayo nimeijenga, inajulikana kwa jina lako. “Watu wako wakienda vitani kupigana na adui yao kokote kule utakakowapeleka, nao wakikuomba wakielekea mji uliouchagua na nyumba niliyoijenga kwa ajili ya jina lako, nakusihi usikie sala yao na maombi yao huko mbinguni, uwapatie ushindi vitani. “Ikiwa watatenda dhambi dhidi yako maana hakuna mtu asiyetenda dhambi, nawe ukiwakasirikia na kuwaacha washindwe na adui, hata wapelekwe mateka mpaka nchi ya adui iliyoko mbali au karibu; kama watakapokuwa huko uhamishoni watajirudi moyoni na kutubu na kukuomba msamaha, wakisema, ‘Tumetenda dhambi; tumepotoka na kufanya maovu;’ pia wakati huo watakapokuwa katika nchi ya adui zao, wakitubu kwa moyo wao wote na kwa roho yao yote, na kama watakuomba wakielekea nchi yao ambayo uliwapatia babu zao, wakielekea mji huu ambao uliuchagua na nyumba hii ambayo nimeijenga kwa ajili ya jina lako, basi, nakusihi kutoka huko mbinguni uliko usikie sala yao na ombi lao uwapatie haki zao. Uwasamehe watu wako dhambi walizotenda dhidi yako na uasi wao, uwahurumie mbele ya adui zao, ili nao wapate kuwahurumia, maana ni watu wako, na ni mali yako; watu ambao uliwatoa Misri kutoka katika tanuri ya chuma. “Uangalie ombi la mtumishi wako na ombi la watu wako, Israeli, uwasikie kila wanapokuomba. Kwa sababu, ee Bwana Mwenyezi-Mungu uliwatenga na watu wa mataifa mengine duniani, ili wawe mali yako – kama ulivyotangaza kwa njia ya Mose, mtumishi wako, wakati ule ulipowatoa babu zetu katika nchi ya Misri.”
Yahweh tunaomba ukabariki Kazi za mikono yetu Mungu wetu tunaomba
ukatupe ubunifu na maarifa katika ufanyaji/utendaji Yahweh nasi tunaomba tukatende sawasawa na mapenzi yako
Mungu wetu tunaomba ukabariki ridhili zetu ziingiazo/zitokazo
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Baba wa Mbibguni tusipungukiwe katika mahitaji yetu Yahweh
ukatupe kama inavyokupendeza wewe..

Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika nyumba/ndoa zetu,Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Jehovah tunaomba ukabariki Maisha yetu,Mungu wetu  ukatamalaki na kutuatamia,Yahweh tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Baba wa Mbinguni tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu..Yahweh ukatupe hekima,busara na tukanene yaliyo yako
tukapate kutambua/kujitambua,Mungu wetu ukaonekane popote tupitapo
Yahweh na ijulikane kwamba upo Baba wa mbinguni..
Ukatufanye chombo Chema Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...

Solomoni alipomaliza kusema sala hiyo yote na ombi lake kwa Mwenyezi-Mungu aliinuka kutoka pale mbele ya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu, mahali alipokuwa amepiga magoti akiinua mikono yake juu. Alisimama, akawabariki Waisraeli wote waliokuwa wamekusanyika hapo, akisema kwa sauti kubwa, “Atukuzwe Mwenyezi-Mungu ambaye amewapatia starehe watu wake Israeli, kulingana na ahadi yake. Ametimiza ahadi zake zote njema alizozitoa kupitia kwa mtumishi wake Mose. Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, awe nasi, kama alivyokuwa na babu zetu; tunaomba asituache, wala asitutupe. Yeye aelekeze mioyo yetu kwake, ili tufuate njia zake, tukishika amri zake, maongozi yake na maagizo yake aliyowapa babu zetu. Basi, maneno yangu haya ambayo ni ombi langu mbele ya Mwenyezi-Mungu, yawe karibu na Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, mchana na usiku, naye amjalie mtumishi wake, na watu wake Israeli, ili wafanikiwe katika haja zao za kila siku. Nayo mataifa yote ulimwenguni yatajua kwamba kweli Mwenyezi-Mungu ndiye Mungu; wala hakuna mwingine. Nanyi, muwe waaminifu kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, mkifuata masharti yake na kutii amri zake zote kama mnavyofanya hivi leo.”
Mfalme wa Amani tunaomba amani yako ikatawale kwa wote
wenye hofu na mashaka,Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono
wako wenye nguvu wenye shida/tabu,Yahweh tunaomba ukawaponye wagonjwa na ukawape uvumilivu/nguvu wanaowauguza,Jehovah ukawavushe salama wote wanaopitia magumu/majaribu Jehovah ukawasamehe wale wote waliokwenda kinyume nawe ..
Mungu Baba tunaomba uwape chakula wenye njaa,Yahweh tazama
wanaotafuta Kazi,wanaotaka kurudi/kuendelea na shule,wanaotafuta watoto,wanaotaka kuingia katika ndoa Mungu wetu ukawape wenza walio wako..
Yahweh tunaomba ukapokee sala/maombi yetu,Mungu wetu tunaomba ukawape sawasawa na mapezni yako wote wanaokuomba kwa bidii na imani..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!

Asanteni Sana wapendwa katika Kristo Yesu kwa kuwa pamoja nami
Yahweh aendelee kuwabariki na kuwatendea katika yote yampendezayo
Amani ya Kristo Yesu iwe nanyi Daima..
Nawapenda.


1Ndipo Samueli akachukua chupa ndogo ya mafuta akammiminia Shauli kichwani, akambusu na kumwambia, “Mwenyezi-Mungu amekutia mafuta uwe mtawala juu ya watu wake. 2Leo tutakapoagana, utakutana na watu wawili karibu na kaburi la Raheli huko Selsa katika nchi ya Benyamini. Hao watakuambia kuwa wale punda uliokuwa unawatafuta wamekwisha patikana. Baba yako ameacha kufikiri juu ya punda, ila ana wasiwasi juu yako, akijiuliza kila mara, ‘Nitafanya nini juu ya mwanangu?’ 3Kutoka hapo utakwenda kwenye mwaloni wa Tabori, mahali ambapo utakutana na wanaume watatu wakiwa njiani kwenda kumtolea Mungu tambiko, huko Betheli. Mmoja wao atakuwa anawachukua wanambuzi watatu, wa pili atakuwa anachukua mikate mitatu na wa tatu atakuwa amebeba kiriba cha divai.
4“Watakusalimia na kukupa mikate miwili, nawe utaipokea mikononi mwao. 5Kisha, utakapofika huko Gibea-elohimu,10:5 Gibeath-elohimu: Mlima wa Mungu. mahali ambapo pana kambi ya kijeshi ya Wafilisti; hapo, utakapokuwa unakaribia mji, utakutana na kundi la manabii. Manabii hao watakuwa wanatoka mahali pa juu huku wakipiga vinubi, matari, filimbi na zeze, na watakuwa wanatabiri. 6Roho ya Mwenyezi-Mungu itakujia kwa nguvu, nawe utaanza kutabiri pamoja nao na kugeuka kuwa mtu mwingine. 7Wakati mambo haya yatakapokutokea, chochote utakachoweza kufanya kifanye, kwani Mungu yu pamoja nawe. 8Utanitangulia kwenda mjini Gilgali, mahali ambapo nitakukuta na kutoa sadaka ya kuteketezwa na tambiko za amani. Utaningojea hapo kwa muda wa siku saba mpaka nije na kukuonesha la kufanya.”
9Shauli alipogeuka ili kumwacha Samueli, Mungu akabadili moyo wa Shauli. Yale yote aliyoambiwa na Samueli yakatokea siku hiyo. 10Shauli na mtumishi wake walipofika huko Gibea,10:10 Gibea: Au Mlimani. alilakiwa na kundi la manabii. Roho ya Mungu ilimjia kwa nguvu, na Shauli akaanza kutabiri pamoja na manabii hao. 11Watu waliomfahamu Shauli hapo awali, walipomwona anatabiri, wakaulizana, “Kitu gani kimempata mwana wa Kishi? Je, hata Shauli ni mmoja wa manabii?” 12Mtu fulani, mkazi wa mahali hapo, akasema, “Je, baba yao ni nani?” Hivyo kukazuka methali isemayo, “Je, hata Shauli ni mmoja wa manabii?” 13Shauli alipomaliza kutabiri, alikwenda mahali pa ibada juu.
14Baba mdogo wa Shauli alipowaona Shauli na mtumishi, akawauliza, “Mlikuwa wapi?” Shauli akajibu, “Tulikwenda kuwatafuta punda, na tulipoona hawapatikani, tulikwenda kumwona Samueli.” 15Yule baba mdogo wa Shauli akamwambia, “Tafadhali, niambie kile alichokuambia Samueli.” 16Shauli akajibu, “Alituambia waziwazi kuwa punda wamepatikana.” Lakini Shauli hakumweleza kuwa Samueli alimwambia kuwa atakuwa mfalme.

Shauli atangazwa kuwa mfalme

17Samueli aliwaita watu wote wakusanyike mbele ya Mwenyezi-Mungu huko Mizpa. 18Walipowasili aliwaambia, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, anasema hivi: Niliwatoa Waisraeli nchini Misri, nikawaokoa nyinyi kutoka kwa Wamisri na falme nyingine zilizowakandamiza. 19Lakini leo hii mmenikataa mimi Mungu wenu ambaye nawaokoa kutoka maafa na huzuni zenu; nanyi mmesema, ‘La! Tuwekee mfalme juu yetu.’ Sasa, basi, jikusanyeni nyote mbele yangu mkiwa katika makabila yenu na kwa maelfu yenu.” 20Kisha Samueli akayapanga makabila yote ya Israeli, kabila la Benyamini likachukuliwa kwa kura. 21Akalileta mbele kabila la Benyamini, kulingana na koo zake, na ukoo wa Matri ukachaguliwa kwa kura. Mwisho akauleta mbele ukoo wa Matri, na Shauli mwana wa Kishi akachaguliwa kwa kura. Lakini walipomtafuta hakupatikana. 22Wakamwuliza Mungu tena, “Je, kuna mtu zaidi anayekuja?”10:22 Je … anayekuja? au Je kuna mtu mwingine? Mwenyezi-Mungu akawajibu, “Anajificha kwenye mizigo.”
23Basi, walikwenda mbio, wakamtafuta Shauli na kumleta. Shauli aliposimama miongoni mwa watu alikuwa mrefu kuliko watu wote, kuanzia mabegani. 24Samueli akawaambia watu wote, “Huyu ndiye mtu aliyeteuliwa na Mwenyezi-Mungu katika watu wote; hakuna yeyote aliye kama yeye.” Watu wote wakapiga kelele: “Aishi mfalme.”
25Kisha, Samueli aliwaeleza watu juu ya wajibu na haki za mfalme, akaziandika katika kitabu ambacho alikiweka mbele ya Mwenyezi-Mungu. Kisha, Samueli aliwaaga watu wote, kila mtu aende nyumbani kwake. 26Pia, Shauli pamoja na wapiganaji hodari ambao awali Mungu aligusa mioyo yao, alikwenda nyumbani kwake huko mjini Gibea. 27Lakini watu wengine wasiofaa kitu, walisema, “Je, mtu huyu anaweza kutuokoa?” Walimdharau Shauli na hawakumpa zawadi yoyote. Lakini yeye hakukasirika.


1Samweli10;1-27
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.