KLABU ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa (IPC) na waandishi wa habari wote mkoani Iringa na nchini kwa ujumla wamepokea kwa mshutuko na masikitiko makubwa kifo cha Mwenyekiti wa IPC, Daudi Mwangosi.
Mwangosi ambaye pia ni Mwandishi wa Habari wa Channel Ten, alifariki jana majira ya saa 10 jioni baada ya kupigwa bomu katika vurugu za wafuasi wa Chadema waliokuwa wakitawanywa na jeshi la Polisi.
Utata wa nani anahusika na tukio hilo umeendelea kugubika huku jeshi la Polisi likitoa tamko linalodhihirisha dhahiri kwamba wanataka kujiondoa katika kosa hilo kabla uchunguzi haujafanyika.
Katika taarifa ya jeshi hilo iliyotolewa na Polisi hii leo imedai kwamba bomu linalodaiwa kumuuawa mwandishi huyo lilitoka katika kundi la wafuasi wa Chadema, wakati Mwangosi akitafuta msaada wa kujinusuru kwa askari waliokuwepo katika eneo hilo.
Lakini wakati jeshi hilo likitoa taarifa hiyo inayokinzana yenyewe, limeshindwa kueleza ni kwasababu gani bomu lililorushwa kutoka katika kundi la wafuasi hao likamdhuru na kumuua mwandishi huyo pekee yake wakati alikuwa ameshikiliwa na mmoja wa askari wa jeshi hilo baada ya kupigwa virungu alipotaka kujua sababu ya kukamtwa kwa mwandishi mwingine Godfrey Mushi aliyekuwa akipiga picha tukio hilo.
Uchunguzi wa awali wa IPC unapingana kwa asilimia zote na taarifa ya jeshi hilo kwa kuzingatia taarifa zilizotolewa na baadhi ya waandishi waliokuwepo katika tukio hilo na zile zilizoandikwa na kurushwa na vyombo mbalimbali vya habari toka jana.
Taarifa kutoka katika vyanzo vyetu zinaonesha kwamba Mwangosi alipigwa kwa virungu kabla ya kulipuliwa na bomu hilo ambalo kwa vyovyote vile muhusika wake mkuu anaweza kuwa jeshi hilo.
Ili taarifa hiyo potofu isiendelee kuugubika umma, IPC imeamua kutoa tamko linalolenga kuviarifu vyombo huru viiingilie kati katika uchunguzi huo.
Na kwa kuzingatia mazingira hayo, IPC kwa kushirikiana na waandishi wote wanaofanya kazi mkoani Iringa, kuanzia leo wanatangaza rasmi kusitisha ushirikiano wa kikazi baina yao na jeshi hilo mpaka pale taarifa au majibu sahihi kutoka kwa vyombo huru vitakavyolifanyia kazi suala hilo yatakapotolewa.
Kazi hizo ni pamoja na kuwataarifu waandishi wa habari kusitisha mara moja kwenda katika Ofisi ya RPC kwa ajili ya kupata taarifa za matukio mbalimbali ya uhalifu yanayotokea kila siku.
Aidha IPC inawataka wanachama au viongozi wake waliokuwa wajumbe wa kamati zozote zile zinazolihusu jeshi hilo ikiwemo ile ya maandalizi ya wiki ya usalama barabarani kujitoa kwenye kamati hizo.
IPC inawaomba waandishi wa habari kushikamana katika kipindi hiki kigumu kwa kuzingatia kwamba yaliyomkuta ndugu yetu Mwangosi yanaelekea kumkuta mwandishi yoyote Yule nchini.
Tukio hilo linadhihirisha jinsi uhuru wa habari na vyombo vya habari unavyozidi kukandamizwa hasa katika kipindi hiki ambacho watanzania kwa ujumla wao wanatakiwa kushiriki kikamilifu kuandika Katiba Mpya wanaoitaka.
Tukio hilo haliwezi kuvumiliwa na kwa msimamo huu, IPC inaomba waandishi wote wawe na wimbo mmoja utakaowezesha muhusika wa mauaji hayo akamatwe na kushitakiwa kwa mujibu wa sheria za nchi.
Pamoja na kukamwata kwa muhusika, IPC inataka kuona jeshi la Polisi ambalo kimsingi halipo juu ya sheria linatimiza wajibu wake kwa kuzingatia sheria kama ilivyo kwa taasisi zingine.
Aidha kwa sasa wanahabari mkoa wa Iringa tunatangaza rasmi kusitisha mahusiano yetu na jeshi la polisi kwa kuandika habari za polisi .
Pia tunatambua kuwa wakati Mwangosi akikamatwa alikuwa katika kutimiza wajibu wake kama mwanahabari hivyo hata kama alikosa kwa kufika hapo hukumu yake haikuwa kuuwawa .
Hivyo kutokana na tukio hilo kubwa ambalo halikuwa na chembe ya siasa kwa mwanahabari huyo kwa kuwa hakuwa ni kiongozi wa chama cha Siasa IPC na Chanel Ten kama mwajiri wake na familia tunachukua dhamana ya kusimamia mazishi hayo bila huku tukiviomba vyama vya siasa kutovuruga taswira ya Tasnia hii ambayo kamwe haifungamani ya chama chochote cha Siasa .
Na tunalitaka jeshi la Polisi litoe ushirikiano kwa kutoa taarifa sahihi na za kweli kwa makundi huru yanayoendelea kulichunguza suala hilo.
Kifo cha Mwangosi kimetufanya wanahabari kote nchini kujipanga upya katika kutathimini upya mahusiano yetu na jeshi la polisi .
Mungu ailaze mahali pema roho ya Marehemu Daud Mwangosi. Amin
Francis Godwin
katibu msaidizi IPC
Shukrani;http://www.mjengwablog.com/