Post yake ya Kwanza
08 MAY 2005
Ngo...ngo...ngo..hodiii!
Ngo...ngo..ngo... hodiii, jamani wenyewe mpoo?...inaelekea wametoka, ngoja niache ujumbe mlangoni. Wanablogu, Nilipita kwenu lakini inaelekea hamkuwepo, nia hasa ilikuwa nikuwapa taarifa kwamba nami nimeingia katika ulimwengu wa blogu. Blogu yangu itajulikana kwa jina la Da'Mija, Da mija atakuwa akizungumzia masuala ya jamii na mabadiliko yake ya kila siku. Atafundisha atakapoona panafaa kufundisha, atajadili pale atakapoona panafaa kujadili, atatoa mawazo pale atakapoona panafaa kutoa mawazo na mengine mengi yatajitokeza kulingana na siku zitakavyokuwa zikienda. Asanteni. |
20 MAY 2005
Huyu ndiye mwanamke wa shoka.
Sifa hizi za mwanamke wa shoka nimezipata katika maandiko matakatifu ya wakristo katika kitabu cha Mithali 31:10-31. Zinasema hivi:-
Mke mwema ni nani awezaye kumwona?
Maana kimachake chapita kima cha marijani.
Moyo wa mumewe humwamini,wala hatakosa kupata mapato.
Humtendea mema wala si mabaya, siku zote za maisha yake.
Hutafuta sufu na kitani,hufanya kazi yake ya mikono kwa moyo.
Afanana na merikebu za biashara,huleta chakula chake kutoka mbali.
Tena huamka kabla haujaisha usiku,
Huwapa watu wa nyumbani mwake chakula, na wajakazi wake sehemu zao.
Huangalia shamba akalinunua, kwa mapato ya mikono yake hupanda mizabibu.
Hujifunga nguvu viunoni kama mshipi, hutia mikono yake nguvu.
Huona kama bidhaa yake ina faida, taa yake haizimiki usiku.
Hutia mikono yake katika kusokota, na mikono yake huishika pia.
Huwakunjulia maskini mikono yake, naam huwanyooshea wahitaji mikono yake.
Hawahofii theluji watu wa nyumbani mwake, maana wote wa nyumbani mwake huvikwa nguo nyekundu.
Hujifanyizia mazulia ya urembo, mavazi yake ni kitani safi na urujuani.
Mume wake hujulikana malangoni, aketipo pamoja na wazee wa nchi.
Hufanya nguo za kitani na kuziuza, huwapa wafanyabiashara mishipi.
Nguvu na hadhi ndiyo mavazi yake, anaucheka wakati ujao.
Hufumbua kinywa chake kwa hekima, na sheria ya wema i katika ulimi wake.
Huangalia sana njia za watu wa nyumbani kwake, wala hawali chakula cha uvivu.
Wanawe huondoka na kumwita heri, mumewe naye humsifu na kusema,
Binti za watu wengi wamefanya mema, lakini wewe umewapita wote.
Upendeleo hudanganya, na uzuri ni ubatili,
Bali mwanamke amchaye Bwana ndiye atakayesifiwa.
Mpe mapato ya mikono yake, na matendo yake yamsifu malangoni.
27 SEPTEMBER 2005
Upendo ni kila kila kitu.
Upendo ni kupenda. Unapopenda kitu hutaki kitu kile kipate madhara ya aina yoyote yale, na pale inapotokea kitu hicho kukumbwa na tatizo basi utafanya juu chini kuhakikisha unatatua tatizo hilo. Mwanao akiumwa utafanya juu chini kuhakikisha anarudia afya yake ya kawaida, unapogombana na Joe Tungaraza wako (mwandani) basi utahakikisha mambo mnayaweka sawa muda si mrefu hii yote ni katika kutaka kuishi kwa raha. Waswahili husema "penye upendo hapaharibiki neno".
Siku zote nimekuwa nikijiuliza ni kwa nini kuna vita, kwa nini kuna matabaka katika jamii zetu, kwa nini kuna rushwa, kwa nini kuna wivu usiokuwa wa maendeleo katika jamii zetu , kwa nini kuna migogoro isiyoisha.. Nimekaa nimefikiria sana na sasa nimepata jibu moja kwamba ni sababu ya ukosefu wa upendo.
Sisemi kwamba kwenye upendo migogoro haitokei hasilani..hapana migogoro hutokea lakini haidumu kwa muda mrefu na kuwa tatizo sugu. Sehemu yoyote yenye upendo watu hujaliana na kuthaminiana, humpenda mwenzie kama anavyojipenda yeye katu hatataka jirani yake apatwe na baya lolote na kama ikatokea mmoja akakumbwa na tatizo basi husaidiana kulitatua. Na huu ndio upendo wa kweli.
Sasa hivi tulio wengi hatuna upendo kabisaaa, si viongozi wa nchi, si raia si yeyote yule. Watu tumegeuka wabinafsi tunajipenda wenyewe tu, kama mtu mambo yako yakiwa swafi basi uhangaiki na mwingine kujua siku imemuendeaje, labda hakula au anauguliwa wewe hujui maadamu siku yako imepita vizuri yeye atajaza mwenyewe. Tukija kwa viongozi wetu....ma-ma-ma-maaa yaani hao ndio usiseme kabisa, kwa jinsi ninavyojua viongozi ndio kama wazazi wetu, husimama badala yetu sisi kama watoto wao na kuhakikisha hatupati matatizo yoyote kuanzia chakula, mavazi, malazi na mienendo ya tabia zetu. Lakini cha ajabu wazazi wetu hawa wamekosa upendo kabisa kwetu sisi watoto wao, wanakula wenyewe kwanza halafu ndio watoto, watoto wasiposhiba wenyewe hawajali, hawajui watoto wamelalaje au wameamkaje, wameenda shule au hawakwenda au wameacha kabisa hiyo wenyewe hawajui wanachojua ni kujishindilia wenyewe basi. Na mimi hili halinishtui kuona kwa nini watoto nao wanaamua kujiingiza katika makundi yaujambazi na unyakuaji au tabia zozote potofu yote hii ni katika kujaribu kujisaidia maana wazazi wao hawajali. Ndio ni kweli watoto hujifunza kutoka kwa wazazi wao na kama mzazi haonyeshi upendo kwa wanae, watoto watajifunzaje upendo wa kumjali jirani yake?
Tanzania tuna watoto wengi wenye vipaji vya hali ya juu sana, lakini tunashindwa kuwaendeleza watoto wetu kwa vile vipato vyetu viko chini, na hatuwezi kumudu gharama za kuwalipia masomo. Sawa ni kweli lakini bado najiuliza hawa viongozi wetu wenye akaunti zao nchi za ulaya wanashindwa nini kujitolea angalau kila mmoja achukue watoto wawili tu na kuwasomesha? nina hakika hawatapungukiwa na kitu na huo ndio upendo ninaouongelea, hebu fikiria hawa matajiri wote wa Tanzania unaowafahamu wajitolee kusomesha watoto wasio na uwezo wa kifedha katika mashule yao ya akademiki ingekuwaje, nina hakika hawa watoto wasingechezea bahati wangeitwa John visomo. Na ni katika watoto hawa ndio tungepata vijana madhubuti wa taifa la kesho, tofauti na wengi wa watoto wa matajiri waliokulia katika fedha hawana shida ya kujishughulisha sana na masomo kwani fedha ipo na wanafikiri itakuwepo milele.
Haya, mimi sina mengi ya kusema lakini akili yangu inanituma kusema kwamba kama watanzania tutarudisha upendo kati yetu basi mabalaa yooote yanayotufuata fuata yatatafuta njia ya kutokea.
07 DECEMBER 2005
Jamani ninaomba ruksa yenu!
Ndugu wasomaji, Kuna hili suala nyeti sana katika ulimwengu huu, suala la MAHUSIANO YA KIMAPENZI. Suala hili ingawa ni nyeti sana na linalomhusu karibu kila mtu mzima hapa ulimwenguni, lakini ni suala la mwisho kabisa katika kuzungumziwa kwa UWAZI, imekuwa ikioneka kama ni ukosefu wa adabu kulijadili hadharani, Matokeo yake watu tumekuwa tukilivamia tu bila kuchukua tahadhari zozote au bila kujua tunacho kihitaji hasa katika mahusiano hayo na hivyo kusababisha wengi wetu kuishia matatizoni.
Binafsi nimekaa nikaona si vyema kuendelea kulifungia macho suala hili, kuna haja ya kuanza kulizungumza kwa uwazi huku wote kwa pamoja tukishirikiana katika kubadilishana mawazo. Nia hasa ikiwa ni kufunguana akili ili tuweze kuwa makini zaidi wakati tunapoamua kuingia katika mahusiano hayo.
Hivyo basi sina budi kuomba ruksa yenu ili kwa pamoja tukubaliane kuliweka sebuleni jambo ambalo ambalo linaonekana ni la chumbani.
Kuna mambo mengi ya kuyajadili, lakini labda tuanze na hili dogo.
NI VITU GANI MWANAUME HUTEGEMEA KUVIPATA KUTOKA KWA MWANAMKE? NA MWANAMKE KUTOKA KWA MWANAUME?
Wasomaji, ninaamini mjadala huu utatusaidia katika kujitambua zaidi, na kuwa makini wakati tunapotaka kufanya maamuzi.
23 DECEMBER 2005
Viti Maalumu ...
Jamani sijui kama na wenzangu mnaliona hili, binafsi ninaona kuna njama za chini kwa chini zinazofanywa na wanaume kuwazima kabisa wanawake katika harakati za ukombozi. Kumkamilishia mtu mahitaji yake ni kumfanya mtu asipambane, na bila mapambano hakuna ushindi, ushindi utabaki kwa yule anayekupigania. Hii tabia ya kutoa viti maalumu kwa wabunge wanawake inatufanya tusiwajibike ipasavyo na kubakia pale pale. Viti hivi vilitakiwa vipiganiwe ili utakapokipata ujue kweli jinsi ya kukifanyia kazi na kukiwajibikia. Hii tabia ya kupewa-pewa ina mambo mengi ambayo wanawake tunatakiwa tuyajue...Kupewa kwa aina yoyote ile kunaendana na kulipa fadhira, kwa hiyo kupewa huku kwa viti maalum tusikuchukulie juu juu, wabunge hawa wajiandae kupangiwa ya kufanya na kuwekewa mipaka ya kufika. Na kama ukitaka kwenda kinyume na mipaka hiyo basi utakumbushwa jinsi ulivyokipata kiti, kwa hiyo itabidi ukubali yaishe.
Sasa wenzangu hali hii kweli itatufikisha tuendako? ..hili nalo ni lazima tulifanyie kazi. Wabunge wenyewe waliotangazwa hawa hapa chini.
2005-12-23 08:32:50
Na Mwandishi wetu.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi, imewatangaza rasmi wanawake 64 wa Vyama vya CCM na CHADEMA kuwa wabunge wa viti maalum.
Wabunge 58 miongoni mwa hao ni wa CCM na wengine sita ni wa CHADEMA.
Hata hivyo taarifa ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, ilisema tume imeshindwa kutangaza wabunge maalum kupitia chama cha CUF kwa sababu chama hicho hakijawasilisha majina.
Taarifa hiyo iliwataja wabunge wa viti maalum kupitia CCM kuwa ni Bi Anna Magreth Abdallah, Bi Faida Mohamed Bakari, Bi Martha Jachumbulla, Bi Elizabeth Nkunda Batenga, Bi Zainabu Matitu Vulu na Bi Cynthia Hilda Ngoye.
Wengine ni Bi Esther Kabadi Nyawazwa, Bi Mariam Salum Mfaki, Bi Anastazia James Wambura, Bi Gaudensia Mugosi Kabaka, Bi Sijapata Fadhili Nkayamba, Dk. Aisha Omari Kigoda, Bi. Salome Joseph Mbatia na Dk Lucy Sawere Nkya.
Hali kadhalika Bi Joyce Nhamanilo Machimu, Bi Eliata Ndumpe Switi, Bi Lediana Mafuru Mng’ong’o, Bi Diana Nkumbo Chilolo, Dk Batilda Salha Burian, Bi Asha Mshimba Jecha na Bi Fatma Othman Ali.
Katika orodha hiyo ya wabunge wa CCM pia kuna Bi Devota Mkuwa Likokola, Bi Bahati Ali Abeid, Dk Maua Abeid Daftari, Bi Fatma ABdallah Mikidadi, Bi Janet Bina Kahama, Bi Aziza Sleyum Ally, Dk Asha-Rose Migiro, Bi Shamsa Selengia Mwangunga, Bi Margreth Agnes Mkanga, Bi Zuleikha Yunus Haji na Bi Lucy Thomas Mayenga.
Wengine ni Bi Amina Chifupa Mpakanjia, Bi. Margreth Simwanza Sitta, Bi Felista Aloyce Bura, Bi Halima Mohamed Mamuya, Bi. Rosemary Kasimbi Kirigini, Bi Mwanne Ismail Mchemba, Bi Anna Richard Lupembe, Bi Halima Omari Kimbau, Bi Dorah Herial Mushi na Bi Mwantumu Bakari Mahiza.
Wabunge wengi wa CCM wa viti maalum vya wanawake ni Bi. Riziki Lulida Said, Bi Mariam Reuben Kasembe, Bi Mwanakhamis Kassim Said, Bi. Janeth Mourice Massaburi, Bi Benadetha Kasabogo Mushashu, Bi. Maida Hamadi Abdallah, Bi Mwaka Abdulrahman Mbaraka, Bi Kumbwa Makame Mbaraka, Bi Joyce Martin Masunga, Bi Josephine Johnson Ngenzobuke, Bi Kidawa Hamid Salehe, Bi Martha Moses Mlata, Bi Shally Joseph Raymond, Bi Maria Ibeshi Hewa, Bi Pindi Hazara Chana na Bi Stella Martin Manyanya.
Kwa upande wa CHADEMA waliotangazwa kuwa wabunge wa viti maalum vya wanawake ni Bi Grace Sindato Kiwelu, Bi Maulidah Anna Komu, Bi Mhonga Said Ruhwanya, Bi Lucy Fidelis Owenye, Bi Susana Anselm Jerome Lyimo na Bi Halima James Mdee
Kuhusu wabunge wa CUF Tume ya Taifa ya Uchaguzi imesema imechukua hatua za kukiomba chama hicho kuwasilisha majina.
"Swahili NA Waswahili na Wanawake Wa Shoka
Pamoja daima.