1Oneni, basi, jinsi Baba alivyotupenda mno hata tunaitwa watoto wa Mungu! Na kweli, ndivyo tulivyo. Ndiyo maana ulimwengu haututambui sisi, kwani haumjui Mungu.2Wapenzi wangu, sisi ni watoto wa Mungu sasa, lakini bado haijaonekana wazi jinsi tutakavyokuwa. Lakini tunajua kwamba, wakati Kristo atakapotokea, tutafanana naye kwani tutamwona vile alivyo. 3Basi, kila mtu aliye na tumaini hili katika Kristo, hujiweka safi kama vile Kristo alivyo safi kabisa.
4Kila mtu atendaye dhambi anavunja sheria ya Mungu, maana dhambi ni uvunjaji wa sheria. 5Mnajua kwamba Kristo alikuja kuziondoa dhambi zetu, na kwamba kwake hamna dhambi yoyote. 6Basi, kila aishiye katika muungano na Kristo hatendi dhambi; lakini kila mtu atendaye dhambi hakupata kamwe kumwona wala kumjua Kristo.7Basi, watoto wangu, msikubali kupotoshwa na mtu yeyote. Mtu atendaye matendo maadilifu ni mwadilifu kama vile Kristo alivyo mwadilifu kabisa. 8Lakini atendaye dhambi ni wa Ibilisi, maana Ibilisi ametenda dhambi tangu mwanzo. Lakini Mwana wa Mungu alikuja duniani kuiharibu kazi ya Ibilisi.
9Kila aliye mtoto wa Mungu hatendi dhambi, maana anayo hali ya kimungu ndani yake; hawezi kutenda dhambi kwa sababu yeye ni mtoto wa Mungu. 10Lakini yeyote asiyetenda mambo maadilifu, au asiyempenda ndugu yake, huyo si mtoto wa Mungu. Hiyo ndiyo tofauti iliyoko kati ya watoto wa Mungu na watoto wa Ibilisi.