4 Hivyo utakubalika na kusifika,
mbele ya Mungu na mbele ya wanadamu.
5Mtumaini Mwenyezi-Mungu kwa moyo wako wote,
wala usitegemee akili zako mwenyewe.
6Umtambue Mungu katika kila ufanyalo,
naye atazinyosha njia zako.
7 Usijione wewe mwenyewe kuwa mwenye hekima;
mche Mwenyezi-Mungu na kujiepusha na uovu.
8Hiyo itakuwa dawa mwilini mwako,
na kiburudisho mifupani mwako.
9Mheshimu Mwenyezi-Mungu kwa mali yako,
na kwa malimbuko ya mazao yako yote.
10Hapo ghala zako zitajaa nafaka,
na mapipa yako yatafurika divai mpya.
11 Mwanangu, usidharau adhabu ya Mwenyezi-Mungu,
wala usiudhike kwa maonyo yake;
12 maana Mwenyezi-Mungu humwonya yule ampendaye,
kama baba amwonyavyo mwanawe mpenzi.
13Heri mtu anayegundua hekima,
mtu yule anayepata ufahamu.
14Hekima ni bora kuliko fedha,
ina faida kuliko dhahabu.
15Hekima ina thamani kuliko johari,
hamna unachotamani kiwezacho kulingana nayo.
16Kwa mkono wake wa kulia Hekima atakupa maisha marefu;
kwa mkono wake wa kushoto atakupa mali na heshima.
17Njia zake ni za kupendeza,
zote zaelekea kwenye amani.
18Hekima ni mti wa uhai kwa wote wampatao;
wana heri wote wanaoshikamana naye.
19Kwa hekima Mwenyezi-Mungu aliweka misingi ya dunia,
kwa akili aliziimarisha mbingu.
20Kwa maarifa yake vilindi vilipasuka,
na mawingu yakadondosha umande.