Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday, 3 February 2017

Wanawake na Maisha;Mwanamke/Mama huyu Mjane amenigusa..;Wanawake wengi wanapitia haya...







Shukrani;BongoStars

Haya mambo yanawakuta wanawake wengi wanapofiwa na waume/wenza wao,Inafikia baba wadogo/Ndugu wa mume wanawagombanisha mama na watoto...
Wewe imeshakukuta/kupitia haya matatizo, Au mtu wako wa karibu?
Mungu awabariki wamama wote na wote wanaopitia/waliopitia haya.

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo12..

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tunamshukuru Mungu muumba wa Mbingu na Nchi,
Muweza wa yote,Bwana wa Mabwana,
Baba wa Yatima,Mume wa Wajane..
Tumsifu,Tumuabudu,Tumuombe,Tumkabidhi mizigo yetu...
Asante Mungu wetu kwa Neema/Rehema hii Baba ya kuiona siku nyingine tena
wengi walitamani kuiona Baba lakini imeshindikana,
 si kwamba si wema au wakosefu sana bali ni kwa Mapenzi yako..
Ukabariki  Kuingia/Kutoka kwetu,Vyombo vya usafiri,kazi zetu Baba wa mbinguni,Biashara,Masomo na ukatupe sawasawa na mapenzi yako.
Utulinde na kutuokoa katika Shida/Tabu,Ukawafariji wafiwa,Utusamehe Baba wa Mbinguni nasi tupate kuwasamehe waliotukosea,Tunakwenda kinyume na Shetani na Tunakutanguliza/Kuja kwako Mfalme wa Amani..Ukatuongoze katika Maisha yetu.
Ameeeen..!!!!
Mungu yu Macho na  Anasamehe,Anasikia, Omba pasipo  kuchoka.
Mbarikiwe sana.


Mungu anamwita Abramu aiache nchi yake

1Basi, Mwenyezi-Mungu akamwambia Abramu, “Ondoka katika nchi yako, acha jamaa yako na nyumba ya baba yako, uende katika nchi nitakayokuonesha. 2Nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, nitakubariki na kulikuza jina lako, nawe uwe baraka.
3Anayekubariki, nitambariki;
anayekulaani, nitamlaani.
Kwako wewe, nitayabariki mataifa yote ya dunia.”
4Kwa hiyo, Abramu akaondoka kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru; na Loti akaenda pamoja naye. Abramu alikuwa na umri wa miaka 75 alipotoka Harani. 5Alimchukua Sarai mkewe, na Loti mwana wa ndugu yake, pamoja na mali yao yote na watu wote waliokuwa wamejipatia huko Harani, wakaondoka kuelekea nchi ya Kanaani. Walipoingia nchini Kanaani, 6Abramu akapita katikati ya nchi mpaka Shekemu, mahali patakatifu, penye mti wa mwaloni wa More. Wakati huo, Wakanaani walikuwa ndio wenyeji wa nchi hiyo. 7Ndipo Mwenyezi-Mungu akamtokea Abramu, akamwambia, “Wazawa wako nitawapa nchi hii.” Basi, Abramu akajenga madhabahu kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu aliyemtokea. 8Baadaye Abramu akaondoka, akaelekea mlimani mashariki ya Betheli akapiga hema kati ya mji wa Betheli, upande wa magharibi, na mji wa Ai upande wa mashariki. Hapo pia akamjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu na kumwomba kwa jina lake. 9Kisha Abramu akaendelea kusafiri kuelekea upande wa Negebu.

Abramu nchini Misri

10Wakati huo, njaa ilitokea nchini. Njaa hiyo ilikuwa kali, hivyo Abramu akalazimika kwenda Misri kukaa huko kwa muda. 11Alipokaribia Misri, Abramu alimwambia Sarai mkewe, “Najua kuwa wewe ni mwanamke mzuri na wa kuvutia. 12Wamisri watakapokuona watasema, ‘Huyu ni mkewe,’ kisha wataniua lakini wewe watakuacha hai. 13Basi, waambie kuwa wewe ni dada yangu ili mambo yaniendee vema, niachwe niishi kwa ajili yako.” 14Basi, Abramu alipowasili nchini Misri, wenyeji wa huko walimwona Sarai kuwa ni mwanamke mzuri sana. 15Maofisa wa Farao walipomwona Sarai, wakamsifia kwa Farao. Basi, Sarai akapelekwa nyumbani kwa Farao. 16Basi, kwa ajili yake, Farao alimfadhili Abramu, akampa kondoo, ng'ombe, punda dume, watumishi wa kiume na wa kike, punda jike na ngamia.
17Lakini Mwenyezi-Mungu akamtesa Farao na watu wote wa nyumba yake kwa mapigo makali kwa sababu ya Sarai, mkewe Abramu. 18Farao akamwita Abramu, akamwuliza, “Ni kitu gani hiki ulichonitendea? Mbona hukunijulisha kwamba Sarai ni mkeo? 19Kwa nini ulisema ni dada yako hata nikamchukua kuwa mke wangu? Basi, sasa mkeo ndiye huyo. Mchukue uende zako!” 20Kisha Farao aliwaamuru watu wake, nao wakamsindikiza Abramu njiani akiwa na mke wake na mali yake yote.
Mwanzo 12;1-20
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN):
Jifunze zaidi

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Thursday, 2 February 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo 11....

Shalom,habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Nimatumaini yangu mmeamka salama na mnaendelea/mmeanza na Mungu.
Mungu aendelee kutulinda,Kutubariki,Kututendea...
Katika Kazi,Biashara,Masomo,
Kwenye vyombo vya usafiri, Tuingiapo/Tutokapo,Vilaji/Vinywaji,Familia na katika yote
tumtangulize yeye Atoshaye,Ikawe siku njema yenye Amani,Furaha,Upendo,Faraja na shukrani...
Akawaguse wote Wanaopitia Magumu/Majaribu,Shida/Tabu Mungu hajawaacha Muite naye Ataitika
Mungu wetu yu mwema sana...!!!!!
Muwe na wakati mwema.


Mnara wa Babeli

1Kwanza, watu wote duniani walikuwa na lugha moja na walitumia maneno yaleyale. 2Basi, ikawa watu waliposafirisafiri kutoka mashariki, walifika katika nchi tambarare huko Shinari, wakakaa. 3Kisha wakaambiana, “Haya! Na tufyatue matofali, tuyachome moto vizuri.” Walikuwa na matofali badala ya mawe, na lami badala ya chokaa. 4Wakasema, “Na tujijengee mji na mnara ambao kilele chake kitafika mbinguni ili tujipatie jina, tusije tukatawanyika duniani kote.”
5Ndipo Mwenyezi-Mungu akashuka chini kuuona mji huo na mnara walioujenga binadamu. 6Mwenyezi-Mungu akasema, “Tazama, watu hawa ni taifa moja na wote wana lugha moja; huu ni mwanzo tu wa yale watakayoyafanya. Lolote wanalokusudia kulifanya watafanikiwa. 7Haya, na tushuke chini na kuivuruga lugha yao ili wasielewane wao kwa wao.” 8Hivyo, Mwenyezi-Mungu akawatawanya mahali pote duniani, nao wakaacha kuujenga ule mji. 9Mji huo ukaitwa Babeli, kwa sababu huko ndiko Mwenyezi-Mungu alikoivuruga lugha ya dunia yote, na kutoka huko akawatawanya watu kila mahali duniani.

Wazawa wa Shemu

10Wafuatao ni wazawa wa Shemu. Miaka miwili baada ya ile gharika, Shemu akiwa na umri wa miaka 100, alimzaa Arfaksadi. 11Baada ya kumzaa Arfaksadi, Shemu aliishi miaka 500 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
12Arfaksadi alipokuwa na umri wa miaka 35, alimzaa Shela. 13Baada ya kumzaa Shela, Arfaksadi aliishi miaka 403 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
14Shela alipokuwa na umri wa miaka 30, alimzaa Eberi. 15Baada ya kumzaa Eberi, Shela aliishi miaka 403 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
16Eberi alipokuwa na umri wa miaka 34, alimzaa Pelegi. 17Baada ya kumzaa Pelegi, Eberi aliishi miaka 430 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
18Pelegi alipokuwa na umri wa miaka 30, alimzaa Reu. 19Baada ya kumzaa Reu, Pelegi aliishi miaka 209 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
20Reu alipokuwa na umri wa miaka 32, alimzaa Serugi. 21Baada ya kumzaa Serugi, Reu aliishi miaka 207 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
22Serugi alipokuwa na umri wa miaka 30, alimzaa Nahori. 23Baada ya kumzaa Nahori, Serugi aliishi miaka 200 na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
24Nahori alipokuwa na umri wa miaka 29, alimzaa Tera. 25Baada ya kumzaa Tera, Nahori aliishi miaka 119, na kupata watoto wengine wa kiume na wa kike.
26Tera alipokuwa na umri wa miaka 70, alimzaa Abramu na Nahori na Harani.

Wazawa wa Tera

27Wafuatao ni wazawa wa Tera, baba yao Abramu, Nahori na Harani. Harani alikuwa baba yake Loti. 28Huyo Harani alifariki wakati Tera baba yake alikuwa anaishi huko Uri alikokuwa amezaliwa. 29Abramu na Nahori walioa. Mke wa Abramu aliitwa Sarai. Mke wa Nahori aliitwa Milka, binti Harani ambaye pia alikuwa baba yake Iska. 30Sarai hakuwa na mtoto kwa sababu alikuwa tasa.
31Tera akamchukua Abramu mwanawe, Loti mjukuu wake aliyekuwa mwanawe Harani, na Sarai mkewe Abramu, wakaondoka wote pamoja toka Uri, mji wa Wakaldayo, wakaenda katika nchi ya Kanaani. Lakini walipofika Harani, wakakaa. 32Tera alifariki huko Harani akiwa na umri wa miaka 205.
Mwanzo11;1-32

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (BHN):
Jifunze zaidi

"Swahili Na Waswahili" Mbarikiwe sana.

Wednesday, 1 February 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo 10....

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Ni mwezi/Siku mpya tena kwa mapenzi ya Muumba wa vyote ametupa Neema/Rehema ya kuiona tena..
Shukrani na Utukufu daima ni kwake Mungu,
Yeye awezaye yote,Yeye aponyae,
Yeye hutengeneza njia pasipo na njia,Yeye Abarikiae, Yeyeagawae ridhiki,Yeye ni mkuu wa vyote,
Yeye ni mwanzo na Yeye ni mwisho..
Jina lake na Litukuzwe milele na Milele.
Akawabariki wenye Shida/Tabu,Yatima/Wajane,Wagonjwa walio mahospitalini/Majumbani,Wafungwa wasio na Hatia
Waliopatwa na misiba akawe mfariji wao...
Wenye kutafuta watoto baba akawaguse...Wenye kukata tamaa wamgeukie Mungu yeye anaweza,
Tua mizigo uliyonayo Mungu anaponya....
Abariki Kazi zetu,Biashara Watoto wetu/Familia,Wanafunzi Mungu akawaongoze wapate kuelewa na kukumbuka wanayo fundishwa..Muombe kwa Kumaani sha,Kumtukuza na Kumsifu yeye Anatosha.!!!!
Mungu atuongoze vyema..


Wazawa wa Noa

1Baada ya gharika, watoto wa Noa, Shemu, Hamu na Yafethi, walipata watoto wa kiume na wa kike. Hii ndiyo orodha ya wazawa wao:
2Watoto wa kiume wa Yafethi walikuwa Gomeri, Magogu, Madai, Yavani, Tubali, Mesheki na Tirasi. 3Watoto wa kiume wa Gomeri walikuwa Ashkenazi, Rifathi na Togama. 4Watoto wa kiume wa Yavani walikuwa Elisha, Tarshishi, Kitimu na Dodanimu. 5Hawa ndio asili ya watu walioenea sehemu za pwani, kila watu kwa lugha yao, kwa jamaa zao na kufuata mataifa yao.
6Watoto wa kiume wa Hamu walikuwa Kushi, Misri, Puti na Kanaani. 7Watoto wa kiume wa Kushi walikuwa Seba, Hawila, Sabta, Raama na Sabteka. Watoto wa kiume wa Raama walikuwa Sheba na Dedani. 8Kushi alikuwa baba yake Nimrodi ambaye alikuwa shujaa wa kwanza duniani. 9Alikuwa mwindaji shujaa mbele ya Mwenyezi-Mungu, ndiyo maana kuna msemo usemao, “Kama Nimrodi mwindaji shujaa mbele ya Mwenyezi-Mungu.” 10Miji ya kwanza ya utawala wake ilikuwa Babuloni, Ereki na Akadi, katika nchi ya Shinari. 11Kutoka huko, Nimrodi alikwenda Ashuru, akajenga miji ya Ninewi, Rehoboth-iri, Kala na 12Reseni ulioko kati ya Ninewi na mji mkubwa wa Kala.
13Misri alikuwa babu wa Waludi, Waanamu, Walehabi, Wanaftuhi, 14Wapathrusi, Wakasluhi (ambao ndio asili ya Wafilisti), na Wakaftori.
15Kanaani alikuwa babu yake Sidoni, mzaliwa wake wa kwanza, na Hethi, 16na pia babu yao Wayebusi, Waamori, Wagirgashi, 17Wahivi, Waarki, Wasini, 18Waarvadi, Wasemari na Wahamathi. Baadaye watu wa jamii mbalimbali za Kanaani walitawanyika, 19hata eneo la nchi yao likawa toka Sidoni kuelekea kusini, hadi Gerari mpaka Gaza, na kuelekea mashariki hadi Sodoma na Gomora, Adma na Seboimu hadi Lasha. 20Hao ndio wazawa wa Hamu kadiri ya makabila yao, lugha zao, nchi zao na mataifa yao.
21Shemu, mkubwa wa Yafethi, alikuwa baba yao Waebrania wote. 22Watoto wa kiume wa Shemu walikuwa Elamu, Ashuru, Arfaksadi, Ludi na Aramu. 23Watoto wa kiume wa Aramu walikuwa Usi, Huli, Getheri na Mashi. 24Arfaksadi alimzaa Shela, Shela akamzaa Eberi. 25Eberi alikuwa na watoto wa kiume wawili; wa kwanza akamwita Pelegi kwa sababu wakati huo watu duniani waligawanyika, na wa pili akamwita Yoktani. 26Yoktani alikuwa baba wa Almodadi, Shelefu, Hasarmawethi, Yera, 27Hadoramu, Uzali, Dikla, 28Obali, Abimaeli, Sheba, 29Ofiri, Hawila na Yobabu. Hao wote walikuwa watoto wa Yoktani. 30Nchi walimokaa ilienea toka Mesha mpaka Sefari katika nyanda za juu za mashariki. 31Hao ndio wazawa wa Shemu, kadiri ya makabila yao, lugha zao, nchi zao na mataifa yao.
32Hao ndio jamaa za watoto wa Noa, kadiri ya vizazi vyao na mataifa yao. Kutokana nao mataifa yote yalienea duniani baada ya gharika.
Mwanzo10;1-32

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN):
Jifunze zaidi

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Tuesday, 31 January 2017

Kikombe Cha Asubuhi Mwanzo 9..

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tumshukuru Mungu kwa kutuamsha tena siku hii iliyompendeza Mungu..
Ikawe yenye Baraka,Amani,Upendo na Furaha..
Abariki Kutoka/Kuingia kwetu,Katika Kazi zetu,Masomo,Biashara na yote..
Akatuongoze kwenye Kunena,Kusikia na Kutenda..
Akawaponye na kuwagusa wote wanaopitia katika Magumu/majaribu Shida/Tabu.
Sifa na Utukufu ni kwakwe Daima!!!!
Mbarikiwe sana.


Mungu anafanya agano na Noa

1Mungu akambariki Noa na wanawe, akiwaambia, “Zaeni, muongezeke, mkaijaze nchi. 2Wanyama wote, ndege wote wa angani, viumbe wote watambaao juu ya nchi na samaki wote wa baharini watakuwa na hofu na kuwaogopa nyinyi. Wote wamewekwa chini ya mamlaka yenu. 3Wanyama wote hai watakuwa chakula chenu kama vile nilivyowapa mimea kuwa chakula chenu. 4Lakini msile nyama yenye damu, kwani uhai uko katika damu. 5Damu ya uhai wenu nitaidai; nitaidai kutoka kwa kila mnyama na binadamu. Atakayemuua binadamu mwenzake, nitamdai uhai wake.
6Amwagaye damu ya binadamu,
damu yake itamwagwa na binadamu;
maana binadamu aliumbwa kwa mfano wa Mungu.
7Nanyi zaeni, mkaongezeke;
zaeni kwa wingi, mkaongezeke nchini.”

Upinde wa mvua

8Kisha Mungu akamwambia Noa na wanawe, 9“Ninaweka agano langu nanyi na wazawa wenu 10na viumbe vyote hai: Ndege, wanyama wa kufugwa na wanyama wa porini, wote waliotoka katika safina pamoja nanyi. 11Nathibitisha agano langu nanyi, kwamba, kamwe viumbe vyote hai havitaangamizwa kwa gharika, wala haitatokea tena gharika kuiharibu nchi.” 12Tena Mungu akasema, “Hii ndiyo alama ya agano ninalofanya kati yangu nanyi na kila kiumbe hai kilicho pamoja nanyi kwa vizazi vyote vijavyo. 13Naweka upinde wangu mawinguni, nao utakuwa ishara ya agano kati yangu na dunia. 14Kila nitakapoifunika dunia kwa mawingu, na huo upinde wa mvua utakapoonekana katika mawingu, 15nitalikumbuka agano langu nanyi na viumbe vyote hai. Kamwe maji hayatageuka kuwa gharika ya kuviangamiza viumbe vyote hai. 16Huo upinde utakapotokea mawinguni, nitauona na kulikumbuka agano hilo la milele kati yangu na viumbe vyote hai duniani.” 17Mungu akamwambia Noa, “Hii ndiyo ishara ya agano ambalo nimefanya na viumbe vyote hai duniani.”

Noa na wanawe

18Watoto wa Noa waliotoka katika safina walikuwa Shemu, Hamu na Yafethi. Hamu alikuwa baba yake Kanaani. 19Hao ndio watoto watatu wa Noa, na kutokana nao watu walienea duniani kote.
20Noa alikuwa mkulima wa kwanza. Alilima shamba la mizabibu, 21akanywa divai, akalewa, kisha akalala uchi hemani mwake. 22Hamu, baba yake Kanaani, aliuona uchi wa baba yake, akatoka nje na kuwaambia ndugu zake wawili. 23Lakini Shemu na Yafethi wakatwaa nguo, wakaitanda mabegani mwao, wakaenda kinyumenyume na kuufunika uchi wa baba yao. Waliangalia pembeni, wala hawakuuona uchi wa baba yao. 24Noa alipolevuka na kujua alivyotendewa na mwanawe mdogo, 25akasema,
“Kanaani na alaaniwe!
Atakuwa mtumwa wa watumwa kwa ndugu zake.”
26Tena akasema,
“Shemu na abarikiwe na Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu!
Kanaani na awe mtumwa wake.
27Mungu na amkuze Yafethi,
aishi katika hema za Shemu;
Kanaani na awe mtumwa wake.”
28Baada ya gharika, Noa aliishi miaka 350, 29kisha akafariki akiwa na umri wa miaka 950.
Mwanzo 9;1-28
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (BHN):
Jifunze zaidi

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Monday, 30 January 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo 8....

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Ni wiki nyingine tena kwa uwezo,Neema/Rehema za Mungu ametujaalia kuiona tena Siku hii..
Tumrudishie Sifa/Utukufu kwa Muumba wa Yote,Yeye akisema atakubariki na hufanyika hivyo,
Yeye akisema ndiyo hakuna wa kupinga,
Tuanze wiki/siku hii na Mungu wetu akawe Mwanzo wa yote na mwisho wa yote.
Akabariki Kazi,Biashara,Masomo,Familia,Ndugu,Jamaa na Marafiki...
Wenye Shida/Tabu Mungu baba akawaguse,Yatima/Wajane baba ukawe nao..
Akatupe sawasawa na mapenzi yake.
Mungu wetu yu Mwema sana...!!!!
Tuanzena Mungu.


Mwisho wa gharika

1Kisha Mungu akamkumbuka Noa na wanyama wote wa porini na wa kufugwa waliokuwa pamoja naye ndani ya safina. Basi, Mungu akavumisha upepo juu ya nchi, maji yakaanza kupungua. 2Chemchemi za maji ya vilindi na madirisha ya mbinguni yakafungwa. Mvua ikazuiwa, 3maji yakaendelea kupungua polepole katika nchi. Baada ya siku 150, maji yakawa yamepungua sana. 4Mnamo siku ya kumi na saba ya mwezi wa saba, safina ikatua juu ya milima ya Ararati. 5Maji yakaendelea kupungua polepole, na siku ya kwanza ya mwezi wa kumi, vilele vya milima vikaonekana.
6Baada ya siku arubaini, Noa alifungua dirisha alilokuwa ametengeneza katika hiyo safina, 7akamtoa kunguru nje, naye hakurudi bali aliruka huko na huko mpaka maji yalipokauka nchini. 8Kisha Noa akamtoa njiwa apate kuona kama maji yalikuwa yamepungua juu ya nchi. 9Lakini, kwa vile maji yalikuwa bado yameifunika nchi yote, huyo njiwa hakupata mahali pa kutua, akamrudia Noa katika safina. Noa akanyosha mkono, akamtwaa na kumrudisha ndani ya safina. 10Noa akangoja siku nyingine saba, kisha akamtoa tena huyo njiwa. 11Njiwa huyo akamrudia Noa saa za jioni akiwa na tawi bichi la mzeituni mdomoni mwake. Kwa hiyo Noa akajua kwamba maji yalikuwa yamepungua katika nchi. 12Kisha akangoja siku nyingine saba, akamtoa tena yule njiwa; safari hii njiwa hakurudi kabisa.
13Noa alipokuwa na umri wa miaka 601, siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, maji yalikuwa yamekauka katika nchi. Noa akafunua kifuniko cha safina na alipotazama, akaona kwamba nchi ilikuwa imekauka. 14Siku ya 27 ya mwezi wa pili, nchi ilikuwa imekauka kabisa.
15Hapo, Mungu akamwambia Noa, 16“Toka katika safina, wewe pamoja na mkeo, wanao na wake zao. 17Toa pia viumbe wote hai wa kila aina waliokuwa pamoja nawe, ndege na wanyama na kila kiumbe kitambaacho, wapate kuzaa kwa wingi duniani, waongezeke na kuenea kila mahali duniani.” 18Basi, Noa akatoka katika safina pamoja na wanawe na mkewe pamoja na wake za wanawe. 19Wakatoka kufuatana na jamii zao, wanyama wote wa porini, viumbe wote watambaao, ndege wote na wanyama wote hai duniani.

Noa anamtolea Mungu tambiko

20Noa akamjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu, akatwaa mmoja katika kila aina ya wanyama walio safi na ndege walio safi, akamtolea Mungu sadaka za kuteketezwa. 21Harufu nzuri ya tambiko hiyo ikampendeza Mwenyezi-Mungu, naye akasema moyoni mwake, “Kamwe sitailaani tena nchi kwa sababu ya binadamu; najua kwamba mawazo yake ni maovu tangu utoto wake. Wala sitaangamiza tena viumbe wote kama nilivyofanya. 22Kadiri itakavyodumu nchi majira ya kupanda na kuvuna, ya baridi na joto, ya masika na kiangazi, usiku na mchana, hayatakoma.”
Mwanzo 8;1-22

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (BHN):
Jifunze zaidi


"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Sunday, 29 January 2017

Natumaini Mlikuwa/Mnaendelea na Jumapili hii Vjema

Natumaini Jumapili Ilikuwa njema/Inaendela vyema,
Mungu yu mwema na andelee kuwabariki katika yote..
hapa kwetu ni baridi inataka moyo kuamka Asubuhi na kwenda kwenye Ibada,
Basi tujitahidi kama tuwezavyo kwenda kutafuta mkate wetu..Mungu atusaidi na tushinde
Jaribu hili....
Tukumbushane kwa Amani na Upendo..




““Mimi ni mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. Kila tawi ndani yangu lisilozaa matunda yeye huliondoa, na kila tawi lizaalo hulisafisha lipate kuzaa zaidi. Nyinyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya ule ujumbe niliowaambieni. Kaeni ndani yangu, nami nikae ndani yenu. Kama vile tawi haliwezi peke yake kuzaa matunda lisipobaki katika mzabibu, hali kadhalika nanyi hamwezi kuzaa matunda msipokaa ndani yangu. “Mimi ni mzabibu, nanyi ni matawi. Akaaye ndani yangu, nami nikiwa ndani yake, huyo huzaa matunda mengi, maana bila mimi hamwezi kufanya chochote. Mtu yeyote asipokaa ndani yangu hutupwa nje kama tawi litupwalo nje hata likakauka. Watu huliokota tawi la namna hiyo na kulitupa motoni liungue. Mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, basi, ombeni chochote mtakacho nanyi mtapewa. Baba yangu hutukuzwa kama mkizaa matunda mengi na kuwa wanafunzi wangu. Mimi nimewapenda nyinyi kama vile Baba alivyonipenda mimi. Kaeni katika pendo langu. Mkizishika amri zangu mtakaa katika pendo langu, kama vile nami nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. Nimewaambieni mambo haya ili furaha yangu ikae ndani yenu, na furaha yenu ikamilike. Hii ndiyo amri yangu: Pendaneni; pendaneni kama nilivyowapenda nyinyi. Hakuna upendo mkuu zaidi kuliko upendo wa mtu atoaye uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. Nyinyi ni rafiki zangu mkifanya ninayowaamuru. Nyinyi siwaiti tena watumishi, maana mtumishi hajui anachofanya bwana wake. Lakini mimi nimewaita nyinyi rafiki, kwa sababu nimewajulisha yote ambayo nimeyasikia kutoka kwa Baba yangu. Nyinyi hamkunichagua mimi; mimi niliwachagueni na kuwatuma mwende mkazae matunda, matunda yadumuyo, naye Baba apate kuwapeni chochote mnachomwomba kwa jina langu. Basi, amri yangu kwenu ndiyo hii: Pendaneni.”
‭‭Yohane‬ ‭15:1-17‬ ‭BHND‬‬
http://bible.com/393/jhn.15.1-17.bhnd














"Swahili Na Waswahili"Muwe na wakati mwema.